Search

Проповеди

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[3-2] Wale Ambao Hawakuyachafua Mavazi Yao Meupe (Ufunuo 3:1-6)

(Ufunuo 3:1-6)
 
Sehemu ya kifungu hiki cha maandiko kinasema kuwa, “Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili.” Kutembea katika mavazi “meupe” maana yake ni kuwa wameilinda imani yao katika haki ya Mungu. 
Mungu anatembea na wale wanaoutunza usafi wa imani yao. Mungu hawaachi peke yao, bali yupo pamoja nao wakati wote. 
Kuna wenye haki katika dunia hii ambao wanatembea pamoja na Roho Mtakatifu. Mungu ameyaandika majina yao katika Kitabu cha Uzima na amewaruhusu uzima wa milele ili waweze kuishi milele. Kwa kuwavika wenye haki kwa mavazi meupe, Mungu amewafanya waweze kumshinda Shetani wakati wote katika mapambano yao dhidi yake. 
 

Kuwa Yule Anayemshinda Shetani 
 
Ili tuweze kuwa yule anayemshinda Shetani, ni lazima tuamini kwanza katika Neno la ukombozi ambalo Bwana ametupatia. Kwa hiyo, hebu tuligeukie Neno na tuone jinsi ambavyo Bwana ametuokoa kwa injili ya maji na Roho. 
Hebu tuanze kwa kuangalia Luka 10:25-35. “Na tazama, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.”
Hapa tunawaona wahusika wakuu wawili katika kifungu hiki cha maandiko: Yesu na mwanasheria. Huyu mwanasheria, hali akijivunia uaminifu wake kwa sheria alimuuliza Yesu: “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Je, unapata maana au mtazamo gani toka katika swali hili? 
Kwa mujibu wa swali hili la mwanasheria inaonekana wazi kuwa mwanasheria alidhani kuwa anaweza kuishika Torati kwa kuitii kama ilivyoandikwa. Lakini Mungu aliwapatia wanadamu Sheria ili watu waweze kuzitambua dhambi za mioyo yao. Sheria ya Mungu inazungumzia na kuzifunua dhambi za msingi ambazo zimo katika mioyo ya watu. Ndani ya mioyo ya watu kuna mawazo mabaya, akili mbaya, mawazo ya uuaji, mawazo ya kuiba, mawazo yanayotoa ushahidi wa uongo, mawazo yaliyochanganyikiwa, na mengine mengi. Ili kuionyesha dhambi iliyokuwemo katika moyo wa huyu mwanasheria, Bwana wetu alimuuliza swali, “Akamwambia, imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?”
Bwana wetu alitaka mwanasheria kufahamu uwepo wa msingi wa dhambi katika moyo wake. Lakini kwa kujidai haki alimuuliza Yesu “nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?,” hapa inaonyesha kuwa mwanasheria huyu alikuwa akijivunia haki yake binafsi. Kwa mujibu wa maneno ya mwanasheria tunaweza kuona kile ambacho mwanasheria alikiwaza: “Nimeishika na kuifuata Sheria vizuri hadi sasa, na nina hakika nitaendelea kuishika na kuifuata hapo baadaye.” 
Lakini ni lazima tutambue kuwa Sheria iliyotolewa na Mungu inaweza kufuatwa na Mungu mwenyewe tu, na kwamba hakuna yeyote anayeweza kuifuata na kuishika Sheria kikamilifu. Hivyo, kitendo cha mtu kujaribu kuishika Sheria ya Mungu ni sawa na kuonyesha ujinga mbele za Bwana. Ni lazima tutambue kuwa sisi ni wenye dhambi ambao hatuwezi kuishika na kuifuata Sheria ya Mungu. 
Jinsi tunavyolisoma Neno la Mungu ni muhimu sana kwetu sote. Tunapolisoma Neno la Mungu, ni lazima tulisome hali tukiwa na ufahamu juu ya lengo la Mungu alilolikusudia kwetu. Ikiwa tutaisoma Biblia pasipokuwa na ufahamu huu wa nia ya Bwana, basi ni wazi kuwa imani yetu inaweza kuelekea katika upande mwingine wa mapenzi yake. Hii ndiyo sababu kuna madhehebu mengi sana tofauti na pia ndio sababu inayowafanya wale ambao imani yao imeungana na Mungu kukataliwa, yaani wale wasemao ukweli. 
Wakati wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wanapoisoma Biblia, wanaweza kulielewa vizuri lengo la Mungu. Lakini mtu anapoisoma Biblia pasipo kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu, basi hali hiyo inaweza kusababisha mtu huyo kutokuelewa vizuri, pia mtu wa jinsi hiyo hawezi kuwa na imani nzuri ya kibiblia hata kama atajaribu kuisoma Biblia kwa juhudi. 
 

Je, Sheria Inasemaje? 
 
