(Ufunuo 9:1-21)
Kati ya mapigo ya matarumbeta saba, tumekwisha lipitia pigo pigo la tarumbeta la tano na la sita katika kifungu hicho hapo juu. Tarumbeta la tano litapigwa na kuleta pigo la nzige, na tarumbeta la sita linatangaza vita katika Mto Frati.
Kitu cha kwanza tunachopaswa kukichunguza ni ikiwa watakatifu watayapitia mapigo ya matarumbeta saba ua la. Hiki ni kitu cha kwanza ambacho tunapaswa kukisikia na kukifahamu na kisha kuamini.
Je, watakatifu watajikuta katikati ya mapigo ya matarumbeta saba? Ni hakika kwamba watakatifu watajikuta katikati ya mapigo haya. Theluthi ya misitu ya dunia itaunguzwa, theluthi ya bahari na mito itageuzwa na kuwa damu, na kisha jua, mwezi, na nyota zitapigwa na kuipoteza theluthi ya nuru yake. Pamoja na kuwa theluthi ya mazingira na vitu vya kiasili vitageuka na kuwa damu au kupoteza nuru yake, hii inaonyesha kuwa sehemu ya dunia bado itabakia.
Neno linatueleza kwamba, sisi watakatifu ambao tumeokolewa, tutajikuta katikati ya mapigo sita ya kwanza ambayo yataharibu theluthi ya ulimwengu. Hata hivyo, hatuyaogopi mapigo haya, kwa sababu Mungu amewaamuru nzige kuwadhuru “wale tu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao”, katika pigo lake la tano, Mungu atawalinda watakatifu walitiwa muhuri yake katikati ya mapigo haya ya matarumbeta saba.
Hata hivyo, hii inaonyesha kwamba watakatifu watayapitia mapigo haya yote. Wewe na mimi, tukiwa ni miongoni mwa wale waliokombolewa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, tutajikuta katikati ya pigo la kwanza, ambalo litaunguza theluthi ya ulimwengu wote kwa moto utakaotelemshwa na Mungu, pia tutajikuta katikati ya pigo la pili, ambalo litageuza theluthi ya bahari na mito kuwa damu kwa anguko la mlima uwakao, pia tutajikuta katikati ya pigo la tatu ambalo litageuza theluthi ya mito na chemichemi kuwa pakanga kwa anguko la nyota kubwa toka angani.
Watakatifu tutaendelea kuwa hai hadi wakati wa pigo la nne, ambalo litaleta giza na kuipiga theluthi ya jua, mwezi, na nyota; pia tutaendelea katikati ya mateso hadi kwenye pigo la tano, ambapo nzige watawadhuru watu kwa nguvu kama za nge; pia tutajikuta tukiishi hadi wakati pigo la sita litakapoleta vita ya dunia katika Mto Frati, na kujikuta tukilipitia hili pigo lote. Hakuna mtu anayeweza kufanya lolote kuhusiana na mapigo haya, kwa sababu mapigo haya yanatokea kwa mujibu wa majaliwa ya Mungu. Kule kusema kwamba tutayapitia mapigo yote sita ya kutisha ni ukweli ulioandikwa katika Neno la Mungu.
Bwana wetu amekukomboa wewe toka katika dhambi zako zote. Bwana amezichukulia mbali dhambi zako zote kwa ubatizo wake, kwa damu yake Msalabani, na kwa kufufuka kwake toka kwa wafu. Tumepokeo upatanisho wetu wa dhambi kwa kuamini kile ambacho Yesu Kristo amekifanya kwa ajili yetu. Kwa wale waliopokea ondoleo la dhambi zao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, hata watakapokuwa wakiishi katikati ya mapigo sita ya kutisha, ulinzi maalumu wa Mungu utakuwa pamoja nao. Kwa maneno mengine, Neno la Mungu linatueleza kwamba neema maalumu ya Mungu itaturuhusu kuendelea kuishi. Tunapaswa kufahamu jinsi ilivyo stahiki kwa Mungu kupokea shukrani zetu zote kwa kutupatia neema na ulinzi maalumu katikati ya mapigo, hasa kwetu sisi tuliookolewa.
