Search

Predigten

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-7] Kuja Kwa Bwana Mara ya Pili na Ufalme wa Milenia (Warumi 8:18-25)

(Warumi 8:18-25)
“Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu tukikutazamia kufanywa wana, yaani ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakiongojea kwa saburi.” 
 

Wale ambao ni wenye haki kwa kuamini katika haki ya Mungu basi hao wameupokea utukufu wa mbinguni. Hii ndiyo sababu wanateseka pamoja na injili ya maji na Roho ya Yesu ili kuwavika watu wote kwa utukufu huo wa mbinguni. Waamini wanajitoa wao wenyewe kwa injili ya haki ya Mungu na kisha wanateseka hapa duniani kwa sababu kushiriki katika mateso ya Kristo ni utukufu na haki. 
Je, si heshima kwetu kuteseka kwa ajili ya Mungu ambaye tunamheshimu kwa kina? Kwa kweli ni heshima; ni mateso yenye utukufu. Hii ndio sababu kuwa wale wote wanaoamini katika haki ya Mungu wanateseka kwa ajili ya haki yake. Je, hivi sasa unateseka kwa ajili ya nani? Je, unateseka kwa ajili ya ulimwengu na mwili wako? Je, ni mambo gani mema ambayo nafsi yako itayapata kwa kubeba mateso ya ulimwengu? Teseka kwa ajili ya haki ya Mungu na kisha uiamini haki hiyo. Kisha utukufu wa Mungu utakuwa pamoja nawe. 
 

Urithi Ambao Kwa Huo Tutabarikiwa Hapo Baadaye 
 
Hebu tufikirie juu ya urithi ambao tutaupokea. Urithi ambao tutaupokea huko mbinguni ni tuzo ya kutawala pamoja na Yesu katika mbingu na nchi mpya. Utukufu ambao tutaupokea katika Ufalme wa miaka Elfu moja na katika Ufalme wa milele wa Mungu ni mkubwa sana kiasi kuwa hauwezi kupimika. Ni wale waliozaliwa tena upya tu ndio watakaoufahamu na kuumiliki utukufu huu unaowasubiria wao. 
 

Utukufu Usiolinganishwa
 
“Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” (Warumi 8:18).
Hali akilinganisha utukufu utakaopokelewa na waamini kutokana na mateso yao katika wakati wa sasa, Paulo alisema kuwa utukufu wao utayazidi mbali mateso wanayoyapata sasa. Hii ni kweli kabisa; utukufu ambao unatusubiri sisi ni mkubwa sana kuliko mateso ambayo tunayabeba hivi sasa. 
 

Tarajio Kuu la Uumbaji 
 
“Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu” (Warumi 8:19-21).
Uumbaji wote wa Mungu unatamani kuwekwa huru toka katika utumwa wa dhambi. Ili viweze kuwekwa huru ni lazima Ufalme wa Mungu uanzishwe kwanza hapa duniani. Viumbe vingine vya uumbaji vinawasubiria watoto wa Mungu kuwa wakuu wa ule Ufalme wa miaka Elfu Moja. Hivyo, uumbaji wote unaisubiria ile siku ambapo wana wa Mungu wakiwa wamevikwa utukufu wa Mungu watakapotawala pamoja na Mungu katika Ufalme ule wa Mungu unaokuja. 
 