Tunaendelea na kifungu cha maandiko toka Luka: “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.”
Warumi 3:20 inasema, “Kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” Pia Biblia inatueleza kuwa, “Kwa maana wale wote walio na matendo ya sheria, wako chini ya laana” (Wagalatia 3:10).
Sheria sio tu inatufanya kuwa watenda dhambi zaidi, yaani sisi ambao tulikwishazaliwa tukiwa wenye dhambi, bali sheria inayafunua mapungufu ya matendo yetu. Hii ndiyo sababu “Wale wote walio na matendo ya sheria wako chini ya laana.” 
Baadhi ya watu wanasema kuwa mtu anaweza kuingia Mbinguni ikiwa mtu huyo anamwamini Mungu na anaishika na kuitunza Sheria vizuri, na kwamba mtu anapaswa kujitahidi kuishika na kuitunza Sheria. Hivyo, watu hawa, pamoja na kuwa wanamwamini Yesu, wanatumia muda mwingi wa maisha yao wakijaribu kuishika na kuifuata Sheria. Lakini ukweli ni kuwa wapo chini ya laana ya Sheria. Wale wambao hawajaokolewa toka katika dhambi zao hata pale wanapomwamini Yesu hawawezi kukwepa toka katika vifungo vya imani yao inayojaribu kuishika Sheria kwa utupu. Watu wa jinsi hiyo wanaweza kumwamini Yesu, lakini ukweli ni kuwa watabakia wakiwa wenye dhambi mbele za Mungu, ni wazi kuwa wenye dhambi watakutana na hukumu ya Mungu ya kutisha. Hii ndiyo sababu, Yesu, ambaye ni Mungu, alikuja kwetu kama Mwokozi na akafanyika kuwa Mkombozi wa wenye dhambi. Kwa maneno mengine, Yesu alizishughulikia dhambi zetu zote kwa kubatizwa katika Mto Yordani. 
Je, unafahamu kuwa ubatizo ni alama ya wokovu inayozisafishilia mbali dhambi zetu zote? Ubatizo wa Yesu ulikuwa ndio mbinu au njia pekee ambayo Mungu aliianzisha ili kuzisafishilia mbali dhambi zetu zote. 
Katika Mathayo 3:15 Biblia inatueleza kuwa, “Kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote.” Neno “kwa kuwa” katika lugha yake ya asili lina maanisha “namna inayofaa zaidi” au “namna nzuri zaidi.” Kwa maneno mengine, ilikuwa inafaa zaidi na vizuri zaidi kwamba Yesu atazichukua dhambi zote katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake toka kwa Yohana. Kwa ufupi, ubatizo wa Yesu Kristo ulizishughulikia dhambi zetu zote. Yesu Kristo alitukomboa toka katika dhambi zetu kwa kubatizwa na kufa Msalabani. Watu wakiufahamu ukweli huu sahihi na kupambana na uongo,  basi Mungu anawaita wao kuwa ndio wale wanaoshinda. 
 

Waliozaliwa Tena Upya Wanapaswa Kupambana Dhidi ya Nani?  
 
Waliozaliwa tena upya ni lazima wapambane dhidi ya washika sheria na kuwashinda. Kwa mtazamo wa kidini, viongozi wa Sheria wanaweza kuonekana kuwa ni wema, lakini kwa ndani ni watu wanaompinga Mungu. Hivyo, mananeo yao ambayo yanaweza kuonekana kuwa ni ya haki, ukweli ni kuwa ni maneno ya Shetani yanayowaweka wafuasi wao chini ya laana ya dhambi. Hii ndiyo sababu watakatifu ni lazima wapambane na kuwashinda hawa wanadini. 
Wanadini wanadai kuwa wokovu unakuja kwa kumwamini Yesu, lakini pia wanadai kuwa mtu anaweza kuingia Mbinguni anapokuwa akiishi maisha mema kwa kuifuata Sheria. Je, imani ya jinsi hiyo inaweza kuitwa ni imani inayomfanya mtu aweze kuokolewa? Kwa kweli hapana!
Hivyo, Bwana alitumia mfano ili kuwaangazia washika sheria na kutuangazia sisi kuhusu suala hili. Hadithi yenyewe inaeleza hivi: Mtu mmoja alikuwa akisafiri toka Yerusalemu kwenda Yeriko akavamiwa na majambazi ambao walimpiga na kumwacha akiwa nusu mfu. Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa akisafiri kwenda Yeriko akitokea Yerusalem, akaja akamkuta huyu mtu aliyekuwa amepigwa. Lakini yule kuhani hakumsaidia, na badala yake akapita pembeni. Mtu mwingine aliyekuwa Mlawi naye alipita na kumwona yule aliyekuwa ameathiriwa na majambazi lakini naye akajifanya hakisikii kilio cha yule aliyekuwa amepigwa akiomba msaada.  
Kisha mtu wa tatu alipita njia ile ile na safari hii alikuwa ni Msamaria. Tofauti na yule kuhani na yule Mlawi, huyu Msamaria aliyafunga majeraha yake kwa kuyamwagia mafuta na divai, akamchukua juu ya mnyama wake na kumpeleka katika nyumba ya wageni na akamtunza. Akamlipa fedha yule mtunzaji wa nyumba huku akisema, “Mtunze mtu huyu. Nitakaporudi nitapitia, ikiwa utakuwa umetumia zaidi ya kile nilichokulipa kwa ajili ya kumtunza nitakulipa. Hivyo fanya uwezavyo kumsaidia mtu huyu.”
Je, ni nani aliye mwema miongoni mwa hawa watu watatu? Kwa kweli ni Msamaria. Huyu Msamaria anafananishwa na Yesu. Kilichotuokoa wenye dhambi kama sisi si Sheria ya Mungu wala si walimu wa sheria, wala si viongozi wa sheria, wala si nguvu zetu, wala si juhudi zetu, wala si maombi yetu ya toba. Ni Yesu tu aliyekuja hapa duniani ili kuzisafishilia mbali dhambi zetu ndiye aliyetuokoa na kuwa Mwokozi wa kweli. Hivyo, Yesu “kwa mujibu wa (Mathayo 3:15)” amewaokoa wenye dhambi wote. Ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani ni alama ya wokovu kwa mwenye dhambi (1 Petro 3:21). Wenye dhambi wote wa ulimwengu huu wameokolewa na ubatizo wa Yesu na Msalaba. Wale wanaoamini katika ubatizo wa Yesu katika Mto Yordani na damu yake Msalabani kuwa ni wokovu wao basi hao ndio walio wakamilifu na wamekombolewa kikamilifu toka katika dhambi zao. 
Yesu ametupatia nguvu ya kupambana na kushinda dhidi ya mafundisho potofu ya kiiimani. Wakati watu wanapodai hivi, “Tunamwamini Yesu, lakini ikiwa utaishika Sheria ya Mungu na ikiwa matendo yako ni mazuri, basi utaokolewa toka katika dhambi zako zote,” basi ni wazi kuwa watu hao wanaonyesha ukaidi wao na wanatangaza uongo. Ikiwa utaongeza au kupunguza chochote kutoka katika ukweli wa wokovu wa Yesu, basi huu hauwezi kuwa ni ukweli. Yesu ametupatia nguvu ya kupambana na kuyashinda mafundisho ya kiimani ya uongo. 
Siku hizi viongozi wa Sheria wanaongea kwa sauti kubwa mbele ya watu kana kwamba wanaishikilia na kuitekeleza Sheria vizuri. Lakini mara nyingi tunashuhudia kuwa hawawezi kuishi kwa mujibu wa maneno yao kama Sheria inavyodai. Wanatambua kuwa ingawa wanataka kufanya mema katika mioyo yao, ukweli unabakia kuwa hawawezi kufanya hayo mema kwa sababu ya udhaifu wa miili yao. Mara nyingi watu hawa wanawadanganya wengine na kuwatwisha mizigo ambayo wao hawaiwezi hali wakiuficha udhaifu wao kwa kujivika taratibu za kidini.  
Washika sheria wa leo wanafanya kama alivyofanya kuhani na yule Mlawi, yaani kupita upande mwingine inapotakiwa kujitoa wao wenyewe. Huu ni uthibitisho wa unyonge wa mwanadamu mbele ya Sheria ya Mungu. Watu wanauficha unyonge huu kwa kujivika vazi linaloitwa dini. Lakini wale wote wanaojificha mbele za Bwana hawawezi kuokolewa. Ni wale tu wanaoifahamu hali yao ya dhambi kwa kuzifunua nafsi zao kwa kipimo cha Sheria ndio wanaoweza kukombolewa toka katika dhambi zao zote kwa Neno la kweli la maji na Roho. 
Ni Yesu tu ndiye asiyeweza kuwapita wenye dhambi wanaokaribia kufa na ndiye pekee anayewaokoa kwa kuwatafuta na kukutana nao. Yesu alizihamishia dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kubatizwa yeye mwenyewe, na aliwakomboa wenye dhambi waliokuwa katika hali ya kufa toka katika dhambi zao zote kwa kulipa mshahara wao wa dhambi kwa kafara ya mwili wake binafsi. Hii ndiyo sababu Yesu amefanyika kuwa Mwokozi wa wenye dhambi wote. 
 