Wakati malaika wa tano alipolipiga tarumbeta lake, Yohana aliona “nyota ikianguka toka mbinguni hadi duniani,” naye “akapewa funguo wa shimo la kuzimu.” Nyota inayotajwa hapa ina maanisha ni malaika; maana ya kiroho ya nyota za Mungu; ina maanisha kuwa nyota hizo zote ni watumishi wa Mungu na watakatifu wake. Wakati malaika huyu alipoanguka duniani aliupokea ufunguo ya shimo la kuzimu na kisha akalifungua kwa ufunguo huo, moshi ukatoka katika lile shimo kama moshi wa tanuru kubwa.
“Shimo la Kuzimu” ina maanisha ni shimo lisilo na mwisho. Pia linajulikana kama Lindi-kuu, ni shimo lenye kina kisicho na mwisho. Wakati malaika wa tano alipolipiga tarumbeta lake, na baada ya kuipokea ile funguo ya shimo hili la kuzimu, alilifungua shimo hili kwa kutumia ufunguo huo. Baada ya kulifungua shimo hilo moshi mkubwa ulitoka ndani yake kama moshi wa moto mkubwa. Moshi huu toka katika lindi-kuu ulilifunika jua na anga, na kuufanya ulimwengu kuwa giza.
Moshi haukuwa kitu pekee kilichotoka katika hilo shimo la kuzimu; pia nzige walitoka katika shimo hilo lilipokuwa limefunguliwa. Hawa “nzige” waliopanda hadi duniani walipewa nguvu kama ile ya nge walioko duniani, wakawauma watu kwa mikia yao. Biblia inawaeleza nzige hao kama waliokuwa na sura kama za binadamu, na maumbile yao yalikuwa ni kama ya farasi aliyeandaliwa kwa vita, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba, na nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake.
Neno “nzige” lililotumika hapa linaonyesha lugha ya wingi, hii ndio maana Biblia inaonyesha kwamba kinachozungumziwa hapa ni nzige wengi na wala si wachache au nzige mmoja, bali ni wingu kubwa la nzige, kama wale nzige ambao huwa wanavamia maeneo ya kitropiki kwa nyakati mbalimbali, huku wakila mimea yote wanapopitia na kutobakiza kitu isipokuwa mizizi yake. Nzige wa jinsi hiyo watatoka katika lile shimo la kuzimu lisilo na mwisho na kuwatesa wanadamu kwa miezi mitano.
Wale watakaopigwa na pigo la tano kati ya mapigo ya matarumbeta saba ni wale tu ambao watakuwa hawajazaliwa tena upya. Pigo hili la nzige litawaruka wale waliozaliwa tena upya. Bwana wetu hatalileta pigo la nzige juu yetu, hii ni kwa sababu anafahamu wazi kwamba ikiwa waliozaliwa tena upya wangeliumwa na hao nzige, basi wangeliweza kuitema injili ya wokovu huku wakishangaa, “ni kwanini niliokolewa?” Tunaweza kulihakikisha hili katika aya ya 4: “Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu chochote kilicho kibichi, wala mti wowote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.”
Tunafahamu kwamba watu 114,000 wa Israeli watatiwa muhuri na Mungu, lakini Biblia haiwataji Wamataifa. Je, hii ina maanisha kwamba tutateswa na hao nzige kama watakavyoteswa wenye dhambi? Hapana kabisa! Kama vile Waisraeli 144,000 watakavyotiwa muhuri, vivyo hivyo na sisi pia—yaani, mioyo ya wale waliopokea ondoleo la dhambi zao wametiwa muhuri mbele za Mungu na Roho Mtakatifu. Je, hauna Roho Mtakatifu katika moyo wako? Kwa sababu wale ambao mioyo yao inakaliwa na Roho Mtakatifu ni dhahiri kwamba wametiwa muhuri kama watoto wa Mungu, hivyo, sisi pamoja na Waisraeli 144,000 tutalikwepa pigo la nzige tukiwa watu wake.
