Search

Проповеди

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[18-1] Ulimwengu wa Babeli Umeanguka (Ufunuo 18:1-24)

(Ufunuo 18:1-24)
“Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake. Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake. Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu. Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe. Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu. Na hao wafalme wa nchi, waliozini naye na kufanya anasa pamoja naye, watalia na kumwombolezea; wauonapo moshi wa kuungua kwake; wakisimama mbali kwa hofu ya maumivu yake, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu, Babeli, mji ule ulio na nguvu! Kwa kuwa katika saa moja hukumu yako imekuja. Nao wafanya biashara wa nchi walia na kumwombolezea, kwa sababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena; bidhaa ya dhahabu, na fedha, na kito chenye thamani, na lulu, na kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na hariri, na nguo nyekundu; na kila mti wa uudi, na kila chombo cha pembe, na kila chombo cha mti wa thamani nyingi, na cha shaba, na cha chuma, na cha marimari; na mdalasini, na iliki, na uvumba, na marhamu, na ubani, na mvinyo, na mafuta ya mzeituni, na unga mzuri, na ngano, na ng`ombe, na kondoo, na farasi, na magari, na miili na roho za wanadamu. Na matunda yaliyotamaniwa na roho yako yamekuondokea; na vitu vyote vilivyo laini na vitu vya fahari vimekupotea; wala watu hawataviona tena kamwe. Na wafanya biashara ya vitu hivyo, waliopata mali kwake, watasimama mbali, kwa hofu ya maumivu yake; wakilia na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule mkuu! Uliovikwa kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na nguo nyekundu, na kupambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu; kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa. Na kila nahodha na kila aendaye mahali popote kwa matanga, na mabaharia, nao wote watendao kazi baharini, wakasimama mbali; wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio mfano wa mji huu mkubwa! Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa. Furahini juu yake, enyi mbingu, nanyi watakatifu na mitume na manabii; kwa maana Mungu amehukumu hukumu yenu juu yake. Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa. Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yo yote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako. Na ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. 
Watu wanaweza kusikia mahubiri juu ya baraka na laana za Mungu kwa kupitia watumishi ambao Mungu amewatuma hapa duniani ili kuzifanya kazi zake. Hivyo, ili muweze kuwekwa huru toka katika dhambi zenu zote na hali ya kutokuwa na furaha, ninyi nyote mnapaswa kulipokea katika mioyo yenu na kuliamini Neno la baraka ya kiroho ya Mbinguni linalohubiriwa na watumishi wa Mungu.
 
Aya ya 2: Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza!”
Hii sentensi inayosema “Umeanguka Babeli ule mkuu,” inaonyesha kile ambacho mara nyingi Biblia imekuwa ikikitaja, ambapo neno Babeli limekuwa likihusianishwa na ulimwengu wa kidunia. Kwa mfano, katika Agano la Kale, tunakutana na habari juu ya Mnara wa Babeli, mnara ambao ulijengwa na wanadamu wakijaribu kumpinga Mungu kwa kuziunganisha nguvu zao binafsi, ambazo baadaye ziliangushwa na Mungu. Wakati kifungu hicho hapo juu kinaeleza kwamba Babeli ule mkuu umeanguka, basi ni dhahiri kwamba kifungu hiki kinatueleza kwamba ulimwengu huu utakuja kuanguka. Kuna baadhi ya watu ambao wanaweza kufikiria hivi, “kwa sasa ulimwengu huu upo vizuri, sasa inawezekanaje basi ulimwengu huu ukaanguka?” Lakini Mungu anatueleza hapa kwamba wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapomiminwa moja baada ya jingine, basi hapo ndipo Mungu atakapouangusha ulimwengu huu kama alivyounganisha ujenzi wa Mnara wa Babeli. 
Sasa, ni kwa nini basi Mungu atauangamiza ulimwengu huu kwa mapigo ya mabakuli saba? Ni kwa sababu watu wa ulimwengu huu watakuwa wamejiunga na Mpinga Kristo katika kuwaua watakatifu waliozaliwa tena upya na wanaoamini katika injili ya maji na Roho, pia ni kwa sababu watu hao watakuwa wamesimama kinyume na Mungu hadi mwisho wao. Pia Mungu atauangamiza ulimwengu huu kwa sababu utakuwa ni “mahali ambapo mashetani yanakaa.” 
Kwa nini hali itakuwa hivi? Kwa nini ulimwengu huu utakuwa ni mahali ambapo mashetani yanakaa? Ni kwa sababu wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, watu wengi watasalimu amri kwa Mpinga Kristo na kugeuka na kuwa watumishi wa huyu mwovu kwa kuipokea chapa ya Shetani toka kwa huyo Mpinga Kristo. 
Katika Maandiko, neno Mnyama linatumika kumaanisha Shetani, na mashetani kumaanisha watumishi wa Mnyama. Hivyo, kifungu hiki kinaeleza hapa kwamba ulimwengu umefanyika kuwa mahali pa mashetani, hii ina maanisha kwamba Mpinga Kristo, ambaye ni mtumishi wa Mnyama, ataukamata ulimwengu kikamilifu. Ulimwengu wa nyakati za mwisho utakabiliana na dhiki za kutisha wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapomiminwa juu ya ulimwengu. Ulimwengu huu utakuwa ni ulimwengu wa Mnyama, na mashetani yatakuwa mengi kana kwamba ulimwengu huu uliumbwa kwa ajili yao. Na ulimwengu huu utaanguka kwa haraka sana, na utaangushwa kwa mapigo ya mabakuli saba yatakayomiminwa na Mungu. 
 
