Search

説教集

Somo la 11: Maskani

[11-16] Mafumbo ya Kiroho Yaliyofichwa Katika Sanduku la Ushuhuda (Kutoka 25:10-22)

Mafumbo ya Kiroho Yaliyofichwa Katika Sanduku la Ushuhuda
(Kutoka 25:10-22)
“Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”
 
 
Sanduku la agano
Mada ya leo ni Sanduku la Ushuhuda. Sanduku la Ushuhuda lilikuwa na vipimo vya sentimita 113 (futi 3.7) kwa urefu, sentimita 68 (futi 2.2) kwa upana, na sentimita 68 (futi 2.2) kwa kimo chake, Sanduku hili lilitengenezwa kwa mti wa mshita na lilifunikwa kwa dhahabu safi. Ndani ya Sanduku kulikuwa na mbao mbili za mawe zilizokuwa zimeandikwa Amri Kumi na bilauri ya dhahabu iliyokuwa na manna, na baadaye iliwekwa ile fimbo ya Haruni iliyochipuka. Je, vitu hivi vitatu vilivyowekwa ndani ya Sanduku hili la Ushuhuda vinatueleza nini? Kwa kupitia vifaa hivyo, nitapenda kutoa ufafanuzi wa kina na wa upana kuhusiana na huduma tatu za Yesu Kristo. Hebu sasa na tuchunguze juu ya ukweli wa kiroho uliodhihirishwa katika vifaa hivi vitatu vilivyokuwa vimewekwa ndani ya Sanduku la Ushuhuda.
 

Mbao Mbili za Mawe Zilizokuwa Zimeandikwa Sheria
 
Yaliyomo ndani ya sanduku la agano
Mbao mbili za mawe zilizokuwa zimeandikwa Sheria na kuwekwa ndani ya Sanduku la Ushuhuda zinatueleza sisi kuwa Mungu ndiye mtunga sheria ambaye ametupatia sisi sheria zake. Warumi 8:1-2 inasema, “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Toka katika kifungu hiki, tunaweza kuona kuwa Mungu alianzisha sheria mbili katika mioyo yetu: sheria ya uzima na sheria ya adhabu.
Kwa sheria hizi mbili, Bwana ameleta adhabu na wokovu kwa wanadamu wote. Kwanza kabisa tunaweza kutambua kwa kupitia Sheria kwamba sisi tu wenye dhambi ambao bila kukwepa tumepangiwa kuzimu. Hata hivyo, kwa wale ambao wanaifahamu hali yao ya asili kuwa wamepangiwa mabaya, Mungu amewapatia watu wa jinsi hiyo sheria yake ya wokovu, “sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu.” Mungu amefanyika kuwa Mwokozi wa kweli kwa watu wote kwa kuwapatia sheria hizi mbili.
 

Mana Iliyowekwa Katika Bilauri ya Dhahabu
 
Ile Bilauri ya dhahabu iliyokuwepo katika Sanduku la Ushuhuda ilikuwa na mana. Wakati watu wa Israeli walipotumia miaka 40 katika jangwa na nyika, Mungu aliwaletea chakula toka mbinguni na waisraeli waliishi kwa kutegemea mana hii wakiipika katika hali tofauti. Mana hii ilikuwa ni nyeupe kama vile mbegu za giligilani, na radha yake ilikuwa ni kama maandazi yaliyotengenezwa kwa asali. Hii mana ambayo Mungu alikuwa amewapatia watu wa Israeli iliwawezesha kuishi maisha yao hadi pale walipoingia katika nchi ya Kanaani. Kwa hiyo, chakula hiki kiliwekwa kwa ajili ya ukumbusho na hivyo kikawekwa katika bilauri hii.
Hii inatueleza sisi kuwa sisi waamini wa leo tunapaswa pia kula mkate wa uzima ambao wana wa kiroho wa Mungu ni lazima waule wanapokuwa hapa duniani hadi pale watakapoingia Mbinguni. Lakini kuna nyakati ambapo tunapenda kuupata mkate wa ulimwengu, ambao ni mafundisho ya ulimwengu huu badala ya Neno la Mungu. Pamoja na hayo, kitu ambacho watoto wa Mungu wanapaswa kukiishia na kuishi kwa hicho hadi pale watakapoifikia nchi ya kiroho ya Kanaani ni Neno la Mungu, ambalo ni mkate wa kiroho wa maisha ya kweli unaotoka Mbinguni.
Mtu hawezi kuchoka kwa kuula mara kwa mara mkate wa maisha ya kweli. Kadri tunavyoupata mkate huu wa kiroho, ndivyo mkate huo unavyofanyika kuwa maisha ya kweli katika nafsi zetu. Lakini ikiwa tunaula mkate wa mafundisho ya ulimwengu badala ya Neno la Mungu, basi hatimaye nafsi zetu zitaishia mautini.
Mungu aliwaamuru watu wa Israeli kuiweka mana iliyotoka mbinguni katika bilauri ya dhahabu na kuitunza. Kama inavyoonyeshwa katika Kutoka 16:33, Mungu alisema, “Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya BWANA, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu.” Ile mana iliyotoka mbinguni ulikuwa ni mkate wa maisha ya kweli kwa ajili ya nafsi za watu. “Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha BWANA” (Kumbukumbu la Torati 8:3).
 


Je, Ni Nani Basi Ambaye Ni Mkate wa Kweli wa Uzima Kwetu Sisi?

