Search

Sermoni

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[11-1] Mizeituni Miwili na Manabii Wawili ni Akina Nani? (Ufunuo 11:1-19)

 (Ufunuo 11:1-19)
“Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo. Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili. Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia. Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa. Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo. Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa. Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini. Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama. Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliosalia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu. Ole wa pili umekwisha pita, tazama ole wa tatu unakuja upesi. Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu, wakisema: 
‘Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, 
Uliyeko na uliyekuwako, 
Kwa sababu umeutwa uweza wako ulio mkuu na kumiliki. 
Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, 
Na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, 
Na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, 
Na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, 
Na kuwaharibu hao waiharibuo nchi.’ 
Kisha Hekalu la Mungu liliko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana.”
 

Neno la Ufunuo 11 ni la muhimu sana kwetu, ni muhimu kama lilivyo Neno lote la Mungu. Ili Mungu aweze kuuangamiza ulimwengu, basi kuna kazi moja ya muhimu sana ambayo anapaswa kuifanya mapema. Na hii ni kuwavuna watu wa Israeli kwa ajili ya nyakati za mwisho. Pia Mungu anayo kazi nyingine ya kuifanya kwa Waisraeli na Wamataifa, na kazi hii ni kuwafanya washiriki katika ufufuo wa kwanza na unyakuo kwa kuwaruhusu wauawe na kuwa wafia-dini. 
Kama Biblia inavyotoa maelezo ya jumla kuhusu mambo haya, basi tunapaswa kutafuta na kufahamu jinsi wokovu wa Mungu wa ondoleo la dhambi ulivyotimizwa katika Agano Jipya. Maandiko yanatueleza kuhusu mada hizi kwa sababu kama hatutayaangalia maandiko haya kwa karibu, basi ni hakika kwamba tutajichanganya kuhusu watakatifu, watumishi wa Mungu, na watu wa Israeli wanaoonekana katika Kitabu cha Ufunuo. 
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo.”
Hii inatueleza kwamba kazi ya kuwaokoa Waisraeli toka katika dhambi kwa neema ya Mungu sasa imepangwa ili kuanza. Hili tendo la “Kupima” linalotajwa hapa lina maanisha kwamba Mungu ataingilia yeye binafsi ili kuwaokoa watu wa Israeli toka katika dhambi zao katika nyakati za mwisho.
Katika kifungu kikuu cha sura ya 11, tunapaswa kuuweka mkazo wetu katika wokovu wa Waisraeli toka katika dhambi. Neno hili linatueleza kwamba injili ya maji na Roho itaenea kwa watu wa Israeli kuanzia wakati huo na kuendelea, na hiyo itamaanisha mwanzo wa kazi ya Mungu kuwabadili Waisraeli kuwa watu wa Mungu waliokombolewa atoka katika dhambi zao zote kwa kupitia neema ya wokovu iliyotolewa na Yesu Kristo. Mungu aliandika Ufunuo 11 ili pia kutoa ondoleo lake la dhambi kwa Waisraeli katika nyakati za mwisho. Kitendo cha “kupima” katika aya ya 1 na ya 2 kina maanisha ni kuweka viwango kwa vitu vyote. Dhumuni la Mungu katika kulipima Hekalu lake, ni kuangalia ikiwa mioyo yao ipo tayari kupokea wokovu wako, alifanya hivi kwa kuwa amekwishapanga kuwaokoa Waisraeli. Na ikiwa mioyo yao haipo tayari, basi upimaji huo utawafanya wawe tayari, ili kwamba mioyo yao isimame sawasawa.
 
Aya ya 2: “Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili.”
Mungu alimpatia mamlaka ya kuwakanyaga mataifa kwa miaka mitatu na nusu. Hivyo, Wamataifa wote ni lazima wapokee katika mioyo yao injili ya maji na Roho, ambayo ni Neno la ukombozi, wanapaswa kuipokea injili hiyo mapema ndani ya kipindi cha miaka mitatu na nusu katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu. Historia ya ulimwengu huu itaisha wakati Dhiki Kuu ikipita kuelekea katika nusu nyingine. Hivi karibuni, utafika wakati ambapo Wamataifa, pamoja na watakatifu ambao wamekwisha okolewa toka katika dhambi zao zote watakanyagwa na Shetani.
Hivyo, Wamataifa ni lazima wapokee ondoleo la dhambi zao na kisha waiandae imani ya kufia-dini mapema katika ile miaka mitatu na nusu ya kwanza katika ile miaka ya Dhiki. Pia wakati huo wataupokea ukweli kwamba Yesu ni Mwokozi wao. Hapo mwishoni, watu wa Israeli wataupokea wokovu wao toka katika dhambi zao zote wakati wa kipindi cha miaka mitatu na nusu katika ile miaka ya Dhiki Kuu. Tunapaswa kufahamu kwamba Mungu ataruhusu ondoleo la dhambi kwa Waisraeli hata wakati wa Dhiki Kuu.
 