Wale Watakaoshinda Watavikwa Mavazi Meupe 
 
Kifungu cha maandiko kinatueleza kuwa wale watakaoshinda watavikwa mavazi meupe. Hii ina maanisha kuwa ni lazima tupambane na kuwashinda waongo katika ulimwengu wa Kikristo. Hata tunapoongea hivi sasa, hawa waongo wanawafundisha watu kumwamini Yesu na kisha kuishi katika wema. Kwa kweli kuishi katika wema ni jambo zuri. Lakini, kimsingi, mioyo ya wanadamu imejazwa na kila aina ya vitu vibaya, uuaji, uasherati, wizi, wivu; kwa hiyo kuwaambia hawa watu waishi katika wema, ambalo ni jambo jema, ukweli ni sawa na kuwafungia katika udini na kuwafanya wafe. Kitendo cha kuwaambia watu ambao dhambi zao zimejaa hadi kwenye makoo yao “ishi katika wema” ni kuwasukumia watu hao katika kujihukumu wao wenyewe.  
Kwa hiyo, wanachohitaji wenye dhambi hao ni kuwasaidia ili waweze kukombolewa toka katika dhambi zao zote kwa kuwafundisha juu ya ukweli wa injili ya maji na Roho inayoweza kuwaokoa toka katika dhambi zao. Hili ndilo fundisho sahihi, na baada ya fundisho hili inafuata kutiwa moyo kuishi maisha ya wema katika Mungu. Kwa lugha nyingine, jambo la muhimu na la haraka sana kwa wale wanaosimama nje ya Kristo kama wenye dhambi ni kuwafanya kuwa wenye haki kwa kuwahubiria injili ya maji na Roho. 
 

