Search

Predigten

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[2-5] Ni Nani Aliyeokolewa Toka Katika Dhambi? (Ufunuo 2:8-11)

(Ufunuo 2:8-11)
 
Kifungu hiki cha maandiko ni barua ya Bwana kwenda kwa Kanisa la Smirna katika Asia Ndogo, kanisa ambalo lilikuwa ni maskini kwa fedha na mali, bali ambalo lilikuwa ni tajiri kiimani. Pamoja na kuteswa na Wayahudi, na hata walipokuwa katika mateso ya kifo, watakatifu na watumishi wa kanisa hili waliilinda imani yao na hawakumkana Bwana na injili yake ya maji na Roho. Walipigana na kushinda kwa kuamini katika Neno la Mungu.
Bwana aliwaambia watakatifu wa Kanisa la Smirna kutoogopa mateso yatakayokuja, bali kuwa waaminifu hadi kifo hali akiwaahidi taji ya uzima.
Mungu aliwaambia watu wake kupigana na kuyashinda mafundisho ya kiimani ya uongo ya wale wanaojiita manabii. Ni lazima tuifahamu aina ya imani inayohitajika ili tuweze kuokolewa toka katika dhambi zetu zote. Ni lazima tutambue kuwa injili ya maji na Roho ndiyo injili ya kweli, na kwamba kwa kutumia imani hii tunapaswa kupigana na kuyashinda mafundisho ya imani ya uongo ambayo yanaukumba ulimwengu wa sasa wa Kikristo. Wakati ulimwengu mzima ulipokuwa umedanganywa na Shetani, Mungu alimtuma Bwana wetu kuitimiza injili ya maji na Roho. Pia amewaokoa wale wote wanaoiamini injili hiyo toka katika dhambi zao zote. Ni lazima tuutambue na kuuamini ukweli huu.
Ni watu gani ambao wameokolewa toka katika dhambi zao zote mbele za Mungu? Si watu walio na miili yenye nguvu au watu waliopendwa, bali ni wale walio kombolewa toka katika dhambi zao zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Hawa ndio watu ambao wamepigana na kuyashinda mafundisho ya kiimani ya uongo kwa kufahamu na kuamini katika injili ya maji na Roho. Mungu atawapatia baraka ya kuiepuka mauti ya pili wale wote wanaoamini katika injili hii na walioyashinda mafundisho ya imani ya uongo.
 

Wokovu wa Mungu Unatolewa Kwa Wale Wanaoshinda 
 
Kama Neno la Ufunuo linavyotueleza, “Yeye ashindaye hatapatikana na mauti ya pili.” Mungu atawapatia maisha mapya na Ufalme wake Mpya wale wote ambao watashinda. Kama tulivyo na masikio mawili, basi ni wazi kuwa mara nyingi tunasikia habari mbili tofauti—yaani tunausikia ukweli na pia tunausikia uongo kwa wakati mmoja. Hatma yetu inaamuliwa na neno tunalolipokea, yaani kati ya Neno la Mungu au neno la Shetani.
Hii ndiyo sababu ni lazima tuamini katika injili ya maji na Roho, na kisha kwa kutumia imani hii ambayo ni Neno la kweli tupambane na kuyashinda mafundisho ya uongo. Kwa kuwa kila mtu katika ulimwengu huu anateseka kutokana na uzito wa dhambi, basi ni lazima tuitafute injili ya maji na Roho ambayo inaweza kutukomboa kikamilifu toka katika dhambi zetu zote. Lakini kuna wengi ambao hawawezi kuupokea ukweli kwa sababu ya uongo ambao wamekwisha lishwa na walimu wa uongo. Wokovu unaotarajiwa kutokana na mafundisho ya manabii hawa wa uongo umejengwa katika msingi kwamba ikiwa hutendi dhambi basi ni hakika kuwa utabarikiwa.