 
Ubatizo ambao Yesu Kristo aliupokea ili kuzichukua dhambi zetu katika mwili wake na kusulubiwa kwake na kuimwaga damu yake hivyo ndivyo vinavyoufanya mkate wetu wa kweli wa maisha. Kwa kutupatia sisi mwili na damu yake, Yesu Kristo amefanyika kuwa ni mkate wa uzima wa milele. Kama ambavyo Yohana 6:48-58 inatueleza sisi: “‘Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.’”
Bwana wetu alisema, “Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.” Je, kile “chakula kishukacho kutoka mbinguni” ni kitu gani? Ina maanisha ni mwili na damu ya Yesu. Katika Biblia, mwili wa Yesu unatueleza sisi kuwa Yesu Kristo alizichukua dhambi za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana katika Mto Yordani. Na damu ya Yesu inatueleza sisi kuwa kwa sababu Yesu alibatizwa, basi alizichukua dhambi za ulimwengu na akabeba adhabu ya dhambi hizo kwa kusulubiwa.
Mana katika ile bilauri iliyokuwa imewekwa ndani ya Sanduku la Ushuhuda ilikuwa ni mkate wa uzima kwa waisraeli walipokuwa nyikani, na katika kipindi cha Agano Jipya, maana yake ya kiroho ina maanisha juu ya mwili wa Yesu Kristo. Ukweli huu unatuonyesha sisi ubatizo ambao kwa huo Yesu Kristo aliyachukua makosa na uovu wa wenye dhambi wote na damu ambayo aliimwaga pale Msalabani. Kwa kuwa Yesu Kristo alichukua dhambi zote za ulimwengu huu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo na akaimwaga damu yake na kufa Msalabani, basi ubatizo wake na damu yake iliyomwagika vimefanyika kuwa vitu muhimu vya kudumu vinavyowawezesha waamini kuzaliwa tena upya.
Mwili ambao Yesu aliutoa ili kuyachukua maovu yote ya wenye dhambi kwa kupitia ubatizo wake na damu yake aliyoimwaga Msalabani ni mkate wa uzima unaowawezesha wenye dhambi kupokea ondoleo la dhambi. Kwa hiyo ni lazima tutambue sababu ambayo ilimfanya Yesu kusema, “msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (Yohana 6:53).
 

Nani ni Mkuu?
 