Aya ya 3: “Kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.”
Kama vile aya hii inavyoeleza hapa, “mataifa yote” hapa duniani wamelewa mvinyo ghadhabu ya uasherati wake. Kwa maneno mengine, watu wa ulimwengu huu wameufikiria ulimwengu huu kama ni Mungu, na wameamini na kufuata hivyo. Wameupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu. Hivyo, ulimwengu huu umekuwa ni kitovu cha dhambi, na watu wake wameishi na wanaishi wakiwa wamelewa dhambi. 
Hivyo, matokeo yake ni anguko la ulimwengu lililetwa na dhambi. Kwa kuwa watu wameupenda na kuufuata ulimwengu kana kwamba ni Mungu, basi Mungu atawaangamiza kwa adhabu yake ya mapigo ya mabakuli saba. Hatimaye kila mtu anayeishi katika ulimwengu huu ataangamizwa kwa haya mapigo saba makuu yaliyoletwa na Mungu na kisha watatupwa Jehanamu. 
Mungu anatupatia onyo la wazi kwamba kila mtu ambaye haamini sasa katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana atakabiliana na mapigo ya mabakuli saba hapo mwishoni. Unapaswa kukumbuka kwamba ikiwa huamini katika injili hii na kisha ukaendelea kusimama kinyume na Mungu, basi unapaswa kutambua kwamba si tu kwamba utaadhibiwa kwa mapigo ya mabakuli saba, bali utapokea pia adhabu ya milele huko Jehanamu. 
Hivyo, watu wanapaswa kutambua kwamba, wanapaswa kuiamini injili ya maji na Roho hivi sasa, ili kwamba waweze kuyakwepa mapigo makuu na ya kutisha ya Mungu, na kwamba wanapaswa kuirudia imani katika injili ya kweli ya maji na Roho mara moja kadri iwezekanavyo. 
Pamoja na kuwa wafalme wengi na wafanya biasara wa nchi watakuwa wamejilundia utajiri mkubwa kwa wingi wa mali, ukweli ni kwamba hao wote wataishia kulia, kuombeleza, kuhuzunika, na kupiga yowe mara watakapouona ulimwengu huu ukivunjika kwa mapigo makuu yaliyoletwa na Mungu. 
Hivyo, sisi sote tusisahau kamwe kwamba tunapaswa kuihubiri injili ya maji na Roho kwa kila mtu, na kwamba tunapaswa kuishi maisha yetu hali tukiitazamia milenia mpya. Tunapaswa kumwongoza kila mtu kuelekea katika injili ya maji na Roho, ili kwamba kila mwanadamu aweze kuyakwepa mapigo makuu.
 