Lakini, kwa asili yetu hatma yetu ni kutenda dhambi, ni asili isiyoweza kuepukwa ya kutenda dhambi, na kwamba hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kubakia tukiwa tumefungwa katika dhambi za ulimwengu huu. Ikiwa mioyo ya wenye dhambi imefungwa katika dhambi za ulimwengu na manabii wa uongo, basi watawezaje kumwamini Mungu na kuokolewa toka katika dhambi zao? Ni lazima walirudie kanisa la Mungu, walisikie Neno la injili ya maji na Roho na kisha wapokee pumziko la kweli katika mioyo yao kwa kuondolewa dhambi zao. Watu wengi katika ulimwengu huu wanalitafuta kanisa la kweli la Mungu na wanautafuta sana wokovu wao, lakini wengi wao wanashindwa kulipata kanisa kama hilo na mwishowe wanaishia katika kanisa la Sheria au kanisa la Torati—na hii ndiyo sababu bado wamefungwa kwenda kuzimu.
Basi ni kanisa gani ambalo ni kanisa la Mungu ambalo wenye dhambi wanalihitaji kwa kweli? Kanisa la Mungu ambalo kila mwenye dhambi analihitaji ni lile linaloihubiri injili ya maji na Roho. Kanisa la Mungu linalozungumziwa katika Biblia linahubiri juu ya ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani. Kanisa la kweli la Mungu linaelezea kwa usahihi na kufundisha jinsi Yesu alivyozichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake na jinsi alivyozitowesha, akifanya yote hayo ndani ya injili ya maji na Roho. Kila mwenye dhambi ambaye amekombolewa toka katika dhambi zake amefanya hivyo kwa imani inayokuja kwa kuisikia injili ya maji na Roho kwa kupitia kanisa la Mungu.
Lakini kwa kuwa Wakristo wengi bado hawajakutana wala kuisikia injili ya maji na Roho, basi hawajaweza kuokolewa toka katika dhambi zao zote. Lakini Mungu anatueleza kuwa atawaokoa toka katika dhambi wale wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho na wale wanaopigana na kuzishinda injili za uongo. Mungu ametuahidi kuwa wale watakaoshinda hawataumizwa na mauti ya pili.
Ukombozi wa kweli toka katika dhambi upo kwa ajili ya wale wanaosimama kinyume na kuwashinda walimu wa uongo. Kwa kuwa tunazaliwa kama wenye dhambi, basi ikiwa hatutaweza kuyashinda mafundisho ya uongo, basi ni hakika kuwa tutaishia kama wafungwa wa Shetani, waliofungwa katika dhambi, na mwishowe waliopangiwa kwenda kuzimu. Hii ndiyo sababu Mungu alimweleza kila mmoja wetu kuwashinda maadui katika vita vyetu vya kiroho.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wanyama kama vile simba au chui wanawafundisha watoto wao kwa kuwasukuma kwa makusudi kabisa chini ya mlima na kisha kuwafanya wapande huo mlima wao wenyewe. Kile kitoto kitakachoweza kufanya jitihada ya kupanda juu ya kilima ndicho kitakachokuzwa. Vivyo hivyo, Mungu ametupatia injili ya maji na Roho na atawaruhusu waingie mbinguni wale tu wanaoshindana na kuyashinda mafundisho ya uongo kwa kutumia injili hii.
Wokovu wetu hauji kwa kuitegemea damu yetu na miili yetu. Tunaweza kuokolewa toka katika dhambi kwa kuamini katika injili ya maji na Roho tu. Wokovu wa kweli unapatikana kwa imani katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani. Wakati mioyo yetu inapoamini katika ubatizo na damu iliyomwagwa ya Mwana wa Mungu ambavyo vimeziondolea mbali dhambi za ulimwengu, basi ni hakika kuwa tutaokolewa toka katika dhambi zetu zote na maangamizi. Kila anayeingia Mbinguni anafanya hivyo kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, na kila anayeishia kwenda kuzimu anafanya hivyo kwa kutokuiamini injili hii. Hii ndiyo sababu tunapaswa kuiamini injili ya maji na Roho na kuzikataa injili za uongo.