Kushuka Kwa Ukristo na Kuwa Kama Dini ya Kidunia 
 
Hatupaswi kudanganywa na dini za kidunia. Sisi tunaweza kuingia Mbinguni ikiwa tu tutapambana na kuzishinda dini za kidunia ambazo zinaeneza uongo. Kwa kuwa hatuwezi kushika na kuifuata Sheria ya Mungu, basi ni hakika kuwa tunahitaji neema ya wokovu ambayo Yesu ametupatia na ni kwa kuamini katika neema hii ndipo tunapoweza kuonana na Bwana.
Lakini watu wengi katika Ukristo, pamoja na kuwa wanamwamini Yesu, wanadanganywa na kupotoshwa na wale wanaoeneza uongo na kwa sababu hiyo wanapelekwa kuzimu. Wanadanganywa na mawazo yanayoshawishi kuwa watu wanaweza na ni lazima wawe wema. Lakini kwa kuwa tunazaliwa tukiwa na dhambi, hatuwezi kuwa wema hata kama tukijaribu kiasi gani. Kwa hiyo, tunaweza kuokolewa kwa kuamini katika injili ya kweli kwamba Yesu ametuokoa kwa maji na Roho. Tunaweza kuishi maisha mapya pale tu tunapotambua kuwa tumefanywa kuwa wasio na dhambi kwa kuamini katika ukweli huu.
Mafarisayo wa Biblia na Wakristo wengi wa siku hizi ambao hawajasafishwa dhambi zao kwa kutoamini katika injili ya maji na Roho wanalingana—yaani wote hao ni wazushi. Mafarisayo walimwamini Mungu, waliamini juu ya ufufuo wa roho, na waliamini juu ya maisha baada ya kifo kama inavyoandikwa katika Maandiko. Lakini hawakumwamini Mungu kuwa ni Masihi. Zaidi ya yote, waliudharau ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani.
Siku hizi kuna Wakristo wengi ambao wapo kama hawa Mafarisayo. Wana tabia ya kuyatambua na kuyakubali mafundisho ya kiimani kuliko Biblia yenyewe. Hii ndiyo sababu siku hizi kuna uzushi mwingi unaochipuka kila siku. Katika Tito 3:10-11, Mungu anatueleza kuhusu wazushi akisema, “Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.” Wale ambao ni wazushi wanawatumaini, wanawaamini, na kuwafuata viongozi wao wa kidini kuliko Biblia, na kwa matokeo hayo wataangamizwa wote. 
Kama ilivyo kuwa hapo zamani, hivi sasa kuna manabii wengi wa uongo wanaochipuka katika ulimwengu huu. Kwa kupitia Neno la kifungu kikuu cha maandiko katika sura hii, Mungu alitueleza kuwa kila mtu ni lazima apambane na kuwashinda hawa manabii wa uongo. Pia Mungu alisema kuwa wale watakaoshinda watavikwa mavazi ya haki. 
Katika Luka 18 kuna “mfano wa Farisayo na mtoza ushuru.” Farisayo alikwenda Hekaluni, akainua mikono yake, na kisha akaomba kwa majivuno: “Mungu, ninafunga mara mbili kwa wiki na ninatoa zaka katika mapato yangu yote.” Kwa upande mwingine, yule mtoza ushuru hakuweza hata kuuinua uso wake wakati alipoomba hivi: “Mungu, siwezi kufanya yale ambayo huyo Farisayo anayafanya. Mimi ni mwenye dhambi niliye na mapungufu mengi, ambaye siwezi kufunga mara mbili kwa wiki wala kukutolea zaka. Si hayo tu pia nimewadanganya watu, nimewaibia, na nimefanya maovu mengi sana. Kwa kweli sifai. Mungu, naomba unihurumie. Tafadhali naomba unirehemu na kuniokoa.”
Biblia inatuelezla kuwa yule mtoza ushuru ndiye aliyehesabiwa haki na Mungu kuliko yule Farisayo. Suala hili linaonyeshwa vizuri katika swali, “ni nani wanaoweza kusamehewa dhambi?” Si wengine bali ni wale wanaoyatambua mapungufu yao binafsi. Wale wanaotambua kuwa ni wenye dhambi, yaani roho na nafsi zinazotambua kuwa ni hakika kuwa zimefungwa kuzimu na kwamba Sheria au hukumu ya haki ya Mungu ingeliwahukumu—basi hao ndio wanaopokea wokovu wa ukombozi toka kwa Yesu.
Mathayo 3:15 inaeleza kuwa Yesu aliongea hivi kabla hajabatizwa. Neno “Ndivyo” katika aya hii lina maanisha kuwa ubatizo wa Yesu ulikuwa ndiyo njia sahihi ya kuwaokoa wenye dhambi—yaani kuwaokoa kwa kuzifanya dhambi zao kutoweka kwa ubatizo wa Yesu ambao ulizikabidhi dhambi zote kwa Yesu.
Je, unaamini katika ukweli kuwa Yesu “ndivyo” alivyokuokoa toka katika dhambi zako? Bwana alizichukua dhambi zako zote katika mwili wake wakati alipobatizwa. Kisha Yesu alizibeba dhambi zote za ulimwengu hadi Msalabani na kisha akalipa mshahara wa dhambi hizi zote kwa damu yake. Hivyo, ili roho yako iweze kuwa hai, basi unatakiwa kuamini hivvyo. Utakapoamini hivi, basi roho yako itapatanishwa, na utakuwa umezaliwa tena upya kama mtoto wa Mungu. 
Lakini bado kuna watu wengi katika ulimwengu huu wanaoukana ukweli wa maji na Roho, ambayo ni injili ya wokovu. Hii ndiyo sababu tunapaswa kupambana katika vita vya kiroho. Sisemi kuwa tufanye matendo mengi mabaya ili kuzitambua vizuri dhambi zetu, bali kwamba tunapaswa kuvikwa katika neema ya Mungu kwa kujitambua sisi wenyewe kuwa ni watu tuliofungwa katika dhambi tayari kwa kuhukumiwa kiroho. Ni lazima uupokee ukweli kuwa Yesu ni Mwokozi wetu. Kila anayetaka kuokolewa ni lazima amwamini Yesu wa ukombozi aliyezichukua dhambi zetu zote katika mwili wake na aliyehukumiwa kwa ajili yetu. Ni hapo mtu atakapoamini hivyo ndipo hakutakuwa na dhambi katika moyo wake.
Je, kuna dhambi katika moyo wako sasa? Wale wanaofikiria kuwa kuna dhambi katika mioyo yao ni lazima waifahamu Sheria ya Mungu kwanza. Kwa mujibu wa Sheria ya Mungu, mshahara wa dhambi ni mauti. Ikiwa una dhambi, basi ni lazima ufe kwa ajili ya hizo dhambi zako. Ikiwa utakufa wakati haujapatanishwa kwa ajili ya dhambi zako, basi ni hakika kuwa utahukumiwa na kutupwa kuzimu. Kwa kuwa kila mtu katika ulimwengu huu hawezi kufanya lolote zaidi ya kutenda dhambi, basi kwa mujibu wa Sheria ya Mungu ni dhahiri kuwa kila mtu hawezi kukwepa kupelekwa kuzimu. Hii ndiyo sababu, Mungu, hali akituhurumia, alituokoa kwa kumtuma Mwana wake pekee Yesu Kristo kuja hapa duniani, akamfanya “(Mathayo 3:15)” kuzichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake katika Mto Yordani, na kisha akamhukumu kifo Msalabani kwa ajili yetu—Mungu alifanya hayo yote ili aweze kutupeleka Mbinguni. 
Kwa kweli hatuwezi kuokolewa kwa sababu ya matendo yetu mema. Watu wanaweza kuwa na viwango tofauti vya unafiki, hata hivyo kila mtu ni mnafiki, na hakuna hata mmoja anayeweza kuufikia wema mkamilifu. Hivyo, watu wanaweza kukombolewa toka katika dhambi zao zote kikamilifu pale tu watakapokuwa wamesamehewa dhambi zao zote kwa kuamini katika upatanisho wa wokovu wa Yesu. Huu ndio ukweli wa msingi wa Biblia.
Hali akielezea jinsi alivyokuwa kabla ya kukutana na Yesu, Paulo alikiri kuwa, “Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo” (Warumi 7:19). Kwa nini Paulo alikuwa hivi? Ni kwa sababu mwanadamu hawezi kutenda mema yoyote. Kila mtu anafahamu kuwa kutenda mema ni kitu chema cha kukifanya, lakini kimsingi hakuna hata mmoja anayeweza kufanya hivyo. Kwa kweli hili ni jambo tofauti kabisa kwa viwango kuhusiana na tamaa za mwili ambazo hata wenye haki wanazo. Hii ndio sababu watu wanaokolewa kwa kuamini katika injili ya kweli ambayo Bwana amewapatia.
Inawezekanaje kwa Mungu mwenye haki na asiye na dhambi kutupokea viumbe wachafu na waovu kama sisi? Mungu alituokoa na kutukubali kwa sababu ya Bwana wetu Yesu. Yesu alizichukua dhambi zote za mwanadamu katika mwili wake kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana, ambaye ni Kuhani Mkuu wa mwandamu, na kisha akazipeleka dhambi hizi kwenda Msalabani, na kisha alihukumiwa kwa niaba yetu. Je, unamwamini Yesu? Kumwamini Yesu ni kuamini yale ambayo ameyafanya kwa ajili yetu.
 

