Search

דרשות

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[2-9] Je, Umeokolewa Kwa Maji na Roho? (Ufunuo 2:18-29)

(Ufunuo 2:18-29)
 
Kanisa la Thiatira lilizifanya kazi za Mungu kwa upendo, imani, na uvumilifu, na matendo yake yaliendelea kuwa mazuri kadri muda ulivyozidi kwenda. Lakini kwa wakati huo huo, lilikuwa ni kanisa ambalo lilikuwa limevamiwa na nabii mwovu wa kike. Kwa lugha tofauti, makosa ya kanisa hili yalitokana na ukweli kuwa baadhi ya waumini wake walikuwa wamedanganywa na huyu nabii wa kike mwovu kuabudu sanamu na kuzini. Hivyo, Mungu alilitaka Kanisa la Thiatira kutubu na kuishikilia imani yake ya kwanza hadi mwisho. Pia Bwana aliahidi kuwa atawapatia mamlaka na nyota ya asubuhi wale ambao wanailinda imani yao hadi mwisho.
 

Baali wa Yezebeli 
 
Yezebeli alikuwa ni binti wa mfalme asiye myahudi ambaye aliuleta mungu wake wa kipagani wa Baali kwa Waisraeli wakati alipokuwa mke wa Mfalme Ahabu (1 Wafalme 16:31). Baali alikuwa ni mungu wa kipagani aliyejulikana kama mungu wa jua, alikuwa ni sanamu ya Wafoinike ambayo watu waliiabudu kwa ajili ya kujitakia mafanikio. Picha za mungu huyu zilichorwa na kuabudiwa ambapo waumini wake waliomba kwa ajili ya uzazi wa familia zao na nchi. Matendo haya yalikuwa ni sawa na matendo ya jumla ya kipagani ya kuiabudu nchi na asili katika sehemu mbalimbali duniani. Kwa mfano, kuamini kuwa uungu au mungu yupo katika mwamba mkubwa na kisha kuabudu mwamba huo ambao ni kitu cha kawaida cha asili. Matendo ya kidini ya namna hiyo yanashikiliwa na wale wanaoabudu miungu wengi.
Kutokana na kutambulishwa kwa huyu mungu wa kipagani na Yezebeli, basi Baali akawa mungu mkubwa wa waabudu sanamu kwa watu wa Israeli. Mfalme Ahabu ambaye alikuwa akimwabudu Mungu wa kweli Yehova alianza naye kumwabudu Baali kwa sababu alikuwa amemwoa mwanamke huyu wa wamataifa. Waisraeli wengi walizifuata nyayo zake na wakamwacha Mungu wao wa kweli na badala yake wakafanya uabudu sanamu kwa kumwabudu Baali. Kwa sababu hiyo walijiletea hasira ya Mungu juu yao.
Mungu alimkemea mtumishi wa Kanisa la Thiatira kwa kuiruhusu imani ya nabii wa uongo wa kike Yezebeli katika Kanisa. Mungu alimwonya Yezebeli na wafuasi wake kuwa kama wasipotubu atawaletea mateso na maangamizi.
Hii ina maanisha kuwa kanisa la kweli la Mungu haliwezi kuruhusu mali na utajiri wa vitu kutawala lengo la kanisa. Hii ina maanisha kuwa waumini wa leo hawawezi kuuabudu ulimwengu kama mungu wao kama Waisraeli walivyomwambudu Baali, mungu wa jua, kwa ajili ya uzazi na mafanikio.
3 Yohana 1:2 inasema, “Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.” Tunapoiangalia imani ya Mtume Yohana, tunaona kuwa mkazo wake wa kwanza ulikuwa ni wa kufanikiwa kiroho au mafanikio ya kiroho. Mkazo wa kufanikiwa katika mambo mengine yote ulifuata baada ya mkazo wa kufanikiwa kiroho. Imekuwaje basi ambapo imani hii imebadilika katika ulimwengu wa sasa? Imani imebadilika na kuwa ile ambayo inatafuta baraka za kimwili tu hali ikiweka mafanikio ya kidunia mbele ya imani, hali ikidharau mambo mengine yote kuhusiana na ukuaji na mafaniko ya kiroho. Watu wengi wanamwamini Yesu si kwa ajili ya kuzilisha na kuzitajirisha nafsi zao, bali ni kwa ajili ya kuilisha miili yao kwanza.
