Search

Khotbah-Khotbah

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 7-5] Mwili Unaitumikia Sheria ya Dhambi (Warumi 7:24-25)

(Warumi 7:24-25)
“Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, Kwa Yesu Kristo Bwana wetu—Basi kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.”
 

Ni Kwa Sheria Ndio Maana Mwili unaitumikia Dhambi
 
Maisha yako ya kiimani yakoje? “roho i radhi lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:41). Je, wewe hauko hivi? 
Biblia inatueleza sisi pia kuwa, “kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.” Na hizo ndio sheria zinazotutawala. Mioyo yetu imeumbwa kumpenda Mungu na kuupenda ukweli, lakini ni kawaida kwa mwili kuitumikia sheria ya dhambi. Neno la Mungu linatueleza sisi kuwa moyo unaitumikia injili na haki ya Mungu ilhali mwili unaitumikia dhambi tu. 
Je, unafahamu kuwa sheria ya dhambi ni nini? Tunahitaji kuishi maisha ambayo ni ya uaminifu, hivyo sisi watakatifu na watumishi wa Mungu tunajisikia kuwa imara kama simba wakati miili yetu inapokuwa haiitumikii dhambi. Lakini hatuna nguvu pale miili yetu inapokuwa ikiitumikia dhambi na kuhusishwa na dhambi. Tunaweza kufikiria kuwa tunaweza kuwa na furaha na kuwa na ujasiri zaidi kwa kutotenda dhambi kamwe, lakini ukweli ni kuwa, hatuna ule ujasiri wa kutofanya dhambi kabisa. Mioyo ya watumishi wa Mungu inanyauka kwa sababu ya jambo hili. 
“♫Dhambi zangu zote zimeondoka! ♪Kwa kupitia neema ya Kalvari! ♫” Ingawa tunao ukombozi na tunamsifu Mungu kwa jinsi hii, ukweli ni kuwa bado hatuna ujasiri binafsi wa kuishi wakati tunapofikiria juu ya maisha yetu ya baadaye kiimani. Tunafikiria juu ya udhaifu wa mwili na hatimaye tunafikia hitimisho hili: “Sistahili kuishi kama hivi hapo baadaye; sistahili kufanya dhambi kabisa.” Lakini tunapomtegemea Mungu kwa mara nyingine na kusimama imara katika haki ya Mungu tunatoa ahadi kwa Mungu tukisema, “Bwana, nakushukuru. Halleluya. Nitakufuata hadi siku yangu ya kifo.” Basi baada ya ahadi hiyo tunamtumikia Mungu kwa mwamko, lakini hali hiyo haidumu muda mrefu kwa sababu mara baada ya kitambo kifupi tunajikuta kukatishwa tamaa na sisi wenyewe tunapofanya dhambi tena. Ukweli ni kuwa, watakatifu wote na watumishi wa Mungu waliookolewa wako hivi. Hivyo ndipo tunapokuja kukubaliana na ukweli kuwa mwili unaitumikia dhambi tu. 
Ninafahamu kuwa Bwana hapendi sisi tufungwe na udhaifu wa mwili. Hii pia ndiyo sababu iliyomfanya Paulo kuitenganisha roho toka katika mwili. “kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” Miili yetu haiwezi kuboreshwa. Mwili unaitumikia sheria ya dhambi tu. Paulo anasema kuwa hii ndiyo sheria. Mwili umeumbwa kufuata na kuitumikia dhambi tu. Je, unaelewa jambo hili? Ni sheria. Ni nani anayeweza kuibadilisha sheria? Wewe na mimi hatuwezi. Ni nani basi ambaye tunapaswa kumtumikia kwa mioyo yetu? Tunapaswa kumtumikia Mungu. Tunapaswa kumpenda Mungu, ukweli, nafsi na haki yake kwa mioyo yetu yote. 
 