Namna ya Kusimama Mbele za Mungu
 
Kaini na Habili walizaliwa kutoka kwa Adamu na Hawa, ambao ni wazazi wa kwanza wa mwanadamu. Wakati Adamu na Hawa walipofanya dhambi, Mungu alimuua mnyama na kisha akawavisha kwa ngozi ya yule mnyama aliyeuawa. Jambo hili linawafundisha wanadamu sheria mbili za Mungu. Moja ni sheria ya Mungu ya haki ambapo “mshahara wa dhambi ni mauti,” na sheria nyingine ni sheria yake ya upendo ambapo sadaka ya mnyama inatumika katika kuzifunika dhambi za aibu za wenye dhambi. Adamu na Hawa walidanganywa na Shetani wakatenda dhambi dhidi ya Mungu. Bila kujalisha jinsi walivyoishia kutenda dhambi, Adamu na Hawa walistahili kuuawa kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mungu mshahara wa dhambi ni mauti. Lakini Mungu alimuua mnyama badala yao na akawafunika kwa kutumia ngozi ya yule mnyama. Tendo hili lilikuwa ni alama ya kivuli lililoonyesha juu ya sadaka ya upatanisho itakayokuja baadaye. 
Baada ya kuzitenda dhambi zao, Adamu na Hawa walifuma matawi ya mtini wakajivisha. Lakini matawi haya ya mtini hayakuweza kukaa kwa muda mrefu kwa kuwa yalikauka juani na kisha kupukutika, na kwa sababu hiyo hayakuweza kuufunika utupu wao uliotokana na dhambi. Hivyo Mungu alimuua mnyama, akawafanyia vazi la ngozi, na kisha akawafunika Adamu na Hawa waliokuwa wakijaribu kuifunika aibu yao kwa matawi ya mtini bila mafanikio. Kwa maneno mengine, Mungu aliifunika aibu yote ya wenye dhambi kwa kupitia utoaji wa sadaka. 
Tendo hili linatueleza sisi juu ya upendo wa Mungu kwetu na wokovu wake wa haki. Adamu na Hawa walitambua kuwa Mungu alimuua mnyama kwa ajili yao, na kwamba ni Mungu mwenyewe ndiye aliyeifunika aibu yao yote na akawaokoa. Kisha Adamu na Hawa waliipitisha imani hii kwenda kwa watoto wao. 
Adamu alikuwa na wana wawili ambao ni Kaini na Habili. Kaini, ambaye ni mtoto wa kwanza alimtolea Mungu sadaka itokanayo na nguvu zake mwenyewe wakati Habili alimtolea Mungu mwanakondoo aliyechinjwa kwa mujibu wa sheria ya upatanisho. Ni sadaka ipi ambayo Mungu aliipokea? Sadaka hizi mbili zilikuwa ni moja ya matokeo muhimu sana katika Agano la Kale ambayo yalionyesha tofauti kati ya sadaka za imani na sadaka za mawazo ya kibinadamu. Mungu aliipokea sadaka ya Habili. Biblia inatueleza kuwa Mungu hakuipokea sadaka ya Kaini ya mazao ya nchi yatokanayo na jasho na taabu, badala yake aliipokea sadaka ya Habili ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama katika kundi lake na mafuta yao. 
Biblia inasema, “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake.” Mungu aliipokea sadaka ya Habili na matoleo yake kwa furaha. Kutoka na Neno hili ni lazima tuyafahamu yale ambayo moyo wa Mungu unayataka toka kwetu. 
Inawezekanaje Mungu akatupokea sisi? Kila siku tunakuwa na mapungufu mbele za Mungu; itawezekanaje basi kusimama mbele za Mungu? Kuna njia moja tu ambayo kwa hiyo tunaweza kwenda mbele za Mungu, yaani njia moja pekee ambayo Mungu ameiweka kwa ajili yetu. Njia hii pekee ni kwa kupitia “sadaka” na si sadaka ya “matendo” yetu bali ni sadaka ya “imani” yetu. Haya ndiyo Mungu anayoyakubali.
Je, ni imani gani ambayo Adamu na Hawa waliipitisha kwa watoto wao? Ilikuwa ni imani ya “vazi la mnyama.” Kwa lugha nyingine, ilikuwa ni imani inayoamini juu ya upatanisho kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa. Siku hizi, imani hii ni ile inayoamini katika injili ya maji na Roho na katika damu ya Yesu: “Ninaamini kuwa dhambi zangu zote zilichukuliwa mbali na ubatizo wa Yesu na damu yake, na kwamba alihukumiwa kwa ajili yetu. Ninaitoa imani hii kama sadaka yangu. Ninaamini kuwa Bwana alizichukulia mbali dhambi zangu zote wakati alipobatizwa. Ninaamini kuwa dhambi zangu zote zilipitishwa kwenda kwa Yesu. Kama Mungu alivyoahidi katika Agano la Kale, Yesu alinifanya mimi kuwa nisiye na dhambi kwa kufanyika mwanakondoo wa sadaka na kwa kufa kwa ajili yangu. Ninaamini katika wokovu huu.”
Tunaposimama mbele za Mungu, hali tukiamini kuwa Bwana ametuokoa, basi ni dhahiri kuwa Mungu anapokea sadaka ya imani hii na anatukubali. Kwa nini? Ni kwa sababu tumefanyika kuwa tusio na dhambi na wenye haki mbele za Mungu kwa kupitia “sadaka ya kuteketezwa”. 
Mungu alitupokea kwa sababu tulimpatia sadaka ya imani yetu inayoamini kuwa Yesu ni Mwokozi wetu. Kwa maneno mengine, Wakati Mungu alipoipokea sadaka ya Yesu, pia alitupokea katika Kristo. Hii ni kwa sababu dhambi zetu zote zilipitishwa kwenda kwa Yesu ambaye alifanyika kuwa sadaka. Kwa kuwa hukumu yetu ya dhambi iliwekwa juu ya sadaka hii, basi hiyo imetufanya sisi kuwa wasio na dhambi. Hii ndiyo haki ya Mungu. Pia huu ndio upendo wa Mungu na wokovu wake mkamilifu. 
 

