Search

Sermones

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[10-2] Je, Unafahamu Kunyakuliwa Kwa Watakatifu Kutatokea Lini? (Ufunuo 10:1-11)

(Ufunuo 10:1-11)
 
Hebu sasa tuangalie juu ya ni lini unyakuo utatokea. Kuna vifungu vingi katika Biblia vinavyozungumzia kuhusu unyakuo. Agano Jipya lina vifungu vingi vinavyozungumzia mada hiyo, vivyo hivyo Agano lake Kale, kwa mfano ni wapi tunapoweza kuona hivyo, Eliya alichukuliwa mbinguni katika gari la farasi la moto, na Enoki aliyetembea na Mungu naye pia alichukuliwa na Mungu. Kama inavyoweza kuonekana, Biblia inazungumzia juu ya kunyakuliwa katika sehemu nyingi. Unyakuo maana yake ni ‘kuinuliwa juu.’ Inahusiana na tendo la Mungu la kuwainua watu wake kwenda Mbinguni kwa nguvu zake.
Hata hivyo, swali ambalo lina fumbo sana katika Biblia ni swali kuhusu unyakuo. Ni lini Mungu atawanyakua watu wake? Swali hili kuhusu wakati wa unyakuo limekuwa ni swali ambalo linaulizwa sana ndani ya Ukristo.
Hebu tugeukie 1 Wathesalonike 4:14-17 kisha tuone kile ambacho Mungu alituambia kwa kupitia Mtume Paulo: “Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.”
Katika Yakobo 1:14, Mungu anatueleza kwamba, “Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu.” Kwa maneno mengine, watakatifu watainuliwa na Mungu wetu kwenda angani kwa mlio wa tarumbeta la malaika mkuu, watakuwepo pale angani kwa kitambo kidogo, kisha watashuka hapa duniani pamoja na Bwana wetu. Haya ndio maelezo sahihi ya kibiblia kuhusu unyakuo.
Sababu iliyotufanya tukiangalie kifungu hicho hapo juu mapema ni kwa sababu Ufunuo sura ya 10 inatueleza kuhusu lini unyakuo utakuja. Kama ilivyotajwa hapo kabla, kifungu cha msingi cha sura hii kinapatikana katika aya ile ya 7, “isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Aya hii ni ufunguo wa kujibu maswali yote na hoja kuhusu unyakuo, kwa kuwa aya hii inatueleza ni lini unyakuo utatokea.
Mungu anamtuma malaika mkuu kwenda kwa Yohana katika maono, na anamwonyesha kile ambacho atakifanya kwa kupitia malaika huyu kwa kumfanya atende kana kwamba Bwana amekuja hapa duniani. Huyu, malaika hali akiuinua mkono wake kuelekea mbinguni, “akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya” Kule kusema kwamba hakutakuwa na wakati baada ya haya maana yake ni kwamba hakuna sababu yoyote ya kuchelewa tena. Hii ina maanisha kwamba “hakuna wakati.” Na huku kusema kwamba hakuna wakati, maana yake ni kwamba katika siku ya mlio wa tarumbeta la malaika wa saba, siri ya Mungu itatimizwa kama Mungu alivyowahubiri watumishi wake manabii.
Kati ya mapigo ya matarumbeta saba, wakati tarumbeta la saba litakapopigwa, ulimwengu utaingia katika mapigo ya mabakuli saba. Sasa, tunapaswa kutambua kwamba wakati huo kutakuwa hakuna muda au wakati uliosalia kwa ajili ya ulimwengu huu. Kwa hiyo, Neno la Mungu katika aya ya 7, kwamba, katika siku za “malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii,” ina maanisha ni juu ya unyakuo. Paulo, pia alisema sehemu mbalimbali kwamba unyakuo utatokea kwa sauti ya malaika mkuu na kwa sauti ya tarumbeta la Mungu. Hiki ndicho ambacho Paulo alikuwa nacho akilini mwake, na huu ndio mwanzo wa nukuu zote za Biblia kuhusu unyakuo.
“isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Hili Neno linatueleza kwamba kunyakuliwa kwa watakatifu kutatokea wakati malaika wa sababu atakapolipiga tarumbeta lake, na kisha kuwainua angani. Wakati watumishi wa Mungu wanapoieneza injili ya maji na Roho kwa nafsi zilizopotea, basi hapo ndipo Roho Mtakatifu anaposhuka katika mioyo ya waamini walioipokea injili ya kweli, na hapo ndipo wanapofanyika kuwa watoto halisi wa Mungu. Hapo ndipo unyakuo, ambao ni siri ya Mungu, utakapogeuka na kuwa uhalisia, huku ukiwainua watakatifu kwenda angani.
Baada ya unyakuo huu, Mungu ataungamiza ulimwengu kikamilifu kwa kuumiminia mapigo ya mwisho ya mabakuli saba, kisha atauleta Ufalme wa Mungu hapa duniani ambapo tutatawala pamoja na Kristo kwa miaka elfu moja, na kisha atatuhamishia kwenda katika Mbingu na Nchi Mpya ambako tutaishi milele.
Baada ya Mungu kumweleza Yohana juu ya unyakuo unaokuja, Mungu alimwamuru Yohana kukila kitabu kidogo na kisha kutoa unabii tena. Somo la msingi sana ambalo watumishi wa Mungu wanapaswa kuwafundisha watakatifu wanaoishi katika siku hizi za mwisho ni kuhusu tukio la unyakuo na wakati maalum ambapo tukio hili litatokea. Wanapaswa kulifundisha somo hili kwa namna ya kibiblia. Pia ni lazima waihubiri injili ya maji na Roho kwa usahihi. Haya ndio mambo ambayo watumishi wa Mungu na watakatifu wake, wanaoishi kuelekea nyakati za mwisho wanapaswa kuyafanya. Hivyo, Mungu amewapatia watakatifu kazi hizi, huku pia akiiwafunulia siri yake. Mungu anatueleza kwamba hatakawia, bali atazitekeleza kazi zake pasipo shaka. Wakati utakapowadia, Mungu atavitimiza vitu vyote kuwa katika uhalisia.
Katika sura ya 11, kunaonekana mizeituni miwili, ambao ni manabii wawili. Watumishi hawa wawili wa Mungu, wanaotajwa kama mizeituni miwili, watauawa na Mpinga Kristo katika mapambano yao dhidi yake, lakini watafufuliwa toka kwa wafu tena na kisha kunyakuliwa kwa siku tatu na nusu. Kwa maneno mengine, Mungu anatuonyesha katika matukio mbalimbali kwamba unyakuo utatokea wakati watakatifu watakapouawa kama wafia-dini katika kipindi hicho cha Mpinga Kristo.
Tunachopaswa kukitambua mapema ni kwamba watakatifu wataishi na kuipitia Dhiki Kuu, watakuwepo hapa duniani hadi pigo la sita kati ya yale mapigo saba ya matarumbeta litakapopita. Naye Mungu atawalinda watakatifu kutokana na mapigo haya ya matarumbeta saba—yaani, Mungu atawalinda hadi wakati wa pigo la sita, lakini hatimaye Mpinga Kristo atawaua wakati wa ukatili wake utakapofikia kimo cha juu wakati akijaribu kupambana na Mungu. Vifo ambavyo watakatifu watavipokea ndiko kuifia-dini. Kwa kuwa watakufa vifo vya haki ili kuilinda imani yao, basi ndio maana tunayaviita vifo hivi kuwa ni kuifia-dini. Hivyo ni lazima tuamini kwamba ufufuo utakuja baada ya mauaji ya kufia-dini, pia ni lazima tuihubiri injili hii kwa wengine.