Aya ya 3: “Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.”
Mungu atawainua mashahidi wawili kama watumishi wake kwa ajili ya watu wa Israeli. Manabii hao wawili ambao Mungu atawainua kwa ajili ya Waisraeli wamepewa nguvu mara mbili kuliko zile za manabii wa kale, na kwa kupitia maneno ya ushuhuda wao, Mungu ataanza kufanya kazi kati ya watu wa Israeli ili kwamba waweze kumpokea Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao. Kwa kupitia kazi za hawa manabii wawili, Waisraeli wengi watakuja kuzaliwa tena upya na kuwa watu wa Mungu.
Mungu, kwa kuwaweka hawa manabii wawili ambao atawatuma kuwaokoa Waisraeli toka katika dhambi zao katika nyakati za mwisho, Mungu kwa kupitia manabii hawa atafanya miujiza na maajabu, na hivyo atawafanya Waisraeli, ambao wakati huo watakuwa wakiongozwa na hawana manabii kumrudia Kristo na kisha kumwamini kama Mwokozi wao. Manabii hawa wawili wawalisha watu wa Israeli Neno la Mungu kwa siku 1,260 wakati wa miaka mitatu na nusu ya kwanza katika kipindi cha Dhiki Kuu. Mungu awataruhusu Waisraeli kupata wokovu ule ule ambao umewaokoa Wamataifa wa kipindi cha Agano Jipya toka katika dhambi zao kwa kuwapatia injili ya maji na Roho na kisha kuwafanya waiamini injili hiyo kwa imani.

