Search

Sermons

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[4-2] Yesu ni Mungu (Ufunuo 4:1-11)

(Ufunuo 4:1-11)
 
Kwa kupitia Neno la Ufunuo sura ya 4 tunaweza kuona jinsi Yesu alivyo Mungu wetu, na kwa ufahamu huu imani yetu inaimarishwa. Wakati ufahamu uliopatikana kwa kupitia Neno unapobadilika na kuwa imani na kupandwa katika mioyo yetu, basi ni hakika kuwa tunaweza kupigana na kumshinda Shetani kwa imani yenye nguvu katika Bwana wakati Yesu atakapokuwa karibu kuja na wakati ambapo Mpinga Kristo atakuwa anainuka ili kututisha.
Kwa sasa tunaitunza imani yetu ili kwamba tuweze kujiandaa kwa majaribu yanayokuja ya miaka mitatu na nusu ya kwanza ya ile Dhiki Kuu. Ikiwa tutaifikia siku hiyo pasipo matunzo haya, basi ni hakika kuwa tutaipoteza imani yetu. Lakini ikiwa tutaiandaa imani imara, basi tunaweza kutangaza kwa ujasiri hata kama kifo kinatukaribia kuwa aliyetuokoa sisi ni Mungu, na kwamba sisi ni wana wa Mungu Mwenyezi ambaye ni mkuu zaidi kuliko Shetani ambaye hawezi kulingana na Mungu kwa lolote.
Lakini ili kufanya hivyo, ni lazima tuamini kwanza kwa kina katika mioyo yetu kuwa Bwana ni Mungu Mwenyezi na kwamba sisi tu wana wake. Je, Bwana wetu ambaye ni sawa na Mungu Baba alijishushaje alipokuja hapa duniani ili kutuokoa toka katika dhambi zetu zote? Bwana alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, katika mfano wa mtumishi, aliyekuwa chini kuliko hata sisi, ambao ni uumbaji wake. Je, kungelitokea nini ikiwa Bwana asingelikuja kwa unyenyekevu kama huo na badala yake akaja na nguvu na mamlaka sawa na watawala wa ulimwengu? Ni kawaida kwa wenye mamlaka kufanya urafiki na wenye nguvu wenzao na kisha kuzipeleka au kuzionyesha nguvu zao kwa watu wa chini, wenye mawaa, na wanyonge. Lakini Bwana alikuja hapa duniani katika hali ya chini na unyonge kuliko sisi, kisha akafanya urafiki na watu wa chini na wanyonge, na amewafanya kuwa watu wake kwa kuwakomboa toka katika dhambi zao.
Hii ndiyo sababu kuwa Mungu ni Mchungaji Mwema na Bwana mwenye rehema. Na hii ndiyo sababu kuwa hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kutoa sifa kwa huyu Mchungaji Mwema wenye rehema kwa ule utukufu wake wa kutufanya sisi kuwa watoto wake. Hivyo tunamsifu Bwana kwa mioyo yetu kwa neema na baraka zake tukiwa hapa duniani, na tutaendelea kumsifu Mungu kwa nguvu na utukufu wake tutakapoingia katika Ufalme wake. Kuungana pamoja katika kumsifu Bwana kwa sauti zetu ni baraka kubwa, kwa kuwa ni wale tu wanaoamini katika injili ya maji na Roho ndio wanaoweza kumsifu Bwana. Tumepewa baraka hii kubwa ambayo inatolewa kwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho tu. Hatupaswi kusahau kamwe kuwa tumefanyika kuwa watu wa Mungu mkuu na watumishi wake.
Baadhi ya watu wanasema kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, na kwamba yeye mwenyewe si Mungu. Lakini kama wanadamu wanavyozaa wanadamu na mnyama anavyozaa mnyama, basi ukweli utabaki kuwa Mwana wa Mungu ni Mungu. Kama wanadamu wasivyoweza kuzaa mbwa, basi Mwana wa Mungu Mwenyezi hawezi kuwa mwanadamu, yaani kuwa kama kiumbe wa Mungu. Wale wasiotambua kuwa Yesu ni Mungu ndio wale wasiofahamu kuwa ndiye aliyetuokoa kwa maji na Roho yake.
Ni lazima tuamini kuwa Yesu ni Mungu (Yohana 1:1). Wakati Mungu Baba alipokiandaa kiti cha enzi kwa ajili ya Yesu Kristo na kuzipitisha nguvu zake kwenda kwa Yesu, basi Yesu—aliyekuwako, aliyepo, na atakayekuja katika siku ya hukumu, na atakayekuwako milele—aliketi katika kiti chake cha enzi akiwa na nguvu za Mungu ili kutawala juu ya wote, akiwa na uweza wa Mungu wa uumbaji, wa wokovu, na hukumu. Kwa kuwa tumefanyika kuwa watu wake kwa kumwamini Bwana, basi ni hakika kuwa tutaingia katika Ufalme wa Mungu na kuishi milele. Huyu Yesu tunayemwamini ndiye Mungu, pia sisi ndio tuliofanyika kuwa watoto wa Mungu kwa kupokea wokovu toka kwake.