Kusubiri Ukombozi wa Miili Yetu
 
“Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu tukikutazamia kufanywa wana, yaani ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakiongojea kwa saburi.” (Warumi 8:22-25).
Wale wanaoamini katika injili ya haki ya Mungu wameokolewa toka katika dhambi zao zote. Wanausubiria Ufalme wa Mungu katika siku ile utakapowadia hali wakivumilia katika mateso yao yote. Wanateseka sana kwa ajili ya injili, na kwa kupitia mateso, tarajio lao kwa Ufalme wa Mungu linakuwa kubwa zaidi. Hili ni jambo la asili na la kawaida kwao. Hawalisubirii aina ya tarajio ambalo linaonekana kwa macho ya kimwili, bali Ufalme wa Mungu ambao hauonekani na kule kubadilishwa kwao. 
Watu pamoja na vitu vingine vyote vinaishi maisha mabaya ya shida na yanayochosha katika ulimwengu huu. Kadri muda unavyozidi kwenda, ulimwengu unazidi kubadilika, na kadri teknolojia na ustaarabu unavyozidi kukua, matarajio ya watu katika mioyo yao yanaongezeka zaidi. Wanatarajia kuiona paradiso hapa hapa duniani katika wakati ujao lakini bado wanakuwa na shaka, hasira, na mashaka, hali wakishangaa kwa nini mchakato huo unachukua muda mrefu hali kuna maendeleo hayo yote. Kompyuta, magari, na teknolojia nyingine na mafanikio mengine ya kisayansi yanaendelea, pamoja na mafanikio hayo bado imekuwa ni vigumu sana kusikia watu wakifurahia kwa vicheko. 
Je, kuna matarajio yoyote kwa wakati ujao kwa mwanadamu? Kwa bahati mbaya jibu litakuwa ni hapana. Kwa mujibu wa Neno la Ufunuo, na pia kwa mujibu wa maoni ya wanasayansi, machafuko yanatusubiri kwa upungufu wa maji, uharibifu wa ukanda wa ozoni, ukame na uharibifu wa mazingira vitu ambavyo vitawafanya wengi kufa kwa kiu na joto. Je, unaweza kuyahisi machafuko haya yote yakitusubiri katika moyo wako?
Je, tunaishi katika ulimwengu mzuri? Ulimwengu unaweza kuonekana kuwa ni mzuri kwa namna fulani. Je, kuna nini ambacho hakiwezi kununuliwa kwa fedha? Lakini tunahitaji maji safi na mazingira safi ya kiafya. Lakini hata sasa ukanda wa ozoni unazidi kuharibiwa jambo linalosababisha miale yenye sumu kupenya na kuingia katika hewa, miale hii isiyoonekana kwa macho ya kibinadamu inasababisha mimea kuwa hafifu na mioyo ya watu kuwa migumu. Watu wanaendelea kuhofia wakisema, “Ni jambo gani litaitokea dunia hii?” Lakini kinyume na watu wa ulimwengu, sisi waamini tuliozaliwa tena upya tuna imani kuwa tutashiriki katika ufufuo wa kwanza na kisha kutawala pamoja na Yesu kwa miaka elfu moja. 
Biblia inatueleza sisi kuwa Bwana mwenyewe atashuka tena kutoka mbinguni kwa sauti kuu, sauti ya malaika mkuu, na tarumbeta ya Mungu (1 Wathesalonike 4:16). Swali ni kuwa “lini” atarudi? Bwana wetu aliahidi kuwa atakuja kuwachukua wote wanaoamini katika injili ya maji, damu na Roho, kwa hiyo tunaisubiria ile siku. 
Wale waliozaliwa upya wanaamini katika injili hii. “Dhambi zangu zilipitishwa kwa Yesu wakati alipobatizwa, na ninamwamini Bwana kuwa ni Mwokozi aliyehukumiwa adhabu kwa ajili ya dhambi zangu na kwa niaba yangu.” Mungu ametupatia wokovu kwa kupitia Mwanawe pekee Yesu Kristo. Yesu Kristo anakuja tena kuwafufua watu wake na kuwafanya kutawala kwa miaka elfu moja katika dunia hii. Biblia ni kama fumbo la picha ambalo linapaswa kuunganishwa pamoja na wasomaji wake. 
Wakati Yesu alipokuja kwanza hapa duniani alikuja kwanza kuwaita wenye dhambi ili watubu. Yesu alizibeba dhambi zao katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake na alihukumiwa kwa ajili ya dhambi hizo kwa kuimwaga damu Msalabani. Wakati Bwana ambaye sasa anakaa mbinguni atakapokuja tena atawafufua wale wote wanaoamini katika haki ya Mungu ili waweze kutawala pamoja naye kwa miaka elfu moja. 
 