Usitegemee Mengi Toka Katika Mwili
 
Mwili unapenda kukuza raha ya mwili, starehe, amani, furaha na majivuno yake, na si haki ya Mungu. Mwili unapenda vitu vyote vifanyike kama unavyopenda. 
Usitegemee mengi toka katika mwili ukisema, “sikiliza mwili, ninakutaka ufanye kazi nzuri.” Naomba uache matarajio yako kuwa mwili utafanya vizuri. Usidhanie kuwa miili yetu inampenda Mungu na haki yake, au kuwa miili yetu inapenda kuitumikia haki ya Mungu na kuteseka kwa ajili yake. 
Wale ambao wanategemea kitu kizuri toka katika mwili ni wajinga. Sasa tufanye nini? Kila kitu kinafanyika kwa mujibu wa sheria ya Bwana. Je, tunaweza kuibadili sheria ya Mungu hata kama tunaifahamu? Kwa kweli hatuwezi kuibadili kwa kuwa ni sheria ya Bwana. 
Ni sheria ya Mungu inayoufanya mwili uitumikie dhambi. Ikiwa tunajisikia kuwa tuna mfadhaiko na nyuso zetu zina giza, basi hii ni kwa sababu tunaitumikia dhambi. Miili yetu inapenda kuishi vizuri na kwa hiyo mara nyingi mwili unajihesabia haki wenyewe. Hebu tusijihesabie haki sisi wenyewe; bali tuuache mwili kama ulivyo. Ninataka wewe uishi kwa imani katika Bwana katika moyo wako. Mwili hauwezi kukwepa dhambi hadi utakapokufa kwa sababu mwili unaitumikia dhambi tu. Sisi wenyewe hatuwezi kuikwepa dhambi kwa kuitegemea nguvu yetu wenyewe. Unaweza kufikiri, “mwili unaweza kuwa mzuri zaidi.” Lakini hali haiko hivyo. Au inapotokea kuwa umetenda dhambi bila kutambua, unaweza kufikiri kuwa “ni kwa sababu ya mazingira mabaya.” Hapana! Kwa kweli si kwa sababu ya mazingira mabaya—bali mwili umeelemea katika kuitumikia dhambi tangu mwanzo!
Mwili haufanyi jambo lolote jema. Mwili unatenda dhambi hadi utakapokufa. “Je, mwili utakuwa mzuri zaidi?” Kwa kweli usitegemee kitu kama hicho kwa sababu utakatishwa sana tamaa. Haijalishi jinsi unavyoweka umakini katika fikra zako na kujisemea moyoni, “sintafanya kitu kama hicho,” mwili hauwezi kukusaidia bali kutenda mambo maovu hata kinyume ya vile unavyopenda. Je, ni nani miongoni mwetu ambaye hajawahi kuazimia katika mawazo yake kutotenda dhambi? Kila mtu ameshawahi kufanya hivyo! Lakini ni sheria ya Mungu kwamba mwili uitumikie dhambi tu. 
Makasisi wa Kikatoliki na watawa wa kila namna kutoka dini mbalimbali wanajitahidi kuishi maisha matakatifu kwa kupitia miili yao. Lakini haiwezekani kwa mwili kuishi pasipo mawaa. Mara nyingi watawa hao wanaishi maisha yao kama wanafiki. Haiwezekani kwetu kutenda mema kwa miili yetu. Mwili unaitumikia sheria ya dhambi. Hii ndiyo sheria ambayo Mungu aliianzisha. Kama ambavyo buu anavyoshinda kupaa angani wakati kereng’ende anafurahia kupaa angani, basi hivyo ndivyo ilivyo sheria. Kama ambavyo buu anapenda kula matope machafu vivyo hivyo mwili wa mwanadamu unapenda kutenda dhambi. Je, unaweza kusema kwa uaminifu kabisa kitu ambacho unaweza kukitegemea toka katika mwili wako? Kwa kweli hapana. Hii ndio sababu Mtume Paulo alisema, “kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” (Warumi 7:25).
Miili yetu inatenda dhambi hadi tutakapokufa. Haiwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea kufanya dhambi. Je, mwili hautatenda dhambi kamwe baada ya muda mrefu wa mafunzo? Hapana! Mwili hauwezi kufanywa bora zaidi. Je, kwa hiyo ni sawa kwa mwili kufanya dhambi kwa kadri utakavyo? Hapana! Hapa sizungumzii kuhusu hilo. Ninachomaanisha hapa ni kuwa mwili hauwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea kutenda dhambi. Dhambi zetu hazitegemei juu ya matakwa yetu au uwezo wetu. Sisi hatuwezi kufanya lolote la kujisaidia zaidi ya kuendelea kufanya dhambi, hata kama hatutaki kufanya dhambi na tunajikuta tunatenda dhambi hata pale tunapojaribu kwa nguvu kujizuia kufanya dhambi. 
“Lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapigana vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” (Warumi 7:23-24) Ni vigumu kwa mwili kufanya mema kwa sababu mwili unatuleta sisi katika utumwa wa sheria ya dhambi. 
Watu wanachukia kuusema ukweli huu na wanaona aibu kuuzungumzia. Wanasema, “unawezaje kulizungumzia jambo hili kwa wazi?” Lakini, Mtume Paulo aliyasema haya waziwazi? Mwili unaitumikia sheria ya dhambi. Tunaitumikia dhambi bila hata kujali ridhaa zetu hadi tutakapokufa. Sisi hatujazaliwa ili kufanya dhambi tu. Lakini, ni ukweli usiopingika kuwa mwili ni chombo cha dhambi. 
 