Watu wengi wamechanganyikiwa sana kwamba ikiwa unyakuo utatokea kabla au baada ya Dhiki Kuu. Watu wengi katika zama za kale walifikiri kwamba Kristo atarudi baada ya Dhiki, na kwamba watakatifu watainuliwa na huu ujio wa Kristo mara ya pili. Lakini siku hizi, Wakristo wengi wanaamini kwamba unyakuo utakuja kabla ya Dhiki Kuu. Wanafikiri kwamba hawatakuwa na la kufanya kuhusiana na mapigo ya matarumbeta saba au yale ya mabakuli saba, na kwamba watainuliwa wakati wakiendelea na maisha yao ya kawaida. Lakini hatupaswi kudanganywa kwa mafundisho haya ya uongo. Watu hawa wanafanya makosa makubwa sana katika ufahamu wao juu ya kunyakuliwa; kadri nyakati za mwisho zinavyozidi kukaribia, utakatifu wao utalegea na imani yao itatoweka.
Ninapokueleza kwamba unyakuo utakuja katikati ya Dhiki Kuu, sielezei hivi ili kukufanya wewe uwe mtakatifu zaidi. Ninachotaka ni wewe uwe na ufahamu sahihi juu ya wakati wa kunyakuliwa ili uyakimbie mafundisho ya uongo ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, hii ni kwa sababu katika aya ya 7 Mungu anatueleza kwa kina kwamba: “katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapomiminwa, tofauti na ilivyo kwa mapigo ya matarumbeta saba, mapigo ya mabakuli saba yatamiminwa moja baada ya jingine kwa kufuatana. Sisi watakatifu tunapaswa kulitambua hili.
Ufunuo 16:1-2 inatueleza kwamba, “Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi. Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.” Umiminaji wa mabakuli yaliyosalia kwa mstari hali ikianzia na hili pigo lakwanza, ni kana kwamba mapigo haya yamo katika ndege isiyotumia mitambo bila rubani, yaani huku malaika saba wakiyamimina mabakuli yao moja baada ya jingine, huku kukiwa hakuna mlio wa tarumbeta wala chochote kile. Kwa maneno mengine, kitendo cha kuyamimina mabakuli saba kwa mstari, kina maanisha kwamba Mungu atauangamiza ulimwengu huu kikamilifu. Kwa nini? Kwa kuwa kila kitu kitaisha kwa kumiminwa kwa mapigo ya mabakuli saba, ambayo kwa ujumla wake yamejumuishwa katika pigo la tarumbeta la saba.
Wakati mapigo ya matarumbeta saba yatakapoletwa, kutakuwa na kiasi fulani cha kupumzika kati ya pigo na pigo, lakini wakati wa mapigo ya mabakuli saba hakutakuwa na mapumziko hayo. Kwa kuwa mapigo haya ya mabakuli saba yamehifadhiwa kwa ajili ya kipindi cha mwisho, basi baada ya mapigo ya matarumbeta saba kuletwa kwa mfuatano wake, na wakati tarumbeta la mwisho litakapopigwa, basi ulimwengu utageuka na kuwa katika hatua nyingine ambapo kial kitu kitafikia mwisho.
Hii ndio maana Ufunuo 11:15-18 inaeleza hivi: “Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu wakisema, Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki. Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.”
Hapa inaelezwa kwamba wakati malaika wa saba alipolipiga tarumbeta lake, sauti kubwa ilisikika ikisema, “Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele!” Lakini hapa hakutajwi juu ya mapigo. Kwa nini? Hii ni kwa sababu mara baada ya tarumbeta la saba, halikuata pigo la saba, bali kulifuata kunyakuliwa. Mungu atawafufua na kisha kuwainua watakatifu, yaani watakatifu wote watakaokuwa wakiishi hapa duniani na wale watakaokuwa wamekwisha lala, na baada ya kuisha kwa unyakuo, basi Mungu atayamimina mapigo ya mabakuli saba na kisha kuuangamiza ulimwengu kikamilifu.
Ikiwa tunataka kufahamu kwa usahihi kwamba ni wakati gani unyakuo utatokea, basi tunachotakiwa ni kuliangalia Neno la Mungu linalopatikana katika Ufunuo 10:7. Ni hakika kwamba siri ya Mungu itakamilika wakati huu, kama alivyowahuburi watumishi wake manabii.
