Search

Khotbah-Khotbah

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[3-3] Barua Kwa Kanisa la Filadelfia (Ufunuo 3:7-13)

(Ufunuo 3:7-13)
“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapa afungaye, naye afunga hapana afunguaye. Nayajua matendo yako, Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu. Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wahayudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele za miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda. Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi. Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
 
 
Mafafanuzi
 
Aya ya 7: “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapa afungaye, naye afunga hapana afunguaye.”
Bwana anatawala juu ya Ufalme wa Mbinguni kama Mfalme wa wote. Yeye ni Mungu mwenye mamlaka kamili na nguvu—anachofungua hakuna anayeweza kufunga na anachofunga hakuna anayeweza kufungua. Bwana ni Mungu mkamilifu aliyekuja hapa duniani na akawakomboa wenye dhambi toka katika dhambi zao zote kwa injili ya maji na Roho. Lango la Mbinguni linaweza kufunguliwa kwa ufunguo wa injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Hakuna kitu kingine kinachoweza kulifungua lango hilo, kwa kuwa kila kitu kilichopo katika Ufalme huu wa Mbinguni kinamtegema Bwana Mungu, aliye Mungu wetu.
 
Aya ya 8: “Nayajua matendo yako, Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”
Bwana ameufungua mlango wa uinjilisti kwa kupitia Kanisa la Mungu. Kwa hiyo, hakuna anayeweza kuufunga mlango pasipo ruhusa toka kwa Bwana. Hivyo, watakatifu ni lazima waishikilie kwanza imani yao ya kwanza hadi siku ya mwisho Bwana atakaporudi. Hii ni aina ya imani ambayo watumishi wa Mungu na watakatifu wake wanatakiwa kuwa nayo. Imani yao haipaswi kuwa ile ambayo mwanzo wake ni mkubwa halafu mwisho wake ni mauti. Wakatifu hao ni lazima waishikilie imani yao ya kwanza, ambayo ni imani isiyobadilika na iliyotolewa na Bwana.
Imani ya watakatifu ni imani katika injili ya maji na Roho, ambayo ni imani inayoamini katika ukweli kuwa Ufalme wa Bwana wetu utakuja pamoja na Mbingu na Nchi Mpya, na kwamba sisi sote tutaishi katika Ufalme huu milele. Watakatifu ni lazima waishikilie imani hii hadi siku watakapokutana na Bwana anayekuja.
Watumishi na watakatifu wa Kanisa la Filadelfia walikuwa na nguvu kidogo. Pia walikuwa na mapungufu mengi. Hata hivyo, jambo ambalo ni la muhimu sana ni kuwa walilishika Neno la Mungu na hawakulikana jina la Bwana.
 
Aya ya 9: “Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wahayudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele za miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda.”
Mungu alisema kuwa atawafanya baadhi ya waamini wa uongo kuwasujudia waamini wa kweli ili kwamba waweze kutambua jinsi Mungu alivyolipenda Kanisa la Filadelfia, ambalo ni Kanisa lake.
Sentensi isemayo “Sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wahayudi, nao sio” ina maanisha ni Wayahudi ambao walijiona wao wenyewe kuwa ni wenye kumtukuza Mungu kwa imani yao. Lakini ukweli ni kuwa wengi wao hawakuwa ni wenye kumtukuza Mungu. Kinyume chake, Wayahudi hao walikuwa wamefanywa kuwa watumishi wa Shetani na walikuwa wakilizuia Kanisa la Mungu na watakatifu wake.
Tunapaswa kutambua kuwa hata sasa, kama ilivyokuwa hapo mwanzo, watu wengi miongoni mwa wale wanaoliitia jina la Yesu na kumwabudu Yesu pia wamegeuka na kuwa watumishi wa Shetani, hali wakitumiwa na Ibilisi kama vyombo vyake. Mungu alionyesha upendo maalum kwa mtumishi wa Kanisa la Filadelfia ambaye alimpenda na kumtumia kama chombo cha heshima.
 
Aya ya 10: “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.”
Mungu alifurahia kitendo cha mtumishi wa Kanisa la Filadelfia kwa kulishika neno la subira la Mungu. Kwa kweli pasipokuwa na aina hii ya subira, basi ni hakika kuwa hatuwezi kungojea kutimizwa kwa ahadi zote za Neno la Mungu. Hivyo, ili tuweze kuwa na subira na kuvumilia ni lazima tuwe na imani sahihi katika Neno la Mungu. Kwa kuwa Mungu alilipatia Kanisa la Filadelfia thawabu maalum kwa sababu ya subira na uvumilivu wake. Aina ya thawabu waliyopewa ni kuliepusha Kanisa la Filadelfia toka katika saa ya majaribu. Saa ya majaribu inayotajwa hapa ina maanisha ni vile vizuizi vya Mpinga Kristo.
 
Aya ya 11: “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.”
Kwa kuwa kurudi kwa Bwana kunakaribia, basi watakatifu ni lazima wailinde na kuitunza imani yao katika injili ya maji na Roho. Pia ni lazima waamini na kusubiri katika tumaini lao kwa ujio wa Mbingu na Nchi Mpya vilivyoahidiwa na Bwana. Watumishi wa Mungu ni lazima wawe pamoja na watakatifu na kuwalinda ili wasiipoteze imani yao, ili kwamba thawabu yao toka kwa Mungu isiibiwe.
 
Aya ya 12: “Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya.” 
Wale watakaomshinda Shetani watajiunga katika orodha ya wafia-dini. Pia majina yao yataandikwa katika Hekalu Takatifu la Ufalme wa Mungu. Hata sasa, watu hao wanatumika kama watenda kazi wakuu wa Kanisa la Mungu, na wataendelea kutumiwa kama vyombo na Bwana.
 
Aya ya 13: “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.” 
Wale walio na masikio ya kulisikia Neno la Mungu ni watumishi na watakatifu wa Mungu. Wanalisikia lile ambalo Roho anawaambia kwa kupitia kanisa la Mungu. Kwa hiyo, watumishi na watakatifu wa Mungu ni lazima wabakie ndani ya kanisa ambalo Mungu amewaruhusu, na ni lazima walitetee na kulilinda kanisa hili.