Shetani anajaribu kuwazuia watu ili wasiokolewe kwa kuiamini injili ya maji na Roho kwa kueneza mafundisho ya uongo. Je, haya mafundisho ya uongo ni yapi? Injili za uongo ni zile zinazofundisha kuwa Yesu hakuzichukua dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake. Zinafundisha kuwa wakati Yesu ameichukua dhambi yetu ya asili, basi dhambi zetu za kila siku ni lazima zisafishwe kwa maombi ya kila siku na toba. Mafundisho kama haya yanaweza kuonekana kuwa yana maana kwa mtazamo wa kidini, lakini yanapotazamwa kwa kupitia injili ya kweli ya maji na Roho basi ndipo yanapoonekana kuwa ni uongo.
Ukombozi wa kila mtu unakuja kwa kuamini katika injili ya maji na Roho; injili za uongo haziwezi kutukomboa toka katika dhambi. Hii ndiyo sababu ni lazima tupambane na kuyashinda haya mafundisho ya uongo. Kupambana dhidi ya Shetani maana yake ni kusimama kinyume na yale ambayo si ya kweli. Hivyo ni lazima tuamue ikiwa tutaamini katika injili ya maji na Roho au katika injili za uongo, na baada ya kuwa tumeyafanya maamuzi yetu, basi ni lazima tupambane na kile kilicho kinyume. Hata wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho hawawezi kumshinda Shetani ikiwa imani yao itabakia kuwa ya uvuguvugu.
Watu wengi ambao wameokolewa ni wale ambao walikuwa wakibishana au kujadiliana kati ya Neno la Mungu na lile la Shetani. Dhambi zao zilisamehewa pale walipoamua kuamini katika injili ya maji na Roho. Kila aliyeokolewa tangu mwanzo wa uumbaji hadi sasa, ni yule ambaye amekuwa akipambana na kuzishinda injili za uongo. Sisi sote ni lazima tuitafute na kuipata injili ya maji na Roho na kisha tuachane na injili za uongo na hatimaye tuweze kukombolewa toka katika dhambi zetu kwa imani.
 

Injili za Uongo ni Nini? 
 
Kwa lengo la kutoa kielelezo, hebu tudhani kuwa kuna kijiji ambacho kila anayeishi ndani yake ana jicho moja, na kwamba mgeni aliye na macho mawili amekwenda kukitembelea kile kijiji. Watu wanaoishi katika kile kijiji wanamwona mtu yule mwenye macho mawili kuwa ni “wa kushangaza,” “asiye wa kawaida,” “aliye tofauti kabisa,” na wengine wanamuona kuwa ni “mzushi.” Sababu inayowafanya watu hawa wamhukumu yule mgeni kuwa ni mzushi ni kwa sababu yupo tofauti na jinsi wao walivyo ambao ndio walio wengi. Vivyo hivyo, kuna mtazamo duni hapa ulimwenguni ambapo “walio wengi ndio wanaotawala,” au kwa lugha nyingine, “ukweli unapatikana kwa walio wengi.” Lakini ni lazima tutambue kuwa kanuni za kupata uamuzi na kupata hitimisho kwa kutegemea wingi wa watu ni potofu.
Katika ulimwengu wa milele, ukweli hauamuliwi na wengi, bali unaamuliwa kwa kufuata misingi na kanuni za kweli. Sasa ukweli huu unaweza kupatikana wapi? Ukweli huu unaweza kupatikana katika ukombozi wa wenye dhambi na kufunguliwa kwao toka katika maangamizi. Wale wote wanaofanyika kuwa wenye haki wanafanyika hivyo kwa kuokolewa toka katika dhambi zao—yaani baada ya kusikia kwa masikio yao juu ya ukweli wa injili ya maji na Roho na kisha kuiamini injili hii kwa mioyo yao.