Hapa, nakupatia tena kifungu kingine ili uweze kikufahamu vizuri na kuwa na imani sahihi. Hapa tena Biblia inasema, “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika” (1 Wakorintho 15:51-52). Je, Biblia haisemi wazi kwamba ufufuo wa watakatifu utatokea wakati wa tarumbeta la mwisho? Tarumbeta litakapolia, wafu katika Kristo watafufuliwa bila uharibifu, nasi pia tutabadilishwa kwa haraka na kisha kunyakuliwa.
Malaika anayeonekana katika sura ya 10 ni malaika mkuu aliyetumwa na Mungu, yeye ni tofauti na wale malaika wengine walioyapiga matarumbeta sita ya mwanzo. Tunapomwangalia malaika huyu mkuu akifanya, anaonekana kuwa ni kama Mungu kiasi kuwa tunaweza kufanya koso la kudhani kuwa yeye ni Mungu: “Amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi. Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.”
Kwa maneno mengine, tunaweza kufanya kosa la kudhania kwamba huyu malaika ni Mungu, kwa kuwa malaika huyu mkuu anayetenda mambo yote ambayo Kristo atayafanya. Hii inatueleza kwamba Mungu atayafanya haya mambo haya yote kwa kupitia malaika huyu mkuu. Kifungu hiki kinatueleza kwamba, huyu malaika, hali akiwa ameweka mguu wake mmoja baharini na mwingine katika nchi, atawaangamiza wanadamu, na kwamba wakati ngurumo zitakapotokea malaika huyu atayatimiza yale yote ambayo Mungu ameyapanga katika Yesu Kristo tangu mwanzo wa uumbaji wa ulimwengu na wa mwanadamu.
Kati ya mapigo ya matarumbeta saba, sisi watakatifu tutaishi na kuyapitia mapigo sita ya kwanza, na tutaendelea kuihubiri injili hadi wakati huo. Mungu alimweleza Yohana kukichukua na kukika kitabu kidogo na kisha kutabiri tena, lakini Neno hili limeelekezwa kwako wewe na kwangu—yaani tunapaswa kuendelea katika imani yetu na kuendelea kuishi hadi siku ya mwisho. Kama vile kunyakuliwa kwetu kutakavyokuja kutokea wakati tarumbeta la saba litakapolia, basi tunapaswa kuutambua ukweli huu wa kunyakuliwa kwetu, na kisha tuushikilie ukweli huo katika imani, na kisha kulisikia Neno na kuihubiri injili hadi siku hii ya kunyakuliwa itakapokuja.
Hadi kufikia tarumbeta la saba, Mpinga Kristo ataendelea kufanya kazi kwa nguvu katikati ya mapigo haya, watakatifu watauawa kama wafia-dini, kisha baada ya hapo watanyakuliwa. Kwa hiyo, hata katika wakati huu, wakati ambapo imani ya waamini wengi katika Yesu itakapokuwa imetikiswa hadi katika kina chake na kisha kupoteza uzima wake, hata katika hali wewe na mimi tunapaswa kuishi kwa imani. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuamini kwamba unyakuo wetu utakuja mara baada ya mlio wa tarumbeta la saba, na kwa sababu hiyo tunapaswa kuishi kwa imani.
Muda si mrefu tutayaona mapigo ya matarumbeta saba kwa macho yetu wenyewe. Tutayaona kwa macho yetu na kuyahesabu mapigo haya, kuanzia la kwanza hadi la sita. Baada ya mapigo haya, na wakati ambapo watakatifu watakuwa wakihisi kwamba wakati wa kuifia-dini umewadia, basi ni hakika kwamba tutauawa na kuifia-dini muda huo huo. Hii si hadithi ya kuelezwa na wala si jambo la kubuni la kisayansi. Wala si kitu ambacho una uhuru wa kukiamini au la kutokana na uamuzi wako binafsi. Hiki ndicho kitakachotokea kwako na kwangu.