Siku hizi kuna vikundi vingi vya kidini vinavyotuzunguka ambavyo vina sumu kali kama madawa ya kulevya, ambavyo vinadai kuwa vinaweza kutoa utajiri kwa wafuasi wao ikiwa tu watakubali kuabudu nao. Ibada ya Yezebeli ilikuwa sawa na ya vikundi hivi. Watu wengi wanavifuata vikundi vya kidini vya jinsi hiyo kwa ajili ya kutafuta mafaniko ya uzazi na mali kimwili.
Katika makanisa ya leo ya waliozaliwa tena upya, baadhi wanaweza kurudi nyuma na kuiruhusu imani ya Yezebeli ili iweze kukuza idadi ya waumini. Lakini kitendo kama hicho ni sawa na kuwa na sanamu za miungu katika Hekalu la Mungu.
Yezebeli aliuleta mungu wa kipagani katika Israeli hata katika Hekalu halisi la Yehova. Kwa kweli aina hii ya imani ambayo inafuata mafanikio ya kimwili na mapato ya kidunia hali ikiwa haiutambui ukombozi wa dhambi katika Yesu ni imani potofu ambayo ni sawa na kuabudu sanamu mbele ya macho ya Mungu.
Makanisa ya leo ulimwenguni kote yana hubiri toka Yohana 1:29 yakisema, “Dhambi zako zote zimekwisha, kwa kuwa Yesu alizichukua dhambi zote Msalabani.” Wameufanya ubatizo wa Yesu kuwa ni kitu cha kawaida tu huku wakidai kuwa wokovu unapatikana kwa kumwamini Yesu kwa sehemu na kwamba si lazima kuuamini ubatizo wake. Lakini ubatizo ambao Kristo aliupokea toka kwa Yohana, yaani ubatizo ambao kwa huo Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake si kitu cha hiari au cha kuchagua ambacho tunaweza kukiamini au la. Kitendo cha kuuchukulia ubatizo wa Yesu kuwa ni kitu cha kawaida tu ni sawa na kumwabudu Baali.
Kwa nini basi watu hawa wanaihubiri injili pasipo ubatizo wa Yesu? Wanafanya hivyo kwa sababu tumaini lao halipo katika Ufalme wa Mungu bali katika utajiri wa kidunia hapa duniani. Watu walio na aina hii ya imani ni sawa na wale waliokuwa wakimwabudu mungu wa kipagani Baali.
Wale ambao walikuwa wameiamini injili ya maji na Roho hapo kwanza, na ambao kwa sasa wanahubiri juu ya damu ya Msalaba tu, basi ni vema watambue kuwa wanafanya dhambi iliyo sawa na ile ya kuabudu sanamu ya Baali.
Hakuna anayeweza kuhudumu vizuri ikiwa lengo lake litakuwa ni mapato ya mali za kidunia. Ikiwa wachungaji wangeliuacha ubatizo wa Yesu na kuhubiri juu ya damu ya Msalaba tu, basi ni hakika kuwa wangeliweza kujilimbikizia mali na mapato ya humu duniani. Lakini ni lazima watambue kuwa imani ya jinsi hiyo na mahubiri ya jinsi hiyo si kweli. 
Tukikiangalia kifungu cha maandiko cha Ufunuo, tunaweza kuona kuwa kiongozi wa Kanisa la Thiatira alimwabudu Baali katika Kanisa lake kama Yezebeli alivyomwabudu Baali.
Ikiwa watu hawaiamini injili ya maji na Roho, basi Roho Mtakatifu hawezi kukaa ndani ya mioyo yao na wala hawezi kufanya kazi ndani yao. Kama Mtume Paulo anavyotueleza, “lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake,” mtu atajulikana kuwa ni mwana wa Mungu ikiwa atakuwa na Roho wa Kristo katika moyo wake. Biblia inatueleza kuwa wale wasio na Roho ya Kristo wataachwa.
 