Tunapoangalia Yohana 6, tunaweza kuona kuwa Wayahudi walio wengi wa wakati huo walimfikiria Musa kuwa ni mkuu kuliko Yesu. Wakati Yesu alipokuja hapa duniani, walimuuliza, “Je, wewe u mkuu kuliko baba yetu Musa?” Kwa kweli, walimwona Musa ni mkuu kuliko wote. Kwa kuwa Wayahudi walishindwa kumtambua Yesu kuwa ni Masihi, walimuona yeye kuwa ni mtu wa kawaida. Kwa hiyo walimpa changamoto kwa kumuuliza, “Je, wewe u mkuu kuliko Musa?” Watu wa Israeli waliamini katika Mungu Yehova, na katika kipindi hicho akatokea kijana wa miaka 30 na kudai kuwa, “pamoja na kuwa baba zenu walikula mana wakafa, wale watakaoula mkate niutoao hawatakufa.” Hii ndiyo sababu iliwafanya waanze kulinganisha nguvu za watu hawa wawili Musa na Yesu.
Kama Yesu alivyosema baadaye, “Kabla Ibrahimu hajakuwako, mimi nipo,” Yesu ni mkuu kuliko mwanadamu yeyote katika historia nzima ya mwanadamu, kwa kuwa yeye ni Muumbaji mwenyewe. Je, inawezekanaje basi kwa viumbe wa kawaida kudiriki kumpa changamoto muumba wao? Hata hivyo, baadhi bado wanasema kuwa Yesu ni mwalimu mkuu, na kwamba ni miongoni mwa wenye hekima wakuu katika historia ya mwanadamu. Huko ni kudhihaki, Yesu ni Mungu, Mfalme wa wafalme, na muumbaji wa ulimwengu wote. Yeye ni Mungu aliye mahali pote ana anayejua vyote. Hata hivyo Yesu alijinyenyekeza akaja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu ili kukuokoa wewe na mimi toka katika dhambi zetu zote na kifo, na ili afanyike kuwa Mwokozi wetu wa kweli.
Yesu Kristo alisema, “Imeandikwa katika manabii, ‘wote watafundishwa na Mungu.’ Hivyo kila mtu aliyesikia na kujifunza toka kwa Baba atakuja kwangu. Hakuna hata mmoja aliyemwona Baba, bali Yeye atokaye kwa Mungu.” Mwishoni, Yesu alikuwa akisema kwa hakika kuwa yeye ni Kristo ambaye Wayahudi wamekuwa wakimngojea. Lakini walishindwa kufahamu kile ambacho Yesu alikuwa akikisema, hawakuweza kuamini wala kuyapokea, na hali hii ilipelekea katika kutokuelewana kwa kuwa walianza kushangaa, “Wawezaje kutupa sisi mwili wako tuule? Je, unamaanisha kuwa sisi tutaupata uzima wa milele ikiwa kweli tutaula mwili wako na kuinywa damu yako? Je, unafikiria kuwa sisi ni aina fulani ya wala watu?”
Lakini wale wanaoula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake wataishi milele. Mwili wa Yesu ni mkate wa uzima. Mwili na damu ya Yesu Kristo ni vitu halisi vya mana vilivyokuwa vimewekwa katika bilauri hii. Yesu ametuwezesha sisi kuula mkate wa uzima na kupokea uzima wa milele kwa kuja hapa duniani na kuutoa mwili na damu yake.
Je, inawezekanaje basi kwa kila mtu kuula mwili na kuinywa damu ya Yesu? Njia pekee ya kuweza kuula mwili wa Yesu na kuinywa yake ni kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani. Ni lazima tuule mwili wa Yesu na kuinywa damu yake kwa imani. Ili kutupatia wewe na mimi ondoleo la dhambi na kutuwezesha kuishi milele katika Ufalme wa Mbinguni, Bwana wetu amezitoweshea mbali dhambi zetu mara moja na kwa ajili ya wote kwa kubatizwa na kwa kuimwaga damu yake, na kwa hiyo amefanyika kuwa ni chakula cha nafsi zetu. Sasa, kwa kuamini katika Neno la Mungu la maji na Roho, ni lazima tule chakula hiki cha kiroho na kupokea uzima wa milele.
Hebu naomba nitoe ushuhuda kwa kina jinsi ambavyo tunaweza kuula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake. Kama ambavyo wewe na mimi tunafahamu vizuri, Yesu Kristo alikuja hapa duniani na akazichukua dhambi zote za mwanadamu kwa kubatizwa na Yohana alipokuwa na miaka 30, kisha akabeba adhabu ya dhambi zetu zote kwa kuimwaga damu yake Msalabani. Ni kwa kuamini katika ukweli huu halisi ndipo tunapoweza kuula mwili wake na damu yake. Kuoshwa kwa dhambi kulitimizwa pale ambapo dhambi za mwanadamu zilipopitishwa katika mwili wa Yesu kwa kupitia ubatizo ambao aliupokea. Kuinywa damu yake kunamaanisha kuwa Yesu alibatizwa na kuimwaga damu yake Msalabani, damu hii aliyoimwaga ilibeba adhabu ya dhambi zetu.
Kwa hiyo, wale wanaoamini katika damu ya Yesu katika mioyo yao basi kiu yao itazimishwa, kwa kuwa adhabu ya dhambi zao zote zilikwisha kabisa kwa ile adhabu ya Msalabani ambayo Yesu aliibeba. Ni lazima tuutambue ukweli huu. Na ni lazima tuuamini ukweli huo. Kwa kuwa Yesu Kristo alikuja hapa duniani na akazichukua dhambi zetu kwa kubatizwa na Yohana, basi kwa kuamini katika ukweli huu sisi tumesafishwa dhambi zetu zote mara moja na kwa ajili ya wote.
Mungu anatueleza sisi kuula mwili na damu ya Yesu kwa imani. Kwa kuwa Yesu alizichukua dhambi zote kwa kupitia ubatizo alioupokea toka kwa Yohana pasipo kuacha dhambi ya mtu yeyote, na kwa kuwa Yesu aliutoa mwili wake katika adhabu ya Msalaba na kisha akaimwaga damu yake ya thamani, basi mioyo ya wale wanaoamini ipo safi na haina kiu, kwa kuwa wamezioshelea mbali dhambi zao zote na kuibeba adhabu yote ya dhambi kwa imani. Hii ndiyo sababu Yesu alisema, “Mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli” (Yohana 6:55).
Hakika nawaambieni, huyu Yesu ni Mwokozi wa kweli, Mwana wa Mungu ambaye amezioshelea mbali dhambi zetu na amebeba adhabu ya dhambi zetu. Ili kutuokoa sisi toka katika sheria iliyotangaza kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, na ili kutuosha sisi toka katika dhambi zetu zote, na ili kutuokoa toka katika adhabu yetu yote, basi huyu Mwokozi na Mwana wa Mungu, aliutoa mwili wake Msalabani, akaimwaga damu yake, na kwa hiyo ameisafisha mioyo ya wale wanaoamini na ameziondoa kiu zao. Haya ni matokeo ya mwili na damu ya Yesu.
Yesu ni Mwokozi aliyezishughulikia dhambi na adhabu ya dhambi ya mwanadamu. Yesu ni Mwokozi aliyezipokea dhambi za mwanadamu kwa kupitia ubatizo wake alioupokea, ambaye alisulubiwa na kuimwaga damu yake ili kubeba adhabu ya dhambi hizi. Kwa kuwa Yesu alizipokea dhambi za ulimwengu zilizopitishwa kwake toka kwetu na ambazo alizibeba kwa kusulubiwa kwake, basi ndio maana adhabu aliyoibeba iliweza kuwa ni adhabu kwa ajili ya dhambi zetu binafsi.
Ni kwa kuamini katika ukweli wa maji na Roho ndipo tunapoweza kupokea ondoleo la dhambi. Ninyi nyote ni lazima muamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake aliyoimwaga kuwa ni ondoleo binafsi la dhambi zenu. Ni kwa kuamini katika injili hii ya kweli ndipo tunapoweza kuula mwili na kuinywa damu ya Yesu kiroho. Kwa maneno mengine, ni kwa kuamini kuwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake, kisha akabeba adhabu ya dhambi hizi juu ya Msalaba ili kwamba tuweze kufanyika wale tunaoweza kuula mwili wake na kuinywa damu yake, na kisha kupokea uzima wa milele. Kwa kuamini katika ubatizo na damu ya Yesu aliyoimwaga, sasa tunaweza kuula mwili wake na kuinywa damu yake. Sisi tunaweza kuondolewa dhambi zetu zote kwa kuula ubatizo wa Yesu na damu yake aliyoimwaga Msalabani. Ni kwa kupitia imani hii ndio maana tumeweza kupokea ondoleo la dhambi zetu, kufanyika wana wa Mungu, na kuishi milele katika Ufalme wa Mungu.
 

