Search

คำสอน

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[22-1] Mbingu na Nchi Mpya, Ambapo Maji ya Uzima Yanatiririka (Ufunuo 22:1-21)

(Ufunuo 22:1-21)
“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele. Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake uwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki. Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nalianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo. Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu. Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia. Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho. Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya. Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi. Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure. Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki. Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu. Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.”
 
 
Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo.
Kifungu hiki kinaeleza kwamba Yohana alionyeshwa “mto safi wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri.” Neno maji linatumika katika ulimwengu huu kama chanzo cha uhai na uzima. Aya hii inatueleza kwamba maji haya ya uzima yanatiririka katika Mbingu na Nchi Mpya mahali ambako watakatifu wataishi milele. Hali ukitiririka toka katika kiti cha enzi cha Mwana-kondoo, mto wa maji ya uzima unaulowanisha Ufalme wa Mbinguni na uvifanya vitu vyote kuwa vipya. Na katika hii sentensi inayosema, “kiti cha enzi cha Mwana-Kondoo,” neno “Mwana-Kondoo” ina maanisha ni Yesu Kristo, ambaye amewaokoa wanadamu kwa injili ya maji na Roho wakati alipokuwa hapa duniani. 
Maji ya uzima yanatiririka katika Mbingu na Nchi Mpya ambayo Mungu amewapatia watakatifu. Kwa kuwa bustani hii ni safi na dhahiri kama vile rangi ya maji, basi ndio maana bustani hiyo inatajwa kuwa ni ya kushangaza. Maji ya uzima ambayo Mungu ametupatia si kama mto wa kawaida, bali ni maji ambayo yanatoa uzima kwa viumba hai vyote. Kwa hiyo, maisha yanachanua kwa kila kitu kitakachokutana na mto huu wa uzima. Watakatifu ambao wataishi pembezoni mwa mto huu wa maji ya uzima watakunywa maji haya, watafurahia uzima wa milele na kisha wataishi milele. 
Mto wa maji ya uzima unatiririka toka katika kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo. Watakatifu hawawezi kufanya lolote zaidi ya kuisifu neema ya Mungu na ile ya Mwana-Kondoo katika Ufalme mpya wa Mbinguni, kwa kuwa Mungu amewapa neema ya uzima. Ninashukuru sana kwa kuwa neema yote ya maisha mapya inatiririka toka katika kiti cha enzi cha Bwana. 
 
Aya ya 2: Katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. 
Kusanyiko la baraka za Bwana za kushangaza kwa watakatifu wake huko Mbinguni zinaendelea, kwa kuwa Neno linatueleza kwamba Bwana atatupatia mti wa uzima upande mmoja wapo wa mto na kisha ataturuhusu kula matunda ya mti huo wa uzima. Mti wa uzima, ambao unazaa aina kumi na mbili za matunda, unazaa matunda yake kila mwezi, na kwa sababu hiyo unaleta nguvu ya uzima mpya. Pia kifungu hiki kinaeleza kwamba majani ya mti huo ni dawa ya kuyatibu mataifa. 
Kwa kuwa neema ambayo Bwana amewapatia watakatifu wake ni kubwa mno, basi kile tunachoweza kukifanya ni kumsifu Bwana na Mungu Baba. Sasa, kitu ambacho watakatifu wanapaswa kukifanya si kujaribu kufanya kitu cha thamani kwa Bwana kwa jitihada zao binafsi, bali wanapaswa kumsifu Bwana kwa mioyo yao yenye shukrani kwa kuwapatia Mbingu na Nchi Mpya na maisha mapya. Ninamsifu Bwana kwa kuifanya mioyo ya watakatifu kuweza kushangilia kwa kusema “Asante Bwana! Helleluya!”
 
