Search

Sermones

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[16-2] Unachopaswa Kukifanya Kabla ya Kumiminwa Kwa Mabakuli Saba Ni… (Ufunuo 16:1-21)

(Ufunuo 16:1-21)
 
Kati ya mapigo ya mabakuli saba, pigo la kwanza ni lile la majipu, pigo la pili ni lile la bahari kugeuka na kuwa damu, na pigo la tatu ni lile la maji ya mito na chemichemi kugeuka na kuwa damu. Na pigo la nne, ni lile ambalo watu wataunguzwa hadi kufa kutokana na joto la jua. 
Kifungu kikuu kinatueleza kwamba, “Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa.” Hii inatuonyesha kwamba Mungu atalisogeza jua karibu na dunia na kisha kuviunguza viumbe hai hadi kifo. Wakati Mungu anaporuhusu hili kutokea, hakuna hata mmoja atakayeweza kulikwepa joto la jua lenye kuunguza, hata kama mtu angelichimba pango chini ya ardhi ya kujificha huko. Hata kuviwasha viyoyozi vitakavyokuwa vimewekwa tayari kwa ajili ya pigo hili havitaweza kulizuia pigo hili la Mungu. Watu wote hawatakuwa na la kufanya zaidi ya kufa. 
Bila shaka tunaweza kufikira jinsi hali hii itakavyotokea hasa wakati pigo hili litakapowadia—ngozi zao zitachubuka; nyama ya miili yao ya ndani itaunguzwa na kuwa nyekundu, na kisha kuoza. Hivyo, kila mtu atakufa kutokana na kansa ya ngozi. 
Hata hivyo, pamoja na kuunguzwa hadi kifo kutokana na joto kali la jua, watu hawatazitubia dhambi zao. Pigo hili la Mungu ni la kushangaza sana, lakini hata hawa watu wanaokataa kutubu pamoja na kuwa katika pigo hili ni kuwashangaza pia. Kadri watakavyozidi kukataa kutubu, ndivyo mapigo ya Mungu yatakavyoendelea. 
Kifungu kikuu kinasema, “Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao.” Tunapouangalia ulimwengu wa leo, hatuwaoni watu wengi ambao wangelipaswa kuhukumiwa na Mungu sasa hivi? Lakini kwa kuwa Mungu anaizuia hasira yake huku akisubiria, ndio maana Mungu bado hawajahukumu. Hata hivyo, ikiwa watakufa hali wakiwa hawaiamini injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu Kristo, Mungu atawafanya kuwa hai katika miili isiyokufa, na kisha watakabiliana na moto wa milele wa kuzimu. 
Jambo hili litakapotokea, watu watataka kufa, hii ni kwa sababu mateso yao yatakuwa ni makubwa sana na watashindwa kuyavumilia. Lakini mateso ya kuzimu yatakuwa ni ya milele. Utafika wakati ambapo wale waliohukumiwa na Mungu watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia, kwa kuwa Mungu atawazuia ili wasife ili aweze kuwahukumu milele. 
Pigo la sita ni la vita ya Har-magedoni. Na pigo la saba ni la mwisho na la tetemeko kuu na mvua kubwa ya mawe. 
Aya ya 17-21 inatueleza kwamba, “Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa. Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo. Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake. Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena. Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.” 
Kifungu hicho hapo juu kinatueleza kwamba Mungu atakapomimina bakuli la saba, tetemeko kuu litaipiga sayari, ulimwengu wote utagawanyika vipande vitabu, na majengo yote yatakayokuwa bado yanasalia katika ulimwengu huu yataangushwa chini, hakuna hata jengo moja litakalosalia. Kwa kuwa ulimwengu huu umewekwa chini ya ghadhabu ya Mungu ya kutisha, basi visiwa vyote na milima vitatoweka. 
Je, Milima ya Himalaya itabakia wakati jambo hili likitokea? Kwa kweli hapana! Milima yote mirefu itatoweka mbele ya macho ya yeye aliye hai. Kimsingi, kila mlima katika ulimwengu huu utatoweka na mahali pake hapataonekana. Kifungu hiki kinatueleza pia kwamba mvua kubwa ya mawe, huku kila jiwe la mvua hiyo likiwa na uzito wa paundi 100 (sawa na kilo 45) yataanguka katika dunia hii. Je, kutakuwa na mtu yeyote atakayesalimika kutokana na matetemeko haya ya ardhi na mvua kubwa za mawe? 
Ufunuo 18 inatueleza kwamba ghadhabu ya Mungu inaletwa juu ya wale ambao hawakumwamini Mungu na ambao walilidharau Neno lake. Baadhi ya watu katika ulimwengu huu wanadai, kana kwamba walikuwa ni kimungu huku wakisema, “sintaangukia katika ghadhabu ya Mungu, wala sintahukumiwa na Mungu.” Hata hivyo, hukumu ya Mungu inaletwa kwa watu kama hawa ambao wamejaa majivuno na kiburi. Ni lazima tuamini kwamba ulimwengu huu utatoweka utakapokuwa umepigwa na mapigo haya ya mabakuli saba yatakayomiminwa na Mungu. 
 