 
Wale Wanaoufahamu na Kuuhubiri Ubatizo wa Yesu
 
Wakati mtu anapoamini katika ubatizo (maji) wa Yesu, ambao kwa huo Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake, na kisha akaamini katika damu ya Msalaba, basi Roho Mtakatifu anaweza kukaa ndani ya moyo wa mtu huyo.
Lakini, ikiwa mtu haamini katika injili ya maji na Roho, basi hata kama mtu huyo angeuawa na kuifia-dini kwa ajili ya Yesu, basi ni hakika kuwa huko kuifia-dini hakutakuwa sahihi bali kutalinganishwa na kujitakia haki binafsi. Baadhi ya watu hali wakiwa wanaiamini damu ya Yesu Msalabani tu, wanakwenda katika maeneo ya mbali ya dunia kuihubiri injili hali wakiyatoa maisha yao yote katika kazi ya utume, na wakati mwingine wanauawa na kuifia-dini kwa ajili ya imani yao.
Hali wakiwa wamevutwa na upendo wa Kristo, baadhi ya watu wanaweza kuuawa na kuifia-dini hata kama wanaiamini damu ya Kristo Msalabani tu. Lakini kama Mathayo 7:23 inavyotueleza, kutakuwa na jambo gani jema ikiwa Bwana atakataa kuzitambua kazi zao zote na huko kujitoa kwao? Haitajalisha jinsi walivyoieneza injili kwa uaminifu na kwa moyo kama Wamomoni wanavyofanya. Kwa kuwa watakuwa hawakuihubiri injili ya maji na Roho, basi imani yao na juhudi zao zote zitakuwa ni bure.
Mungu alimkemea mtumishi wa Kanisa la Thiatira kwa kuwa aliwaruhusu wafuasi wa imani ya Yezebeli kuchipua katika Kanisa na pia alivumilia ukuaji wa wafuasi hao. Siku hizi kuna viongozi wengi wa kidini ambao wapo hivi, yaani wale wanaotafuta kuzidanganya nafsi. Kanisa la kweli la Mungu ni lazima liwe na imani sahihi na kuieneza injili inayojengwa katika kuzaliwa kwa Yesu, ubatizo wake, kusulubiwa kwake, kifo chake, kufufuka kwake, na kupaa kwake mbinguni. Vinginevyo imani pasipo mambo kama hayo itakuwa haina maana.
Manabii wa uongo wanadai kuamini katika damu ya Yesu kunatosha na kunaweza kumsaidia mtu ili aweze kuokolewa na kwamba si lazima kutambua umuhimu wa ubatizo wa Yesu. Kwa kuwa wameuacha ukweli wa maji, ndio maana Ukristo umeharibika na kugeuka kuwa kama sehemu ya dini za ulimwengu. Na hii ndiyo sababu kwamba Ukristo umeshindwa kuleta wokovu kwa watu wote ulimwenguni.
Ukristo umegeuka na kuwa kama dini ya kawaida inayokazia juu ya maadili ya kiulimwengu kwa sababu imekosa ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani. Huko Ulaya na Marekani ya Kaskazini, ambapo idadi kubwa ya watu ni Wakristo, dini za mashariki zimekuwa maarufu sana. Kwa nini? Kwa sababu dini ya Ukristo haikuweza kuwapatia watu ondoleo kamili la dhambi zao na wala haikuweza kuwapatia imani ya kweli katika Mungu, na kwa sababu hiyo watu wengi wamevutwa na hali ya kimafumbo ya dini za mashariki na wanafikiri kuwa ndio mbadala mzuri kwa dini za magharibi.
Sasa ni wakati wetu kuitafakri kwa upya injili ya maji na Roho na hali ya Ukristo wa sasa. Ni lazima tujiulize kuwa ni kwa nini ukweli wa Ukristo umegeuka na kuwa kama ulivyo hivi leo, na kwamba ni kwa nini Ukristo wa leo unaonekana kuwa hauna maana machoni pa watu wengi hivi leo. Jibu la maswali haya linapatikana katika injili ya maji na Roho. Tendo la kumwamini Yesu pasipo kuifahamu injili ya maji na Roho ni sawa na kumwabudu Baali mbele ya macho ya Mungu mwenyewe. Kitu ambacho ni kiovu kabisa mbele za Mungu ni kile cha kukataa kuiamini injili ya maji na Roho kuwa ndio ukweli wa wokovu halisi.
Ukristo wa leo unapambwa na uzuri wa kidunia badala ya kupambwa na uzuri wa injili ya maji na Roho. Makanisa saba ya Asia yalimtumikia Bwana kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani. Lakini, kama ilivyoonyeshwa katika Biblia, kwa sehemu na wao pia waliufuata ulimwengu hasa kadri injili ya maji na Roho ilivyokuwa ikizidi kusukumiwa nje na mahali pake kuchukuliwa na ulimwengu ndani ya mioyo ya watu.
Ni kitu gani ambacho kitatokea ikiwa kanisa haliuhubiri ukweli wa wokovu, ambayo ni injili ya maji na Roho, na badala yake likahuburi juu ya damu ya Msalaba tu? Nimetoa swali hili kwa sababu hata kanisa la Mungu ikiwa litaufuata ulimwengu, basi ni hakika kuwa litaharibiwa na ulimwengu na litaanza kusema si mbaya ikiwa tutauacha ubatizo wa Yesu katika kuokolewa.
 