Kwa kuwa pigo la nzige litawadhuru wale ambao hawajazaliwa tena upya, basi ni hakika kwamba watu watatuchukia na pengine kututesa zaidi. Wakati wa kipindi cha miezi mitao ya pigo hili, ni wale tu ambao hawajazaliwa tena upya ndio watakao dungwa na nzige hawa, watateswa kwa maumivu makuu lakini hawataweza kufa. Sura za nzige hawa zinaonekana ni kama sura za wanadamu, na nywele zao ni kama nywele za wanawake, na meno yao yanatisha kama meno ya simba, na maumbo yao ni kama farasi walioandaliwa kwa vita, na wana mikia ya nge. Nzige hawa watamtisha kila mtu kwa vichwa vyao katika maeneo yote wanayopita, watawauma kwa meno yao, na watawadunga kwa mikia yao yenye sumu, na kwa sababu hiyo wataleta maumivu makubwa kwa wahanga.
Kitendo cha kudungwa mara moja kitaleta maumivu makubwa sana, pengine itakuwa ni sawasawa na kupigwa na umeme wenye kiwango kikubwa, na maumivu hayo yatadumu kwa miezi mitano. Hata hivyo, hata kama watakuwa wameteswa kiasi gani na hao nzige na kutamani kufa badala ya kuishi kwa mateso hayo, ukweli ni kwamba hawataweza kufa. Kwa kuwa pigo la kutokufa limejumuishwa katika pigo hili la nzige, basi kwa miezi hiyo mitano hakutakuwa na kifo chochote duniani. Pigo hili litautesa ulimwengu kwa miezi mitano.
Hatujawahi kuona mapigo kama hayo kwa macho yetu, lakini mapigo hayo yamepangwa na Mungu. Mungu anatueleza kwamba atayaleta mapigo haya hapa duniani, kwa watu wa ulimwengu huu—yaani, kwa wale wasiomwamini Mungu, na wasio fahamu upendo wake na wokovu, na wasio fahamu injili yake ya ukombozi. Mambo haya yote yamepangwa na Mungu. Kwa kuwa Mungu amepanga kufanya mambo haya yote, basi tunapaswa kuamini kwamba Mungu atayaleta mambo hayo yote.
Tunachoweza kukifanya sasa ni kumwamini Mungu, kwa kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kubishania kile ambacho Mungu amekipanga. Hata katika hali hii, ambapo watu watakuwa wakiteseka kwa nzige, Mungu hatawaruhusu nzige kutudunga na hivyo atatulinda dhidi ya pigo hili, kwa maana atawaamuru wasiwadunge wale wote walio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.
Kwa Nini Mungu Anayaleta Mapigo ya Matarumbeta Saba?
Dhumuni la Mungu la kuyaleta mapigo ya matarumbeta saba ni, kuwafanya wale waliozaliwa tena upya kupokea utukufu ndani ya mapigo hayo; na kwa wale ambao bado hawajazaliwa tena upya, ni kuwapatia nafasi nyingine ya kuzaliwa tena upya; na kwa kila mtu ambaye Mungu amemuumba katika ulimwengu huu, Mungu atalenga kuwaonyesha kwamba Bwana ndiye Mungu, na kwamba ndiye Muumba wa ulimwengu huu, Mwokozi na Hakimu wa wote.
Kwanza, Mungu anawafanya wenye haki kuusifu ukuu wa Bwana, neema yake na baraka na utukufu wake kwa kuleta mateso kwa wenye dhambi kupitia mapigo haya na kwa kuwaruhusu wenye haki kuyakwepa mapigo hayo.
Pili, Mungu anaruhusu mapigo yake kwa ajili ya mavuno yake ya mwisho. Mungu anayaleta mapigo ya matarumbeta saba ili kwa mara ya mwisho kuwaokoa wale ambao wameifahamu injili ya maji na Roho lakini hawakuiamini. Pia Mungu analenga kuwapatia wale wote aliowaumba, yaani Wamataifa na Waisraeli nafasi ya mwisho ili waweze kuokolewa na kumrudia Mungu wakati wa Dhiki.