Bwana Anatuwezesha Sisi Kumtumikia Yeye kwa Ukamilifu
 
Wapendwa watakatifu, unawaza nini? Unafikiri kuwa unaweza kumtumikia Bwana kwa mwili wako ikiwa utajaribu kufanya hivyo? Je, inawezekana? Hapana!
Ni nani aliyetuokoa toka katika dhambi zetu zote? Yesu alituokoa. Je, ni kweli kuwa Yesu Kristo alitukomboa toka katika dhambi zetu zote za mwili ambazo zinaitumika sheria ya dhambi? Je, ni kweli kuwa Yesu alituokoa sisi ambao tunaitumikia sheria ya dhambi na kutenda dhambi katika kipindi chote cha maisha yetu zikiwamo dhambi za mwili? Kwa kweli jibu ni Ndiyo isiyo na shaka? Kwa kweli Yesu alifanya hayo! Kwa kweli ni vigumu kwa mwili kutofanya dhambi, na ni vigumu sana kwako kusamehewa dhambi zako na kukombolewa toka katika adhabu ya Mungu kwa kupitia mwili wako. Lakini Bwana aliyafanya hayo yawezekane. Bwana alitufanya sisi kuwa wenye haki na alituokoa toka katika dhambi zetu zote hata kama tunafanya dhambi mara kwa mara. 
Yesu Kristo Bwana wetu ametuokoa. Je, ni Bwana yupi aliyetuokoa sisi? Ni Yesu Kristo. Basi Yesu ni nani? Yeye ni Mwana wa Mungu na Bwana wa waamini wote. Yeye ni Bwana ambaye ametuokoa. Yesu Kristo Bwana wetu alitufanya sisi kuwa wakamilifu toka katika dhambi zote. Yesu Kristo alituwezesha sisi kumtumikia yeye. 
Bwana alituwezesha sisi kuishi pasipo kuwa na dhambi. Bwana asiyeonekana na mwenye uwezo aliyetuumba sisi alituokoa toka katika dhambi zetu zote. Hata kama mwili unaitumikia sheria ya dhambi hadi utakapokufa, Bwana wetu alituokoa kikamilifu na ametufanya kuwa wenye haki. Hii ni sababu Mtume Paulo alimshukuru Mungu kwa kupitia Yesu Kristo ambaye ni Bwana. Hata sisi hatuna shukrani za kutosha kumpatia Mungu kwa kumtuma Bwana wetu Yesu Kristo. 
Ni lazima tutambue jinsi ambavyo wokovu wa Bwana ulivyo wa kushangaza na jinsi ulivyo mkuu na wenye neema. Kwa kweli hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kumshukuru Bwana kwa nguvu zake kuu ambazo zimeikoa miili yetu yenye ufisadi ambayo haifanyi lolote zaidi ya kutenda dhambi hadi itakapokufa. Bwana alituokoa kwa nguvu zake na amevifanya viungo vyetu kuwa ni vyombo ya kumtumikia yeye kwa imani. Bwana alituokoa kikamilifu ili kwamba tusiendelee kamwe kuwa watumishi wa dhambi. 
Je, Bwana wetu hajatuokoa kikamilifu? Kwa kweli ametuokoa! Ametuokoa sisi kikamilifu na kwa usahihi. Bwana alituwezesha sisi kumtumikia yeye kwa ukamilifu. Ni nani aliyefanya hayo mambo makubwa? Bwana wetu aliyafanya hayo! Ni nani aliyewabadili wale ambao hawakuweza kufanya lolote zaidi ya kuendelea kufanya dhambi kwa miili yao kufanyika wenye haki na kisha kumtumikia Mungu? Bwana wetu aliyafanya hayo! Bwana alituokoa sisi ambao tunafanya dhambi katika kipindi chote cha maisha yetu toka katika dhambi zetu zote. Pia alitubadilisha ili kwamba tuweze kuitumikia haki yake. 
 

