Search

Sermones

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[1-1] Lisikie Neno la Ufunuo wa Mungu (Ufunuo 1:1-20)

(Ufunuo 1:1-20) 
“Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana; aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona. Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu. Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia: Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi; tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina. Mimi ni alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi. Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme wa subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Fildelfia, na Laodikia. Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto; na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kama kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi. Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking’aa kwa nguvu zake. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo. Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana,”
Kitabu cha Ufunuo kiliandikwa na Mtume Yohana, ambaye aliuandika ufunuo wa Yesu Kristo alioupata alipokuwa akiishi katika kisiwa cha Patmo kilichopo katika Bahari ya Aegan mahali ambapo alikuwa amepelekwa uhamishoni katika miaka ya mwisho ambapo Utawala wa Rumi ulikuwa ukififia chini ya Kaisari Dominitian (takribani AD 95). Yohana alihamishiwa katika Kisiwa cha Patmo kwa sababu ya ushuhuda aliokuwa akiutoa juu ya Neno la Mungu na juu ya Yesu; Yohana aliuona ulimwengu wa Mungu ulioonyeshwa kwake na Yesu Kristo kwa kupitia uvuvio wa Roho Mtakatifu na malaika zake.
Je, huu “Ufunuo wa Yesu Kristo” ni kitu gani? Kule kusema Ufunuo wa Yesu Kristo maana yake ni kwamba kwa kupitia mwakilishi wake Yesu Kristo, Mungu atatufunulia juu ya yale ambayo yataupata ulimwengu huu na Ufalme wa Mbinguni hapo baadaye. Je, kimsingi Yesu ni nani? Yeye ni Mungu Muumbaji na Mwokozi ambaye amewakomboa wanadamu toka katika dhambi za ulimwengu.
Yesu Kristo ni Mungu wa Ufalme Mpya utakaokuja, ni mfunuaji anayetuonyesha kila kitu juu ya ulimwengu huu mpya unaokuja, na pia Yesu Kristo ni mwakilishi wa Mungu Baba. Kwa kupitia Neno la Ufunuo lililoandikwa na Yohana tunaweza kuona jinsi ambavyo Yesu atakavyoushughulikia ulimwengu wa zamani na jinsi atakavyoufungua ulimwengu mpya.
 
Aya ya 2: “aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona.”
Yohana aliweza kulishuhudia Neno la kweli kwa sababu ya yale ambayo aliyaona ambayo Yesu Kristo atakuja kuyafanya hapo baadaye akiwa kama mwakilishi wa Mungu Baba. Yohana aliona na alisikia yale ambayo yatatimizwa kwa kupitia Yesu Kristo, na kwa sababu hiyo aliweza kuyashuhudia mambo hayo yote.
 
Aya ya 3: “Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.”
Hapa maandiko yanasema heri asomaye na kulisikia Neno la Mungu linaloshuhudiwa na Yohana. Ni nani walio heri? Kwanza kabisa, ni waamini ambao wamefanyika kuwa watu wa Mungu kwa kukombolewa toka katika dhambi zao zote kwa kupitia imani yao katika Neno la Mungu. Ni watakatifu tu ndio wanaoweza kubarikiwa kwa kuwa ndio wao wanaosoma, wanaosikia, na kuutunza ushuhuda wa Neno la Mungu—yaani mambo yote ambayo yatakuja kutokea kwa kupitia Yesu Kristo—yaani yote yaliyoandikwa na Yohana. Kwa sababu hii, wale waliofanyika kuwa watakatifu wa Mungu watapokea baraka za Mbinguni kwa kulisikia Neno la Mungu na kwa kuiweka imani yao juu yake.
Kama Mungu asingelitueleza siri ya ukweli juu ya yale yote ambayo yatakuja kutokea kwa dunia na Mbingu hii kwa kupitia Yohana, basi ingeliwezekanaje kwa watakatifu kusikia na kuona? Wangeliwezaje kuwa na baraka ya kuyafahamu mapema na kuamini juu ya mabadiliko yote ambayo ulimwengu unayapitia? Ninamtolea Mungu shukrani na utukufu kwa kutuonyesha kwa kupitia Yohana yale yote ambayo yanaingojea dunia na mbingu hii. Katika nyakati za sasa, wana heri wale ambao wanaweza kuona na kulisoma Neno la Mungu la ufunuo kwa kupitia Yesu Kristo kwa macho yao.
 
