Search

Sermones

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[5-1] Yesu Aliyetawazwa Kuwa Mwakilishi wa Mungu Baba (Ufunuo 5:1-14)

(Ufunuo 5:1-14)
“Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa satui kuu, Ninani astahiliye kukifungua kitabu na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama, Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie; tazama, Simba aliye wa kabila la Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba. Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema:
‘Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu,
Na kuzifungua muhuri zake;
Kwa kuwa ulichinjwa, 
Na ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
Ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchi;
Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu:
Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa,
Kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. 
Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi na juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia vikisema:
Baraka na heshima na utukufu na uweza
Una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye
Mwana-Kondoo, hata milele na milele. 
Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka wakasujudu.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba.”
Hapa maandiko yanasema kuwa Mungu Baba alikuwa na kitabu chenye mihuri saba katika mkono wake wa kuume. Bwana wetu Yesu Kristo alikichukua kitabu hiki kilichokuwa kimeshikiliwa katika mkono wa kuume wa Baba, hii ina maanisha kuwa Yesu alipewa mamlaka yote ya Mbinguni.
 
Aya ya 2-4: “Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa satui kuu, Ninani astahiliye kukifungua kitabu na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama, Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.”
Hapakuwa na yeyote zaidi ya Yesu ambaye angeliweza kuuhukumu ulimwengu, kuumba Mbingu na Nchi Mpya, na kisha kuishi ndani ya ufalme huo pamoja na watakatifu kama mwakilishi wa Mungu Baba.
 
Aya ya 5: “Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie; tazama, Simba aliye wa kabila la Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.”
Hii sentensi isemayo “Simba aliye wa kabila la Yuda, Shina la Daudi” inauthibitisha ukweli kuwa Yesu Kristo ni Mungu Mwenyezi na Mfalme wa wafalme ambaye anastahili na mwenye uwezo wa kuutimiza mpango wa Baba. Yesu Kristo ni Mungu mwenyewe na mwakilishi wa Mungu ambaye atautimiza mpango wa Baba.
 
Aya ya 6: “Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.”
Baada ya kuwa ameyapokea mamlaka yote juu ya mbingu na nchi toka kwa Mungu Baba, Yesu Kristo ni Mungu Mwenyezi aliyeviumba vitu vyote. Yeye ndiye aliyekuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, akazipokea dhambi zote za ulimwengu, na akafa kwa ajili ya dhambi hizi ili kutukomboa toka katika dhambi zetu zote.
 
Aya ya 7: “Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi.”
Kwa kuwa Yesu Kristo alistahilishwa kuwa Mungu, basi ndio maana aliweza kukichukua kitabu toka kwa Baba. Hii ina maanisha kuwa tangu wakati huo Bwana wetu atazifanya kazi zote za Baba.
 
Aya ya 8: “Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.”
Hii ina maanisha kuwa Yesu Kristo atafanya kwa niaba ya Baba kama Mungu, na jukumu lake la kwanza ni kusikia maombi ya watakatifu yaliyomiminwa na wazee 24 na wale wenye uhai wanne.
 
Aya ya 9: “Nao waimba wimbo mpya wakisema: ‘Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu, Na kuzifungua muhuri zake; Kwa kuwa ulichinjwa, Na ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa”
Hapa Yesu Kristo anasifiwa na watumishi wa Mbinguni baada ya kufanyika kuwa mwakilishi wa Mungu. Watumishi wa Mbinguni walimsifu Yesu Kristo kwa kuwaokoa wenye dhambi hapa duniani toka katika dhambi za ulimwengu. Alipokuwa hapa duniani, Yesu alibatizwa na Yohana na kisha akafa Msalabani ili kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zote za ulimwengu, na akawapatanisha wenye dhambi hawa kwa Mungu Baba kwa kuulipa mshahara wa dhambi kwa damu yake mwenyewe. Hii ndiyo sababu watumishi wa Mbinguni wanazisifu kazi za haki za yeye aliyefanyika kuwa Mungu wao.
 
Aya ya 10: “Ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchi” 
Yesu Kristo, aliyefanyika kuwa mwakilishi wa Mungu Baba, aliwabadilisha watakatifu kuwa watu na makuhani wa Ufalme wa Mungu, na akawafanya kutawala juu ya ufalme huo. Hivyo alistahili sana kupokea utukufu wote na sifa toka kwa watumishi wa Mbinguni.
 
Aya ya 11-12: “Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, Kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.” 
Kwa kuwa Yesu alikuwa amezichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake toka kwa Yohana, basi ndio maana aliweza kuimwaga damu yake Msalabani, na kwa sababu hii anastahili kupokea uweza, utajiri, hekima, heshima, utukufu, na baraka toka kwa viumbe wote Mbinguni kama yule anayemwakilisha Baba. Hali akiwa amezungukwa na watumishi wa Mbinguni na malaika, Yesu anapokea sifa zao zote na anaabudiwa. Wale wenye uhai wanne na wazee 24 walikuwa wamekizunguka kile kiti cha enzi cha Mungu, Halleluya! Bwana Asifiwe! Walimsifu Mungu aliyezikomboa nafsi zote toka katika dhambi kwa kuwa utukufu wake hauna mwisho.
 
Aya ya 13-14: “Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi na juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia vikisema: Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele. Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka wakasujudu.”
Hatimaye, Yesu Kristo aliyefanyika kuwa mwakilishi wa Mungu aliinuliwa kuwa yule anayestahili kupokea sifa na kuabudiwa toka kwa watumishi wa Mbinguni. Watumishi wote wa Mbinguni walimbariki na kumpatia heshima, na utukufu milele na milele, kwa kweli lilikuwa ni jambo la kushangaza na lenye kutolewa shukrani kwamba Mungu ni mwenye kustahili kiasi hicho. Wakatifu wote Mbinguni na duniani ni lazima wampatie heshima na utukufu yeye aliyetawazwa kama mwakilishi wa Mungu Baba.