Aya ya 3: Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia. 
Mungu ametoa baraka ya kuiondoa laana milele kwa watakatifu wanaoishi katika Ufalme wa Mbinguni. Kule kusema kwamba kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kipo miongoni mwa watakatifu kinatuonyesha kwamba watakatifu wanaoishi katika Ufalme wa Mbinguni wamemweka Mwana-kondoo katikati ya mioyo yao. Hivyo, mioyo ya watakatifu imefurika kwa uzuri na ukweli, na maisha yao yamejawa na furaha. 
Kutokana na sentensi hii, “Na watumwa wake watamtumikia,” tunaona kwamba watakatifu wanaoishi katika Ufalme wa Mbinguni wamevikwa utukufu wa kumtumikia Bwana huku wakiwa karibu naye. Ufalme wa Mbinguni, mahali ambapo Bwana wetu anaishi, ni Ufalme mzuri na bora zaidi. 
Kwa hiyo, watumishi wake wanaomtumikia karibu na Bwana wanaweza kuufurahia utukufu wake kwa ukaribu. Hii inatueleza kwamba katika Ufalme wa Mbinguni, kutakuwepo pia na watumishi wa Bwana. Neno mtumishi ni neno linaloonyesha hali ya kuwa chini, lakini watumishi wanaoweza kumtumikia Bwana wetu mwenye utukufu hali wakiwa karibu naye ni wale waliobarikiwa sana katika Ufalme wa Mbinguni, kwa kuwa wamefunikwa katika fahari kuu isiyoweza kuelezeka. Wale waliofanyika kuwa watumishi wa Bwana katika Ufalme wa Mbinguni na katika dunia hii ni wale ambao watavikwa utukufu wote wa Mbinguni na hao ndio wenye furaha kuliko wengine wote. 
 
Aya ya 4: Nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. 
Je, watakatifu na watumishi wote wa Bwana ni mali ya nani? Ni mali ya Bwana. Wao ni watu wa Bwana na wana wa Mungu. Hivyo, wale wanaomtumikia Bwana katika Ufalme wa Mbinguni, jina la Bwana limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao. Bwana anawalinda na kuwabariki wakati wote, kwa kuwa wamefanyika kuwa watu wake. Kule kusema kwmaba watakatifu wamefanyika kuwa watu wake kuna maanisha kwamba wamevikwa moja ya fahari yenye furaha na utukufu zaidi. Wale wanaoona aibu kuwa watu wake na kuwa watumishi wa Bwana ndio wale wasioifahamu fahari yake, na kwa sababu hiyo hawawezi kamwe kuwa wenyeji wa Mbinguni. 
Jina la Bwana limeandikwa katika vipaji vya nyuso za watakatifu wanaoishi Mbinguni. Hii ni baraka iliyotolewa na Bwana. Kuanzia sasa na kuendelea, watakatifu wamefanyika kuwa watu wake. Kwa hiyo, hata Shetani hawezi kuwadhuru watakatifu ambao wamefanyika kuwa watu wa Bwana. Watakatifu pamoja na Bwana wataishi milele katika fahari yote ya Mbinguni. Kule kusema kwamba watakatifu watauona uso wa Bwana wenye utukufu kila siku maana yake ni kwamba wataishi katika upendo wa Bwana na baraka zake za ajabu milele na milele. 
Kuna kitu kimoja ambacho watakatifu wanapaswa kukifahamu: Sambamba na Bwana Yesu, Mungu Baba na Roho Mtakatifu watakuwa pamoja nao kama familia. Hatupaswi kusahau kwamba katika Ufalme wa Mbinguni, Mungu Baba, Mwanae Yesu, Roho Mtakatifu, Watakatifu, na malaika na vitu vyote wataishi pamoja kama familia moja katika amani kamilifu. Ninamsifu Bwana kwa kutufanya sisi kuwa watu wake. 
 
Aya ya 5: Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele. 
Kama Biblia inavyotueleza hapa, watakatifu watatawala katika Mbingu na Nchi Mpya pamoja na Bwana. Wale waliofanyika watakatifu wake kwa kuamini katika injili ya maji na Roho wamepokea wokovu utakaowawezesha kutawala Mbinguni pamoja na Bwana na kisha kuishi katika utajiri, fahari, na mamlaka milele. Kwa kweli kwa mara nyingine tunashangazwa na injili hii, kwa kuwa injili hii tuliyonayo ina nguvu na baraka za ajabu! 
Ninamsifu Mungu wetu wa Utatu kwa baraka hizi zote na utukufu. Watakatifu walioamini katika injili ya maji na Roho wakati walipokuwa hapa duniani watautawala Ufalme wa Mbinguni. Baraka hii ya kuyashangaza sana! Hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kumsifu Bwana. Na kwa sababu hiyo ni sahihi na haki kumsifu Mungu. 
Katika Mbingu na Nchi Mpya mahali ambapo watakatifu wanaishi, hakuna haja ya taa, balbu za umeme, au jua. Kwa nini? Kwa kuwa Mungu Mwenyewe amefanyika kuwa mwanga wa Mbingu na Nchi Mpya, na huko hakutakuwa na giza kamwe. Mungu amewaruhusu watakatifu kutawala huko milele wakiwa kama watoto wake. Baraka hii inatukumbusha tena jinsi neema ambayo watakatifu wameipokea toka kwa Bwana ilivyo kubwa. 
Sisi watakatifu ni lazima tutambue jinsi baraka ya Mbinguni iliyowekwa kwetu ilivyo kuu hasa baada ya wokovu wetu. Neema ambayo Bwana wetu amewapatia watumishi wake ipo juu na kuu kuliko anga. Watakatifu hawapaswi kuiachia baraka hii kubwa ambayo Bwana ameitoa kuwapita. Hivyo, watakatifu wanachoweza kukifanya ni kutoa shukrani na kumsifu Bwana kwa ukuu wake, utukufu, na kwa baraka yake ambayo amewapatia, na kisha kuishi katika utajiri na fahari milele. Amin! Halleluy! Ninamsifu Mungu wetu!
 