Aya ya 4: Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.
“Miti miwili ya mizeituni” ina maanisha ni manabii wawili wa Mungu (Ufunuo 11:10). Kwa upande mwingine, “vinara viwili vya taa,” vina maanisha ni Kanisa la Mungu ambalo amelianzisha kati ya Wamataifa, na Kanisa ambalo ameliruhusu kwa watu wa Israeli. Mungu amelijenga Kanisa lake miongoni mwa Wayahudu na kwetu sisi Wamataifa, na ataendelea kuifanya kazi yake ya kuziokoa nafsi toka katika dhambi hadi siku ya mwisho.
Kwa kupitia hii “mizeituni mwili” na hivi “vinara viwili vya taa”, Mungu anatueleza kwamba kama alivyowainua manabii wake katika kipindi cha Agano la Kale ili kuwaokoa Waisraeli toka katika dhambi zao na akatenda kwa kupitia manabii hao, basi nyakati za mwisho zitakapowadia, Mungu atawainua manabii wawili kati ya watu wa Israeli ambao watalihuburi Neno lake, na kisha kuwaongoza watu Waisraeli kwenda kwa Yesu kwa kupitia manabii hao.
Waisraeli walishindwa kuwaamini kwa umakini watumishi wa Mungu ambao wana asili ya Wamataifa, na hawakusikiliza kile ambacho watumishi hawa wa Mungu waliwaambia. Kwa kuwa wanafahamu kila kitu kuhusu utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa na unabii wa Agano la Kale, basi manabii wa Mungu wa nyakati za mwisho wanapaswa kuinuliwa toka katika watu wa Israeli. Waisraeli wanayaelewa vizuri Maandiko kiasi kuwa wanaweza kuikariri na kuinukuu Torati yote hata pale wanapokimbia. Hii ndio sababu hawaamini kamwe kile ambacho watumishi wa Mungu ambao ni Wamataifa wanawaambia.
Lakini watumishi wa Mungu, hali wakiisikia injili ya maji na Roho ambayo mimi na wewe tunaihubiri sasa, watainuka toka miongoni mwa Waisraeli wenyewe. Wakati waamini katika injili ya maji na Roho watakapoinuka kati yao, na kisha manabii wawili kuinuka kati yao wakiwa wameletwa na Mungu na ambao watalielezea na kulihubiri Neno la Mungu kwao, basi ni hapo tu ndipo Waisraeli watakapoamini.
Watu wa Israeli watafahamu kwamba hawa mashahidi wawili ni manabii waliotumwa na kuinuliwa na Mungu Mwenyewe ili kuwaokoa toka katika dhambi zao katika nyakati za mwisho. Manabii hawa watazionyesha nguvu zao kuu, kama walivyofanya watumishi wa Mungu katika Agano la Kale, ambao Waisraeli wanawafahamu vizuri na kuwaamini. Hivyo, Waisraeli watayaona kwa macho yao maajabu ya kushangaza ambayo mashahidi hawa wawili watayafanya. Kuanzia wakati huu, watu wa Israeli watamrudia Yesu Kristo na kisha kumwamini Bwana. Watakapomtambua Yesu Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wao, kama sisi tunavyofanya, basi hapo watakuwa na imani kama yetu—yaani, wao pia wataokolewa kwa kuiamini injili ya maji na Roho.
Mashahidi hawa wawili watalieleza Neno la Mungu na kisha kuwalisha watu wa Israeli kwa miaka 1,260 wakati kipindi cha miaka saba cha Dhiki Kuu. Kama ambavyo wewe na mimi, ambao ni Wamataifa wa wakati wa Agano Jipya tulivyookolewa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, basi Mungu atawaruhusu Waisraeli kuokolewa katika nyakati za mwisho kwa kuiamini injili ya maji na Roho.
Kama vile aya ya 4 inavyotueleza, “hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi,” Biblia inawaita hawa mashahidi wawili kuwa ni “mizeituni miwili.” Mizeituni hii miwili ina maanisha ni manabii wawili wa nyakati za mwisho. Katika aya ya 10, imeandikwa hivi, “Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.” Hapa, tunapaswa kulitazama Neno hili kwa kuangalia juu ya hii mizeituni miwili.
Katika kipindi cha Agano la Kale, mizeituni ilitumika katika kutengenezea madhabahu na mimbari katika Hema la Mungu kwa kuiweka wakfu kwa mafuta ya mizeituni. Mafuta haya ya mizeituni pia yalitumika kwa matumizi mengine, kama vile kuwashia taa za Hekaluni. Ni mafuta safi tu ya mizeituni ndiyo yaliyotumika kuwashia taa za Hekaluni. Mungu hakuruhusu mafuta mengine kutumika katika Hekalu lake, bali alihakikisha kwamba ni mafuta ya mizeituni tu ndiyo yanayotumika. Hivyo, tunapaswa kufahamu kwamba mafuta ya mizeituni, pamoja na mti wa mtini, vinawakilisha watu wa Israeli.
Kuna mafafanuzi mengi kuhusiana na hii mizeituni miwili na vinara hivi viwili vya taa. Baadhi ya watu wanadai kwamba wao wenyewe ndio hiyo mizeituni miwili. Lakini mizeituni hii miwili inawamaanisha wale waliotiwa mafuta. Katika nyakati za Agano la Kale, mtu alitiwa mafuta wakati alipofanywa kuwa nabii, mfalme, au kuhani. Wakati mtu alipowekwa mafuta Roho Mtakatifu alishuka juu yake. Kwa hiyo, mti wa mzeituni una maanisha ni Yesu Kristo ambaye alitungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Warumi 11:24). Lakini watu wanaielewa vibaya dondoo hii.
Hata hivyo, mizeituni mwili, ambayo ni mashahidi wawili wanaotwaja katika kifungu hiki, ina maanisha ni watumishi wawili wa Mungu ambao atawainua kipekee katika nyakati za mwisho kwa ajili ya wokovu wa watu wa Israeli.
Hiki ndicho ambacho aya ya 4 inatueleza. Na hivi vinara viwili vya taa vina maanisha ni Kanisa la Mungu ambalo ameliruhusu kati ya Wamataifa, na Kanisa aliloliruhusu kwa watu wa Israeli. Kwa asili, katika kipindi cha Agano la Kale, Waisraeli walikuwa na hili Kanisa la Mungu. Lakini kuanzia katika kipindi cha Agano Jipya, Waisraeli hawana tena hili Kanisa la Mungu. Kwa nini? Kwa sababu bado hawamtambui Yesu Kristo, na pia ni kwa sababu hawana Roho Mtakatifu katika mioyo yao.
Kwa kuwa hawajaipokea injili ya maji na Roho wala hawajampokea Yesu Kristo, basi Kanisa la Mungu haliwezi kuwemo ndani yao. Hata hivyo, kabla ya mwisho wa dunia, yaani wakati wa miaka mitatu na nusu ya kwanza katika ile miaka ya Dhiki Kuu, Mungu ataliruhusu Kanisa lake kwa watu wa Israeli pia. Hii ndio sababu Biblia inatueleza kuhusu mizeituni miwili, ambayo ni mashahidi wawili wa Mungu.
Bwana atalianzisha Kanisa lake na kisha kuifanya kazi yake ya kuziokoa nafsi toka katika dhambi miongoni mwa Wayahudi na sisi Wamataifa. Kwa kwa kupitia makanisa haya, Mungu atawafanya waifanye kazi hii ya kiroho ya kuziokoa nafsi toka katika dhambi hadi atakapoonekana Mpinga Kristo. Hii ina maanisha kwamba Mungu atatengeneza vyombo miongoni mwa watakatifu, ambao ni washiriki wa Kanisa lake, ili kuwafanya waitumikie huduma yake ya kuziokoa nafsi zilizopotea katika dhambi. Hivyo ni lazima tuitende huduma yetu iliyosali kwa juhudi na katika imani.
 