Fimbo ya Haruni Iliyochipuka
 
Miongoni mwa vitu vilivyowekwa ndani ya Sanduku la Ushuhuda, fimbo ya Haruni iliyochipuka ina maanisha juu ya Yesu Kristo kuwa ni Kuhani Mkuu wa milele wa Ufalme wa Mbinguni. Pia inatueleza sisi kuwa uzima wa milele unapatikana katika Yesu Kristo. Ili kuuwezesha ufahamu wetu wa jambo hili, hebu tugeukie Hesabu 16:1-2: “Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni. Nao pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele za Musa.” 
Kifungu hiki kinatueleza sisi kuwa miongoni mwa Walawi, viongozi mashuhuri 250 wa watu walijikusanya na kuinuka dhidi ya Musa. Wakamwambia, “Musa na Haruni mmetufanyia nini kwa kutuongoza sisi toka katika nchi ya Misri? Je, mmetupatia mizabibu? Je, mmetuongoza sisi katika vyanzo vya maji ya jangwani? Mmetufanyia nini? Je, hamkutuleta sisi huku nyikani ili hatimaye tufe katika jangwa la mchanga? Je, mwawezaje kujiita ninyi wenyewe kuwa ni watumishi wa Mungu? Je, Mungu anatenda kazi kwa kupitia ninyi tu?” Kwa maneno mengine, kulikuwa kumeinuka upinzani na uasi dhidi ya uongozi wa Musa na Haruni.
Kwa wakati huo, Mungu akamwambia Kora, Dathani, Oni, na viongozi wengine wa watu waliokuwa wameongoza uasi, “Niletee fimbo kutoka katika kila nyumba ya baba na andika kila jina la mtu wa nyumba hiyo katika fimbo hiyo. Kisha ziweke hizo fimbo katika Hema Takatifu la Kukutania. Ziache pale kwa usiku mmoja na kisha uje kuziangalia siku inayofuata.” Kisha Mungu akasema, “Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manungu’uniko ya wana wa Israeli, wanung’unikiayo juu yenu” (Hesabu 17:5). Katika aya ya 8, tunaona kuwa “Ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa milozi mabivu.”
Kisha katika aya ya 10, tunaona kuwa, “Kisha BWANA akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung’uniko yao waliyoninung’unikia, ili wasife.” Hivi ndivyo ambavyo fimbo ya Haruni iliyochipuka ilivyokuja kuwekwa ndani ya Sanduku la Ushuhuda.
Hii inaonyesha kuwa Haruni wa ukoo wa Lawi alipakwa mafuta kuwa Kuhani Mkuu wa watu wa Israeli. Musa alikuwa ni nabii wa Mungu na Lawi pamoja na ukoo wake walikuwa ni Makuhani Wakuu wa watu wa Israeli. Mungu mwenyewe alikuwa amewakabidhi majukumu ya Kuhani Mkuu wa kidunia kwa Haruni. Mungu alikuwa amemwonyesha Musa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, ambapo watu wa Israeli walileta sadaka ya kuteketezwa na kumtolea Mungu kila walipofanya dhambi, na Mungu alimfanya Haruni kusimamia utoaji wa sadaka hizi kwa mujibu wa kanuni za utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa. 
Hata pale ambapo Mungu alikuwa ameyakabidhisha majukumu yote ya kikuhani kwa Kuhani Mkuu Haruni, bado kulikuwa na watu waliomletea changamoto dhidi ya ukuhani wake, na hii ndiyo sababu Mungu aliifanya fimbo ya Musa kuchipuka ili kuthibitisha kuwa ukuhani wake ulitoka kwa Mungu. Kisha Mungu aliwafanya watu wa Israeli kuitunza fimbo hii ndani ya Sanduku la Ushuhuda ili kuwa ukumbusho wa fundisho hili. Na hii ndio sababu mbao mbili za mawe zilizokuwa na sheria, bilauri ya dhahabu iliyokuwa na manna, na fimbo ya Haruni iliyochipuka viliwekwa vyote ndani ya Sanduku la Ushuhuda. Je, vitu hivi vitatu vinamaanisha nini kiroho? Vitu hivi vinamaanisha juu ya huduma za Yesu Kristo Mwokozi wetu. 
 


Je, Ni Huduma Gani Ambazo Yesu Alizitimiza Ili Kuzitoweshea Mbali Dhambi Zetu Zote?

