Search

Sermones

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[16-1] Mwanzo wa Mapigo ya Mabakuli Saba (Ufunuo 16:1-21)

(Ufunuo 16:1-21)
“Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi. Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake. Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa. Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu. Nami nikamsikia malaika wa maji akisema: 
‘Wewe u mwenye haki,
Uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu,
Kwa kuwa umehukumu hivi. 
Kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, 
Nawe umewapa damu wainywe. 
Nao wamestahili.’ 
Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, ‘Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.’ 
Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua. Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni. Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa. Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo. Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake. Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena. Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.”
 
 
Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.”
Mungu ataileta hasira yake juu ya watumishi wa Mpinga Kristo na watu wake wataokuwa wakiishi katika dunia hii kwa mapigo ya mabakuli saba ya hasira. Viumbe wote pamoja na watu watafutwa na dhoruba ya ghadhabu ya Mungu, ambayo italipuka baada ya miaka mingi ya uvumilivu, kisha wanadamu watateseka kwa mapigo makuu yatakayomiminwa juu yao katika kipindi kitakachokuwa kimebakia katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu. Wakati huo, ulimwengu huu utafinyangwa na kuwa kama majivu maana utakuwa umevunjwavunjwa katika vipande, na utasahauliwa kabisa. 
Ufunuo 16 ni sura ambapo mapigo ya mabakuli saba yanamiminwa. Wale ambao wakati huo watakuwa bado hawajaifahamu wala kuiamini injili hii ambayo inabeba ushuhuda wa wokovu, ambayo ingeliwawezesha kunyakuliwa angani na Bwana—yaani, injili ya maji na Roho—wataangamizwa wote na mapigo haya. 
 
Aya ya 2: Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake. 
Pigo la jibu baya na bovu ambalo Mungu atalimimina kwa kupitia malaika wake litawashukia wale walioipokea alama ya Mnyama. Pigo hili la jibu ni ugonjwa wa ngozi ambao hauna tiba ambao utatungisha usaha katika ngozi ya aliyeathiriwa, na maambukizi yake yataenea katika sehemu yote ya ngozi. Mateso haya yatakuwa ni makubwa sana, maana waathirika watateswa na pigo hili hadi kifo chao, je, si jambo la kutisha? Lakini, Mungu hatalishusha pigo la jipu tu kwa wale wote walioipokea alama ya Mnyama, bali atayashusha pia mapigo sita mengine yatakayofuata baadaye. Hivyo, watu wote wanapaswa kutafuta njia ya kuepukana na mapigo haya kwa kuipokea injili ya maji na Roho, na kwa kufanya hivyo watayakwepa haya mapigo ya kutisha hasa watakapoiamini injili hii sasa hivi. 
Bwana wetu anasema atayashusha mapigo mengine sita kwa wale wanaomwabudu Mnyama na sanamu yake. Je, ni dhambi gani ambayo Mungu anaichukia zaidi? Dhambi anayoichukia zadi ni kutengeneza sanamu ya kitu fulani au mtu fulani zaidi ya Mungu, na kisha kuichukulia kama Mungu na kuisujudia. Hivyo tunapaswa kufahamu kikamilifu jinsi Bwana Mungu wetu na Yesu Kristo walivyo, na kisha tukamwamini na kumwabudu Kristo Yesu. Hakuna yeyote yule katika ulimwengu huu zaidi ya Bwana Mungu Mwenyewe anayeweza kuwa Mungu wetu. 
Ikiwa unataka kulikwepa pigo la jibu na mapigo mengine sita ya nyongeza, basi jifunze na uamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Idadi kubwa ya watu ambao wamesimama kinyume na Mungu katika maisha yao ya kila siku, na waliokataa kuiamini injili ya maji na Roho watateseka kwa mapigo haya hadi watakapokuwa wameangamizwa kabisa.
 
Aya ya 3: Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa. 
Pigo la pili ni wakati ambapo bahari itageuka na kuwa kama damu ya mfu. Mungu ataviua viumbe vyote baharini kwa pigo hili. Kutokana na pigo hili pili litakalokuwa limemiminwa na Mungu, bahari itaoza na viumbe vyake vyote havitaweza kuishi ndani yake. Mungu atakapolileta pigo hili lapili hakutakuwa na mtu atakayeweza kula mazao ya baharini. Kwa kupitia pigo la pili, Mungu atajidhihirisha kwamba yupo hai, na kwamba yeye ni Bwana juu ya uhai wote. 
Pigo hili la pili ni hukumu ya Mungu ambayo itakuwa imeshushwa kwa watu wote wa ulimwengu huu, ambao badala ya kumwabudu Bwana Mungu kwa ajili ya uumbaji wake, watakuwa wakiisujudia sanamu ya Mnyama, ambayo ni adui wa Mungu, na ambao wataimwaga damu ya watakatifu. Pigo hili la pili ni miongoni mwa mapigo sahihi na ya haki. Mungu anatueleza kuwa atauchukulia mbali utajiri wa asili kwa wale wote ambao hawamshukuru Bwana kwa viumbe vyote vilivyoumbwa na Mungu. 
 
