Search

Predigten

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[6-1] Nyakati Saba Zilizopangwa na Mungu (Ufunuo 6:1-17)

(Ufunuo 6:1-17)
“Kisha nikaona hapo Mwana-Kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda. Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Na alipoifungua muhuri ya tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai. Na alipoifungua ile muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi. Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao. Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tatemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Kisha nikaona hapo Mwana-Kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo!”
Aya hii inatueleza kuwa Yesu anafungua mpango wa kwanza wa kitabu alichokipokea toka kwa Baba, ambacho kina maelezo kuhusu mpango mzima wa Mungu kwa mwanadamu.
 
Aya ya 2: “Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda.” 
Muhuri wa kwanza wa Mungu unaeleza juu ya kuanzishwa kwa injili ya maji na Roho katika Yesu Kristo kama sehemu ya mpango wa Mungu ili kuwakomboa wanadamu toka katika dhambi, na kwa ajili ya ushindi wa mpango huu. Mpango wa Mungu Baba kwa kuwafanya wanadamu kuwa watu wake kwa kuwaokoa toka katika dhambi zao ulianza na injili ya maji na Roho katika Yesu Kristo—yaani, ulianza na ukombozi wa mwanadamu toka katika dhambi kwa kupitia ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani.
Mungu amezikomboa nafsi toka katika dhambi zote za ulimwengu kwa injili ya maji na Roho, na anaendelea kufanya hivyo hata sasa tunapoongea. Huu ndio mpango wa kwanza ambao Mungu ameupanga kwa mwanadamu. Mpango huu wa kwanza wa Mungu ni kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu kwa kupitia kuja kwa Yesu Kristo hapa duniani, kwa ubatizo wa Yesu, kwa kusulubiwa kwake, na kwa ufufuo wake.
Wakati huu wa farasi mweupe unazungumzia juu ya ushindi wa Mungu katika vita ya haki ya injili ambayo aliitimiza ili kuwakomboa wanadamu toka katika dhambi zote. Hii inatueleza pia kuwa injili ya maji na Roho itaendelea kushinda.
 
Aya ya 3-4: “Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.” 
Hii inatueleza kuwa katika wakati au kipindi cha pili kilichopangwa na Mungu, ulimwengu utabadilika na kuwa ulimwengu wa Shetani. Kuonekana kwa farasi mwekundu kunamaanisha kuwa ulimwengu utakuwa chini ya himaya ya Shetani.
Shetani ameleta vita hapa ulimwenguni hali akiichukua amani ya dunia. Ulimwengu uliweza kuingia katika vita kuu mbili za dunia, na katika vita hizo idadi ya watu wengi wasio na hesabu walipoteza maisha yao, na wale waliofanikiwa kupona waliishi katika maisha ya taabu na katika amani iliyovunjika, haya yote yalitokea kwa sababu ya Shetani. Hata sasa, mataifa ulimwenguni kote hayaaminiani na yanatangaza vita dhidi yao hali wakiiharibu amani katika maeneo mengi. Wakati huu ni wakati wa vita na mauaji ya kimbari.
 
Aya ya 5-6: “Na alipoifungua muhuri ya tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai.”
Wakati wa kipindi cha tatu ambao Mungu anauzungumzia ni wakati wa farasi mweusi, wakati wa njaa ya kimwili na ya kiroho kwa wanadamu. Katika maeneo mengi duniani, kuna watu wengi hata sasa ambao bado hawajaokolewa kwa sababu ya njaa yao ya kiroho, pia kuna wengi wanaokufa kutokana na njaa ya kimwili. Ni lazima tukumbuke kuwa sasa tunaishi katika wakati huu au kipindi hiki cha tatu. Mara baada ya wakati huu kupita, utakuja wakati wa farasi wa kijivujivu.
 