Watakatifu, wafanyakazi, na watumishi wa Mungu, ambao wamezaliwa tena upya wanapaswa kujivunia wokovu. Ingawa tuna mali chache katika ulimwengu huu, ukweli ni kuwa tunapaswa kujivunia mfalme wetu tukiwa kama watoto wa Mungu ambao tutatawala juu ya ulimwengu mzima. Ninamshukuru Mungu mwenyezi kwa kutukomboa toka katika dhambi za ulimwengu na kwa kutufanya sisi kuwa watoto wake!
Sifa ambazo wale wazee 24 wa Mbinguni walizitoa kwa Mungu ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu ameyafanya hapa duniani. Sifa walizozitoa zilikuwa zinasema kuwa Mungu alistahili kupokea utukufu wote, heshima, na nguvu, kwa kuwa vitu vyote viliumbwa na yeye Mungu na vipo kwa ridhaa ya mapenzi yake.
Tunachopaswa kukitambua hapa ni kuwa yeye aketiye katika kiti cha enzi ni Yesu Kristo, na kwamba yeye ndiye Mungu. Huyu Yesu Kristo tunayemwamini ndiye Mungu halisi aliyetuokoa. Katika Ufalme wa Mbinguni, mamlaka yote yapo kwa Yesu Kristo Mungu wetu. Pia hukumu ya mwisho itatolewa na Yesu Kristo Mungu Mwokozi wetu. Wakati Kristo atakapotuhukumu toka katika kiti chake cha enzi, basi wale ambao majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima wataingia katika Mbingu na Nchi Mpya, na wale ambao majina yao hayataonekana katika Kitabu hicho cha uzima watatupwa katika ziwa la moto.
Kwa hiyo, kutomwamini Yesu ni sawa na kutomwamini Mungu, na kutomwamini Mungu ni sawa na kusimama kinyume na Mungu. Hii ndiyo sababu wale wasioamini kuwa Yesu ni Mungu, na kwamba ndiye Mwokozi wetu, na kwamba ndiye Mfalme wa Mbinguni, watakutana na hukumu ya kutisha mbele za Mungu.
Miongoni mwa wale wanaomwamini Mungu kuna hili kundi linaloitwa Mashahidi ya Yehova, ambao wanaamini kimakosa kuwa pamoja na kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu yeye si Mungu mwenyewe. Lakini kama Yesu asingelikuwa Mungu, basi asingeliweza kutuokoa toka katika dhambi zetu, kwa kuwa anayeweza kutupatia wokovu mkamilifu ni lazima yeye mwenyewe awe mkamilifu.
Sisi ni wadhaifu sana kiasi kuwa mioyo yetu inabadilika kwa urahisi kutokana na hali inavyobadilika. Pamoja na mapungufu yetu, sababu inayotufanya tumsifu Yesu Kristo Mungu wetu milele ni kwa sababu huyu Yesu, anayeishi milele na ambaye ni mkamilifu milele, amefanyika kuwa Mwokozi wa wenye dhambi. Ni wale tu waliookolewa kwa kupitia Yesu Kristo, ambaye ni Mungu mkamilifu aliyezifanya dhambi zote kutoweka, ndio wanaoweza kumsifu Bwana. Imani yetu katika Yesu Kristo, katika akili na mawazo yetu haipaswi kuwa kama ile ya dini za kidunia. Tunapomfahamu na kumfikiria Yesu kuwa ni Mungu huku imani yetu kwake ikiwa sahihi, basi ni wazi kuwa tunaweza kuupata uzoefu wa Mungu halisi.
Ni lazima tuishi katika imani yetu inayoamini katika Yesu Kristo kuwa ni Mungu Mwokozi wetu, na kwa imani hii tunaweza kupambana na kuwashinda adui zetu. Kwa maneno mengine, tunapomwamini Yesu Mungu wetu, basi imani hii itamfanya Shetani kutetemeka kwa hofu na hivyo kutuwezesha kusimama imara na kuyashinda majaribu na mateso ya nyakati za mwisho. Kwa upande mwingine, ikiwa hatumwamini Yesu kuwa ni Mungu wetu, basi Shetani atatucheka na kututenga toka katika imani yetu.
Baada ya kuwa amekipokea kiti chake cha enzi toka kwa Mungu Baba, Yesu ameketi katika kiti hiki cha enzi kama Mungu wetu. Kwa kupitia Neno la Ufunuo tunatambua kuwa Yesu ni Mungu Mwenyezi anayetawala juu ya vitu vyote katika ulimwengu mzima kwa kuwa amepokea mamlaka yote na nguvu za Mungu toka kwa Baba.
Imani yako katika ukweli huu itakuwezesha kumshinda Shetani kwa nguvu. Kwa kuwa nyuma yetu tuna nguvu za Mungu zisizo na ukomo kama watoto wa Mungu, basi hakuna anayeweza kututisha, na kwa sababu hiyo sisi sote tunaweza kuzishinda nyakati za mwisho kwa ujasiri na bila kutikisika. Ninamshukuru na kumsifu Mungu kwa kila kitu alichokifanya kwa ajili yetu!