Tofauti Kati ya Injili Yenye Ubatizo wa Yesu na Injili Isiyo na Ubatizo wa Yesu 
 
Wewe na mimi, tumepokea ondoleo la dhambi zetu zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Injili hii ya maji na Roho ndio ukweli wa Bwana, huku ubatizo wa Yesu, damu yake Msalabani, na Roho Mtakatifu ndio ushahidi wa wokovu wetu.
1 Yohana 5:5-7 na 1 Petro 3:21 zinatueleza kuwa “maji”—yaani ubatizo, ni alama ya wokovu, na hili ni Neno lilelile la wokovu linalopatikana katika Mathayo 3:15 ambapo Yesu alizichukua dhambi zote za mwanadamu katika mwili wake kwa ubatizo wake. Wakati ubatizo wa Yesu ni wa muhimu sana kiasi hiki, inawezekanaje basi kuudharau ubatizo wa Kristo na kisha kuhubiri juu ya damu yake Msalabani tu? Wale waliokombolewa toka katika dhambi ni lazima wachore mstari wa wazi kuhusiana na wokovu kwa kuliamini Neno. Ni lazima wajikumbushe mara kwa mara ili mstari huo wa wokovu uweze kuwa wazi zaidi.
Ikiwa mtu hawezi kuuchora mstari wa wazi wa mpaka kuhusiana na wokovu wake, basi hii inaweza kumaanisha kuwa mtu huyo bado hajaokolewa. Ni makosa kufikiri kuwa ukombozi wetu toka katika dhambi ni hatua ya juu katika imani yetu. Ukombozi toka katika dhambi si hatua ya uthibitisho wa kiroho, bali ni msingi hasa wa imani yetu, ambayo ni hatua muhimu katika kujenga nyumba yetu ya imani juu ya mwamba.
Pia hatupaswi kufikiria juu ya suala la wokovu kama “sehemu ya mafundisho ya kiimani” ya madhehebu tofauti. Mafundisho ya kiimani yanaweza kutofautiana kati ya dhehebu na dhehebu, lakini ukweli wa Biblia, yaani ule ukweli kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, hauwezi kutofautiana toka imani hata imani. Hii ndio sababu hatuwezi kuacha suala muhimu la ubatizo wa Yesu tunapoihubiri injili ya maji na Roho.
Hatuwezi kuuacha ubatizo wa Yesu na kisha kumhubiri Yesu kuwa ni “Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu” tu, au kuhubiri kuwa watu wanaweza kuokolewa kwa kuiamini damu ya Msalaba tu. Ni lazima tupokee ondoleo la dhambi zetu kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo na pia katika damu yake Msalabani. Inawezekanaje kwa mtu kuondolewa dhambi zake zote kwa kuamini katika damu ya Kristo Msalabani pasipo pia kuamini juu ya ubatizo wa Yesu? Wakati watu wanapoamini juu ya damu ya Msalaba tu, je, dhambi za dhamiri zao zinaondoka pia? Kwa kweli hapana!
Yesu anaishuhudia haki ya Mungu, dhambi zetu, na hukumu yetu kwa kupitia Biblia. Imani ya kweli ambayo tunatakiwa kuwa nayo ni imani katika ufahamu huu wa kweli kuhusiana na agano la Kristo. Nina maanisha nini ninaposema kuhusu ufahamu wa kweli? Nina maanisha ni kuwa na uelewa wa wazi kuhusu dhambi zetu ambazo zitakuhukumiwa na Mungu, kuifahamu haki ya Mungu, na kuifahamu aina ya imani ambayo haikubaliki mbele za Mungu. Ni kwa kuyafahamu haya ndipo imani ya kweli inapoweza kuchipua toka katika ufahamu wetu wa kweli.
Ikiwa tunapoihubiri injili tunauacha ubatizo wa Yesu au damu ya Yesu Msalabani, basi kile tunachokihubiri hakiwezi kuwa ni injili ya maji na Roho. Ikiwa tunauchukulia ukweli wa Mungu kwa viwango vyetu vya kibinadamu na kisha tukahubiri kuwa mtu yeyote anaweza kuwa asiye na dhambi kwa kumwamini Yesu tu, basi ni hakika kuwa wale wanaohubiri na wale wanaohubiriwa hivyo watabakia kuwa wenye dhambi. Tendo linalohusiana na ukweli kuwa tunauhubiri ubatizo wa Yesu au la linaleta tofauti kubwa katika kuziokoa roho za watu.
Tunapoiangalia imani ya mitume, tunaona kuwa hawakuihubiri damu ya Msalaba tu. Mitume wote waliamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani kama kazi moja ya wokovu. Hoja inayosema kuwa Yesu alizishughulikia dhambi zetu zote pale Msalabani pasipo kuamini kuwa alizichukua kwanza dhambi hizo kwa ubatizo wake, ni hoja ambayo haipatani na ufahamu wa kibinadamu lakini kubwa zaidi ni kwamba hoja hiyo haiendani na kukubaliana na ukweli wa maji na Roho. Wale wanaoimani injili nusu ya jinsi hiyo hawawezi kukombolewa toka katika dhambi zao.
 