Aya ya 4: “Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia: Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi,”
Hapa Yohana anasema kuwa anaipeleka barua yake kwa makanisa saba ya Asia. Baada ya kuwa amekwisha kuuandika unabii na ufunuo ambao Mungu alimpatia wakati wa kipindi chake cha uhamisho katika kisiwa cha Patmo, basi Yohana anaipeleka barua yake kwa makanisa saba ya Asia na pia kwa makanisa yote ya Mungu katika ulimwengu mzima.
 
Aya ya 5: “tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,”
Kwa nini Yohana anamtaja Yesu Kristo kama “shahidi mwaminifu”? Bwana wetu alikuja hapa ulimwenguni na alibatizwa na Yohana Mbatizaji ili kuwakomboa wote walio katika dhambi na ambao walikuwa wamefungwa ili kuangamizwa. Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake mara moja na kwa wote kwa kupitia ubatizo wake, alikufa na kuimwaga damu yake Msalabani ili kuulipa mshahara wa dhambi kwa uhai wake mwenyewe, na kisha alilifufuka tena toka kwa wafu katika siku ya tatu—Yesu aliyafanya hayo yote ili kuwaokoa waamini na kuwasafisha toka katika dhambi zao. Kwa kuwa hakuna mwingine bali ni Yesu mwenyewe ndiye aliyewaokoa wenye dhambi wote ulimwenguni toka katika dhambi zao zote, basi Kristo anakuwa ndiye shahidi aliye hai kwa wokovu huu.
Bas kwa kule kusema “mzaliwa kwa kwanza wa waliokufa,” Yohana anatueleza kuwa Yesu alifanyika kuwa malimbuko kwa kuja hapa ulimwenguni na kuyatimiza mahitaji yote ya Sheria—kwa maneno mengine ni kwa kuulipa mshahara wa dhambi—kwa kuzichukua dhambi zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, kwa kufa Msalabani, na kwa kufufuka tena toka kwa wafu. Na kama Kristo “alivyotupenda na akatusafisha kwa damu yake,” basi Mungu amewaweka huru wale wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho toka katika dhambi zao zote.
 
Aya ya 6: “na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”
Kama mwakilishi wa Mungu Baba, Yesu Kristo alikuja hapa duniani katika mwili na akawaokoa wenye dhambi kwa ubatizo wake na damu yake Msalabani. Kwa matendo haya ya neema, Kristo ametusafisha na kutufanya kuwa watu na makuhani wa Mungu. Utukufu, sifa, na shukrani apewe Baba aliyetupatia baraka hizi za neema ya ajabu, na apewe Mwana ambaye ni mwakilishi wa Mungu na Mwokozi wetu milele na milele! Dhumuni la Kristo kufanyika mwili ilikuwa ni kutufanya sisi kuwa watu na makuhani wa Ufalme wa Mungu kwa ajili ya Baba. Kwa maneno mengine, tumefanywa kuwa “wafalme” wa Ufalme wa Mbinguni ambapo tutaishi pamoja na Mungu milele.
 