Aya ya 5: Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa.
Mungu aliwapatia nguvu hii hawa manabii wawili ili kwamba waweze kuifanya kazi yake maalumu. Mungu anatuonyesha kwamba yeyote atakayejaribu kuwaua hawa mashahidi wawili yeye mwenyewe ndiye atakayedhuriwa, na kwamba nguvu ya Neno lake itakuwa pamoja na mashahidi hawa wawili, hii yote ni ili kuwafanya watu wa Israeli kutubu na kisha kumshinda Shetani katika nyakati za mwisho.
Kwa hiyo, watu wa Israeli, hali wakiamini juu ya mafundisho ya hawa manabii wawili, watamrudia Yesu Kristo. Hii ndio sababu ni kwa nini Mungu ataruhusu uwepo wa hii mizeituni miwili—yaani mashahidi wawili—kwa Waisraeli, ili kwamba waweze kuokolewa toka katika dhambi zao katika nyakati za mwisho.
 
Aya ya 6: Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo.
Kwa kuwa watu wa Israeli hawatatubu hadi pale watumishi wa Mungu ambao atawainua kwa ajili yao watakapoyafanya matendo haya yenye nguvu, basi ndio sababu Mungu atawaruhusu hawa mashahidi wawili kutenda kazi kwa nguvu zake. Hawa manabii wawili sio tu kwamba watawaongoza Waisraeli kwenda kwa Yesu, bali pia watawashinda maadui wa Mungu kwa nguvu na kisha kuitimiza kazi yote ya wito wao. Mungu atawapatia nguvu maalumu ili kwamba waweze kulihubiri Neno lote la unabii kwa watu wa Israeli, na kushuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye Masihi waliyemsubiri kwa muda mrefu na kisha kuwafanya Waisraeli waamini.
 
Ayay ya 7: Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua.
Neno hili linatueleza kwamba Mpinga Kristo ataonekana hapa ulimwenguni baada ya kupita kwa miaka mitatu na nusu katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu. Ni wakati huu ndipo wale wote wanaomwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wako anayesubiriwa watakapoinuka miongoni mwa watu wa Israeli. Lakini wengi wao watauawa na Mnyama na kuwa wafia-dini ili kuilinda imani dhidi ya Mnyama, ambaye ni Mpinga Kristo na wafuasi wake. Manabii wawili wa Mungu pia watauawa na kuwa wafia-dini mara watakapokuwa wameukamilisha wito wao.
Kule kusema kwamba mashahidi hawa wawili watauawa na Mpinga Kristo ni kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Kwa nini? Kwa sababu Mungu atataka kuwapatia thawabu kwa ajili ya wao kuifia-dini. Thawabu hii ni ile ya wao ya kushiriki katika ufufuo wa kwanza, kisha kuungana na bwana katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo, kurahi milele, na kisha kupokea uzima wa milele. Ili Mungu aweze kuwapatia watakatifu wote baraka hii, basi anataka watakatifu wote wauawe na kuwa wafia-dini kwa sababu ya imani yao. Hivyo, watakatifu wote ni lazima wasiogope wala kukwepa kuifia-dini, bali wanapaswa kuyapokea mauaji hayo ya kufia-dini kwa imani na kisha kupokea thawabu iliyobarikiwa.
 