Aya ya 4-7: “Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu. Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi. Kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe. Nao wamestahili. Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.” 
Pigo la tatu ambalo litaigeuza mito na vyanzo vya maji kuwa damu kwa kweli ni moja kati ya mapigo ya kutisha sana. Pigo hili, linalokuja kama adhabu kwa wale wote wasiomwamini Mungu, litazibadili chemichemi na kuzifanya kuwa damu na kisha litawafanya wanadamu hao washindwe kuishi hapa duniani. Mungu atazigeuza chemichemi na mito yote katika dunia hii kuwa damu. Pigo hili pia ni hukumu iliyowekwa kwa ajili ya watu wa ulimwengu kama mshahara na adhabu yao kwa kusimama kinyume na Mungu, ambaye aliwapatia maji, ambayo ni mzizi na msingi wa uhai wote. 
Sababu itakayomfanya Mungu kuleta pigo hili juu ya wale waliosimama kinyume Naye ni kwa sababu waliwaua watakatifu wake na manabii walipokuwa hapa duniani. Hao ndio wale ambao sio tu walikataa kumwamini Mungu kuwa ni Mungu, bali pia ndio waliosimama kinyume na Mungu hali wakiungana na Mpinga Kristo. 
Hali wakiwa wamegubikwa na nguvu za Mpinga Kristo, wale wanaosimama kinyume na upendo wa Mungu katika ulimwengu huu watawatesa na kuwaua watakatifu na watumishi wanaopendwa na Mungu. Wale wasioiamini sasa injili ya maji na Roho, ambayo Bwana wetu ameitoa ili kuwakomboa watu wa ulimwengu huu toka katika dhambi, watawaua watakatifu wengi na manabii wa nyakati za mwisho na kuimwaga damu yao. Hivyo, Mungu atalimimina pigo lake la tatu juu ya ulimwengu huu ambao maadui zake watakuwa wanaishi, na kwa pigo hilo atayageuza maji, ambayo ni mzizi na msingi wa uhai wote, kuwa damu na kwa sababu hiyo atawaangamiza. 
Hii ni hukumu ya Mungu ya haki, na watakatifu wakiwa angani wataifurahia hukumu hii? Kwa nini? Kwa sababu Mungu atalipiza kisasi cha vifo vya watakatifu kwa kuileta hukumu yake ya haki kwa maadui ambao waliwaua watakatifu. Hivyo, watakatifu na watumishi wa Mungu hawapaswi kuogopa, bali wanapaswa kuilinda imani yao katika Bwana Mungu, na kisha waiangalie ahadi ya Mungu na mamlaka yake wakati wanapokabiliana na mauaji ya kuifia-dini. 
 
Aya ya 8-9: Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. 
Wakati malaika wa nne alipolimimina bakuli la pigo la nne katika jua, watu wataunguzwa maunguzo makuu hadi kifo kwa sababu ya joto kali. Mungu atalileta pigo la jua linalochoma kwa wale waliosimama kinyume naye. Dunia hii inalizunguka jua kwa usahihi, lakini ikiwa dunia ingelikwepa na kutoka katika njia yake na kusogea hata kama ni kwa umbali mdogo tu kuelekea liliko jua, basi ni hakika kuwa wakazi wake wote wangeliunguzwa na kufa. Hivyo, wakati pigo hili la nne litakapokuwa limemiminwa, watu wote watakaokuwa wakiishi katika dunia hii watateseka sana kwa kuungua. 
Hata hivyo, bado wanadamu hawataitubia dhambi yao ya kusimama kinyume na Mungu. Kwa nini? Kwa sababu kwa kusimama kinyume na injili ya maji na Roho, basi wanakuwa wamekwishapangiwa kuangukia katika uharibifu. Hivyo, kila mtu ni lazima aiandae imani yake ambayo itamwezesha kuikwepa hasira ya Mungu. Na imani hiyo ni ile ya kuamini katika injili ya maji na Roho kuwa ni wokovu wa mtu. Hivyo, kila mtu ni lazima auamini ukweli wa maji na Roho. 
 
Aya ya 10-11: Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. 
Pigo la bakuli la tano ni lile ambalo litaleta giza na maumivu. Mungu atalimimina bakuli hili la pigo la tano juu ya kiti cha enzi cha Mpinga Kristo na kisha kulileta pigo la giza na maumivu. Kutokana na pigo hili, watu watazitafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu na kuteseka. Mungu atahakikisha alipiza kisasi cha mateso ya watakatifu juu ya wanadamu kwa maumivu makubwa mara mbili zaidi. 
Kwa maneno mengine, Mungu atawafanya wateseke, zaidi ya vile walivyowafanya wakatifu kuteseka. Lakini bado watamkufu Mungu na kutotubu, hata pale watakapokuwa wakiteseka kutokana na majibu yao. Hivyo, kwa sababu hiyo watapokea adhabu ya milele ya kuzimu kwa kuunguzwa na moto na kibiriti. 
 