Ufunuo 10:7, aya inayoonyesha kwa wazi juu ya unyakuo katika Kitabu cha Ufunuo, inatueleza kwamba unyakuo wa watakatifu utakuja kwa mlio wa tarumbeta la saba, nakwamba ulimwengu utaisha kwa mapigo ya mabakuli saba. Baada ya kuwainua watakatifu, Mungu atauleta ulimwengu wote kufikia mwisho wake. Wakati watakatifu wote watakaponyakuliwa, watamsifu Bwana angani. Lakini hapa duniani, mapigo ya mabakuli saba yatamiminwa, na yatauangamiza ulimwengu kikamilifu, na wakati mapigo ya mabaukuli saba yatakapoisha, watakatifu watashuka na katika ulimwengu utakaokuwa umefanywa upya na Bwana. Kisha Ufalme Milenia na Ufalme wa Kristo utajengwa katika dunia hii.
Wakristo wa leo siku hizi wanaunga mkono dhana ya kunyakuliwa kabla ya dhiki na siku hizi baadhi yao wamefikia hatua ya kutetea fundisho la amilenia—yaani kwamba hakuna Ufalme wa Mileni. Je, Ufalme wa Milenia si kitu halisi? Siku hizi kuna watu wengi sana wanaoamini hivyo. Baadhi yao, na wengine ambao wanahudumu katika makanisa makubwa hapa Korea, wamefikia hatua ya kutangaza kwamba kila kitu katika kitabu cha Ufunuo, kuanzia alama 666 hadi unyakuo, si vitu halisi bali ni lugha ya picha. Kama Bwana wetu alivyowahi kuuliza, “mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?” ni hakika kwamba ni vigumu kuwapata waamini wa kweli katika nyakati hizi za mwisho.
Lakini Bwana anatueleza kwamba ni hakika kwamba unyakuo wetu utatokea. Tutakaponyakuliwa, tutakutana na Bwana angani na kisha kumsifu, tutalindwa na kufarijiwa naye, kisha tutarudi pamoja naye hapa duniani. Baada ya kushuka na kuja katika Ufalme wa Milenia, basi tutaishi maisha mapya katika miili yetu iliyofufuliwa na kubadilishwa, hali tukiwa katikati ya kila kitu kilichofanywa upya, yaani toka katika miili iliyobadilishwa hadi katika baraka zilizobadilishwa. Tutaishi katika utukufu wa jinsi hiyo hali tukiwa tumefunikwa na Mungu. Wewe na mimi tunapaswa kuishi kwa imani hii na katika tumaini hili. Na wakati Ufalme wa Milenia utakapokuwa umefikia mwisho tutaingia katika Mbingu na Nchi Mpya, tutatawala pamoja na Kristo katika heshima na utukufu milele.
Tutakapoingia katika Ufalme wa Milenia na Mbinguna Nchi Mpya, malaika wote watakuwa watumishi wetu. Ulimwengu wote ulioumbwa na Mungu na Yesu Kristo, na viumbe vyote vya kiroho, na vitu vyote vilivyomo ndani yake ni mali ya nani? Vitu vyote hivyo vitakuwa ni mali yetu. Hii ndiyo sababu Biblia inasema kwamba wale watakaorithi kila kitu ni watakatifu. Kwa kuwa wewe na mimi tu watakatifu ambao tulizaliwa tena upya kwa injili ya maji na Roho, basi sisi ni warithi wa Mungu na warithi wenza pamoja na Kristo, ambaye vitu vyote vitakuwa mali yake. Kwa hiyo, wewe na mimi ni lazima tuyashinde magumu hapa duniani kwa imani, na kisha tuvumilie hali tukiitazamia siku ya urithi wetu. Pia tunapaswa kuwa na imani inayoshinda tukiwa kama vikosi makini vya Mungu.
Mungu ametueleza kwamba mambo haya yote yatatimizwa hivi punde pasipo kuchelewa. Kwa maneno mengine, mambo haya yatatimizwa hivi karibuni. Wengine wanaweza kushangaa ni kwa nini Mungu hakutueleza kuhusu hili kwa kina. Jibu la swali hili ni kwamba kitendo cha Mungu kuficha matendo ya Mungu ni sehemu ya hekima yake (Mithali 25:2, Luka 10:21).