Aya ya 6: Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. 
“Maneno haya ni amini na kweli.” Ni hakika kwamba Bwana atazitimiza ahadi zake zote ambazo amezifunua kwa watakatifu kwa kupitia Ufunuo. Hii ndio sababu Bwana wetu ameelezea kabla kila kitu kwa watakatifu wake akiongea kama Roho Mtakatifu kupitia watumishi wa Mungu. Je, ni neno gani ambalo limebarikiwa zaidi katika Kitabu cha Ufunuo? Kuna Maneno mengi sana yaliyobarikiwa katika Kitabu cha Ufunuo, lakini Neno lililobarikiwa zaidi ni hili kwamba Mungu atawaruhusu watakatifu kutawala pamoja na Bwana katika Mbingu na Nchi Mpya na kisha kuishi kwa mamlaka na utukufu. 
Kwa kuwa Mungu atalitimiza hili tendo hivi karibuni, basi watakatifu hawawezi kuiruhusu imani yao kuanguka na kuangukia katika mtego wa kukata tamaa. Watakatifu ni lazima wayashinde majaribu yote na dhiki kwa imani yao yenye tumaini. Bwana wetu hatashindwa kuutimiza unabii wake na kuzitimiza ahadi zake zote kwa watakatifu na Kanisa la Mungu. Bwana wetu aliwatuma watumishiw ake hapa duniani na akawafanya kuyazungumza Maneno ya unabii, ili kwamba aweze kuwaeleza watakatifu na Kanisa lake kuhusu baraka hizi zote. 
 
Aya ya 7: “Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
Kwa kuwa Maneno ya unabii wa Kitabu hiki cha Ufunuo yanatueleza juu ya mauaji ya watakatifu wakiifia-dini, basi kitabu hiki kinatudhihirishia kwamba utafika wakati ambapo watakatifu watateswa na Mpinga Kristo na kisha watapaswa kuilinda imani yao hadi kifo. Watakatifu ni lazima wayapokee mauaji ya kufia-dini kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu. Kisha watashiriki katika ufufuo na unyakuo wao, watatawala katika Ufalme wa Kristo kwa miaka elfu moja itakayofuata, kisha wataishi katika Mbingu na Mchi Mpya milele. Kwa hiyo, watakatifu ni lazima waliamini Neno lote la Mungu ambalo Bwana wetu amezungumza nao na kisha wanapaswa kuilinda imani yao. Wale waliobarikiwa zaidi katika nyakati za mwisho ni wale wanaoamini katika Neno la Bwana wetu na wanaoishi kwa imani. 
Mungu amewaeleza watakatifu wake kwamba atakuja haraka. Bwana atakuja kwetu pasipo kukawia. Bwana wetu atakuja hapa duniani haraka ili kuzitimiza baraka zote za Mungu zinazotoka katika Neno la maji na Roho, Neno ambalo linawaletea watakatifu wokovu toka katika dhambi. 
Baada ya kuokolewa, watakatifu ni lazima walishikilie Neno la baraka za Bwana zilizoahidiwa kwao, na kisha wanapaswa kuilinda imani yao. Ikiwa mioyo yao itaipoteza imani katika Neno la Bwana, basi ni hakika kwamba watapoteza kila kitu, na hii ndio sababu wanapaswa kuilinda imani yao katika Neno la Bwana. Kwa maneno mengine, Mungu anawaeleza watakatifu kuilinda imani yao katika Bwana. 
 