Aya ya 4: Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.”
“Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.” Hili ni Neno la Mungu linalozungumzwa kwa watakatifu wake. Kwa maneno mengine, watakatifu hawapaswi kujihusisha na ulimwengu wa nyakati za mwisho na kuishi maisha yao kama watumwa wa ulimwengu huo. Hata kwa wale ambao walikwishafanyika kuwa watakatifu, ukweli ni kwamba kama wataangukia katika dhambi za ulimwengu wa nyakati za mwisho, basi ni hakika kwamba hawatakwepa kuhukumiwa na mapigo ya kutisha ya Mungu. Kwa maneno mengine, Mungu anawaeleza watakatifu wote kutojirundikia hasira ya Mungu kwa kukubali kuwa watumwa wa ulimwengu. 
 
Aya ya 5: “Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.”
Ni hakika kwamba Mungu anazikumbuka dhambi na matendo yote ya ulimwengu huu na anaisubiria tu siku yake ya hukumu. Maangamizi yataugubika ulimwengu mzima kama Mungu alivyopanga baada ya kuonekana kwa Mpinga Kristo. Hata hivyo bado kuna watu ambao wanaamini kwamba ulimwengu huu hautaangamizwa, na kwamba ulimwengu huu utadumu milele. 
Hata hivyo, ulimwengu huu hautadumu milele kama wanavyofikiria, bali ulimwengu huu utaangamizwa mara baada ya mapigo ya matarumbeta saba na ya mabakuli saba yatakayoletwa na Mungu. Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, Mungu ataleta dhiki kila mahali hapa ulimwenguni na kisha kuuangamiza. Hivyo, ni lazima tuwe na subira na uvumilivu katika maisha yetu ya kiimani hadi mwisho, hali tukiishikiria kwa nguvu imani yetu kwamba ni hakika kuwa Ufalme wa Yesu Kristo utakuja. 
Kabla ya Mungu kuwaamuru malaika zake kuyamimina mabakuli saba hapa duniani, ni wazi kuwa dhambi za ulimwengu zitakuwa nyingi mno na zitakuwa zimeenea sana kiasi kuwa zitakuwa zinastahili kupokea adhabu ya Mungu. Hivyo, Mungu atazikumbuka dhambi za ulimwengu huu, na hatayazuia maangamizi yake tena. Zaidi ya yote, Mpinga Kristo na watu wa kidunia watawatesha watu wa Mungu, huku wakiwalazimisha watakatifu kuikana imani yao, na kisha watawaua wengi wao kama wafia-dini. Wakati mambo haya yatakapo tokea, ulimwengu huu utakabiliana na mapigo ya mabakuli saba. 
 
Aya ya 6: “Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu.”
Hapa imeandikwa kwamba, “Mlipeni kama yeye alivyolipa.” Je, hiki kiwakilishi kinachowakilisha jinsia ya “kike” kinamhusu nani? Kina maanisha ni ulimwengu, yaani mahali ambapo wenye dhambi wanaishi ndani yake, ambao ni Mpinga Kristo na Shetani. Hii inatueleza kwamba Mungu atawalipa kama wao walivyoleta mateso, unyanyasaji, dhiki na vifo kwa watakatifu. 
Aya ya 6 pia inasema, “Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu.” Hii ni amri ya Mungu iliyotolewa kwa malaika wake ili kuziadhibu dini zote za uongo za hapa ulimwenguni ambazo ziliwaongoza watu kwenda kuzimu kwa kuueneza uongo wa Ibilisi. Hii ina maanisha kwamba Mungu ataileta ghadhabu yake na adhabu juu ya Ukristo wa leo kwa dhambi yake ya kutoa mafundisho ya uongo, yaani kwa kulichanganya Neno la Mungu pamoja na mafundisho ya Shetani, na hatimaye kuwaongoza watu kwenda kwa Ibilisi. Hivyo, Wakristo wasioamini katika injili ya maji na Roho wataipokea adhabu iyo hiyo kwa ajili ya dhambi kama watu wa ulimwengu watakavyopokea.
 