Sisi Pia Tunaitoa Imani ya Habili 
 
Biblia inatueleza kuwa Mungu aliipokea sadaka ya Habili ya imani kwa furaha. Je, ni sadaka ipi ya imani ambayo Mungu anaweza kuipokea toka kwetu siku hizi? Tunapoamini katika mioyo yetu kuwa Yesu ni Mwokozi wetu, na kwamba alizishughulikia dhambi zetu zote na akahukumiwa kwa ajili yetu, na tunapompatia Mungu imani hii, basi Mungu atatupokea tunapoitoa imani hii kwake kama sadaka. Haijalishi jinsi matendo yetu yanavyoweza kuwa na mapungufu, lakini ukweli ni kuwa dhambi zetu zilipitishwa kwenda kwa Yesu, na kwa kuwa Yesu alihukumiwa kwa ajili yetu, basi ukweli ni kuwa Mungu Baba anaziona dhambi zetu ndani ya Mwanawe na wala si ndani yetu. Hivyo, Mungu alizipitisha dhambi zetu zote kwenda kwa Mwanawe, alimhukumu kwa niaba yetu, na siku ya tatu akamfufua toka kwa wafu, na amemketisha katika mkono wake wa kuume.
Mungu amewaokoa wale wote wanaoamini hivi. Mungu amezipokea sadaka zetu za imani. Kwa kweli pasipo  Yesu Kristo hatuwezi kusimama kamwe mbele za Mungu. Lakini kwa kuwa Yesu alifanyika kuwa Mwokozi wetu mkamilifu, basi sisi tunaweza kwenda kwa Mungu hali tukiwa na sadaka ya imani, Mungu anaweza kutupokea sisi kwa sababu ya sadaka hii ya imani. Je, imani yetu katika ukweli huu ni kamilifu? Kwa kweli ni kamilifu!
Kwa kweli sasa tumefanywa kuwa tusio na dhambi. Kwa kuwa dhambi zetu zilipitishwa kwenda kwa Yesu, basi Mungu ametuvika sisi tuliofanywa kuwa hatuna dhambi kwa mavazi meupe. Mungu ametufanya sisi kuwa wenye haki. Kama Bwana wetu alivyotuahidi, “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima,” Bwana atayakiri majina yetu mbele ya malaika zake.
Katika Kanisa la Mungu la Sardi, kulikuwa na watu wachache ambao walitembea pamoja na Bwana katika mavazi meupe. Watu hao si wengine bali ni wale waliokuwa watumishi wa Mungu na wale waliokuwa watoto wa Mungu na watakatifu.
Mungu aliipokea sadaka ya Habili. Pia alimpokea Habili. Lakini Mungu hapokei sadaka ikiwa sadaka hizo si kamilifu. Hivyo ndiyo sababu Mungu hakumpokea Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa nini Mungu hakumpokea Kaini pamoja na sadaka yake? Mungu hakumpokea Kaini na sadaka yake kwa sababu sadaka aliyoitoa haikuwa sadaka ya uhai iliyoandikwa kwa damu ya upatanisho. Biblia inatueleza kuwa Kaini alitoa sadaka ya mazao ya nchi, ambayo ni mazao ya juhudi zake binafsi, na sadaka yake binafsi. Kwa lugha rahisi, Kaini aliyatoa mazao yake binafsi. Pengine mazao haya yalikuwa ni matikiti maji, mahindi, au viazi, au mazao mengine, na bila shaka mazao hayo yote yalisafishwa na kuandaliwa vizuri. Lakini Mungu hakuipokea aina hii ya sadaka.
Sadaka hii ya Kaini ina maana muhimu sana ambayo Wakristo wa leo wanapaswa kuifahamu ili waweze kuokolewa. Lakini katika ulimwengu wa sasa ni watu wachache sana ndio wanaoufahamu moyo wa Mungu, hii ni kwa sababu wengi wao hawafahamu wala kwa ndoto kuwa wanampatia Mungu sadaka kama ya Kaini.
Wakati mtu anaposimama mbele za Mungu, basi mtu huyo ni lazima ajitambue kuwa amefungwa kuzimu kwa sababu ya dhambi zake. Je, unalitambua hili mbele za Mungu, kwamba umefungwa na unastahili kwenda kuzimu kwa sababu ya dhambi zako? Ikiwa hukubaliana na ukweli huu, basi hakuna haja kwako kumwamini Yesu, kwa kuwa Yesu ni Mwokozi wa wenye dhambi. Bwana alitueleza kuwa, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.” Bwana wetu anahitajika na zile roho ambazo zinateseka chini ya kongwa la dhambi, na wala si zile roho ambazo hazizitambui dhambi zao binafsi na ambazo zinadai kuwa hazina dhambi wakati hazijazaliwa tena upya.
Kimsingi, kila mtu ni mwenye dhambi. Hivyo, Mungu atamhukumu mwanadamu, na mwanadamu amefungwa ili kukabiliana na hukumu hii ya hasira ya Mungu. Kwa maneno mengine, wewe na mimi tumepangiwa kuangamizwa. Lakini ili kuepusha tendo la kutupeleka kuzimu ili tukaangamie, Bwana alizichukulia mbali dhambi zote zote kwa ubatizo wake katika Mto Yordani na kisha akaipokea hukumu ya Mungu kwa ajili yetu. Kwa sababu ya tendo hili, Bwana aliweza kutuokoa kikamilifu mbele za Mungu. Hivyo, Mungu amefanyika kuwa Mwokozi kwa wale wote ambao wanatenda dhambi mbele za Mungu na wanaokubali wao wenyewe kuwa ni wenye dhambi, hao ndio wanaotakiwa kumwamini Mungu. 
 