Aya ya 8: Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa.
Aya hii inatueleza kwamba “mashahidi wawili” wanatoka hasahasa miongoni mwa watu wa Israeli. Watumishi wawili ambao Mungu atawainua kwa ajili ya Waisraeli si kutoka kwa Wamataifa, bali kutoka miongoni mwa watu wa Israeli. Kwa hiyo, mashahidi wawili wanauawa mahali pale pale ambapo Yesu alisulubiwa. Ukweli huu unatueleza kwa wazi kwamba mashahidi hawa wawili ni Waisraeli. Hawa ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya watu wa Israeli.
Mungu atawaleta manabii wake wawili kwa watu wa Israeli, ambao kiroho ni kama vile watu wa Sodoma na Misri, atawapatia nguvu, na kisha atawafanya washuhudie kwamba Yesu ni Masihi ambaye Waisraeli walikuwa wakimngojea, ili kwamba watu wa Israeli waweze kutubu na kumwamni Yesu.
Mpinga Kristo atawaua watumishi wawili wa Mungu mahali panapoitwa Golgota, mahali ambapo Yesu alisulubiwa. Kwa kuwa wafuasi wa Mpinga Kristo wana roho chafu, watawachukia hawa mashahidi wanaomwamini na kumshuhudia Yesu hadi kifo. Ni kama vile askari wa Kirumi waliomsulubisha Yesu na kicha kumchoma kwa mkuki ubavuni, basi wale walio na roho chafu hawatamchukia Yesu tu, bali pia watawachukia mashahidi wa Mungu na kisha kuwaua.
 
Aya ya 9: Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini.
Miongoni mwa watu wa Israeli, kuna watu pia ambao hawamwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao. Hivyo baada ya kuona miili iliyokufa ya hawa watumishi wawili (mizeituni miwili), basi watafurahia wakidhani wameshinda, na ili kuonyesha hii fikra ya kushinda, basi hawatafikiria hata kuwazika watumishi hao. Lakini ushindi wao utavunjwa vunjwa na kuwa vipande wakati Mungu atakapofanywa “mashahidi wawili” kufufuka na kuwa hai tena, na hapo ndipo watakapomwogopa Mungu.
Wanaweza kujisifia kwa vifo vya watumishi wawili wa Mungu, lakini furaha hii haitadumu kwa muda mrefu, maana ghafla watatambua kwamba Mpinga Kristo hawezi kulingana na Yesu Kristo—hivyo hali ya kukata tamaa na utupu ndivyo vitakavyowagubika.
Watu hawa wanalichukia Neno la Mungu la unabii linalohubiriwa na manabii wawili. Kwa kitendo chao cha kusimama kinyume na watumishi ambao Mungu aliwainua, basi ni hakika kwamba wao sasa watakatwa toka katika mavuno ya mwisho ya wokovu na kisha wataishia na kuwa wafuasi wa Shetani.
 
Aya ya 10: Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.
Kwa kuwa watalihubiri Neno la Mungu la unabii, basi hawa mashahidi wawili walioinuliwa kwa ajili ya wokovu wa Waisraeli watakua ni maumivu makubwa katika shingo za wafuasi wa Shetani. Kwa hiyo, wote hao watafurahia sana baada ya kuona vifo vya hawa mashahidi wawili na kisha watatumiana zawadi na kusifiana.
Sisi pia, tunakuwa na furaha pale tunapowaona watu waliotusumbua wakitoweka. Mpinga Kristo na wafuasi wake watachukia sana wakati Mungu atakapowainua mashahidi wawili ili kulihubiri Neno lake. Kila wakati wanapolisikia Neno la Mungu, roho zao zitakabiliwa na masumbuko. Kwa kuwa watakuwa wamesumbuliwa sana kila wakati mashahidi hao wanapozungumzia kuhusu Yesu, basi ndio maana watafurahia sana watakapowaona wameuawa na Mpinga Kristo. Na hii ndio sababu watabadilishana zawadi kama sehemu ya kupongezana.
 
Aya ya 11: Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama.
Hata hivyo, Mungu atawafanya mashahidi wawili kushiriki katika ufufuo wa kwanza. Hili Neno ni ushahidi kwamba watakatifu, ambao wameuawa na kuwa wafia-dini ili kuilinda imani yao baada ya kuwa wameokolewa toka katika dhambi kwa kuliamini Neno la wokovu lililotolewa na Bwana, watashiriki katika ufufuo wa kwanza.
Kule kusema kwamba roho ya uhai ikawaingia baada ya “siku tatu na nusu” kunatueleza kwamba Bwana ataruhusu ufufuo wao kwa muda mfupi, kama vile yeye alivyofufuka toka katika kifo cha mwili. Kule kusema kwamba Mungu amewaruhusu watakatifu kuwa na imani hii ya ufufuo wa kwanza, ina maanisha kwamba watakatifu wenyewe imani hiyo ni baraka kubwa ya Mungu, lakini kwa wenye dhambi wote, ufufuo huo utawaletea hofu kuu na kufa moyo. Ufufuo wa kwanza wa watakatifu ni ahadi ya Mungu na thawabu yake kwa ajili ya imani yao.
 