 
Kwanza, Yesu aliitimiza huduma ya Nabii. Yeye ni Alfa na Omega. Yeye anaufahamu mwanzo na mwisho, na ametufundisha sisi mambo yote kuhusu mwanzo na mwisho. Bwana wetu alifahamu kile ambacho kitatokea kwa mwanadamu, kwako wewe na mimi ikiwa tungelibakia ni wenye dhambi. 
Pili, Yesu amefanyika kuwa ni Kuhani Mkuu wa milele wa Ufalme wa Mbinguni. Yesu alikuja hapa duniani kwa sababu alitaka kutuokoa sisi toka katika dhambi kwa yenye mwenyewe kufanyika Mwokozi wetu na kwa kufanyika kikamilifu Kuhani wetu Mkuu wa kweli wa Ufalme wa Mbinguni. 
Tatu, Yesu Kristo ni Mfalme wetu. Biblia inatangaza kuwa, “Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.” (Ufunuo 19:16). Yeye ni Muumbaji halisi wa ulimwengu wote na kwa hiyo ana mamlaka ya kutawala juu ya kila kitu. 
Sisi sote ni lazima tutambue kuwa Yesu Kristo, ambaye ni Mfalme wa kweli, Nabii ambaye ametufundisha ukweli wa wokovu wetu toka katika dhambi, na Kuhani Mkuu wa milele wa Mbinguni, sasa amefanyika kuwa Mwokozi wetu wa kweli. 
Bwana wetu ametukomboa wewe na mimi toka katika dhambi, ametufanya kuwa watu wa Mungu, ametufanya kuwa watoto wake na watenda kazi wake, na ametuwezesha kuzitenda kazi njema. Yesu amezifanya nafsi zetu kuzaliwa tena upya ili kwamba tuweze kuishi maisha mapya hata hapa duniani, na pia ametupatia maisha mapya ili kwamba wakati ukifika Yesu aweze kuifufua miili yetu na kuishi milele pamoja naye huko Mbinguni. Je, Yesu Kristo ni kwa ajili yako na mimi? Yesu Kristo ni Mwokozi wetu wa kweli. Na Yesu Kristo ni Nabii wetu, Kuhani wetu Mkuu wa milele na Mfalme. 
Pamoja na kuwa hatupendi kuyadharau mapenzi ya Mungu, sisi tuna mapungufu mengi na udhaifu kiasi kuwa hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea kufanya dhambi wakati wote. Ikiwa tutaendelea kuishi kama hivi, kufa kama hivi na kisha kwenda kusimama mbele za Mungu, je, unafikiria kuwa ni mahali gani ambapo patakuwa ni pazuri kwa sisi kupaendea? Je, itakuwa ni kuzimu au Mbinguni? Ikiwa sisi sote tungehukumiwa kwa mujibu wa Sheria inayosema kuwa, “Mshahara wa dhambi ni mauti,” Je, sisi sote si tungeangamizwa? Yeye aliyewaokoa watu wa jinsi hiyo kama sisi toka katika dhambi na uharibifu na kufanyika Mwokozi wetu ni Yesu Kristo. Yeye mwenyewe alikuja hapa duniani, alitupenda sisi, na amefanyika kuwa Mwokozi ambaye ametukomboa toka katika dhambi, na hivyo amefanyika kuwa Mchungaji Mkuu wa kundi lake. 
Yohana 3:16 inasema, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanae pekee, ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.” Mungu alikupenda sana wewe na mimi kiasi kwamba alikuja hapa duniani kwa ajili yetu, alibatizwa ili kuzichukua dhambi za ulimwengu katika mwili wake, alisulubiwa na kufa Msalabani, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo amefanyika kuwa Mwokozu wetu wa kweli. Kwa hiyo Kwa kuamini katika Yesu Kristo ambaye amefanyika kuwa Mwokozi wa mioyo yetu, sisi tumefanyika kuwa wale waliosafishwa toka katika dhambi, wale waliopokea karama ya ondoleo la dhambi ambalo limetuwezesha sisi kufanyika wana wa Mungu na kuupata uzima wa milele.
Kuna kitu kimoja ambacho ni lazima tuhakikishe kuwa tunakiamini mbele za Mungu. Na kitu hicho ni kuwa kwa sababu Mungu alitupenda sana sisi, na ili kuzitoweshea mbali dhambi zetu Mungu alikuja hapa duniani akafanyika katika mwili wa mwanadamu, alibatizwa, akafa Msalabani, akafufuka toka kwa wafu, na kwa hiyo amefanyika kuwa Mwokozi wetu wa kweli. Ni kwa kuula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake kwa imani katika mioyo yetu ndipo uzima wa milele unapoweza kuongezwa ndani yetu. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kinachoweza kuwa cha wazi kuliko ukweli huu, basi sisi hatuna la kufanya zaidi ya kuukubali ukweli huu na kuuamini.
Ni lazima tuule mwili wa Yesu na kuinywa damu yake kwa imani. Na kila mtu anaweza kuwa na imani hii moja inayotambua na kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotimizwa na Yesu kama ilivyo. Kuna nini basi tunachapaswa kukifanya zaidi ya kuamini? Hatuwezi kufanya kitu chochote kile zaidi ya kujikuta tukisimama kinyume na Mungu. Mara nyingi tunafanya haraka kutomtii Mungu na kutenda dhambi. Lakini Mungu bado amekuokoa wewe na mimi toka katika dhambi zetu zote mara moja na kwa ajili ya wote kwa kuwa anatupenda sisi sote.
 

Je, Mungu Alizungumzia Vipi Juu ya Wokovu Wake Katika Kipindi cha Agano la Kale?
 