Tatu, kwa kuwa hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea hapa ulimwenguni pasipo Bwana, Yesu Kristo—aliyekuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, akazichukua dhambi za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake, na akazisafishilia mbali dhambi hizo kwa kifo chake Msalabani—Bwana, kwa kupitia mapigo haya ya kutisha, atazionyesha nguvu zake kuu kwa wale wote ambao hawajaupokea upendo wake na upendo wa Baba yake, na wale ambao hawajaiamini injili ya wokovu. Kwa wale ambao hawajazaliwa tena upya, Bwana atawaletea mateso katika ulimwengu huu na atawaletea adhabu ya milele kuzimu.
Mungu anayaleta mapigo katika ulimwengu huu hali akiwa na madhumuni na mipango kama hiyo. Ni lazima tufahamu na kuamini kwa hakika kwamba mapigo haya yatakuja. Pamoja na kwamba tutaepushwa na pigo la nzige, ukweli ni kwamba tutayapitia mapigo haya yote. Sisi sote tutayapitia mapigo haya, pigo la moto ambalo litaunguza theluthi ya uoto wa asili na misitu ya ulimwengu, pigo la maji ambalo litabadili theluthi ya bahari kuwa damu na theluthi ya mito na chemichemi kuwa pakanga, pigo la giza ambalo litaleta giza kwenye jua, mwezi, na nyota, na pigo la vita ambalo litauangamiza ulimwengu—sisi sote tutakuwemo katikati ya mapigo haya. Lakini ni lazima tufahamu kwamba hata tutakapokuwa tukiyapitia mapigo hayo yote, tutakuwa tumejawa na furaha kuu.
Tutapoteza hamu yote ya kuishi kutokana na mapigo ya matarumbeta haya saba. Hebu tufikirie, kwa muda mfupi, kwamba volkano zinafumuka na kuwaka kila mahali, matetemeko ya ardhi yanaiharibu ardhi, milima inaungua kwa moto na kutoa moshi, na theluthi ya bahari, mito, na chemichemi imegeuka na kuwa damu na pakanga. Vumbi, moshi, na majivu yameifunika dunia; jua linachomoza saa 4 asubuhi na linazama saa 10 jioni; na mwezi na nyota zimepoteza nuru yake kiasi kwamba hatuwezi kuziona tena. Je, katika hali hiyo utafurahia kuishi maisha yako katika ulimwengu wa jinsi hiyo? Kwa kweli hapana!
Hii ni maana watakatifu watamwangalia Mungu na kuyaweka matumaini yao katika Ufalme wake na nyakati zake. Tumaini letu lote, kwa asilimia 100 linapatikana kwa Mungu tu. Hata kama tungelipewa utajiri wote wa ulimwengu huu na kisha kuishi ndani yake kwa miaka elfu moja, ni hakika kwamba hatutakuwa na hamu ya kuishi katika ulimwengu huu tena, wala hatutaweza kufanya hivyo. Kwa kuwa mapigo haya yote yamepangwa na kuruhusiwa na Mungu, hakuna hata mmoja anayeweza kuyasimamisha. Kwa kuwa Mungu ameyapanga mapigo haya, basi ataruhusu yatokee.
Kwa nini mapigo yaliyopangwa na Mungu yameandikwa katika Biblia? Kwa nini Mungu alimwinua Yohana na kumpeleka Mbinguni, na akamfanya aweze kusikia na kuyaona mapigo yote ambayo yatatokea kwa milio ya matarumbeta, na kisha akamfanya aweze kuandika kile alichokisikia na kukiona? Mungu alifanya hivyo ili kuonyesha kile ambacho kitatokea hapa ulimwenguni, na ili kuwafanya watakatifu waliweke tumaini lao katika Ufalme wa Mungu, na kuwafanya waihubiri injili katika dunia hii, na kumfanya kila mtu aweze kumwamini Yesu Kristo.