Ufalme wa Milenia
 
Wale ambao wanawapenda wengine kwa kweli katika ulimwengu huu basi hao ni watoto wa Mungu. Ni watu pekee ambao ndio wanaitoa injili ya haki ya Mungu kwa kila nafsi iliyopotea ili kuwavuta hao kwa Kristo. Je, watu wa dunia hii wanawapa tuzo watoto wa Mungu? Hapana. Basi ni nani anayetoa tuzo kwa watoto wa Mungu? Wakati Yesu atakapokuja tena atawatuza kwa kuwafufua wale ambao wamezaliwa tena upya na kuwaruhusu kutawala kwa miaka elfu moja. 
Ufalme wa miaka Elfu moja ni kwa ajili yetu sisi waamini ambao tumezaliwa tena upya. Hata pale ambapo ulimwengu wa sasa unazidi kuwa mpweke, wakati Bwana wetu atakapokuja tena sisi tutaishi katika ulimwengu mpya. Katika ulimwengu huo Bwana ataturuhusu kutawala na kukaa pamoja naye kwa maisha ya raha kwa muda mrefu kadri tupendavyo. 
Katika Warumi 8:23 Paulo alisema kuwa, “Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani ukombozi wa mwili wetu.” Je, unaisubiria siku hiyo? Hata sisi tulio na malimbuko ya Roho tunaugua katika nafsi zetu hali tukitazamia ukombozi wa miili yetu. Mungu alisema kuwa atatufufua, ataibadilisha miili yetu, na ataturuhusu kuishi pamoja naye. Sisi ambao tumezaliwa tena upya kama wenye haki tunatazamia na kusubiri kuja kwake mara ya pili kwa kupitia Roho Mtakatifu. 
Tunaugua katika nafsi zetu. Waamini waliozaliwa upya wanafahamu kuwa ulimwengu huu utakuwaje hapo baadaye. Yale ambayo wabashiri wanabashiri kuhusiana na hapo baadaye haya maana yoyote. Waamini waliozaliwa tena upya wanafahamu kwa usahihi yale ambayo yatatokea hapo baadaye. Hata kama ulimwengu ungebadilika na kuwa kama tulivyotabiri kwa usahihi hakuna hata mmoja atakaye tuamini wakati huu. Lakini wale wanaoamini katika Neno la Mungu lililoandikwa wanasubiri pasipo hata kujivuna. Hata kama watu wengine wasiolitambua Neno la Mungu wakiwachukulia kwa dharau bado wataishi wakiwa na tumaini. 
Kwa hiyo wale wasioamini ni lazima waupokee wokovu kabla maisha yao hayajafikia mwisho. Ni lazima waamini kwamba Yesu alizichukua dhambi zao katika mwili wake kwa ubatizo wake na kisha akahukumiwa kwa ajili yetu pale Msalabani. Ni hapo tu ndipo wanapoweza kuingia katika Ufalme wa Mungu siku hiyo ya mwisho itakapowadia. Hapo ndipo tutakapopewa tuzo na kisha kuingia katika Ufalme wake ili kupata uzima wa milele. 
Je, una huzuni? Je, unahofu na umechoka? Au umeridhishwa na maisha yako? Ni lazima tufahamu kwa usahihi na kuamini jinsi ambavyo Yesu amefanyika kuwa Mwokozi wetu kabla hatujafariki. Pia ni lazima tujiandae kuyaisha maisha yetu huko Mbinguni. Ulimwengu huu si kitu, hali tukiufahamu ukweli huu basi ni lazima tujiandae kuishi Mbinguni. Hivyo ndivyo wenye busara na hekima wanavyofanya. Je, unaishi katika anasa siku hadi siku? Ikiwa ndivyo, basi wewe ni mtu mjinga. Kwa upande mwingine, wale ambao wanayatamani mazuri, yaani nchi ya Mbinguni na kisha wanajiandaa kuzifanya ndoto zao kuwa kweli kwa kuingia katika Mbingu, basi hao ndio wenye busara na hekima ambao wanazijenga nyumba zao katika mwamba. 
 

Katika Ufalme wa Milenia
 
Mungu alituumba sisi katika sura na mfano wake na alitaka sisi tuishi pamoja naye milele. Hii ndiyo sababu Bwana alikuja hapa duniani, akaupokea ubatizo wake, na akaimwaga damu yake ili kutukomboa toka katika dhambi zetu zote. Wale wanaoamini katika haki ya Mungu wanaishi pamoja na Bwana, na Bwana atawapa tuzo kwa ajili hiyo. Bwana wetu atayafuta machozi toka katika macho yetu na kisha atatupa tuzo sisi sote kwa magumu yote na upweke tuliyokutana nayo. 
Mungu anavifanya vitu vyote kuwa vipya. Atauruhusu ulimwengu mpya kutokea ambapo mtoto anyonyae ataweza kuweka mkono wake katika tundu la nyoka na wala hatang’atwa (Isaya 11:8). Ni lazima tuamini na kukisubiri kile ambacho hakionekani hali tukiisubiria siku hiyo kwa shauku na uvumilivu. Ikiwa tutasema kuwa tunasubiri kwa kile kinachoonekana basi sisi ni wajinga. Kwa upande mwingine, ikiwa tutasubiri kwa kile kisichoonekana na kisha tukaliamini Neno la Mungu basi sisi ni wenye busara. Baada ya wokovu wetu, sasa tunausubiria utukufu ambao japokuwa sasa hauonekani kwa macho yetu tuna hakika kuwa utakuja. 
Mungu mwenyewe anaugua kuliko sisi tunavyofanya lakini bado anatufanya sisi kusubiri. Kwa kweli tunakutazamia sana kubadilishwa kwa miili yetu kwenda katika miili ya kiroho na kisha kutawala wakati muda wetu utakapowadia. Je, Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu anasema nini? Anatufanya tusubiri kwa jambo gani? Anatufanya tuusubiri Ufalme wa Milenia. Bwana anasubiri kuifanya upya miili yetu na kisha kuishi pamoja nasi. Sisi pia tunasubiri kutawala kwa miaka elfu moja pamoja na Mungu. 
Halleluya! Tunamtolea Bwana shukrani zetu.
Wakristo wanaishi hali wakiwa na tumaini lao la mbinguni na wanaujasiri katika tumaini hilo. Ujasiri huu haujengwi katika hisia zetu bali unajengwa katika Neno la Mungu ambaye hadanganyi.