Lakini kwa kuwa watu wengi sana wameangukia katika injili za uongo kwa muda mrefu, basi wakati ukweli halisi unapofunuliwa mbele yao wanauona ukweli huo kuwa ni kitu kigeni, cha kushangaza na chenye uzushi na hatimaye wanaukataa ukweli huo. Lakini injili ya maji na Roho ambayo wanaikataa ni injili ya ukweli ambayo ilifunuliwa, ikaaminiwa, na ikahubiriwa na mitume wenyewe tangu enzi hizo za Mitume. Tatizo la dhambi linaweza kutatuliwa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho tu mbele za Mungu.
Yesu, ambaye ndiye Kweli yetu, alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake mara moja na kwa wote kwa ubatizo wake toka kwa Yohana, ambaye anatoka katika ukoo wa Haruni, na kisha akaimwaga damu yake Msalabani kwa ajili yetu. Neno la Mungu linashuhudia kuwa Yesu alizibeba dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake. Kisha alikufa Msalabani, akafufuka toka kwa wafu, na kisha akapaa Mbinguni kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. Ukweli huu ulitimizwa miaka elfu mbili iliyopita wakati Yesu alipofanyika kuwa Bwana wa ukweli kwa kuzichukulia mbali dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake na damu yake Msalabani.
Hata hivyo, wale wanaodanganywa na uongo bado hawafahamu kuwa imani yao katika Yesu inaleta ukombozi mkamilifu toka katika dhambi; mbaya zaidi, nafsi nyingi katika ulimwengu wa Kikristo siku hizi zimepotea katika dhambi hali zikiwa zimechanganywa na injili za uongo. Hii ndiyo sababu wale wanaoamini katika injili ya kweli ya maji na Roho ni lazima waihubiri na kuieneza injili hii sehemu mbalimbali. Watu wanaweza kukombolewa toka katika dhambi zao zote kwa kuisikia na kuiamini injili hii ya kweli.
Ukweli uliofunuliwa katika Biblia ni injili ya maji na Roho (Mathayo 3:13-17, Waefeso 1:13). Katika kifungu cha maandiko toka Ufunuo, Mungu alilisifia Kanisa la Smirna kwamba pamoja na kuwa walikuwa ni maskini kwa maana ya mali, ukweli ni kuwa walikuwa ni matajiri katika imani. Lakini Mungu aliwataja Wayahudi kama watumishi wa Shetani, hii ni kwa sababu pamoja na kuwa walidai kumwamini Mungu, bado walikataa kuipokea injili yake ya ukombozi katika mioyo yao. Hawakumwamini Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wao pamoja na kuwa amezichukulia mbali dhambi zao zote kwa injili ya maji na Roho. Kwa kuwa walikataa kuupokea ukweli kuwa Yesu amezichukua dhambi zao, basi dhambi zao zilibakia kuwepo katika mioyo yao hata pale walipodai kumwamini Yehova Mungu.
Watu wa jinsi hiyo wanadai kwa midomo yao kuwa wanamwamini Mungu lakini ukweli ni kuwa wao ni “sinagogi la Shetani” ambalo halimwamini Mungu. Wale ambao wanadai kumwamini Yesu lakini bado hawajaupokea ukombozi wake katika mioyo yao, ni vema watambue kuwa na wao ni sehemu ya hili sinagogi la Shetani.
Katika ulimwengu huu kuna masinagogi mawili: moja ni sinagogi la Shetani na la pili ni Sinagogi la Mungu. Wakati Bwana atakaporudi, basi sinagogi la Shetani litaharibiwa na kuangamizwa milele na Sinagogi la Mungu litabarikiwa milele. Kwa maneno mengine, Mungu atawatenganisha wenye haki kati ya wenye dhambi. Si kila mtu anayedai kumwamini Yesu kama Mwokozi wake atakwenda Mbinguni.
Habari hii inaweza kuonekana vizuri katika yale ambayo Yesu alituambia katika Mathayo 7:21-23: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”
Kwa maneno mengine, hatuwezi kusema kuwa Mbingu ipo kwa ajili ya kila mtu anayedai kuwa anamwamini Yesu na kuliitia jina lake. Hata kama wanamwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao, ukweli ni kuwa kama hawaamini katika injili ya maji na Roho, basi hatimaye na wao watakuwa ni watumishi wa Shetani ambao watakuwa wamefungwa kuzimu. Kwa kuwa wanazifuata injili za uongo hata pale wanapodai kuwa wanamwamini Yesu, basi ni sahihi kwao na haki kutupwa kuzimu.