Kazi za Mhubiri wa Injili
 
Tukiongea kwa mtazamo wa kibiblia, washenga wa kiroho ni wale ambao wanaihubiri injili ya maji na Roho. Washenga hawa wa wokovu wa kiroho ni lazima wawe wapatanishi kati ya Bwana na mabibi harusi. Kitu cha kwanza ambacho wanapaswa kukifanya ni kuwahubiria wenye dhambi juu ya yale ambayo Bwana ameyafanya kwa ajili yao. Ni lazima wafundishe kuwa Yesu alibatizwa ili kuzichukua dhambi zao katika mwili wake, na kwamba alihukumiwa Msalabani kwa ajili ya dhambi hizi zote. Pia ni lazima wapambanue ikiwa mabibi harusi wanaelewa hivi au la, na kwamba ni lini wanapoamini hivi, na ikishafikia hapo basi kazi ya hawa washenga inakuwa imekamilika.
Ili kuweza kulifikia hili, ni muhimu sana kwa washenga kuelezea kwa mabibi harusi kuwa bwana harusi ni nani na juu ya yale yote ambayo ameyafanya kwa ajili yao ili kwamba mabibi harusi waweze kuelewa kwa urahisi. Mioyo ya mabibi harusi inapotambua yale ambayo bwana harusi ameyafanya kwa ajili yao, basi washenga ni lazima wawafundishe tena mabibi harusi ule ukweli kuwa bwana harusi amezichukulia mbali dhambi zao zote kwa maji na damu yake.
Mabibi harusi wanapoyapokea mambo yote ambayo bwana harusi ameyafanya kwa ajili yao, basi hapo ndipo wanapofanyika kuwa mabibi harusi wa Kristo. Wale waliofanyika kuwa mabibi harusi wa Yesu Kristo wanatambua kuwa bwana harusi aliwanunua kwa gharama ya injili ya maji na Roho. Ni lazima watambue kuwa, bwana harusi amezisafishilia mbali dhambi zao zote kwa maji na damu yake, akawafanya kuwa weupe kama theluji, na akawapokea kama mabibi harusi kwa lengo la kuwafanya kuwa watu wake.
Hapo ndio mabibi harusi wanapoweza kumheshimu na kumtambua bwana harusi milele. Wale waliopokea ondoleo la dhambi zao zote ndio walio wenye haki, wenye haki hawana dhambi, na wasio na dhambi ni mabibi harusi wa Yesu Kristo. Mabibi harusi wanapokuwa na imani kama hiyo, basi wanaweza kuolewa na bwana harusi, na bwana harusi anaweza kuwapokea mikononi mwake. Kwa hiyo, ni pale tu washenga wanapokuwa wamewaandaa mabibi harusi kwa Neno la kweli ndipo mabibi harusi hao wanapoweza kuandaa vema ndoa yao.
Ili waweze kufanikiwa, washenga wa wokovu wa kiroho ni lazima wafahamu aina ya mabibi harusi ambayo bwana harusi anataka. Yesu, ambaye ni bwana harusi wetu, hana dhambi. Yeye ni mtakatifu. Hii ndiyo sababu inayofanya Yesu kutaka mabibi harusi wasio na dhambi wala mawaa. Na hii ndiyo sababu washenga wanatumia kazi au matendo ya bwana harusi kuwasafisha na kuwapamba mabibi harusi. Upambaji wa mabibi harusi una maanisha kuwa wataletwa kwa bwana harusi wakati dhambi zao zitakapokuwa zimesafishiliwa mbali kikamilifu kwa injili ya maji na Roho iliyotimizwa na bwana harusi. Ikiwa wangeliletwa kwake wakati dhambi zao zimesafishwa nusu yake, basi ni hakika kuwa bwana harusi asingeliwapokea, kwa kuwa anataka mabibi harusi wawe hawana dhambi kabisa. Watumishi wa Mungu wanaofanya jukumu hili ni washenga wa wokovu wa kiroho.
Hivyo, watumishi wa Mungu, ni lazima waendelee kuwaandaa mabibi harusi kwa ajili ya wokovu wao wa kiroho. Wakati huo huo, ni lazima tutambue kuwa katika Ukristo wa leo kuna washenga wengi sana wa kimwili ambao wapo kwa ajili ya kupata faida na vitu mahali popote. Hawa washenga wa kimwili watapigwa na Yesu Kristo na hata na mabibi harusi waliokataliwa. Hatupaswi kuwa washenga wa kimwili.
 