Aya ya 8: Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nalianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo. 
Neno la Mungu la unabii linaenezwa na manabii na watakatifu. Hivyo ni lazima tumsifu Mungu anayetenda kama alivyoongea na hao manabii na watakatifu, na tunapaswa kumwabudu yeye tu. Katika nyakati fulani, baadhi ya watu hujaribu kujiinua juu kama Mungu. Wao hufanya hivyo kwa sababu wao ni matapeli au manabii wa uongo. Ni Mungu tu ndiye anayestahili kupokea sifa, kuabudiwa, kutukuzwa, na kutumikiwa. 
 
Aya ya 9: “Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu.” 
Tufanye nini ili tuweze kuwa manabii wa kweli wa Mungu? Kwanza ni lazima tuliamini fumbo la injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Hapo ndipo tutakapofanywa kuwa watu wa Mungu, watakatifu, na kaka na akina dada kati yetu. Ni baada ya kufanya hivi ndipo Mungu anapoweza kutubadilisha kwa matendo yake. Wale waliofanyika kuwa watumishi wa Bwana ni lazima waliamini Neno lake na kisha kulitunza kwa imani yao. Hawa ndio wale ambao wanampatia Mungu utukufu wote badala ya kukaa nao wenyewe. Bwana wetu anastahili kupokea ibada zote na utukufu toka kwa kila mtu hapa ulimwenguni. Helleluya!
 
Aya ya 10: “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.”
Neno la ahadi lililoandikwa katika Ufunuo halipaswi kufichwa. Kwa kuwa Neno hili litatimizwa hivi punde, na kwa sababu hiyo Neno hili linapaswa kushuhudiwa kwa kila mtu. Amini! Hebu sisi sote tuliamini Neno la unabii wa Kitabu cha Ufunuo na kisha tulihubiri. 
 
Aya ya 11: “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.”
Wakati siku ya Bwana itakapokaribia, Bwana atawaruhusu wale wanaotafuta dhambi kuendelea kufanya dhambi, wale walio watakatifu kuendelea kuwa watakatifu, na wale walio wachafu kuendelea kuwa wachafu. Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, wale ambao mioyo yao imekuwa haina dhambi kwa kuamini katika injili ya Bwana ya maji na Roho wataendelea kuitumikia injili hapa duniani, na wale walioutunza utakatifu wao uliotolewa na Bwana na walioyaishi maisha yao kwa imani wataendelea kuishi hivyo. Bwana wetu anatushauri kuilinda imani tuliyonayo sasa. 
 
Aya ya 12: “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” 
Kwa maneno mengine, Bwana wetu atakuja hivi punde, na kisha atawapatia watakatifu paradiso hapa duniani na katika Mbingu na Nchi Mpya, yaani kwa watakatifu ambao walifanya kazi ya kuieneza injili ya maji na Roho, na kisha kuwapa ujira kwa kujitoa kwao. Wakati watakatifu wanapoamini katika Neno la unabii wa kitabu cha Ufunuo, basi wataweza kuilinda imani yao hadi mwisho, kwa kuwa watakuwa wameiweka imani yao katika Bwana. Tunapaswa kutambua na kuamini kwamba Bwana atawapa ujira watakatifu kwa kazi yao pamoja na baraka kuu, hii ni kwa sababu Bwana wetu ni mwenye utukufu na mwenye rehema. 
 
Aya ya 13: “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.”
Bwana wetu ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu. Yeye ni Mwokozi wetu na Mungu wetu, ni yeye ambaye atauleta ukamilifu wa wokovu ambao ni yeye tu ndiye anayeweza kutupatia. Historia yote katika ulimwengu mzima, historia ya Mbingu na dunia, ilianza na Bwana na itahitimishwa na Bwana. 
 
Aya ya 14: Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. 
Kwa kuwa kile ambacho Bwana amekiongea kwetu ni uzima, basi watakatifu wanaliamini Neno lake, wanalihubiri na kulilinda. Wanafanya hivyo kwa sababu Neno ambalo Bwana wetu amelizungumza kwa watakatifu wake na kwa vitu vyote hapa ulimwenguni ni vya kweli. Hii ndio sababu watakatifu na watumishi wa Mungu wanalitunza Neno la Bwana katika akili zao. Wanailinda imani yao kwa kuliamini Neno la Mungu kwa nguvu zaidi, ili kwamba hatimaye wawe na haki ya kula matunda ya mti wa uzima uliopandwa katika Mbingu na Nchi Mpya. 
Watakatifu waliofanyika kuwa wasio na dhambi kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana wanajaribu kuilinda imani yao, kwa kuwa wana haki ya kula matunda ya mti huu wa uzima huko Mbinguni. 
 