Kama mpango wa Mungu ungeliandikwa kwa kina, basi maelezo haya yangelisababisha kuwepo kwa wasiwasi mkubwa ulimwenguni. Hivyo watakatifu wasingeliweza kuishi hadi siku ya mwisho. Karibu watakatifu wote watauawa na wasioamini, na hakuna hata mtakatifu mmoja atakayesalia. Ikiwa kila taarifa kuhusu nyakati za mwisho imeandikwa katika Biblia, basi wale ambao hawajazaliwa tena upya kwa maji na kwa Roo watawachinja waamini wote waliozaliwa tena upya. Baada ya kuwa amelificha dhumuni lake, Mungu analifunua dhumuni hilo kwa wale wanaostahili, zaidi ya hapo ni kwamba Mungu anaziweka habari hizo kama fumbo kwa wengine—hii ni hekima ya Mungu. Mungu ameufunua mpango wake kwetu na ameturuhusu kuufahamu mpango huo, hii ni kwa sababu jambo hili ni la muhimu sana kwa watakatifu wa kipindi hiki.
Kule kusema kwamba makanisa ya Mungu yaliyozaliwa tena upya yanazizungumzia nyakati za mwisho kwa kina maana yake ni kwamba siku za mwisho zinatukaribia. Kwa kuwa kipindi cha Dhiki kinakaribia, basi Neno la Ufunuo linahubiriwa ili kwamba watakatifu wawe na ufahamu sahihi wa nyakati za mwisho na ili waweze kuivumilia na kuishinda hii Dhiki. Hata kwa wale waliozaliwa tena upya, ikiwa watakabiliana na Dhiki pasipo kuwa na ufahamu wowote, ukweli ni kwamba hawatafahamu cha kufanya na kwa sababu hiyo watajikuta katika mkanganyiko mkubwa hasa wakati ambapo Dhiki itakuja. Mkanganyiko huu utakuwa mkubwa zaidi kwa wale wanaozitegemea imani zao binafsi.
Tunaweza kudhania kwamba nafsi nyingi ambazo hazijajiandaa, na katikati ya ujinga wao na mkanganyiko, wataanza kwenda katika njia isiyo sahihi katika nyakati za mwisho. “Je, Mungu amekuambia kitu fulani?” “Mungu amekuonyesha maono wakati ulipokuwa unasali?” Watu wengi watapata wasiwasi kiasi cha kutafuta maono toka kwa Mungu, na katika nyakati za wisho, watu wengi sana watadai kwamba wameona maono. “Je, Mungu amekuambia kitu wakati ulipokuwa ukisali?” Basi, ikiwa watakatifu watabaki katika ujinga, basi maswali kama haya yatakuwa ni ya kawaida sana miongoni mwa watakatifu wa nyakati za mwisho.
Lakini Mungu hafanyi kazi kwa namna hiyo, hii ni kwa sababu amekwisha kutuamuru, “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.” Kwa maneno mengine, watakatifu ni lazima wakisikie kile ambacho Roho Mtakatifu anakiongea kupitia makanisa. Kwa kuwa Roho Mtakatifu, analithibitisha Neno la Mungu, na anashuhudia kile ambacho ni cha kweli na sahihi, basi wakati mapigo yatakapokuja katika nyakati za mwisho, sisi watakatifu hatatushangaa kuziona dhiki, bali tutaishi kwa imani—hii ni kwa sababu wakati huo tutakuwa tumeshalisikia Neno la kweli na kulisimika katika mioyo yetu kwa imani.
Hii ndio sababu Yohana alitufunulia mapema kile ambacho kitatokea baadaye, na kwamba ni kwanini watumishi wa Mungu wanauhubiri ukweli ndani ya mipaka ya Neno lililoandikwa. Kutoa unabii si kwingine bali ni kule kufahamu kile ambacho kitatokea toka katika Neno la Mungu lililoandikwa; lakini kitendo cha kudai kuona maono katika ndoto au katika maombi huko si kutoa unabii!