Kukifahamu Kina cha Shetani
 
Hata miongoni mwa watumishi na watu wa Mungu kuna wengi ambao hawakifahamu kina cha hila za Shetani. Kwa maneno mengine, kuna wengi ambao hawatambui jinsi Shetani anavyojaribu kwa nguvu kutukwaza. Watumishi wengi sana wa Mungu wameshindwa kutambua jinsi Shetani alivyoibadilisha injili ya maji na Roho, na jinsi alivyowafanyia hila waamini katika kufuata imani ya uongo. Kwa matokeo hayo, waamini wengi katika Yesu wameishia kuwa na injili iliyoharibiwa badala ya injili ya kweli ya maji na Roho, na kwamba hata nafsi zao ambazo zipo kinyume na mapenzi ya Mungu zimeharibiwa.
Mungu anatueleza kuwa, “Msiyafuate mafundisho ya kiimani ya Yezebeli. Aminini na muihubiri kwa nguvu injili ya maji na Roho hadi siku nitakapokuja. Ndipo nitakapowapatia mamlaka juu ya mataifa.” Lakini, Mungu anatueleza kuwa atawatupa katika mateso wale ambao wamedanganywa na imani ya Yezebeli.
Utakapowadia wakati wa kurudi kwa Kristo, basi hapo tutaweza kuwaona wale ambao waliuhubiri wokovu kwa damu ya Yesu tu wakiisaliti imani zao. Mara nyingi watu hawa wanajivunia imani yao huku wakijiona kuwa ni bora kuliko wale wenye imani inayotofautiana na yao. Lakini Mungu anatofautisha kati ya imani yao na imani ya wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho: “Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyazi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.”
Wakati Bwana wetu atakaporudi katika dunia hii, kutakuwa na Wakristo wengi ambao watakutana na Bwana pasipo kuzaliwa tena upya. Kwa kuwa hawakuiamini injili ya maji na Roho, basi Wakristo hao watakutana na Bwana hali wakiwa na dhambi katika mioyo yao. Lakini kwa upande mwingine, wale ambao mioyo yao imesamehewa dhambi zao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho watabadilishwa kufuatia ujio wa Bwana na watatawala pamoja naye. Kama inavyosemwa hapa, mamlaka ya Bwana na watu wake ni kama nguvu ya fimbo ya chuma inavyoponda vyombo vya mfinyanzi.
Ni hakika kuwa Mungu atawapatia mamlaka juu ya mataifa wale wote wanaoilinda imani yao katika injili ya maji na Roho hadi mwisho. Bwana wetu anatueleza kuwa mamlaka haya ni sawa na mamlaka ambayo ameyapokea toka kwa Baba. Ni lazima tupambane na kuwashinda manabii wa uongo kama Yezebeli na Balaam ili kwamba tuweze kutawala milele kwa mamlaka juu ya mataifa ambayo Bwana atatupatia.
 

Uwazi wa Kweli ya Wokovu!
 
Ili kuwaokoa wenye dhambi ilimpasa Bwana wetu kuja hapa duniani na kuzichukua dhambi zote za mwanadamu katika mwili wake, na kwa sababu hiyo ilimpasa kubatizwa na Yohana. Kwa kuwa Bwana wetu alibatizwa ili kuzichukua dhambi zetu katika mwili wake, basi aliweza kuzibeba dhambi hizi hadi Msalabani, kufa juu ya Msalaba, na kisha kufufuka tena toka kwa wafu. Yesu aliyafanya haya matendo ya haki kwa ajili yetu kwa sababu hakutaka kuwaona wanadamu wakiendelea kuhangaika na dhambi zao. Injili ya maji na Roho ni ukweli unaoweza kukukomboa toka katika dhambi zako zote.