Bwana Ametuokoa Sisi Toka Katika Dhambi Zetu Zote. 
 
Ni lazima tulifikirie jambo hili kwa sababu sisi ni wanadamu. Kwa sababu mimi ni mwanadamu ninafikiria jinsi wokovu wa Bwana ulivyo wa kushangaza. Kama ningalitambua kuwa mwili unaitumika dhambi tu basi kwa kweli ninge katishwa tamaa wakati wote. Pamoja na kuwa nilikuwa nimeshapokea msamaha wa dhambi, bila shaka ningekuwa nimeyakatia tamaa maisha ya kiimani kwa sababu ya dhambi zangu. 
“Kabla sijaokolewa, niliweza kuvumilia hata kama nilitenda dhambi. Lakini kama ninaendelea kufanya dhambi hadi sasa, basi kunakuwa hakuna tofauti kati ya kuokolewa au kutookolewa. Je, matumizi ya kuzaliwa tena upya ni yapi?” Unaweza kufikiria kuwa unapaswa kuwa mzuri zaidi ya ulivyokuwa hapo awali. Unaweza kujihisi kuwa kwa kuwa sasa umeokolewa bila shaka mwili wako unaweza kuwa mzuri zaidi kuliko zamani ulipokuwa bado hujaokolewa. Wale ambao hawajazaliwa tena upya bado hawaelewi kile ninachokisema. 
Tunaweza kumshukuru Yesu pale tu tunapofahamu na kuamini kuwa dhambi zote za mwili zimesamehewa. Ninamshukuru Bwana ambaye alizichukulia mbali dhambi zangu zote ambazo ninazozifanya hadi nitakapokufa. 
Katika toleo la awali la kitabu cha nyimbo cha Kikorea, kulikuwa na wimbo uliokuwa ukisema: “♪Halleluya! Msifuni Mungu! ♫Dhambi zangu zote zilizopita zimesamehewa! Na ninatembea na Bwana Yesu, basi sasa kila ninakokwenda ni Ufalme wa Mbinguni ♪” Je, hii ina maanisha nini? Ikiwa Bwana alizichukua dhambi zetu zilizopita tu, je ni nini kinachofuata? Maana yake ni kuwa tusitende dhambi tena kwa mwili; na kwamba tunapaswa kuomba toba kwa kina kila inapotokea kuwa tumefanya dhambi, na kwamba tuishi vizuri. Lakini ufahamu kama huu ni mbinu mbaya ya Shetani. 
Hakuna kitu ambacho ni kitamu kama mbinu hii. Shetani anaturubuni akisema, “dhambi zako zote zilizopita zimesamehewa. Kwa hiyo ikiwa utatembea pamoja na Yesu na ikiwa hutatenda dhambi tena basi unaweza kuingia katika Ufalme wa Mungu. Lakini kila inapotokea umetenda dhambi hapo baadaye basi unapaswa kutoa sala za toba ili uweze kusamehewa na uweze kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. Umenielewa?” Basi watu wengi wanaamini hivi wanapoisoma Biblia. Wanaimba nyimbo hali wakilia, “♪Halleluya! Msifuni Mungu! ♫Dhambi zangu zote zilizopita zimesamehewa! Na ninatembea na Bwana Yesu, basi sasa kila ninakokwenda ni Ufalme wa Mbinguni ♪”. 