Aya ya 7: “Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.” 
Hapa Mungu anatueleza kwamba atazilipa dhambi za watu hawa wenye majivuno kwa maumivu na huzuni. Mungu ataziulizia dhambi za kila mmoja wao na kuwaadhibu, yaani kwa watu wote wa kidini wa hapa ulimwenguni ambao hawajazaliwa tena upya, na kwa watu wa kidunia wasioamini. 
Hata hivyo, watu hao bado ni wenye majivuno, hali wakijisemea hivi, “Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.” Hivyo, Mungu atawaletea mapigo kwa ajili ya maangamizi yao. Watu hao wote watateseka kwa huzuni ya kupoteza mali zao zote za kidunia na wapendwa wao mara moja na kwa wakati mmoja kwa mapigo makuu yatakayoletwa na Mungu. 
 
Aya ya 8: “Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.” 
Kwa ujio wa mapigo saba, ambayo ni mapigo ya kifo, kuomboleza na njaa vitafuatia katika ulimwengu huu kwa siku moja. Mpinga Kristo na wafuasi wake wote wa hapa ulimwenguni wataadhibiwa na kuchomwa katika moto wa Jehanamu milele yote. 
 
Aya ya 9: “Na hao wafalme wa nchi, waliozini naye na kufanya anasa pamoja naye, watalia na kumwombolezea; wauonapo moshi wa kuungua kwake,”
Watu na wafalme wa ulimwengu huu watashuhudia kwa macho yao ulimwengu wao ukigubikwa na moto na matetemeko ya ardhi na kuharibiwa na mapigo ya mabakuli saba. Hivyo, wafalme wa hapa ulimwenguni watalia na kuomboleza, na kupiga yowe kwa sababu ya hasara yao. 
 
Aya ya 10: “wakisimama mbali kwa hofu ya maumivu yake, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu, Babeli, mji ule ulio na nguvu! Kwa kuwa katika saa moja hukumu yako imekuja.’”
Watu ambao hawakuamini kwamba ulimwengu huu utaanguka watashtushwa kwa hofu mara watakapouona ulimwengu mzima ukianguka mbele ya macho yao. Hukumu ya Mungu itashuka siku moja juu ya ulimwengu ambao unametameta kwa uzuri wake, na hivyo ulimwengu utaanguka mara moja. 
 
Aya ya 11-13: “Nao wafanya biashara wa nchi walia na kumwombolezea, kwa sababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena; bidhaa ya dhahabu, na fedha, na kito chenye thamani, na lulu, na kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na hariri, na nguo nyekundu; na kila mti wa uudi, na kila chombo cha pembe, na kila chombo cha mti wa thamani nyingi, na cha shaba, na cha chuma, na cha marimari; na mdalasini, na iliki, na uvumba, na marhamu, na ubani, na mvinyo, na mafuta ya mzeituni, na unga mzuri, na ngano, na ng`ombe, na kondoo, na farasi, na magari, na miili na roho za wanadamu.”
Ni nani atakayenunua au kuuza wakati maangamizi ya ulimwengu yatakapokuwa yamewadia? Wafanyabiashara wa nchi, pia, watalia na kuomboleza kwa hasara ya ulimwengu wao. Wakati Mungu atakapoyashusha mapigo ya mabakuli saba, hakuna mtu katika ulimwengu wote atakayekua akinunua kitu chochote. Ulimwengu huu hautaweza kujengwa tena, na badala yake Ufalme wa Kristo ujengwa juu yake. 
Hapa kuna orodha ya wafanyabiashara ambao walijistarehesha hadi siku hii ilipowadia. Lakini mambo haya yote yatakuwa hayana maana kwa muda wa siku moja, na hakuna hata mmoja ambaye atakuwa akiyatafuta mambo hayo ya kidunia. Mambo haya yote ndio yale ambayo dini za kidunia zinayafanyia biashara. Dini za ulimwengu zimefanya mambo yasiyodhaniwa kwa ajili ya tamaa yao ya fedha, zikiwa hazihofii hata kuuza roho za binadamu kwa ajili ya fedha. 
 