Je, ni kwa njia ipi ambayo kwa hiyo Mungu ametuokoa, je, Bwana ametuokoa sisi? Katika Agano la Kale, Mungu alizungumzia juu ya wokovu huu kwa kupitia rangi zilizodhihirishwa katika mlango wa Hema Takatifu la Kukutania na katika lile vazi lililovaliwa na Kuhani Mkuu. Nyuzi za rangi ya bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilizodhihirishwa katika mlango wa Hema Takatifu la Kukutania ni ufunuo unaoonyesha sisi wokovu wake mkamilifu. Pia dhahabu iliongezwa katika mavazi ya Kuhani Mkuu. 
Nyuzi za bluu zinatuambia sisi kuwa Yesu Kristo alikuja hapa duniani kama Mwokozi wetu na akazichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kubatizwa. Nyuzi za zambarau zinatueleza sisi kuwa Yesu Kristo ni Mfalme wa wafalme na Mungu muumbaji aliyeufanya ulimwengu wote. Nyuzi nyekundu zinatueleza kuwa kwa sababu Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake, basi alizibeba dhambi za ulimwengu na akaadhibiwa kwa sababu ya dhambi hizo Msalabani kwa kuimwaga damu yake na kufa na kwa hiyo ametupatia wokovu ambao umetukomboa toka katika adhabu ya dhambi zetu zote. 
Kitani safi ya kusokotwa inamaanisha juu ya Neno pana na la kina la Agano la Kale na Agano Jipya ambalo linatueleza sisi kuwa Bwana wetu alikuja hapa duniani, alibatizwa, alikufa Msalabani, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo amezitoweshea mbali dhambi za wale wanaoamini kwa kweli, amezisafisha roho zao na kuwa nyeupe kama theluji, na amewaokoa. Nyuzi za dhahabu zinamaanisha juu ya imani inayoamini katika katika yale ambayo Yesu Kristo ameyafanya kwa ajili yetu. Hii ndiyo sababu uzi wa dhahabu unang’aa. Wewe na mimi hatuna kitu cha kujivunia, lakini pale tunapoamini kwa mioyo yetu yote juu ya yale ambayo Yesu Kristo, Mungu mwenyewe na Mwana wa Mungu amefanya kwa ajili yetu. Basi kwa kweli tunaweza kuvikwa katika upendo wa Mungu, na kupokea baraka zake, na kufurahishwa naye kwa kuwa na imani katika matendo ya haki ambayo Mungu ameyafanya. Hivi ndivyo Mungu anavyotuambia sisi kwa kupitia Hema Takatifu la Kukutania. 
Ni lazima tutambue lile ambalo Mungu anatueleza sisi kwa kupitia Sanduku la Ushuhuda ambalo liliwekwa ndani ya Hema Takatifu la Kukutania. Ni lazima tufahamu na kuamini kuwa Yesu Kristo alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi za mwanadamu na dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana Mbatizaji, alibeba hukumu na adhabu ya dhambi kwa kufa Msalabani, na kisha akafufuka toka kwa wafu ili kuishi tena. Kwa kupitia Sanduku la Ushuhuda, Mungu analifanya Sanduku hili kudhihirisha kuwa ni lazima tuamini kwa kweli katika Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wetu na Mungu wetu. Wale wanaoamini katika ubatizo wa Yesu kuwa unazichukua dhambi zao, na wale wanaoamini katika damu ya Yesu iliyomwagika kuwa ni adhabu kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, wale wanaoamini katika kifo cha Yesu Kristo kuwa ni kifo chao wenyewe, wale wanaoamini katika ufufuo wa Yesu kuwa ni ufufuo wao, basi hawa ndio wale ambao Mungu amewaokoa. 
Kwa hiyo, Je, hili Hema Takatifu la Kukutania linamwelezea nani? Linamwelezea Yesu Kristo. Linatuelezea juu ya mbinu ya wokovu ambayo kwa hiyo Yesu Kristo amekuokoa wewe na mimi toka katika dhambi zetu. Katika Agano Jipya, ni Yesu Kristo ambaye ndiye aliyebatizwa na kufa Msalabani, na kwa hiyo amezitoweshea mbali dhambi zetu zote, amezioshelea mbali dhambi hizo, aliadhibiwa kwa sababu ya maovu yetu yote na kutuokoa toka katika dhambi zetu mara moja na kwa ajili ya wote. 
Katika Agano la Kale, ni kule kutoa sadaka ya kuteketezwa ambako ndiko kulikowaokoa wenye dhambi kwa kumfanya mwanasadaka kuzipokea dhambi zao kwa kuwekewa mikono juu ya kichwa chake, na kuimwaga damu yake na kufa. Agano la Kale linakielezea kifo cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa ambaye alizichukua dhambi za hawa wenye dhambi kwa kuwekewa mikono na kisha kufa kwa niaba yao kuwa ni kifo cha upatanisho. Utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ya upatanisho iliyodhihirishwa katika Agano la Kale, inapolinganishwa na Agano Jipya, inaonyesha juu ya Yesu Kristo ambaye ni mkamilishaji wa injili ya maji na Roho aliyekuja kwa ubatizo na damu. 
Ni nani basi ambaye aliiunda na kuipanga hii sheria ya wokovu? Mungu Mwokozi wetu aliipanga sheria hiyo. Mungu alianzisha sheria ya wokovu ambayo inawaokoa wenye dhambi toka katika dhambi, na Mungu ametupatia sheria hiyo kwetu sisi. Katika Sanduku la Ushuhuda kulikuwa na mbao mbili za Sheria, bilauri ya mana, na fimbo ya Haruni iliyochipuka, vitu hivi vyote vinatueleza sisi kuhusu sifa na huduma za Yesu Kristo. 
Fimbo ya Haruni iliyochipuka inatueleza sisi kuwa Mungu anatuokoa sisi tunapoamini katika Yesu Kristo ambaye kiroho amefanyika kuwa Kuhani Mkuu wa Ufalme wa Mbinguni na Mchungaji wetu Mkuu. Bilauri ya mana inatueleza sisi juu ya mwili na damu ya Yesu Kristo ambaye amefanyika kuwa mkate wetu wa uzima. Pia mbao mbili za mawe zenye Sheria zinatueleza sisi kuwa Mungu ni muundaji wa Sheria. Sheria zilizoanzishwa na Mungu ni sheria ya kifo na sheria ya ondoleo la dhambi na wokovu. Kama Mungu wetu, Yesu ameanzisha sheria ya uzima na sheria ya adhabu kwetu sisi. 