Aya ya 7-8: “Na alipoifungua ile muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.” 
Wakati wa nne uliopangwa na Mungu ni wakati wa farasi wa kijivujivu. Biblia inatueleza kuwa ni katika kipindi hiki ndipo Mpinga Kristo atakapoanza shughuli zake, na kwamba wakati huu ni wakati pia wa kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini. Huu ndio wakati ambapo Mpinga Kristo atawatesa na kuwaua wale wasiomwamini yeye au wale ambao hawajaipokea alama yake ili apate kuwapokonya watakatifu imani yao ya kweli. Kuanzia hapo, ulimwengu utajikuta chini ya mateso ya mapigo ya matarumbeta saba. Katika wakati huu kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini ni kitu kisichokwepeka.
 
Aya ya 9-11: “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vilevile kama wao.”
Wakati au kipindi cha sita cha Mungu ni wakati wa ufufuo na kunyakuliwa kwa watakatifu. Mara baada ya wakati huu utafuata Ufalme wa Milenia. Kifungu cha maandiko hapo juu kinatueleza kuwa sisi sote tunapaswa kuamini katika kuuawa na kuifia-dini, katika ufufuo, na katika kunyakuliwa mambo ambayo yanatungojea, na kwamba tunapaswa kuishi kwa imani yenye tumaini juu ya Mbingu na Nchi Mpya ambavyo Mungu ametuahidia.
 
Aya ya 12: “Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tatemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu,”
Wakati wa saba wa Mungu ni wakati wa maangamizi ya ulimwengu wa kwanza ambao Mungu aliuumba. Huu ni wakati ambapo mapigo ya yale mabakuli saba yataushukia ulimwengu, wakati ambapo jua, mwezi, na nyota zitakapoipoteza nuru yake, na ni wakati ambapo ulimwengu utazama katika maji kwa sababu ya tetemeko la nchi.
 
Aya ya 13: “na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi.”
Katika wakati huu wa sita, maangamizi ya ulimwengu huu ulioumbwa na Mungu yatatokea kwa sababu ya yale mapigo ya mabakuli saba. Wakati nyota zitakapoanguka toka angani na ulimwengu kupinduliwa, basi ni wakati ambapo mkanganyiko mkuu utaighubika dunia.
 
Aya ya 14: “Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.”
Aya hii inatueleza kuwa wakati mapigo toka katika yale mabakuli saba yatakapokuwa yamemiminwa, basi mbingu zitapotea na kuondolewa kama vile ukurasa unavyokunjwa, na kwamba milima na visiwa vyote vitahamishwa toka mahali pake— haya ni machafuko ambayo yataibadili kabisa sura halisi ya dunia.
 
Aya ya 15: “Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,”
Katika wakati huu wa muhuri wa sita, yaani wakati ambapo Mungu atayamimina mapigo toka katika mabakuli saba, hakutakuwa na mtu yeyote atakayekuwa akiishi hapa duniani, kwamba ni mfalme au mwenye mamlaka ambaye hatatetemeka kwa hofu juu ya hasira ya Mwana-Kondoo.
 
Aya ya 16: “wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.”
Hasira ya Mungu itakuwa ni kubwa sana kiasi kuwa wanadamu wote watatetemeka kwa hofu. Huu utakuwa ndio wakati wa kwanza na wa mwisho ambapo kila mwanadamu atapatwa na hofu.
 
Aya ya 17: “Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?”
Wakati mapigo toka katika mabakuli saba yatakapomiminwa, basi kila mmoja bila kujalisha kuwa ni mwenye mamlaka au ni mwenye nguvu atatetemeka kwa hofu kutokana na mahangaiko yatakayoshuka toka katika hasira ya Mungu. Hakuna hata mmoja anayeweza kusimama mbele ya hasira ya Mungu pasipo hofu.
Je, kipindi au wakati wa saba ni upi? Wakati wa saba uliopangwa na Mungu ni wakati ambapo watakatifu wataishi katika Ufalme wa Milenia ambao utafuatiwa na Mbingu na Nchi Mpya ambamo wataishi ndani yake milele.