Aya ya 14-18: “Na matunda yaliyotamaniwa na roho yako yamekuondokea; na vitu vyote vilivyo laini na vitu vya fahari vimekupotea; wala watu hawataviona tena kamwe. Na wafanya biashara ya vitu hivyo, waliopata mali kwake, watasimama mbali, kwa hofu ya maumivu yake; wakilia na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule mkuu! Uliovikwa kitani nzuri, na nguo ya rangi ya zambarau, na nguo nyekundu, na kupambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu; kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa. Na kila nahodha na kila aendaye mahali popote kwa matanga, na mabaharia, nao wote watendao kazi baharini, wakasimama mbali; wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio mfano wa mji huu mkubwa!’”
Hivyo, watu hawataweza kuziona mali zao za kidunia kamwe. 
Wafanyabiashara ambao walipata utajiri kwa kupitia ulimwengu huu watalia na kuomboleza mara watakapouona ulimwengu wao ukivunjika. Wataomboleza kwa huzuni sana, maana ulimwengu utakapoanguka, wao nao wataanguka pamoja na huo ulimwengu, na mali zao walizojilundikia zitatoweka kwa siku moja. 
Wakati dini zilizojengwa katika misingi ya utajiri wa kidunia zitakapoanguka, watu wa ulimwengu huu watajikuta wakiomboleza, “ole, ole!” Pia wafanyabiashara wa kimataifa na manahodha wanaouzunguka ulimwengu nao wataomboleza. Watu hawa watalia kwa huzuni, “ni ustaarabu upi uliowahi kujengwa na mwanadamu uliokuwa mkuu na mzuri kuliko huu wa sasa?” 
 
Aya ya 19: “Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa.’” 
Wale wote ambao walifikiri kwamba ulimwengu huu utadumu milele watakuwa wakilia kwa huzuni mara watakapouona ulimwengu ukiangushwa kwa mapigo ya mabakuli saba. Wale watakaokuwa wamesalia katika ulimwengu huu watakuwa wakilia na kuomboleza baada ya kushuhudia ulimwengu mzima ukiangamizwa mara moja kwa mapigo ya mabakuli saba yakiletwa na Mungu, lakini kulia kwao kote hakutakuwa na maana yoyote, kwa kuwa wakati huo kila kitu katika ulimwengu huu kitakuwa kimeshafikia ukomo. Kama watakuwa na nguvu ya kulia wakati huo, basi wanapaswa kulia hivi sasa kwa ajili ya majaliwa yao, yaani kwamba wamepangwa kwenda kuzimu kwa sababu ya dhambi zao, na ili waweze kukombolewa toka katika maangamizi yao ya milele basi wanapaswa kuiamini injili ya maji na Roho. 
 
Aya ya 20: “Furahini juu yake, enyi mbingu, nanyi watakatifu na mitume na manabii; kwa maana Mungu amehukumu hukumu yenu juu yake!”
Watakatifu walionyakuliwa angani watafurahia wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapoletwa, maana Mungu atawalipia kisasi kwa mapigo haya. Ni jambo sahihi kwamba Mungu atayamimina mapigo makubwa na ya kutisha kwa maadui zake. 
 
Aya ya 21: Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa.”
Hapa Mungu anatueleza kwamba ulimwengu huu hautaonekana tena kama vile jiwe ka kusagia lilivyotupwa katika bahari. Kisha Bwana wetu ataufanya ulimwengu huu kuwa mpya pamoja na vitu vyote ndani yake, na ataitimiza kazi yake ya kuubadili ulimwengu huu kuwa Ufalme wa Kristo. 
 
Aya ya 22: “Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yo yote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa;”
Wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapoisha, hakuna sauti ya muziki ambayo watu waliwahi kuisikia katika ulimwengu huu itakayosikiwa tena, wala hakutakuwa na sauti ya fundi wa aina yoyote ile itakayosikika. 
 
Aya ya 23: “Wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako.”
Wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapokamilika, ulimwengu huu hautaona tena mwanga wa taa, wala kusikia sauti ya bibi na bwana harusi. Pia uongo wa wachawi hapa ulimwenguni pia utaisha, maana ulimwengu utakuwa umeisha. 
 
Aya ya 24: “Na ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.”
Sababu itakayomfanya Mungu kuyamimina mapigo makuu ya mabakuli saba juu ya dunia hii ni kwa sababu watumishi wa Shetani watakuwa wameimwaga damu ya manabii na watakatifu wake.