Aya ya 15: Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya. 
Wale wanaotajwa katika kifungu hicho hapo juu ndio wale wasioamini katika injili ya maji na Roho, na kwa sababu hiyo hawajazaliwa tena upya hadi nyakati za mwisho. Mpinga Kristo na wafuasi wake, hali akiwapotosha watu kwa ishara zake na miujiza, atakuwa amewadanganya kwa kitambo fulani huku akitoa madai ya uongo kuwa yeye Mpinga Kristo ni Mwokozi. Watakuwa wamewaongoza watu kuelekea katika maangamizi kwa kuwafanya waiabudu sanamu ya Mpinga Kristo. Bwana wetu atawaweka watu wa jinsi hiyo nje ya lango la Mji Mtakatifu, ili kwamba wasiweze kuingia katika Mbingu na Nchi Mpya. Mji wa Bwana upo wazi kwa ajili ya watakatifu tu ambao wameilinda imani yao inayoaminni katika injili ya maji na Roho. 
 
Aya ya 16: “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung`aa ya asubuhi.”
Bwana wetu ametutumia watumishi wa Mungu, na amewafanya washuhudia mambo yote ambayo yatakuja kutokea, amefanya haya yote kwa ajili ya Kanisa la Mungu na watakatifu wake. Yeye aliyewafanya waweze kushuhudia mambo haya yote ni Yesu Kristo, Mungu Mwenyewe ambaye amefanyika kuwa Mwokozi wa watakatifu. 
 
Aya ya 17: Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure. 
Kwa wale wote hapa duniani wanaoona njaa na kiu juu ya haki ya Mungu, basi Bwana wetu anawaalika katika Neno la maji ya uzima. Yeyote anayeona kiu na njaa juu ya haki ya Mungu basi mtu huyo amepewa baraka ya kuja kwa Bwana, amepewa baraka ya kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana, na hivyo kuyanywa maji ya uzima. Hii ndio sababu Bwana wetu anamwambia kila mtu kuja kwa Yesu Kristo. Mtu yeyote anaweza kupokea ukweli wa injili ya maji na Roho bure. Lakini maji ya uzima hayatapatikana kwa wale ambao hawana tamanio hili. Ikiwa unaitamani injili hii, wewe nawe, unaweza kuyanywa maji ya uzima yaliyotolewa na Bwana kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. 
 
Aya ya 18: Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 
Maandiko ni Neno la Mungu. Kwa hiyo, watu wanapoliamini Neno hili, basi ni hakika kwamba hatuwezi kuliongeza au kulipunguza. Aya hii inatueleza kwamba kwa kuwa Neno la Maandiko ni Neno la Mungu, hakuna anayeweza kuliamini kwa kuongeza au kupunguza Neno la kweli lililo andikwa, wala hakuna anayeweza kuamini kwa kuuacha ukweli ulioandikwa. Hivyo ni lazima tuwe waangalifu. Kila Neno lililozungumzwa na Mungu ni la muhimu; hakuna linaloweza kuachwa kana kwamba si la muhimu. 
Hata hivyo, bado watu wanaendelea kuidharau injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Hii ndio sababu watu hao bado hawajakombolewa toka katika dhambi zao, na ndio sababu bado wamebakia ni wenye dhambi, na ndio maana wanaingia katika maangamizi yao—pamoja na kuwa wanadai kumwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao. Bwana wetu amewapatia maji na damu yake ili kuwakomboa wenye dhambi toka katika dhambi (1 Yohana 5:4-5, Yohana 3:3-7). Hata hivyo bado kuna watu wengi wanaiwekea umuhimu damu ya Yesu ya Msalaba tu; na kwa sababu hiyo bado hawajakombolewa toka katika dhambi zao, na hivyo watakabiliana na mapigo yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki cha Ufunuo. 
Wale wanaodai kumwamini Yesu na huku wakiudharau ukweli kwamba Kristo alizishughulikia dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake toka kwa Yohana watakabiliana na adhabu ya kutisha zaidi huko kuzimu. Kwa nini? Kwa sababu hawaiamini injili ya maji na Roho ambayo Bwana amewapatia, na kwa sababu hiyo bado hawajazaliwa tena upya. Yeyote anayeidharau injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana ataingia katika ziwa la moto unaowaka milele na atakabiliana na mateso ya milele—kwa kweli siku ya kujuta itawajia watu wote wa jinsi hiyo. 
 