Imani Inayotuvisha Mavazi Meupe ya Wokovu
 
Kama Biblia inavyotueleza, “Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu,” vivyo hivyo uzima wa mtu upo katika damu yake. Hivyo, ni lazima tufe kwa sababu ya dhambi zetu. Kwa nini ilimpasa Yesu kufa Msalabani? Yesu alikufa Msalabani kwa kuwa alikuwa amezichukua dhambi zetu zote katika mwili wake, na kwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, basi Yesu aliimwaga damu yake ya uzima ili kuulipa mshahara huo wa dhambi na akafa kwa ajili yetu. Ili kuushuhudia ukweli huu, Yesu alisulubiwa, akaimwaga damu yake Msalabani kwa niaba yetu.
Kama Biblia inavyosema, “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu,” Kwa kweli Yesu alikufa kwa ajili ya makosa na maovu yetu. Hivyo, kifo chake, ni kifo chetu, na kufufuka kwake ni kufufuka kwetu. Je, unaamini hivi?
Yesu alikuja hapa duniani ili kutuokoa na alibatizwa ili kuzifanya dhambi zetu ziweze kutoweka. Pia Yesu alisulubiwa. Watu walimdharau na kumdhihaki, waligawana mavazi yake, walimtemea mate, na wakampiga uso wake. Kwa nini Yesu ambaye ni Mungu, alikutana na uonevu huu wote wa kupigwa na kutemewa mate? Bwana wetu alidharauliwa kwa sababu ya dhambi zetu.
Hivyo, kifo na ufufuo wa Bwana ni kifo na ufufuo wa kila mmoja wetu. Hakuna kiongozi wa kidini wa ulimwengu aliyezishughulikia dhambi zetu. Katika ulimwengu huu, hakuna aliyeweza kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu, si Muhammad wala Buddha aliyeweza kufanya hivyo.
Lakini, Yesu Kristo, ambaye ni Mwana wa Mungu, alikuja hapa duniani na akazichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake katika Mto Yordani na akatufanya sisi kuwa tusio na dhambi. Yesu aliyatoa maisha yake binafsi ili kutukomboa toka katika kifo, hukumu, maangamizi na laana.
Hivyo, kama Biblia inavyotueleza, “Kwa kuwa kama mlivyobatizwa katika Kristo, mlimvaa Kristo,” imani yetu ni lazima iyavae au ivalishwe mavazi ya haki, ipatanishwe kwa ajili ya dhambi zetu kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu ambao ulizichukulia mbali dhambi zetu zote. Hivyo, imani hii katika ubatizo wa Yesu inajumuisha imani katika kifo na kufufuka kwetu.
Mungu ametufanya sisi kuwa watoto wake kwa kuiangalia hii imani yetu inayomwamini Mwana wa Mungu. Huku ndiko kupokea. Mungu anatupokea kwa kuiangalia sadaka ya imani yetu ambayo tunamletea. Mungu hatupokei kwa kuyaangalia matendo yetu, bali anatupokea sisi kama watoto wake kwa kuiangalia imani yetu katika Mwana wa Mungu kama Mwokozi wa wote, ambaye alizibeba dhambi zetu, akahukumiwa kwa niaba yetu, na kisha akafufuka tena toka kwa wafu.
Kaka zangu na dada zangu hii ndiyo imani ya kweli. Sisi tunaokolewa si kwa ajili ya matendo yetu, bali tunavishwa mavazi meupe kwa matendo ya Yesu Kristo. Hakuna matendo ya mtu yanayoweza kuwa safi kwa asilimia 100. Kwa kuwa ili mioyo yetu iweze kuwa isiyo na dhambi ni lazima tuachane na jitihada zetu binafsi, na badala yake tumwamini Bwana kuwa ni Mwokozi wetu. Tunaweza kuvishwa mavazi meupe kwa kuamini hivi tu.
Kisha majina yetu yataandikwa katika Kitabu cha Uzima, na tutathibitishwa na Mungu mbele ya malaika. Yesu mwenyewe atatutambua kuwa sisi tu watoto wa Mungu kwa kusema, “Nimewaokoa, ninyi ni wenye haki kwa kuwa nimezifanya dhambi zetu zote kutoweka.” Hii ndio maana halisi ya kifungu kikuu toka katika kitabu cha Ufunuo ambacho tumekuwa tukikijadili hadi sasa. Tunaweza kupatanishwa pale tu tutakapokuja katika kanisa la Mungu, na wale waliopatanishwa wanapatikana katika Kanisa la Mungu tu.
Mungu Baba ametupokea kwa kuitazama imani yetu katika Mwana wake. Ingawa kwa sababu ya mapungufu yetu hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea katika misingi ya maisha ya kila siku na kujikuta tukiangukia katika udhaifu wetu, ukweli ni kuwa Mungu anaitazama imani yetu katika Mwana wake, na anatupokea kwa sababu ya imani hii kama alivyompokea Mwana wake mwenyewe. Bwana wetu ametuokoa.