Aya ya 7: “Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina.”
Hapa inaelezwa kuwa Kristo atakuja na mawingu, kwa kweli ninaamini hivyo. Habari hii si hadithi ya kisayansi iliyotungwa. Huu ni unabii unaosema kwamba Yesu Kristo atarudi na kuujia ulimwengu huu toka Mbinguni. Na pia inaelezwa hapa kuwa “hata wale waliomchoma” watamwona. Je, hawa waliomchoma ni watu gani? Hawa ni wale ambao waliliona na kulichukulia Neno la maji na Roho kama moja ya mafundisho ya kiimani ya dini za ulimwengu, wakati Neno hili lina nguvu ya kuwaokoa.
Basi ni hakika kuwa wakati Kristo atakaporudi, wale waliomchoma kwa kutokuamini kwao wataomboleza. Watalia na kuomboleza kwa kuwa kwa wakati huo watatambua kuwa injili ya maji na Roho ndiyo injili ya ukombozi toka katika dhambi zao, na kwamba Yesu alibatizwa na Yohana ili kuzichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake. Kwa kweli watakuwa wamekwisha chelewa.
 
Aya ya 8: “Mimi ni alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja”
Kwa kule kusema “Alfa na Omega,” Yohana anatueleza kuwa Bwana wetu ni Mungu wa hukumu ambaye kwake unapatikana mwanzo na mwisho wa historia ya mwanadamu na ulimwengu mzima. Bwana atarudi kuwapatia thawabu wenye haki na kuwahukumu wenye dhambi. Yeye ni Mungu Mwenyezi ambaye atazihukumu dhambi za watu na kuwapatia thawabu ya haki wale wote wanaoamini katika haki yake.
 
Aya ya 9-10: “Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme wa subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,”
Neno “ndugu” linatumika wakati waamini wanapoitana wao kwa wao. Katika kanisa la Mungu la watu waliozaliwa tena upya, yaani wale waliofanyika familia kwa kuamini katika injili ya maji na Roho wanaitana ndugu au kaka na dada, na namna hii ya kuitana inapatikana kwetu kwa kupitia imani yetu katika injili ya maji na Roho.
“Siku ya Bwana” inayotajwa hapa ina maanisha kuwa ni siku baada ya Sabato, yaani siku ambayo Yesu alifufuka toka katika kifo. Hii ndiyo siku ambayo Yesu alifufuka, na ndiyo maana tunaiita Jumapili “Siku ya Bwana.” Siku hii inaonyesha mwisho wa kipindi cha Sheria au Torati na ndiyo siku ya kufunguliwa kwa kipindi kipya cha wokovu. Pia kwa ufufuo wake, Bwana wetu anatueleza kuwa Ufalme wake si wa ulimwengu huu.
 
Aya ya 11: “ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Fildelfia, na Laodikia.”
Yohana aliandika yale aliyoyaona kwa kupitia ufunuo wa Yesu Kristo na akawatuma kama barua kwa yale makanisa saba ya Asia. Hii inatueleza kuwa Mungu anaongea na Kanisa zima kwa kupitia watumishi wake ambao walitangulia kabla yetu.
 
Aya ya 12: “Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu”
Kwa kuwa Maandiko ya Mungu yalikuwa bado hayajakamilika katika siku za mitume, basi kulikuwa na haja ya kuonyesha ishara na maono kwa wanafunzi. Wakati Yohana alipogeuka ili kuisikia sauti ya Mungu aliviona “vinara saba vya dhahabu.” Vinara vina maanisha ni makanisa ya Mungu, yaani makusanyiko ya watakatifu wanaoamini katika ufunuo wa injili ya maji na Roho. Mungu alikuwa ndiye Bwana wa makanisa saba ya Asia, na bado alikuwa ni Mchungaji anayewatunza watakatifu wote.
 
Aya ya 13: “na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini.”
“Mtu mfano wa Mwanadamu,” ambaye Yohana alimwona “katikati ya vinara saba” ni Yesu Kristo. Akiwa kama Mchungaji wa watakatifu, Yesu anawatembelea na kuongea na wale wanaoamini katika Neno la kweli la ubatizo wake na kusulubiwa kwake. Maelezo ya Yohana juu ya Kristo akiwa na “vazi ambalo limefika miguuni na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini” yana maanisha juu ya hali ya Bwana kuwa ni Mwakilishi wa Mungu Baba.
 