Aya ya 12: Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.
Hili Neno linaeleza juu ya ufufuo na unyakuo wa watakatifu. Baada ya kuliamini Neno la Bwana la unabii, basi wale waliookolewa toka katika dhambi zao zote hawatakuwa na la kufanya zaidi ya kuuawa na kuifia-dini ili kuilinda imani yao. Aya hii inatuonyesha kwamba Bwana atawafufua watakatifuhawa wote na kisha kuwanyakua. Watakatifu na watumishi wa Mungu waliouawa na kuwa wafia-dini kwa sababu ya utii kwa Mungu watabarikiwa kwa kuinuliwa kwenda angani (unyakuo) kwa sababu ya imani yao katika Bwana. Hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kumshukuru Bwana kwa kutupatia ufufuo wetu pamoja na unyakuo kama thawabu ya kuuawa na kuifia-dini baada ya kuokolewa kwa kuamini katika ondoleo la dhambi ambalo Bwana ametupatia.
Mungu Baba ataruhusu ufufuo na unyakuo kwa wale wote wanaosimama kinyume na Mpinga Kristo na kisha kuuawa kama wafia-dini kwa kuiamini injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu Kristo. Tunapaswa kuuamini ukweli huu. Ufufuo wa watakatifu na unyakuo ni baraka ambazo zinatoka katika wokovu wao kwa kupitia imani yao katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu. Shetani na wafuasi wake wa nyakati za mwisho watafanya jitihada zote ili waweze kutowekea angani kama mvuke mara watakapowaona watakatifu ambao waliwatesa na kuwaua wakifufuliwa na kunyakuliwa.
Mungu atawafufua na kuwanyakua watakatifu waliouawa na kuwa wafia-dini, lakini atawaangamiza wale ambao watakuwa bado wapo duniani kwa kuwamiminia mapigo ya mabakuli saba. Baada ya kazi hii kukamilika kwa haraka, Bwana atakuja hapa duniani pamoja na watakatifu na kisha atawaalika wenye haki katika karamu ya harusi ya Kristo. Bwana wetu ataifanya karamu hii kudumu kwa miaka elfu moja. Baada ya kuisha kwa hii milenia, Mungu atamruhusu Shetani kuibuka toka katika shimo la kuzimu lisilo na mwisho kwa muda mfupi na kisha kupigana na Mungu na watakatifu wake, lakini hatimaye Bwana atamwangamiza Shetani na wafuasi wake na kisha kuwahukumu kutupwa katika moto wa milele. Hata hivyo, wenye haki wataingia katika Ufalme wa Bwana wa Mbinguni na kisha kuishi naye milele.
 
Aya ya 13: Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliosalia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu.
Baada ya kuuawa na kuifia-dini, ufufuo, na unyakuo wa manabii wawili ambao Mungu atainua kwa ajili ya wokovu wa Waisraeli, Mungu atawaruhusu malaika zake kuyamimina kwa uhuru mapigo ya mabakuli saba katika dunia. Wale watakaokuwa wamebakia katika dunia hii baada ya watakatifu kunyakuliwa watayapokea mapigo haya ya mabakuli saba kama thawabu yao. Ni hapo tu ndipo watakapogubikwa na hofu na kisha kumpatia Mungu utukufu, lakini jambo hili halitakuwa na maana yoyote kwao, kwa kuwa jambo hili halitakuwa ni tendo la imani ya kweli katika upendo wa Mungu.
Wakati ulimwengu huu ukiangamizwa, wenye haki watakuwa na Mbingu yao ya milele, ufufuo wa milele, na baraka za milele, lakini wenye dhambi, watakuwa wakingojewa na mateso ya moto wa milele huko kuzimu. Hii ndio sababu kila mtu anapaswa kupokea ondoleo la dhambi zake kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Na kwa kuwa wale waliokwisha kukombolewa toka katika dhambi zao wanaamini juu ya ulimwengu mpya ambao Mungu aliwaahidia, basi ndio maana wanaihubiri injili ya maji na Roho kwa kila mtu.
 