Mungu amepanga na ameruhusu mambo haya yote ili kwamba kwa kupitia mapigo haya, watu waweze kufikiri na kutoteseka katika ziwa la moto na kibiriti huko kuzimu. Kwa maneno mengine, Mungu amewapatia kimbilio ili kuyakwepa mapigo. Kwa kuwa Mungu hapendi yeyote kati yetu kuishia kuzimu, basi anataka mioyo ya wenye dhambi kumrudia kwa kupitia mapigo. Ninaamini kwamba Neno liliandikwa na kuonyeshwa kwetu ili kwamba kila mtu aweze kuongozwa kuelekea Mbinguni.
Kwa maneno mengine, mapigo ambayo Mungu anayaleta kwetu, hayalengi kutufanya tuteseke. Mungu anayaleta mapigo haya ulimwenguni na kwetu ili kwamba tusiliweke tumaini letu katika dunia hii bali katika Ufalme wa Mungu. Pia tunapaswa kutambua kwamba Mungu anaruhusu mambo haya yote ili kutufanya tuuhubiri upendo wake wa wokovu kwa nafsi nyingi zilizopotea na ambazo zimefungwa kuangukia katika moto wa milele wa kuzimu, ili kwamba nafsi hizo ziweze pia kuliamini Neno la wokovu, na kisha kuokolewa, na kuikwepa Dhiki hii.
Miongoni mwa mambo mengine, baadhi ya samaki aina ya kambale wanajulikana sana kwa maumivu ambayo wanaweza kusababisha mara wanapokudunga. Usipokuwa mwangalifu katika kuwakamata samaki hawa, mikono yako inaweza kudungwa na mapezi yenye sumu, na baada ya hapo maumivu makubwa yatafuatia, kana kwamba umepigwa na shoti ya umeme. Maumivu haya si kitu ukilinganisha na maumivu ya kudungwa na nzige.
Sasa, hebu fikiria kuwa na maumivu hayo kwa miezi mitano. Kwa kweli yatakuwa ni maumivu makubwa sana, hata watu watatamani kufa kuliko kuishi katika mateso hayo, lakini hawataweza kufa. Watu hawataweza kujiua, maana Neno linatueleza kwamba, “Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.” Lakini kwa kuwa tumefanyika kuwa wana wa Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, na kwa kuwa sasa tunaye Roho Mtakatifu ndani yetu, Mungu atatulinda na pigo hili ili kwamba tusiteseke na maumivu yatakayoletwa na hawa nzige. Tunalindwa katikati ya pigo kama hili kwa sababu tumepokea ondoleo la dhambi kwa kuamini katika injili ya maji na Roho.
Hatupaswi kukiangalia Kitabu cha Ufunuo kwa hofu peke yake, bali kwa kupitia Neno la Ufunuo, tunapaswa kutambua jinsi ambavyo Mungu atatupatia ulinzi wake maalumu toka katika mapigo hayo, na jinsi ambavyo Mungu atatukuzwa kupitia sisi, na jinsi ambavyo Mungu atatuvika utukufu wake. Kwa kuyafahamu mambo haya, ni hakika kwamba tutakuwa imara zaidi, tutaihubiri injili zaidi, na tutampatia Mungu utukufu zaidi wakati wa Dhiki utakapowadia. Hivyo, ni lazima tuishi katika kipindi hiki pasipo hofu katika mioyo yetu, wala pasipo kutamani maisha yetu hapa duniani. Mungu anatufundisha mambo haya yote mapema, ili kwamba tuwe na ujasiri. Hivyo, tunapaswa kuwa na imani yenye ujasiri.
Mungu anayapanga mapigo saba katika makundi mawili, mapigo manne ya kwanza na ole tatu za mwisho, na anaweka wazi kwamba kundi hili la mwisho litakuwa ni kuogofya na kutisha zaidi kwa kiwango na madhara. Hivyo, ndio maana mara baada ya kuisha kwa pigo la tano, Mungu anatangaza kwamba, “Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili, zinakuja baadaye.”