Vivyo hivyo, Sanduku la Ushuhuda na kila kitu kilichomo ndani yake vyote vinatuelezea sisi kuhusu Yesu Kristo. Ni kwa kuamini katika Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wetu ndipo tunapoweza kusafishwa toka katika dhambi zetu zote na kupokea wokovu wetu. Haijalishi ni kwa kiasi gani tunaweza kuwa na mapungufu na udhaifu, kama tutakubali na kuzifuata sheria hizi mbili ambazo Yesu Kristo amezianzisha, basi tunaweza kuwa ni wenye dhambi mara moja, na kisha kufanyika wenye haki kwa kupokea ondoleo la dhambi zetu zote mara moja na hivyo kufanyika watu wa Mungu. Je, unaamini? 
Sasa, kwa wakati huu uliopo, karibu Wakristo wote ulimwenguni kote wanavutwa kuamini katika Yesu kwa utupu, kwa kuwa hawaufahamu ukweli uliodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania. Wao wanaamini kuwa wanaweza kupokea ondoleo la dhambi kwa kuamini katika damu ya Yesu Msalabani tu. Kwa maneno mengine, wanaamini kuwa Yesu amewaokoa wao kwa damu ya Msalaba tu. Lakini ni kweli kuwa Yesu alikufa Msalabani kwa ajili ya wokovu wetu? Je, ni hilo tu ndilo alilolifanya kwa ajili ya ukombozi wetu? Je, kinyume na hapo juu, Yesu hakuzichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake mara moja na kwa ajili ya wote kwa kubatizwa na Yohana (Mathayo 3:13-15, 1 Petro 3:21, 1 Yohana 5:6)? 
Pamoja na hayo bado Wakristo wa leo wanaamini katika damu ya Yesu tu Msalabani, na kwa hiyo wanapokea ondoleo la dhambi lililo nusu. Baada ya kuwa wameondolewa dhambi zao za asili kwa kuamini katika Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao, basi wanaendelea kutoa sala zao za toba kila siku wakijaribu kuziosha dhambi zao halisi za kila siku kwa jitihada zao binafsi. Kwa kweli wokovu wa jinsi hii ni wa kuchanganya sana? Ni kama vile kuziosha nusu ya dhambi zao kwa imani, na kisha kujaribu kuziosha dhambi zilizosalia kwa kupitia jitihada zao binafsi. 
Hali inapokuwa kama hivi, ninawezaje basi kutofanya lolote zaidi ya kuendelea kuhubiri tena kwa kurudia hali nikiuleta ubatizo na damu ya Yesu pamoja? Hadi sasa, Wakristo wengi wa ulimwengu huu, mbali na Wakristo wa Kanisa la Mwanzo, wamekuwa wakiamini katika wokovu-nusu. Je, hii si ndio sababu inayowafanya watu wauamini Ukristo kana kwamba ni sawa na dini nyingine za kidunia? 
Si zamani sana, kulikuwa na mwanamke aliyeitwa Valeria Jones kutoka Marekani alipokea ondoleo la dhambi baada ya kusoma mfululizo wa kitabu cha kwanza juu ya Hema Takatifu la Kukutania. Kabla hajasoma kitabu hiki alikuwa amekwishasoma machapisho yetu kadhaa. Pamoja na kuwa alikuwa akikubaliana na yale ambayo vitabu vyetu vilikuwa vikiyasema, bado hakuweza kufikia katika ile hatua ya kuwa na hakika kabisa juu ya injili ya maji na Roho. Alitueleza kuwa bado ana mashaka fulani, akishangaa, “Hii inaonekana kuwa sahihi, sasa inawezekanaje basi watu wengi hawauhubiri ukweli huu?” Lakini alikiri kuwa alipomaliza kusoma toleo la kwanza la mfululizo wa Hema Takatifu la Kukutania, alifikia kuwa na imani sahihi ya wokovu akiamini kuwa injili ya maji na Roho ni sahihi, na kwamba ndio ukweli halisi uliodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania. 
Msomaji wa kitabu hicho hicho kutoka Benin alituandikia sisi kuwa, “Mtashangazwa sana kufahamu kuwa baada ya kupokea ondoleo la dhambi baada ya kukisoma kitabu chenu, sasa nimeliacha kanisa langu. Kwa nini nimeliacha kanisa ambalo nimekuwa nikihudhuria?” Ni kwa sababu walikuwa wakihubiri mafundisho ya utakaso unaoongezeka au unaojilimbikiza kitu ambacho hakifundishwi katika Biblia. Fundisho hili la utakatifu unaoongezeka au unaojilimbikiza kwa kweli ulikuwa si wa kibiblia kabisa. Kwa kuwa waliendelea kufundisha kuwa ni lazima na ninaweza kutakaswa wakati ukweli ni kuwa mwili wangu hauwezi kutakaswa, kwa kweli ilikuwa ni vigumu sana kwangu kuendelea kukaa kanisani na kusikia mahubiri ya jinsi hiyo. 
Ndio sababu niliamua kuondoka ndani ya kanisa hili na kujitenga nalo. Kwa kuwa nimepokea ondoleo la dhambi zangu kwa kukisoma kitabu chako, sina chaguo zaidi ya kuliacha lile kanisa ambalo nimekuwa nikihudhuria na kujitenga nalo. Kwa kuwa sisi ambao tumeyapitia haya yote sasa tumefanyika kuwa watu wa imani na tumejiunga na Kanisa la Mungu, watu wote wa ulimwengu huu wanaweza kubadilika pia ikiwa tu wataufahamu ukweli, kama Neno lisemavyo, ‘Nanyi mtaifahamu kweli na hiyo kweli itawaweka huru.’
Sanduku la Ushuhuda la Hema Takatifu la Kukutania pia linamdhihirisha Yesu Kristo. Sanduku la Ushuhuda liliwekwa katika mahali pa ndani kabisa pa Hema Takatifu la Kukutania. Mtu aliweza kuliona kwa kuinua kisitiri cha Hema Takatifu la Kukutania na kisha kuingia kwa kupitia hapo, na kisha kulifunua pazia la Patakatifu pa Patakatifu na kisha kuingia ndani yake. Kwa maneno mengine, Mlango wa Hema Takatifu la Kukutania ulikuwa upande wa mashariki na Sanduku liliwekwa mbali kabisa mwishoni mwa magharibi mwa Hema Takatifu la Kukutania.
 