Wale walio na dhambi na ambao kwa sababu hiyo wapo upande wa Shetani ni wazi kuwa wamefungwa ili kwenda kuzimu. Lakini, malango ya Mbinguni yatafunguliwa kwetu sisi ambao tumepokea ondoleo la dhambi zetu zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Kila anayemwamini Yesu ni lazima aingie Mbinguni kwa kuamini katika injili ya maji na Roho.
Ili tuweze kuokolewa toka katika dhambi za ulimwengu hatupaswi kuwa na ufahamu kuhusu dhambi zetu tu, bali tunapaswa kuwa na uwezo wa kiroho wa kuweza kupambanua kati ya ukweli na uongo. Ili tuweze kufanya hivyo tunapaswa kujikita katika Neno la Mungu lililoandikwa na kisha kuamini kwa mujibu wa Neno hilo. Ikiwa hupendi kutupwa katika ziwa la moto, basi ni lazima uzikatae injili za uongo kwa imani. Ni lazima ushinde katika vita vyako dhidi ya injili za uongo. Na ili uweze kuupata ushindi wa imani ni lazima uifahamu injili ya maji na Roho. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo unapoweza kuiepuka mauti ya pili na ndipo hapo unapoweza kuingia katika Paradiso ya Mungu.
2 Yohana 1:7 inatueleza kuwa, “kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.” Kwa kusema mdanganyifu kuna maanisha kuwa ni wale wanaokana kuwa Yesu Kristo hakuja hapa duniani katika mwili. Kwa namna nyingine, wadanganyifu ni wale wanaoukana ukweli kuwa Bwana aliyekuja katika mwili ni Mwana wa Mungu, na kwamba alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake katika Mto Yordani, na kwamba alihukumiwa kwa ajili ya dhambi zetu kwa kuimwaga damu yake Msalabani.
Wale wasioupokea ukweli huu, kwamba Yesu ametuondolea mbali hukumu na adhabu ya dhambi zetu zote, basi hao ndio wadanganyifu na watumishi wa Shetani. Hao ni maadui wa Mungu na ni watumishi waaminifu wa Ibilisi. Wanawachanganya na kuwapeleka watu wengi katika maangamizi kwa kufundisha na kuzieneza injili zao za uongo na kusimama kinyume dhidi ya injili ya kweli ya maji na Roho.
Wale wanaodai kuiamini injili ya maji na Roho lakini hawapambani katika vita vya kiroho dhidi ya injili ya uongo ya Shetani wataishia wakiwa maadui wa Ufalme wa Mungu na watu wake. Watu wa jinsi hiyo hawajali ikiwa waamini wao wanaamini katika injili ya maji na Roho au la. Wanachokijali ni utukufu wao binafsi na mali. Hawa ni watumishi wa uongo ambao wanatamani kuyajaza matumbo yao tu. Kwa ufupi, hao ndio wale walio wa Mpinga Kristo ambaye Biblia inamwongelea.
 

Mbinu za Wazushi
 
Ezekieli 13:17-18 inasema, “Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, useme, Bwana MUNGU asema hivi; ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; Je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe?” Katika kifungu hiki tunaweza kuona kuwa watumishi wa Shetani wanatafuta kuziwinda roho za watu.
Kifungu hiki kinatueleza kuwa watumishi wa Shetani walikuwa wakishona hirizi katika mikono ya watu. Katika toleo la Biblia la Mfalme Yakobo, kifungu hiki cha maandiko kimetafsiriwa kama “Ole kwa wanawake washonao folonya katika maeneo ya mikononi.” Ni jambo lisilo la raha kwa mtu kuwa na folonya iliyoshonewa katika mikono, na je watu watakuona vipi? Wale ambao hawaifahamu wala kuiamini injili ya maji na Roho na waliopewa nafasi za uongozi katika kanisa wanafanana na mambo haya: hawana raha, wabaya, na vipofu. Kwa nini? Kwa kuwa nafasi za uongozi katika kanisa walizopewa haziendani na wao. Wanafahamu kuwa hawajahesabiwa haki wala hawajazaliwa tena upya kwa kuwa bado hawajaamini katika injili ya maji na Roho.