Ni Lazima Tuwe na Imani Katika Neno la Mungu
 
Mungu anatueleza kwamba ataufanya ulimwengu huu kupotea. Hivyo, ulimwengu huu hautadumu milele. Hivyo, wale wote wanaoukabili mwisho wa ulimwengu huu wanapaswa kuiamini katika ukweli huu na kuushikilia kwa imani yao ya kiroho. Hivyo, watu wote wa ulimwnegu huu ni lazimwa waamshwe toka katika usingizi wao wa kiroho. Sijui umekuwa ukiishi maisha yako ya kiimani kwa imani ipi hadi sasa, lakini sasa ni wakati wako kuzingatia yale ambayo yatatokea katika nyakati za mwisho, na kisha kuamka na kuamini. Unapaswa kuwa na ufahamu sahihi juu ya mapigo yaliyotabiriwa katika Ufunuo, na unapaswa kuwa macho. 
Bwana wetu ametuambia kwamba muda si mrefu dunia hii itakuwa chini ya mapigo ya mabakuli saba ya Mungu. Kwa hiyo, ni lazima tumsubiri Bwana hali tukiendelea kuihubiri injili, hata kama watu hawaipokei vizuri. 
Hatma ya ulimwengu huu sasa imekaribia na kuwa tete. Ulimwengu wa leo upo katika kila aina ya hatari, kuanzia vita hadi hali mbaya ya hewa, uharibifu wa mazingira, kuzidi kwa migongano ya kijamii, na kila aina ya magonjwa. Hivyo, Mungu anatueleza kwamba wakati wa sasa ni kama wakati ule wa Nuhu. Ikiwa wakati wa sasa ni kama ule wa wakati wa Nuhu, basi hii ina maanisha kwamba ulimwengu huu umeingia katika siku zake za mwisho. Ishara ya nyakati za mwisho ni kwamba watu watapendelea zaidi vitu vya kimwili, kama vile kula, kunywa, kuoa, na mambo mengine kama hayo. Hivyo wamestahili kuhukumiwa na Mungu. Wakati wa Nuhu, watu wa jinsi hiyo hawakusikia kile ambacho Nuhu aliwaambia, hivyo waliangamizwa wote, isipokuwa kwa Nuhu na familia yake ya watu nane. Ulimwengu unaokuja utakuwa vivyo hivyo. 
Karibu vitu vyote ambavyo Mungu ameviahidi vimeshatimia kama vilivyoandikwa katika Biblia. Kati ya mambo hayo, ni takribani asilimia 5 ndio bado haijatimia, lakini asilimia nyingine yote imekwisha timia. Neno la wokovu na ukombozi pia limetimizwa. Katika Neno la Mungu, kilichobakia ni hukumu kwa wale wasioiamini injili ya maji na Roho. Na kwa wale waliozaliwa tena upya, Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya, mahali ambapo wenye haki wataingia na kuishi vinawangojea. 
Mungu ni mwenye rehema, anasimama upande wa wenye haki. Hata hivyo, kwa wale ambao wanastahili ghadhabu ya Mungu, ni hakika kwamba Mungu ataishusha ghadhabu yake juu yao, na kwa wale wanaostahili rehema yake, Mungu atawashushia rehema. 
Pigo hili litatokea lini? Pigo la bakuli la saba litakuja baada ya mauaji ya watakatifu ya kufia-dini, wakati ambapo alama ya 666 itakapokuwa imewekwa katika ulimwengu huu na kisha kupingwa na watakatifu. Baada ya mapigo haya, ufufuo wa kwanza, Ufalme wa Milenia, na hukumu ya mwisho Yesu akiwa ameketi katika kiti cha enzi vitakuja. Hii itafuatiwa na kufunguliwa kwa Ufalme wa Mbinguni wa milele. Tunapaswa kuupata ufahamu wa majaliwa ya Mungu kupitia Biblia. 
Je, unauamini ukweli kwamba Yesu alifufuka tena toka kwa wafu? Je, unaamini kwamba Bwana amezifanya dhambi zote za mwanadamu kutoweka kwa kupitia ubatizo wake na damu yake? Bwana wetu alizichukua dhambi zote za mwanadamu kwa maji na damu yake, akafufuka tena toka kwa wafu baada ya siku tatu, na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Hivyo, dhambi za wale wanaoamini katika Yesu Kristo zimetoweka kikamilifu, na kama vile Kristo alivyofufuka tena toka kwa wafu, vivyo hivyo na wao watafufuliwa. 
Hivyo, watakatifu watatukuzwa pamoja na Bwana, lakini wakati wakiwa hapa duniani, watakabiliana na mateso mengi kwa ajili ya Bwana. Lakini mateso ya wakati huu wasasa hayawezi kulinganishwa na utukufu unaowangojea, kwa kuwa utukufu wa Mungu ndio kitu pekee kinachowangojea watakatifu waliozaliwa tena upya. Hivyo, watakatifu hawapaswi kuhofia kuhusu hatma yao ya baadaye. Kile ambacho wenye haki wanapaswa kukifanya ni kuishi maisha yao yote kwa ajili ya injili na kwa imani yao. Ni lazima tujitoe katika kazi ya kuziokoa nafsi, na si kuufuata ulimwengu. 
 