Ole wa pili ni pigo la tarumbeta la sita: “ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue hao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati. Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.” Katika aya ya 16, inasema hivi, “Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi.” Inaonyesha kwamba vita kubwa itatokea, na theluthi ya wanadamu wote watauawa na vita hii. Kwa maneno mengine, Mungu atalileta pigo la kutisha la vita katika dunia hii.
Aya ya 17-18 inasema, “Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoa moto na moshi na kiberiti. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao.” Mungu ataruhusu idadi kubwa ya watu kuuawa kwa jeshi kubwa la wapanda farasi. Hili ni pigo ambalo litakuja mara baada ya kupigwa kwa tarumbeta la sita.
Nini kitatokea mara baada ya kupigwa kwa tarumbeta la saba? Ufufuo na unyakuo vitatokea. Hadi kufikia tarumbeta la sita, mapigo yote yaliyotangulia yatakuja kama majanga ya asili au vita ambayo yataleta vifo kwa watu. Kwa kuwa haya yote yameandikwa na kujumuishwa katika mapigo ya matarumbeta saba katika Biblia, basi ndio maana ninaliamini Neno hili. Vipi kuhusu wewe? Je, unauamini ukweli huu?
Je, umepokea ondoleo la dhambi zako kwa kuamini katika injili ya maji na Roho? Pamoja na kuwa umejumuishwa katika mapigo haya, ili uweze kuyakwepa mateso ya pigo la milele na ili kwamba usiweze kuingia kuzimu, unapaswa kuiamini injili ya maji na Roho sasa, hii ni injili ambayo Mungu amekupatia ili kuzifanya dhambi zako kutoweka, ili kukuokoa toka katika Dhiki Kuu, na ili kukupatia Ufalme wa Mbinguni na Mbingu na Nchi Mpya. Unapaswa kuwa na imani inayoamini katika injili hii. Hakuna njia nyingine ya kwenda mbinguni za ya kuamini katika injili hii ya maji na Roho.
Yesu alimwambia Petro, “Nami nitakupatia funguo za ufalme wa mbinguni.” Funguo za Ufalme wa Mbinguni zinatolewa kwetu mara tunapomwamni Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wetu—na kwamba alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi za mwanadamu na dhambi za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji katika Mto Yordani, na kwamba alizibeba dhambi hizo zote na kisha kufa Msalabani, na kwamba alifufuka tena toka kwa wafu. Tunaweza kuingia Mbinguni na kisha kulindwa dhidi ya mapigo haya pale tu tunapokuwa na imani hii—yaani imani inayoamini kwamba dhambi zetu zote zimetoweshewa mbali.
Unyakuo na mauaji ya kufia-dini yanayoelezwa katika Ufunuo 13 vitafuata sambamba na kupigwa kwa tarumbeta la saba. Mpinga Kristo atakapoonekana hapo ndipo tutakapokabiliana na vifo vya haki, kuuawa na kuifia-dini kwa ajili ya injili.
Unapaswa kufahamu jinsi injili hii ilivyo ya thamani na kisha uiamini. Iamini injili hii ya maji na Roho. Hapo ndipo unapoweza kuzishinda nyakati za mwisho kwa ujasiri na kisha kuishi katika Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya iliyoahidiwa na Bwana. Ili kuweza kumwabudu Bwana kama mmoja wa wale wazee 24 wanaosimama kumzunguka Yesu Kristo, ambaye ni Mungu, basi ni hakika kwamba hakuna njia nyingine zaidi ya kuishinda Dhiki kwa kuamini katika injili ya maji na Roho.
Ninatumaini na kuomba kwamba, mkiwa kama watakatifu mliozaliwa tena upya kwa kuamini katika injili hii kwa mioyo yenu yote, basi mtaweza kuzishinda nyakati za mwisho na kisha kuurithi Ufalme wa Mungu wa Milenia na Ufalme wake wa Mbinguni wa Milele.