Usisahau kwamwe kwamba kwa hakika kunyakuliwa kwetu kutakuja, na kwmaba sisi ni watakatifu wa Mungu. Pia usisahau kwamba sasa umefanyika kuwa mtakatifu, ambaye utakuwa pamoja na Kristo angani baada ya unyakuo wako kutokea, na ambaye utashuka katika ulimwengu uliofanywa upya na kisha kuishi kwa miaka elfu moja, na ambaye utaishi milele katika Mbingu na Nchi Mpya. Kama utawasikia watu wakizungumzia juu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki au kunyakuliwa baada ya dhiki, au wakidai kwamba hakuna Ufalme wa Milenia kabisa, basi hebu uwaambie ukweli wa kurejea kifungu ambacho tumekuwa tukikitazama hapa. Pia unaweza kurejea 1 Wathesalonike 4 na 1 Wakorintho 15, kisha uwaambie bayana kwamba Bwana atashuka pamoja na sauti ya malaika mkuu na kwa sauti ya tarumbeta la mwisho, kisha atawainua watakatifu angani ili kuwa pamoja nao. Ni mpaka pale utakapouamini unyakuo huu ndipo unapoweza kuilinda imani yako.
Ili kunyakuliwa, ni lazima kuwe na mauaji ya wafia-dini kwa imani na ufufuo wa miili. Kwa kuwa unyakuo utakuja sambamba na ufufuo, basi mara baada ya kufufuliwa, tutanyakuliwa na kuinuliwa angani. Hivyo, unyakuo na ufufuo vitu vinavyofuatana. Kushiriki katika ufufuo wa kwanza maana yake ni kuishi na Bwana katika Ufalme wa Milenia. Kunyakuliwa pia maana yake ni kuishi na Bwana kwa miaka elfu moja katika dunia hii.
Sasa, ni kwa nini tunyakuliwe? Ni kwa sababu Mungu ataangamiza kila kitukatika ulimwengu huu kwa kuyamimina mapigo ya mabakuli saba—yaani, Mungu atawanyakua watakatifu mapema ili kuwakomboa watoto wake toka katika mapigo haya ya kumaliza. Mungu atawanyakua watakatifu ili kuwatenga watakatifu na wenye dhambi, na ili kuonyesha hatma zao ambazo pia ni tofauti. Kwa hiyo, tunapaswa kuyaamini mambo haya yote—yaani kunyakuliwa kwetu, kufufuliwa kwetu, na kuuawa kwetu kama wafia-dini.
Kwa baadhi yao, injili ya maji na Roho imefunuliwa kwa kina, ilhali kwa wengine imebakia kuwa ni siri iliyofichwa. Vivyo hivyo, mauaji ya watakatifu ya kufia-dini, ufufuo, kunyakuliwa, na kutawala kwao katika Ufalme wa Milenia na katika Mbingu na Nchi Mpya, yote hayo ni siri za Mungu. Mungu amewawezesha watakatifu kuishi hadi nyakati za mwisho na kuyashinda magumu yao yote kwa tumaini lao katika kunyakuliwa na katika Ufalme wa Mungu, na kwa sababu hiyo Mungu amewafanya waziamini hizi siri zake.
Wewe na mimi tunapaswa kuwa na aina hii ya imani. Pasipo kuwa na aina hii ya imani—yaani kutoamini kwamba tutanyakuliwa, na kwamba tutaishi katika Mbingu na Nchi Mpya, na kwamba Bwana atatufufua toka kwa wafu baada ya kuwa tumechinjwa na Mpinga Kristo, na kutunyakua, na kuturuhusu kukaa angani, na kisha baadaye kurudi hapa duniani ili kutawala pamoja naye kwa miaka elfu moja—basi pasipo kuamini hivi, ni wazi kwamba hatutaweza kuvumilia magumu na maisha ya dhiki ya kipindi hiki cha mwisho.
Watakatifu wana ndoto nzuri, na hakuna mwingine zaidi ya Bwana wetu anayeweza kuifanya ndoto hii kuwa halisia. Pasipo tumaini hili, tutaishi kwa huzuni na mateso katika ulimwengu huu wa kuhuzunisha.