Aya ya 14: Ole wa pili umekwisha pita, tazama ole wa tatu unakuja upesi.
Ole wa tatu toka kwa Mungu utawangojea watu wote Wamataifa na Waisraeli isipokuwa wale walioshiriki katika ufufuo wao na unyakuo kwa kuokolewa na kisha kuuawa kama wafia-dini.
Pigo linalotokana na malaika kulipiga tarumbeta la sita ambalo linadumu hadi hadi kupigwa kwa tarumbeta la saba ambalo linaleta mwanzo wa mapigo ya mabakuli saba linaitwa ni ole wa pili. Mapigo ya matarumbeta saba yamegawanyika katika vipindi vitatu—kipindi cha mwanzo, cha kati, na cha mwisho. Mapigo ya kiasili na kuuawa kwa watakatifu kama wafia-dini na Mpinga Kristo kunajumuishwa katika ole ya kwanza na ya pili. Kwa maneno mengine, hii ole ya tatu, ni mapigo ambayo yataungamiza ulimwengu kikamilifu. Hii ole ya tatu ni mabakuli ya ghadhabu ya Mungu ambayo yatamiminwa kwa wenye dhambi watakaokuwa wamesalia hapa duniani.

Aya ya 15: Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele!”
Hii sentensi inayosema, “pakawa na sauti kuu katika mbingu,” inatuonyesha kwamba watakatifu na watumishi ambao wameokolewa toka katika dhambi zao zote watakuwa tayari wapo Mbinguni wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapokuwa yakianza hapa ulimwenguni. Kwa hiyo, wakati huo watu wa Mungu hawataonekana tena hapa ulimwenguni. Tunapaswa kutambua jambo hili. “Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele!”
Wakati huu, watakatifu watamsifu Bwana Mbinguni, lakini baada ya mapigo ya mabakuli saba kumiminwa, basi watakatifu hao watashuka katika ulimwengu utakaokuwa umefanywa upya na bwana na kisha watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moka hapa ulimwenguni. Kisha itafuatiwa kwa Bwana na watakatifu kutawala milele katika Mbingu na Nchi Mpya.
Bwana wetu ametuokoa sisi kama watumishi wake badala ya kututawala kama mfalme ili kutukomboa toka katika dhambi zetu. Bwana amewapatia neema yake inayowafanya wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho kama wokovu wao kuwa wana wa Mungu. Kwa kuwa Bwana wetu ni Mfalme wetu wa milele, basi atatufanya sisi watu wake kutawala milele. Haleluya! Mshukuruni Bwana!
 
Aya ya 16: Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu,
Mungu anastahili kupokea utukufu wote. Ni sahhihi kabisa kwa wale ambao wameokolewa toka katika dhambi zao kuanguka na kusujudu na kumsifu Mungu. Bwana wetu, ambaye amefanya kazi hizi zote ili kuwaokoa wenye dhambi, anastahili kupokea sifa na kuabudiwa toka kwa watakatifu wote na uumbaji wote milele na milele.
 
Aya ya 17: wakisema: “Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki.”
Ili aweze kutawala milele pamoja na watu wake, Bwana wetu atamshinda Shetani na kupokeo nguvu kuu toka kwa Mungu Baba. Kwa hiyo, Bwana atatawala milele. Bwana anastahili kufanya hivyo. Ninampatia Bwana utukufu, hii ni kwa sababu Bwana ndiye aliyezifanya dhambi zote za ulimwengu kutoweka, na ni yeye ndiye aliyewaokoa wale wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho, na ni yeye ndiye aliyewahukumu maadui zake, kwa sababu hiyo anastahili kupokea nguvu kuu na kisha kutawala milele. Kwa hiyo, wale wote wanaotambua ukuu wa Mungu watavikwa utukufu wa kumsifu Mungu milele pamoja na nguvu kuu na upendo wa Bwana.
 
Aya ya 18: “Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.”
Sambamba na kumiminwa kwa mapigo ya mabakuli saba kutaambana na maangamizi ya mwili kwa wale wote ambao watabakia kiroho kuwa Wamataifa. Neno hili linatueleza kwamba wakati huo utakuwa ni wakati wa Mungu kumhukumu kila mtu huku yeye akiwa Hakimu wa wote, naye atawapa thawabu watumishi wake na manabii, watakatifu, na wale wote wanaomheshimu Yeye, kisha atawaangamiza wale wote wanaosimama kinyume na kutoyaheshimu mapenzi yake. Bwana ataileta hukumu ya ghadhabu yake juu ya wale wasioutambua ukuu wake, lakini atawaruhusu watakatifu kutukuzwa pamoja naye. Hii ina maanisha kwamba Bwana amefanyika kuwa Hakimu wa wote, wema kwa waovu. 
Wakati Bwana atakapoketi katika kiti chake cha enzi kama Mfalme wa wale waliozaliwa tena upya na kisha kumhukumu kila mtu, basi wenye dhambi wote na wenye haki wa hapa ulimwenguni watapokea hukumu yao ya haki. Wakati huo, kama maamuzi ya hukumu yake, Bwana atawapatia watakatifu Mbingu na uzima wa milele, lakini atawapatia wenye dhambi maangamizi ya milele na adhabu ya kuzimu. Ukuu wa Yesu Kristo na baraka kwa watu wake ya kutawala itaendelea milele. Wakati huu, ulimwengu wa kwanza utafikia ukomo, na hivyo ulimwengu wa pili, ambao ni Ufalme wa Kristo utaanza.
 