Pia Mungu ametuvika katika mavazi meupe. Imani inayoamini juu ya kutokuwepo dhambi katika mioyo yetu ni uthibitisho wa sisi kuvishwa hayo mavazi meupe. Bwana ametuahidi kuwa, tunaposimama mbele yake tukiwa na mioyo iliyovikwa katika mavazi meupe, basi Mungu ataibadilisha miili yetu kuwa katika miili ya kimungu.
Katika ulimwengu huu kuna makanisa ya Mungu ambapo wenye haki na watumishi wa Mungu wanaweza kupatikana. Katika makanisa haya kuna wale ambao wamevikwa haya mavazi meupe, na Mungu anatenda kwa kupitia makanisa yake na watumishi wake.
Hebu tugeukie Ufunuo 3:5 tena: “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele za malaika zake.”
Kwa mujibu wa kifungu hicho hapo juu, moja ya sharti ambalo Mungu ametupatia ni kwamba atamvika mavazi meupe “yule atakayeshinda.” Ni lazima tushinde. Lakini wale ambao wanamwamini Yesu huku wakiamini kuwa dhambi zao za kila siku zinatakiwa kusamehewa kwa toba zao za kila siku, ni hakika kuwa watu kama hao si wale waliomshinda Shetani katika mapambano yao dhidi yake, bali ni wale ambao wameshindwa na Shetani. Watu walio na imani kama hiyo hawawezi kuvikwa mavazi meupe. Hawezi kamwe kufanyika wenye haki.
Wale wanaoshinda ni wale wanaoamini katika kazi kamilifu ya Bwana ya wokovu. Bwana amekwishakupatia imani inayoweza kuyashinda mafundisho ya uongo ya kiimani kama fundisho la kutakaswa au kuhesabiwa haki. Pia Mungu ametuokoa kwa injili yake ya kweli, yaani injili ya ubatizo na damu ili kwamba tuweze kupambana na kuzishinda injili za uongo ambazo hazituletei wokovu mkamilifu na kutuweka huru toka kwa Shetani.
Ni lazima tuzikabidhi dhambi zetu kwa imani, hali tukitambua kwa uhakika katika mioyo yetu kuwa dhambi zetu zote zilikwishapelekwa kwa Yesu. Vilevile ni lazima tuamini kuwa tulikufa wakati Yesu alipokufa, na kwamba kifo chake kilikuwa cha haki kwa ajili yetu. Pia ni lazima tuamini kuwa alifufuka toka kwa wafu ili kutufanya sisi kuishi tena. Tunapokuwa na ukweli huu imara wa imani, basi Mungu akiiangalia imani yetu anatuthibitisha sisi kuwa wenye haki.
Kwa lugha nyingine, hii ndiyo maana ya Neno linalosema, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12). Watu hawafanyiki kuwa watoto wa Mungu kwa kutamka kwa midomo yao tu kuwa, “Ninamwamini Yesu,” wakati hawana hata ule ufahamu sahihi kuhusu Yesu.
Neno la Mungu linaendelea kusema, “waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Hiyo ni sahihi. Kufanyika watoto wa Mungu kunawezekana kwa imani tu. Hivyo, ni lazima tupambane na kuwashinda waongo kwa ajili ya kuulinda ukweli huu. Wale waliopokea ondoleo la dhambi kwa kuwashinda waongo ni lazima watembee na Mungu na kuzishinda tamaa za miili yao. Kwa maneno mengine, ni lazima waishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu.
Je, haya mapenzi ya Mungu ni kitu gani? Mapenzi ya Mungu ni kuona wale waliovikwa katika mavazi meupe wakiungana pamoja na kuitumikia injili yake. Mapenzi ya Mungu ni kuona kuwa wenye haki, hata kama kila mmoja anaishi kipekee, hukutana pamoja na huabudu, hutumika, na kumsifu Mungu, na kisha huieneza injili kwa wenye dhambi ili kwamba na wao waweze kuvikwa katika mavazi meupe. Maisha ya jinsi hii, yaani maisha ya kufanya kazi kwa ajili ya wokovu wa roho nyingine ni maisha ya watu wa Mungu, yaani maisha ya watumishi wake.
Tunapoishi maisha kama hayo, si tu kwamba Mungu anatuvisha katika “haki yake,” bali pia anatupatia baraka zote za kufanikiwa hapa duniani na baraka za kiroho za Mbinguni. Mungu ametufanya sisi kuihubiri injili hii kwa wale wanaotuzunguka, ili kwamba Mungu aweze kuwafunika na wao mavazi meupe. Mungu amewavika mavazi meupe wenye haki na wale wote wanaowazunguka. Mungu ameturuhusu kushinda katika mapambano yetu dhidi ya uongo kwa kuliamini Neno la kweli. Hivyo, Mungu amewapatia wenye haki wanaoshinda katika mashindano ya kiroho baraka ya kuvikwa mavazi meupe. Bwana Asifiwe!