Na hapo ndipo Bwana wetu alipofanyika kuwa Mwokozi kwa wale wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho. Kwa kuwa Bwana alibatizwa na Yohana, ndio maana aliweza kuzaa matunda yenye matokeo kama inavyoshuhudiwa katika Yohana 1:29 na Yohana 19:30: “Tazama! Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” na “Imekwisha!” Wale walio na uhakika wa ukombozi wao kwa kupitia hili Neno la Mungu wanaweza kuwa na imani yenye nguvu kwa Yesu kwa sababu wanafahamu kuwa Yesu alizishughulikia dhambi zao zote kwa ubatizo wake. Kwa kweli ni lazima tuiangalie mioyo yetu, kwa kuwa kama hatuiamini injili ya maji na Roho, basi dhambi zetu zitaendelea kuwemo katika mioyo yetu.
Tunapojaribu kuiangalia kwa karibu mioyo ya wale wanaoudharau ubatizo wa Yesu na kuiamini damu yake ya Msalaba tu, tunaona kuwa uwepo wa dhambi katika mioyo yao hauwezi kuepukwa. Ni lazima tuuzingatie kipekee ubatizo wa Yesu alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji na kuuamini kwa nguvu zaidi, kwa kuwa hatuwezi kuongeza mawazo yetu wala kupunguza chochote katika Neno la Mungu. Sisi sote ni lazima tuzipinge injili za uongo kwa kuwa zinaweza kuharibu imani ya wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho.
Yesu mwenyewe alitueleza kuwa, “Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo.” “Chachu” inayotajwa hapa haimaanishi kuwa ni ile inayotumika katika kutengeneza pombe au mkate, bali ina maanisha kuwa ni injili isiyo na ubatizo wa Yesu. Ni lazima tufahamu na kuamini katika ukweli kuwa Yesu alizibeba dhambi za ulimwengu kwenda Msalabani baada ya kuwa amezichukua katika mwili wake kwa ubatizo wake, na kwamba kwa sababu hiyo amefanyika kuwa Mwokozi wetu wa kweli kwa kusulubiwa Msalabani na kwa kufufuka tena toka kwa wafu.
Kwa upande wake, Yesu alizipokea dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake toka kwa Yohana, na akazifanya dhambi hizo kutoweka kwa damu yake Msalabani. Lakini kwa upande wa watu, kwa kuwa hawaamini katika ubatizo ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana, basi dhambi zao zitaendelea kuwepo. Pasipo watu kuuamini ukweli kwamba Yesu alibatizwa na Yohana ili kuzipokea dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake, basi kimsingi, dhambi zao haziwezi kutoweshewa mbali. Injili ya maji na Roho ni injili yenye mamlaka na nguvu inayozisafishilia mbali dhambi zetu zote na kutufanya kuwa weupe kama theluji pale tunapoamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani.
 