Aya ya 19: Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki. 
Je, kuna yeyote miongoni mwetu ambaye imani yake ya Kikristo inaliacha Neno la kweli, kwamba Yesu alizichukua katika mwili wake dhambi zote za mwanadamu kwa kuupokea ubatizo toka kwa Yohana, na kwamba alizisafishilia mbali dhambi hizo mara moja wakati aliposulubiwa? Ikiwa ni hivyo, basi ni hakika kwamba watu wa jinsi hiyo watapoteza haki ya kuingia katika Mji Mtakatifu wa Mungu, kwa kuwa hawaamini katika ubatizo ambao Bwana wetu aliupokea toka kwa Yohana ili kuzichukua dhambi zote za mwanadamu katika mwili wake mara moja. Na kwa kufanya hivyo wanafanya dhambi ya kuidharau injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. 
Kwa hiyo, Wakristo ni lazima wauchukue katika mioyo yao ukweli kwamba Yesu alizichukua katika mwili wake dhambi za mwanadamu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana. Pasipo kuamini hivyo, watu hao wataondolewa toka katika utukufu wa kuingia katika Mji Mtakatifu uliotolewa na Bwana. Ikiwa unaamini kwamba Yesu ni Mwokozi wako, basi ni lazima usafishwe dhambi zako zote kwa kuamini kwa moyo wako wote kwamba Yesu alikuja hapa duniani, alibatizwa na Yohana katika Mto Yordani ili kuwaokoa wanadamu kikamilifu toka katika dhambi za ulimwengu, na kwamba kwa sababu hiyo alizisafisha dhambi zote zilizotendwa na mwanadamu kwa kuzichukua dhambi hizo katika mwili wake. Kijito ambacho unaweza kusafishwa uchafu wako wote ni ubatizo ambao Bwana wetu aliupokea. Baada ya kuzichukua katika mwili wake dhambi zetu za ulimwengu, Bwana wetu aliimwaga damu yake na kufa Msalabani ili kulipa mshahara wa dhambi zetu zote kwa kifo chake. 
Ubatizo ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana ni ushahidi uliothibitishwa juu ya wokovu wetu toka katika dhambi. 1 Petro 3:21 inatueleza kwamba, “Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo.” Ni lazima tutambue kwamba Yesu alizichukua dhambi za ulimwengu kwenda Msalabani na akaimwaga damu yake ili kulipa mshahara wa dhambi za wanadamu kwa kifo chake, alifanya hayo yote kwa ajili yetu. 
Hii ndio sababu Mungu anatupatia tena Neno lake la kutuonya wanadamu wote katika aya ya 19. Ni lazima tuliamini Neno la injili ya maji na Roho kama lilivyo, pasipo kuliongeza au kulipunguza. 
 
Aya ya 20: Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu!
Hivi punde Bwana wetu atakuja hapa ulimwenguni. Na watakatifu, waliopokea ondoleo la dhambi zao kwa kumwamini Bwana na waliofunikwa utukufu wa Mbinguni, wanasubiria kwa hamu zaidi ujio wa Bwana mara ya pili. Kwa kuwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wamejiandaa wote kukutana na Bwana anayekuja, wanasubiria ujio wa Bwana ili awavike baraka yake iliyoahidiwa kwa watakatifu. Kwa hiyo, watakatifu wanasubiri kwa shauku ujio wa Bwana mara ya pili katika imani na shukrani. 
 
Aya ya 21: Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.
Mtume Yohana anahitimisha Kitabu cha Ufunuo kwa sala ya baraka kwa neema ya Bwana wetu Yesu Kristo kuwa pamoja na wale wanaotamani kuingia katika Mji Mtakatifu uliotolewa na Mungu. Hebu sisi nasi, tuwe watakatifu wanaoingia Mji Mtakatifu uliotolewa na Yesu Kristo kwa imani pasipo kushindwa.