Mihimili Haitaondolewa Toka Katika Sanduku
 
Kutoka 25:14-15 inasema, “Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.” Je aya hizi zina maanisha nini? Kwa kupitia aya hizi Mungu anatueleza sisi kuwa tunapaswa kuihudumia injili ya maji na Roho kwa kujitoa sisi wenyewe kwake. Injili inaenea pale tunapojitoa sisi wenyewe kwa kazi yake. Ili kumtumikia Bwana kwa kujitoa sisi wenyewe katika injili ni kwa kuifuata njia ya Msalaba ambayo Bwana wetu aliipitia kabla yetu. Ndio maana Yesu alisema kwa wanafunzi wake kuwa, “Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate” (Marko 8:34). 
Ili kuieneza injili katika ulimwengu mzima kunahitajika kujitoa kwa hali ya juu, pia kunahitaji kuvumilia mateso. Tunaweza kulifahamu jambo hili kwa kutazama jinsi ambavyo Mtume Paulo alivyoteseka kwa ajili ya injili ya maji na Roho: “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyanga’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote” (2 Wakorintho 11:23-28).
Hata hivyo, wale wanaojipenda wenyewe zaidi kuliko kumpenda Bwana aliyejitoa mwenyewe ili kuwakomboa wao toka katika adhabu zote hawawezi kujitoa mhanga kwa Ufalme wa Mungu. Hakuna njia rahisi ya kuihudumia injili ya maji na Roho. Inawezekanaje mkulima akategemea kupata mavuno mazuri pasipo kutoa jasho lolote? 
Vivyo hivyo, Sanduku la Ushuhuda ni lazima libebwe kwa sadaka zetu. Mfalme Daudi alijaribu wakati mmoja kulileta Sanduku katika tolori jipya lililokuwa likivutwa na ng’ombe badala ya watu wake kulibeba kwa kutumia mihimili yake kama ambavyo lilipaswa kubebwa. Walipokuwa njiani, ng’ombe walijikwaa na mtu mmoja aliyeita Uza aliunyoosha mkono wake kuelekea katika Sanduku la Mungu na kulidaka. Hasira ya Mungu iliwaka juu ya Uza na Mungu alimpiga pale kwa utisho wake. Kisha Uza akafa pale karibu na Sanduku la Mungu (2 Samweli 6:1-7). Kwa hiyo, Daudi, hali akiwa ameogopeshwa na jambo hili na kumwogopa Mungu siku ile, alilichukua Sanduku ndani ya nyumba ya nyumba ya Obed-Edom Mgiti. Ilikuwa ni kwa kulibeba kwa kutumia watu ndipo alipoweza kulileta sanduku lile katika mji wake baada ya miezi mitatu. Kama ambavyo masimulizi haya yanavyoelezea, ni lazima tulibebe Sanduku la Ushuhuda sawasawa kama Mungu alivyotueleza, kwa jasho na damu yetu, kwa sadaka zetu, kwa kujitoa kusikokoma kwa ajili ya injili yake. 
Wale ambao wamepokea kweli ondoleo la dhambi kwa shukrani kuu wana furaha sana kujitoa wao wenyewe kwa ajili ya Bwana ambaye alijitoa yeye mwenyewe kwa ajili yetu. Tunatoa shukrani zetu tena na tena kwa Bwana, Mwokozi wetu na Mungu. Tunamshukuru kwa kuturuhusu kuitumikia injili hapa duniani. 
Sisi sote tunashangazwa na kufurahishwa sana kwa ndoto hii yenye ukweli kwamba Bwana ametuchagua sisi ili kufanya sisi kuitumikia injili ya kweli, kufuata na kuishi aina ya maisha inayomfurahisha Mungu. Kule kuturuhusu kuufahamu ukweli wa wokovu kulitosha kabisa kutufanya tujazwe na furaha, pamoja na hayo Bwana ameturuhusu hata kuitumikia injili yake. Kufuatia baraka hizo kuu, inawezekanaje basi tusimshukuru Mungu? Tunatoa shukrani zetu zote kwa Mungu. Hii ndio sababu tupo tayari kujitoa sisi wenyewe kuieneza injili ya kweli bila kubakiza wakati, jitihada, au mali zetu kwa ajili ya jukumu hili takatifu la uinjilisti ulimwenguni. 
Kwa kweli kule kusema kuwa tumepokea ondoleo la dhambi ni kitu ambacho kinatufanya kuonyesha kuwa tuna shukrani nyingi sana. Lakini Mungu hajasimama katika jambo hili, lakini zaidi ya yote Mungu ametuwezesha kukutana na kuieneza injili ya ukweli, injili ya maji na Roho—kitu hiki ni nini? Ni baraka kubwa sana kwetu. 
Je, ni nani mwingine anayeweza kudiriki kuitumikia injili hii ya maji na Roho? Kwa kweli si kila mtu anaweza kuitumikia injili hii. Je, wanasiasa wanaweza kuitumikia injili hii? Mameya je? Maraisi je? Wafalme je? Haijalishi kuwa watu hao wana nafasi au vyeo gani katika jamii, ikiwa watu hao hawafahamu na hawaamini katika injili ya maji na Roho hawawezi kuitumikia injili ya kweli. Pamoja na hayo Mungu ametupatia fursa tusiyostahili na kwa kweli ametuwezesha sisi kuitumikia injili hii. Hii ni baraka kubwa sana. 
Ninamshukuru Mungu kwa neema ambayo imetuokoa, kwa kuwa Mungu alitupenda. Kaka na dada zangu, tunaamini kuwa Yesu Kristo ni Mungu na Mwokozi wetu. Sisi ni watu wa Mungu ambao tunaula mwili wa Yesu na damu yake kwa kupitia imani yetu ya kiroho. Biblia inasema kuwa Yesu si Mungu wa waliokufa, bali wa walio hai (Luka 20:38), na hawa walio hai si wengine bali ni wale waliopokea uzima wa milele kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Yeyote asiyeamini katika ukweli wa injili hii amekufa kiroho na yeyote anayeamini yupo hai kiroho. Kwa kweli Mungu ni Mungu wa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho. 
Kaka na dada zangu, Yesu mwenyewe ametupatia sisi ondoleo la dhambi kwa kupitia mwili wake na damu. Ni lazima utambue kuwa ikiwa huamini katika ukweli huu, basi hautakuwa na kitu chochote cha kufanya pamoja na Yesu. Yesu Kristo anakupatia wewe baraka za mbinguni, uzima wa milele, na ondoleo la dhambi zako. Ni nani ambaye amefanyika kuwa Mchungaji ambaye amekupatia wewe baraka za milele, anaye kuongoza na kukutunza? Ni Yesu Kristo Mkamilishaji wa injili ya maji na Roho. Yesu ndiye huyu Mungu. Ninaamini na kuomba kuwa kila mtu miongoni mwenu na wengine wote mtamwamini huyu Yesu kuwa ni Mungu wenu. 
Kwangu mimi, si kwamba ninaamini tu katika ukweli huu na kumtumikia Mungu sasa, bali nitaendelea daima kufanya hivyo hapo mbeleni. Lakini ni vipi kuhusu wewe? Je, unaamini katika injili ya maji na Roho? Na je unaamini kuwa ni lazima uishi na kukaa katika Kanisa la Mungu na upendo wa Kristo kwa imani yako? Hebu sote tuishi maisha yetu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho hadi siku ile tutakapoonana na Bwana wetu.