Hebu Tuwe Wale Wanaoshinda
 
Toka katika kifungu hiki cha Ufunuo, tumeona Neno la Mungu likitamkwa kwa Kanisa la Thiatira. Mungu aliahidi kwa mtumishi wa Kanisa la Thiatira kwamba atampatia mamlaka juu ya mataifa. Kila mtakatifu aliyezaliwa tena upya anaishi katika uwanja wa vita vya kiroho hali akiwa katika vita vya kiroho. Ni lazima tushinde katika uwanja huu wa vita kwa imani yetu katika injili ya maji na Roho. Vita hii ya kiroho inaanza mara moja pale mtu anapoanza kuamini katika injli ya maji na Roho.
Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho ni lazima wamshinde Shetani katika mapambano yao dhidi yake. Baadhi yetu tunapambana dhidi ya Shetani na tutazishinda injili za uongo hadi siku ile tutakaposimama mbele za Mungu. Wale wanaoshinda wanaamini kuwa Bwana wetu amezichukulia mbali dhambi zetu zote kwa kuja hapa duniani, kwa kubatizwa, kwa kufa Msalabani, na kwa kufufuka tena toka kwa wafu. Haijalishi kuwa wengine wanasema nini, ukweli ni kuwa mahali ambapo dhambi zao zilianza kuchukuliwa na hatimaye kusafishwa ni katika Mto Yordani, ambapo dhambi zote zilikabidhiwa kwa Yesu kwa kupitia ubatizo ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana.
Bwana wetu ametuamuru kupambana na kumshinda Shetani. Miili yetu inaweza kutaabika sana na wakati mwingine kuchoka, lakini imani yetu katika injili ya maji na Roho haiwezi kupoteza vita hivyo dhidi ya injili za uongo.
Bwana wetu anatueleza kuwa, “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache” (Mathayo 7:13-14). Nabii Eliya wa Agano la Kale alipambana na kuwashinda zaidi ya manabii 450 wa Baali.
Pia Mtume Paulo alisema kuwa hakukuwa na injili nyingine zaidi ya ile aliyoieneza (Wagalatia 1:7). Injili hii ya Paulo haikuwa nyingine bali ni imani katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani. Wale wanaoamini katika injili hii hata kama wataendelea kuwa na mapungufu baada ya kuwa wamezaliwa tena upya ukweli unabaki kuwa hawana dhambi katika mioyo yao milele. Bwana wetu amezisafishilia mbali dhambi zetu zote kwa maji yake na aliipokea hukumu yote kwa ajili ya dhambi hizo kwa damu yake. Ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani vimeleta ukombozi wa milele kwa wale wote wanaoamini.
Bwana anawapatia wale waliookolewa mamlaka na nguvu ya kuilinda imani, na kupambana na hatimaye kushinda hadi mwisho.