Hebu Tuyatoe Maisha Yetu Yaliyosalia Kwa Mungu 
 
Ninahofia kwamba anaweza kuwepo miongoni mwetu mtu ambaye ataikana injili. Yeyote anayeikana injili ya maji na Roho atakuwa amemkana Bwana Mwenyewe. Pamoja na kuwa sisi ni dhaifu, ikiwa tunaiamini na kuifuata injili ya maji na Roho iliyotimizwa na Bwana, basi hapo sisi sote tunaweza kuishi kwa imani. Watakatifu hawawezi kuishi kwa kuitegemea hekima yao na nguvu binafsi. Ikiwa watafanya hivyo, wataishia kuikana imani yao na kukabiliana na maangamizi yao. Hivyo, ili kukwepa hali hiyo, tunapaswa kuishi kwa imani. 
Kwa nini Bwana wetu atawaruhusu wanadamu kuipokea alama ya 666? Hii ni kwa lengo la kutenganisha nafaka na makapi. Kabla ya kuruhusu watakatifu kunyakuliwa, basi kitu ambacho Mungu atakifanya itakuwa ni kutenganisha nafaka na makapi. 
Zipo vita za kiroho ambazo watakatifu wanapaswa kupigana nazo. Kwa hiyo, watakatifu hawapaswi kuogopa kupigana dhidi ya maadui ya Mungu. Ikiwa watasita kupigana dhidi ya Shetani, basi wategemee kupigwa kumbo na Shetani. Hivyo, watakatifu wote ni lazima wapigane vita ya kiroho kwa ajili yao. Vita vyote vya kiroho vinavyopiganwa na watakatifu ni halali. Ili kumfuata Mungu, kila mtakatifu ni lazima apigane na kumshinda Shetani na watumishi wake. 
Watakatifu ni lazima wapigane kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Pia ni lazima wateswe kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, na kisha kuchukiwa na watu wa ulimwengu. Kule kusema kwamba watakatifu wanapewa fursa ya kupigana kwa ajili ya Bwana ni jambo zuri sana. Ikiwa ungelipewa fursa hii ya kupigana kwa ajili ya Mungu, basi ni hakika kwamba ungelipaswa kumshukuru Mungu kwa ajili ya fursa hiyo. Vita ya jinsi hiyo ni vita nzuri, kwa kuwa ni vita kwa ajili ya haki ya Mungu. 
Mungu anawasaidia wenye haki. Hakuna siku nyingi zilizosalia katika maisha yetu, ni tumaini langu na ombi langu kwamba sisi sote tuishi maisha yetu yote yaliyosalia tukipigana vita vya kiroho na kuzifanya kazi za kiroho hadi tutakapo simama mbele za Bwana. Haijalishi watu wa ulimwengu huu watasema nini kwetu, tunapaswa kupigana vita vya kiroho, kuzaa matunda ya kiroho, na kisha kuyatoa matunda haya mbele ya Bwana wetu. Wakati siku ya kurudi kwa Bwana wetu itakapowadia, hebu tuweze kusimama mbele yake kwa ujasiri. Wakati siku hii itakapowadia, Bwana atayafuta machozi yetu yote na atatuweka mahali ambapo hatutalia tena, mahali ambapo hatutaona maumivu tena, na wala hatutaiona dhambi tena. 
Hebu sisi sote tuishi kwa imani, na kisha sisi sote tuingie katika Ufalme wa Mungu kwa imani hii.