Aya ya 19: Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana.
Mungu atawaruhusu watakatifu wake, ambao ni wenye haki, kupata baraka ya kuishi katika Hekalu lake. Mambo haya yote yanatimizwa kwa mujibu wa Neno la Mungu la ahadi kwa mwanadamu katika Yesu Kristo. Ufalme wa Mungu unaanza na Neno la Mungu la unabii, kisha unakamilishwa kwa utimilifu wa unabii huu.
Ahadi zote za Mungu, kuanzia ufufuo hadi unyakuo wa watakatifu hadi kushiriki kwao katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo pamoja na Yesu Kristo pamoja na baraka yao ya kutawala milele kama wafalme zitagawanywa sawa kwa watu wa Israeli na kwa Wamataifa. Pia Mungu anauchukulia wokovu wa Waisraeli katika nyakati za mwisho na ule wokovu wetu kuwa ni mmoja, anatufanya sisi sote kuuawa na kuifia-dini wakati huo, anaturuhusu kushiriki ufufuo mmoja na baadaye unyakuo ule ule, na anatuvika sote utukufu ule ule. Neno linatueleza kwamba pamoja na kuwa Waisraeli na sisi Wamatafa ni watu wawili tofauti katika mwili, ukweli ni kuwa kiroho sisi ni watu wamoja wa Mungu.
Watu wengi wanadai na kuamini kwamba waliozaliwa tena upya watanyakuliwa kabla ya Dhiki Kuu ya miaka saba haijaanza. Lakini ukweli sio huu. Tukiongea kibiblia, watu wataendelea kuisikia injili ya kweli na kisha kuokolewa katika ile miaka mitatu na nusu ya kwanza kati ya ile miaka saba ya Dhiki Kuu. Kisha Mpinga Kristo atatokea, watakatifu watauawa na kuifia-dini, na baada ya ufufuo na unyakuo itafuata karamu ya harusi ya Mwana-kondoo, na kisha kuwaruhusu watakatifu kutawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.
Watakatifu wanapaswa kuwa na ufahamu sahihi juu ya muda wa wao kuuawa na kuifia-dini, na juu ya ufufuo na unyakuo. Pasipo kuufahamu wakati huu, basi ni hakika kwamba wataendelea kushangaa hali wakiwa wamekanganyikiwa na kisha kufa kiroho kwa sababu ya mkanganyiko huo.
Wale walio na ufahamu sahihi wa majaliwa ya Mungu juu ya nyakati za mwisho wanautumaini ufufuo na unyakuo wao, na wataendelea kuitumikia injili kwa juhudi. Wale wanaofahamu kwamba hakuna tumaini katika dunia hii wanapaswa kuwa na tumaini lile lile la wale waliozaliwa tena upya kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Pia ni vizuri ifahamike kwamba watakatifu wanauawa na kuifia-dini kwa sababu ya kuliamini Neno la Mungu.
Ni kweli kwamba imani inayoweza kupambanua nyakati inahitajika sana katika nyakati hizi. Kwa kweli wakati umekaribia wa mapigo ya kutisha na dhiki kushuka juu ya ulimwengu mzima na kwa Mpinga Kristo kutokea. Sasa ni wakati wako wa kuamka toka katika usingizi. Tunapaswa kuzingatia kwamba tutapaswa kuyapitia mateso yote ya ile Dhiki Kuu. Ni muhimu tuamini juu ya kurudi kwa Kristo, na juu ya ufufuo na unyakuo, na juu ya ushiriki wetu katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo pamoja na Kristo. Ili tuweze kuwa na imani sahihi katika kipindi hiki, basi ni lazima tuingie katika sanduku la injili ya maji na Roho.
Ninatumaini na kuomba kwamba kwa kukifahamu kipindi hiki, basi utakuwa na imani ambayo inahitajika sana na ambayo ni sahihi kabisa kwa wakati huu.