Aya ya 14: “Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto”
Bwana wetu ni mtakatifu aliyekamili, mwenye uwezo, na mwenye heshima. Kule kusema “macho yake ni kama mwali wa moto” kuna maanisha kuwa akiwa kama Mungu Mwenyezi, basi yeye ni Hakimu wa haki wa wote.
 
Aya ya 15: “na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kama kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi.”
Je, tunafikiri kuwa Yesu ni nani? Watakatifu wanaamini kuwa Yesu ni mkamilifu na Mungu aliyekamilika. Bwana wetu ni mwenyezi na hana udhaifu wowote. Lakini kwa kuwa aliupitia udhaifu wetu alipokuwa akiishi hapa duniani, basi yeye ana uelewa mzuri wa mazingira na hali yetu na hivyo anaweza kutusaidia vizuri. Kule kusema kuwa sauti yake ilikuwa ni kama sauti ya maji mengi kunaonyesha jinsi Bwana wetu alivyo mkuu na mtakatifu. Kwa kweli hakuna aina yoyote ya uchafu au udhaifu kwa Bwana wetu, yeye amejazwa na utakatifu, upendo, ukuu, na heshima.
 
Aya ya 16: “Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake”
Kule kusema kuwa “Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume” kuna maanisha kuwa Bwana analitunza kanisa la Mungu. Kwa upande mwingine, kule kusema “upanga wa makali kuwili” unaotoka katika kinywa chake unaonyesha kuwa Yesu ni Mungu Mwenyezi anayefanya kazi na Neno lenye mamlaka na nguvu ya Mungu. Kule kusema “kama jua liking’aa kwa nguvu zake zote,” kuna maanisha kuwa Bwana wetu ni Mungu wa Neno, yaani Yeye aliye mahali pote na mwenye uwezo wote.
 
Aya ya 17: “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho”
Aya hii inatuonyesha jinsi tulivyo wadhaifu na wenye giza mbele ya utakatifu wa Mungu. Bwana wetu ni mwenye uwezo na mkamilifu wakati wote, na wakati mwingine anajifunua kwa watumishi wa Mungu kama rafiki, na wakati mwingine anajifunua kama Mungu wa hukumu kali.
 
Aya ya 18: “nami nalikuwa nimekufa, na tazama ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”
Bwana wetu anaishi milele na ana mamlaka yote ya Mbinguni kama mwakilishi wa Mungu Baba. Akiwa kama Mwokozi na Hakimu wa wanadamu, Yesu ni Mungu aliye na mamlaka juu ya uzima wa milele na kifo.
 
Aya ya 19: “Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.”
Watumishi wa Mungu wana jukumu la kuandika dhumuni na kazi za Mungu, yaani kazi zote zilizopo na zitakazokuja baadaye. Hivyo, Bwana alimwambia Yohana kuyaeneza kwa imani yale ambayo alikuwa amemfunulia, yaani imani ya kanisa la Mungu ambayo inaweza kuupata uzima wa milele, na pia juu ya mambo yote ambayo yatakuja hapo baadaye. Haya ndiyo mambo ambayo Mungu ametuamuru na sisi kwa kupitia Yohana.
 
Aya ya 20: “Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.”
Je, “siri ya nyota saba” ni nini? Ni kwamba Mungu ataujenga Ufalme wake kwa kutufanya sisi kuwa watu wake kwa kupitia watumishi wake. “Vinara vya dhahabu” vina maanisha ni makanisa ya Mungu yaliyojengwa kwa kupitia watakatifu walioamini katika injili ya maji na Roho ambayo Mungu aliwapatia wanadamu.
Kwa kupitia watumishi wake na makanisa yake, Mungu amewaonyesha waamini kuhusu lengo lake na juu ya kile kinachoungojea ulimwengu huu hapo baadaye. Kwa kupitia Neno la ufunuo ambalo alimwonyesha Yohana, sisi nasi tutaweza kuyaona matendo yake kwa macho yetu. Ninamshukuru na kumsifu Mungu kwa neema yake ya kimungu ambayo imeyafunua mambo yote ambayo yatakuja kutokea katika ulimwengu huu.