Lakini bado hawawezi kuacha kutenda dhambi. Hiyo ni sheria ya Mungu juu ya mwili. Mwili hauwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea kufanya dhambi tena na tena. Na kwa hiyo wanafikiria kuwa wanapaswa kuomba toba. Wanazitamka sala za toba kwa juhudi ili waweze kupokea msamaha wa dhambi zao za kila siku. Wanaimba nyimbo hizi baada ya maombi hayo, “♪Halleluya! Msifuni Mungu! ♫Dhambi zangu zote zilizopita zime samehewa! Na ninatembea na Bwana Yesu, basi sasa kila ninakokwenda ni Ufalme wa Mbinguni ♪”. Lakini hali hii inadumu kwa siku mbili au tatu? Mara nyingi wanatenda tena dhambi ndani ya masaa kadhaa tu na sio siku kadhaa. Wanaweza kuomba na kufunga kwa ajili ya msamaha, lakini hawawezi kukwepa toka katika sheria hii ya Mungu isiyobadilika hali wakiwa wanaishi katika mwili. 
Je, maneno ya wimbo huu ni ya kweli? Je, ni dhambi zako za kale tu ndizo zilizosamehewa? Bwana wetu amezichukulia mbali dhambi zetu zote na wala si dhambi zetu za kale tu. Sasa tunaweza kumsifu Mungu tukisema, “♪Halleluya! Msifuni Mungu! ♫Dhambi zangu ZOTE zimesamehewa! Na ninatembea na Bwana Yesu, basi sasa kila ninakokwenda ni Ufalme wa Mbinguni ♪”. 
Wale waliookolewa wanaweza kuchanganyikiwa baada ya kutenda dhambi tena hasa pale wanapokuwa hawafahamu kuwa ni sheria ya Mungu kwamba miili yao itatenda dhambi hadi watakapokufa. Kila wanapoyaona maovu ya miili yao sawasawa na wale ambao hawajazaliwa upya basi wanapoteza amani ya fikra zao kirahisi. Wanakuwa na amani wakati wasipotenda dhambi tu. Hii ni hali ambayo inaweza kupatikana katika maisha ya kila Mkristo ambaye bado hajapokea ondoleo la dhambi. Wanaweza kuimba kwa midomo yao, “♫Dhambi zangu zote zimetoweka. ♪Dhambi zako zote zimetoweka. Dhambi zetu zote zimetoweka! ♫”. Lakini ikiwa watatenda dhambi tena basi wanafikiri kuwa wanapaswa kuomba toba kwa mara nyingine. Basi kadri wanavyozidi kutenda dhambi ndivyo wanavyozidi kuimba kwa polepole, “♫Dhambi zangu zimetoweka, ♫dhambi zako zimetoweka...,” na hatimaye wanafikia hatua ya kukatishwa tamaa kabisa kadri muda unavyozidi kwenda. 
Bwana wetu ametuokoa kiusahihi toka katika dhambi zetu zote. Bwana wetu ametuokoa toka katika dhambi zetu zote ili kwamba tuweze kumsifu na kumshukuru Mungu wakati wote na katika mazingira yote. Tunaweza kuifurahia amani pamoja na Bwana na kisha kumwomba Mungu atusaidie wakati wote kwa kupitia Yesu Kristo. 
 