Paulo alimwambia Timotheo kuvitunza vitu vizuri ambavyo alikuwa amekabidhiwa. Injili hii ni nzuri; vivyo hivyo vifo vyetu vya kufia-dini, ufufuo na unyakuo ni vizuri pia; pia kuishi katika Ufalme wa Milenia na katika Mbingu na Nchi Mpya. Vitu hivyo vyote ni vyema na vizuri. Vitu hivyo ni vya watakatifu, na vitu hivyo ni imani na tumaini linalotambulika, si hisia au mambo ya kudhania. Mambo haya ni tumaini letu katika imani iliyotolewa na Bwana. Tunapaswa kuishi katika kipindi hiki hali tukiitarajia siku ambapo Ufalme wa Mileni na Mbingu na Nchi Mpya zitaletwa kwetu.
Wale watakaonyakuliwa si wengine bali ni wewe na mimi. Tunapaswa kuishi kwa imani, hali tukiisubiri siku ambayo tutanyakuliwa ili kusimama mbele za Bwana na kisha kutawala katika Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya.
Mungu anatueleza kwamba Yeye atakayekuja atakuja hivi punde. Mapigo ambayo yatakuja katika miaka mitatu na nusu katika ya ile miaka saba ya Dhiki Kuu yatakuwa ni madogo na yatakayodumu kwa muda mfupi. Ikiwa mapigo yangeliendelea katika kipindi chote cha miaka saba ya Dhiki Kuu, ingewezekanaje basi kwa yeyote yule kuvumilia? Mapigo ya kwanza ni mafupi, na kadri muda unavyokaribia mwishoni, basi kutakuwa na mengi ya kuyaona. Wakati pigo la tarumbeta la saba litakapokuja, litafikia kiwango cha kustaajabisha.
Wakati Shetani atakapojaribu kuitikisha imani ya watakatifu, atatoa mfano kwa kuwa baadhi ya viongozi wa makanisa. Pengine Shetani ataweza kusema hivi, “Nitauhifadhi uhai wenu ikiwa tu mtamkana Mungu!” Hata kama ulimwengu utageuka na kuwa mzuri, ukweli ni kwamba mtu atafikiria mara mbili juu ya hili ambalo Shetani amelisema. Ni nani basi aliye na akili timamu ambaye anaweza kumkana Bwana wakati anafahamu dhahiri kwamba Bwana atayamimina mapigo ya mabakuli saba, na kwamba atapaswa yeye kuyapitia mateso hayo yote yatakayoletwa na mapigo hayo? Watakatifu wanaofahamu juu ya mwisho wa ulimwengu hawawezi kamwe kumkana Bwana wala kuisaliti imani yao. Pia, kwa kuwa katika mioyo yetu kuna Roho Mtakatifu, basi huyu Roho Mtakatifu atatutia nguvu.
Kwa kuwa mipango yote ya Mungu itatimizwa kwa haraka katika nyakati za mwisho, ukweli ni kwamba hakutakuwa na nafasi ya kujificha. Baada ya mapigo ya muda mfupi kuisha, kutafuatiwa na ufufuo, na baada ya huu ufufuo kutafuatiwa na unyakuo, ambao utatunyakua kwenda angani. Hebu fikiria miili yetu ikibadilishwa kwenda katika miili ya kiroho, huku ikimsifu Bwana. Katika Ufalme wa Mungu, tunaweza kuufurahia ulimwengu mwingine tofauti, ulio mzuri, wa kuvutia, yaani ubora ambao hatujawahi kuuona katika dunia hii. Kwa kuwa miili ya kiroho ipo huru kutokana na ukomo wa muda na nafasi, basi tutaishi katika ulimwengu mzuri na wa ajabu ambapo tutaweza kwenda kokote kule tunapotaka.
Ninamtolea Mungu shukrani zangu za dhati kwa kutupatia baraka baraka hizi kubwa. Ninamshukuru Mungu kwa kutufunulia kwa kina juu ya Dhiki Kuu, juu ya mapigo yake, juu ya kuuawa kwetu na kuifia-dini, na juu ya ufufuo na unyakuo kwa kupitia Neno lake. Pia ninaomba ili kwamba mioyo yetu iweze kuishi wakati wote huku ikikifahamu kipindi hiki cha mwisho na kisha kuamini.