Inawezekanaje basi kwa watu kama hao kufanya kazi ya Bwana? Ili kuweze kuzifanya kazi za Mungu, mtu anatakiwa kwanza kupokea ukombozi toka katika dhambi kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, kuwa na hakika kuwa Roho Mtakatifu anakaa katika moyo wako, na kisha kufundishwa vya kutosha katika Neno la Mungu na ukweli wake; baada ya hapo ndipo unapoweza kushika nafasi yoyote katika kanisa.
Kwa kupitia Biblia, Mungu anatueleza sisi watu wake kuwa tunapaswa kupambana na kuwashinda manabii wa uongo kwa kuamini katika ukweli wake. Kuzaliwa tena upya kwa kuamini katika injili ya maji na Roho hakupatikana kwa kutofanya lolote. Kunapatikana kwa kuipata haki ya Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Mathayo 11:12 inasema, “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.” Wale walio na nguvu ndio wanaoingia katika Ufalme wa Mungu—nguvu, maana yake ni katika vita au mapambano yao dhidi ya uongo. Ni lazima ukumbuke kuwa unaweza kuokolewa kikamilifu kwa kuipokea injili ya maji na Roho katika moyo wako na kuyashinda mafundisho ya uongo, na hapo ndipo Roho Mtakatifu anapoweza kukaa ndani ya moyo wako.
Ili kuweza kuufikia wokovu mkamilifu, basi kila aliyezaliwa tena upya katika dunia hii ni lazima apambane na kuushinda uongo kwa Neno la Mungu la kweli. Ulimwengu huu ni uwanja wa vita kati ya nguvu za kweli na nguvu za uongo, kati ya wale waliozaliwa tena upya na wale ambao hawajazaliwa tena upya. Ulimwengu huu ulifanyika kuwa uwanja wa vita kati ya Mungu na Shetani kwa sababu Adamu na Hawa, pamoja na kuwa walikuwa wamepewa uzima na Mungu, waliishia katika kuuamini zaidi uongo wa Ibilisi kuliko Neno la Mungu.
Wakati wa sasa ndio wenye hatari zaidi, kwa kuwa Shetani, hali akijua ya kuwa muda wake umekwisha, anajaribu kuwazuia watu ili wasiiamini injili ya maji na Roho kwa kuwachanganya na manabii wa uongo, kwa kuwadanganya na miujiza ya uongo, na kwa kuwapoteza kwa matendo yake maovu yakiwa yamefanywa kama matendo ya Roho Mtakatifu. “Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.” (2 Wakorintho 11:14). Baada ya kuwa amezishinda dini kuu, sasa hivi Shetani anasimama dhidi ya wenye haki. Ingawa kwa sasa ni wakati ambapo uongo unaufunika ukweli, hali halisi ni kuwa hapo mwishoni wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho watawekwa huru toka katika uongo huo wote, na watakuwa ni washindi dhidi ya waongo wote.
Ili tuweze kuokolewa toka katika dhambi zetu zote ni lazima tuamini katika injili ya maji na Roho na kisha kujitenga mbali na mafundisho ya uongo ambayo yanadai kuwa ili tuweze kusamehewa dhambi zetu basi ni lazima tutubu dhambi zetu kila siku. Mungu ametuahidi kuwa wale watakaoushinda uongo wa jinsi hiyo kwa kutumia ukweli wake hawatapatikana na mauti ya pili. Hebu na tujitahidi kama walivyofanya watakatifu wa Kanisa la Smirna waliotutangulia kabla yetu katika kuilinda imani yetu mbele za Mungu ili na sisi tuweze kusifiwa na Mungu kwa sababu ya uaminifu wetu kwa Bwana.