Aya ya 12: Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua. 
Pigo la bakuli la sita litakalomiminwa na Mungu ni pigo la njaa ambalo litaufanya Mto Frati kukauka. Wanadamu watakabiliana na mateso makuu kutokana na pigo hili. Pigo la njaa ni pigo linalotisha zaidi kwa maisha ya kila mtu. Pigo hili ambalo litamiminwa juu ya wale wote ambao watakuwa wameikataa injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana linaonyesha jinsi adhabu itakavyokuwa kubwa kwa wale wote walioukataa upendo wa Mungu na kusimama kinyume naye. Baadaye, jeshi la Mungu la Mbinguni na jeshi la Shetani la hapa duniani yatapigana katika uwanja huu wa vita. Shetani na wafuasi wake watazimishwa na kuangamizwa na Mungu. 
 
Aya ya 13: Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. 
Aya hii inatuonyesha kuwa kazi za roho zote chafu na mapepo zinatoka katika kinywa cha Shetani, Mnyama wa Shetani, na kutoka katika manabii wa uongo. Kazi za mashetani zitaendelea kuwepo katika ulimwengu hadi mwisho wa ulimwengu utakapokaribia. Mashetani watawadanganya watu na kuwaongoza kuelekea katika maangamizi kwa kufanya miujiza na ishara kupitia Shetani, manabii wa uongo, na kwa kupitia Mpinga Kristo. Hivyo, ulimwengu wa nyakati za mwisho utakuwa ni ulimwengu wa mapepo. Lakini ulimwengu huo utafikishwa mwisho kwa mapigo ya mabakuli saba yatakayomiminwa na Yesu Kristo pamoja na ujio wake mara ya pili. 
 
Aya ya 14: Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. 
Roho za mashetani zitaivutia mioyo ya wafalme wa ulimwengu mzima kukusanyika mahali pamoja ili kupigana na Mungu. Katika ulimwengu wa nyakati za mwisho, moyo wa kila mtu utatawaliwa na roho za mashetani, na hivyo mtu mke na mtu mme watageuzwa na kuw watumishi wa Shetani huku wakizifanya kazi za Ibilisi. 
 
Aya ya 15: “Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.”
Bwana atakuja katika ulimwengu huu kama vile mwizi, na kwa sababu hiyo wamebarikiwa sana wale wanaoilinda imani yao na kuihubiri injili hadi mapigo ya mabakuli saba yatakapomiminwa. Bwana wetu anawaeleza watakatifu watakaokuwa wakiishi katika nyakati za mwisho za ulimwengu kwamba wanapaswa kuishi kwa imani yao katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu na kwamba wanapaswa kuilinda imani hii hadi siku ya mwisho. Wale wanaoilinda imani yao katika Bwana kabla ya kumiminwa kwa mapigo ya mabakuli saba watapokea thawabu kubwa toka kwa Mungu. Ni hakika kuwa Bwana wetu atakuja tena ili kuwachukua wale ambao atawapatia baraka zake. 
 
Aya ya 16: Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni. 
Biblia inatabiri kwamba vita ya mwisho kati ya Shetani na Mungu itapiganwa mahali panapoitwa Har-Magedoni. Lakini kwa kuwa Mungu ni Mungu Mwenyezi, atamshinda Shetani na kisha kumtupa yule Mnyama katika ziwa la moto na kibiriti. Ni lazima tutambue kwamba Shetani ni mdanganyifu wakati wote, na kwa sababu hiyo ni lazima tuilinde imani yetu katika bwana kwa uimara wote hadi siku tutakayosimama mbele za Mungu. 
 
Aya ya 17-21: Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa. Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo. Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake. Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena. Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.
Wakati Mungu atakapolimimina pigo la bakuli la saba angani, ngurumo na umeme vitatawala angani, wakati huo pia tetemeko kuu litatokea, tetemeko ambalo halijawahi kutokea hapo kabla na litaipiga dunia. Ulimwengu wa kwanza utatoweka kwa sababu ya machafuko haya na mahali pake hapataonekana tena. Baada ya pigo hili, watakatifu wataishi katika utukufu pamoja na Yesu Kristo katika ulimwengu utakaokuwa umefanywa upya kwa miaka elfu moja itakayofuata. 
Baada ya miaka elfu moja kupita na wakati wa kuitimiza ahadi ya Mungu ya Mbingu na Nchi Mpya kwa watakatifu itakapowadia, Mungu ataufanya ulimwengu wa kwanza kutoweka kisha atawapatia watakatifu Mbingu na Nchi ya pili. Kisha watakatifu watatawala pamoja na Mungu katika Mbingu na Nchi mpya milele. Watakatifu ni lazima waamini kwamba wataishi katika Ufalme wa Kristo kwa miaka elfu moja na kwamba wataishi milele katika utukufu katika Mbingu na Nchi mpya. Watakatifu ni lazima waishi katika tumaini hili, hali wakisubiria kuja kwa Bwana.