Ikiwa Tunafahamu Kuwa Mwili Unaitumikia Sheria ya Dhambi Tu, Basi Tunaweza Kuikwepa Dhambi kwa Imani
 
Kwa nini maisha yako ya kiimani ni magumu sana? Unasumbuliwa na maisha magumu ya kiimani kwa sababu huifahamu kweli kuwa mwili unaitumikia sheria ya dhambi tu. Ni lazima tuyaongoze maisha yetu ya kiroho kwa kuufahamu ukweli huu. 
Tunafikia kuufamu ukweli wa Mungu na kubadilika pale tunapolisikiliza Neno la Mungu na kuwa na ushirika sisi kwa sisi. “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:31-32). “Ninamshukuru Mungu—kwa kupitia Yesu Kristo Kristo Bwana wetu!” Bwana ametuokoa kiusahihi na kiukamilifu toka katika dhambi zetu zote ili kwamba tuweze kumshukuru Mungu wakati wote. Je, unaamini katika hili? Bwana ametuokoa toka katika dhambi zetu zote. 
Kamwe usielemewe na kufungwa na mawazo yako binafsi kwa sababu mawazo hayo hayatakupeleka popote. Tunaweza kumfuata Bwana, kumshukuru, na kisha kuishi maisha ya kiimani pale tunapokuwa hatupo chini ya kongwa la dhambi. Ikiwa imani yetu itahusianishwa na matendo yetu, na ikiwa tunatambua kuwa tutatenda dhambi tena, basi hatuwezi kufurahi na kumfuata Bwana. Ikiwa wokovu wa Bwana ungekuwa una dosari hata ile ndogo basi tusingeweza kabisa kumfuata Bwana kwa uhakika zaidi. 
Tunamshukuru Bwana kwa kuwa alizichukua dhambi zetu zote. Tunamsifu na kumfuata kwa nguvu. Ikiwa siwezi kulishughulikia tatizo la dhambi zangu binafsi, ninawezaje basi kuwaokoa wengine toka katika dhambi? Ninawezaje kuihubiri injili kwa wengine? Inawezekanaje kwa mtu anayezama majini kuwaokoa watu wengine wanaozama? Ikiwa tunakiri kuwa miili yetu haiwezi kufanya lolote zaidi ya kutenda dhambi basi kwa njia hiyo tunaweza kuikwepa dhambi. Lakini ikiwa hatuukiri ukweli huo, basi kwa hakika tutashawishiwa na mafundisho ya uongo ya dini inayoitwa “Ukristo.”
Kuna hadithi ya kuchekesha na pengine unaweza kuwa unaifahamu. Wakati mmoja kijana mmoja ambaye ni Kasisi wa Kikatoliki alikuwa amepanda mkokoteni wa farasi pamoja na watawa wa kike toka katika kanisa lake ili kumtembelea muumini mmoja aliyekuwa katika hatua za kifo katika kijiji kimoja cha pembeni. Huyu kasisi alikaa katikati ya wale watawa wa kike wawili ili aweze kuwaendesha farasi. Mtawa wa kike aliyekuwa kijana na mrembo alikuwa amekaa mkono wake wa kuume na mtawa mwingine wa kike aliyekuwa mzee alikuwa amekaa upande wake wa kushoto. Hakukuwa na shida wakati mkokoteni huo ulipokuwa ukipita katika njia nzuri na pana za mjini, lakini mara walipokuwa katika barabara nyembamba na mbaya katika milima ule mkokoteni ulianza kuyumba sana. Jaribu kufikiria ni kitu gani ambacho kasisi huyu wa kikatoliki alikuwa akikifikiria katika mawazo yake. Wakati ule mkokoteni ulipokuwa ukielemea mkono wake wa kushoto yule kasisi alikuwa akiomba hivi, “Ooh Mungu, tafadhari fanya vile upendavyo!” Lakini wakati mkokoteni ulipoegemea upande mwingine wa kuume, yule kasisi aliomba hivi katika moyo wake “Ooh Bwana. Usinitie majaribuni!” Kasisi huyu alikuwa akiomba sala mbili: “Ooh Mungu, tafadhari fanya vile upendavyo” na “Ooh Bwana. Usinitie majaribuni.” 
Sisi sote tupo sawa na kasisi huyu alivyo. Miili yetu inaitumikia sheria ya dhambi tu, lakini ni lazima tuyatambue mapenzi ya Bwana na kisha tumfuate kwa imani kwa mujibu wa mapenzi yake kwa kuwa hatuna kitu ambacho twaweza kukitegemea sisi wenyewe. Sisi tu wafu na hakuna uwezekano wa miili yetu kuboreshwa zaidi. 
 

Tunamfuata Bwana Kwa Kuwa Ametuokoa Kikamilifu
 
Ni uzito kiasi gani tungeuona ikiwa tungalipaswa kuingia katika Ufalme wa Mbinguni kwa kutenda matendo mema, au ikiwa wokovu wetu ungetegemea kiwango cha matendo mema tuliyoyatenda au dhambi tulizozifanya? Bwana anatueleza sisi kuwa, “Unatenda dhambi maisha yako yote. Lakini nilizichukulia mbali dhambi zote ambazo utakuja kuzifanya hadi utakapokufa. Nimekufanya kuwa mwenye haki. Nimekufanya kuwa mwenye haki usiye na dhambi. Nimekuokoa kikamilifu. Je, unanishukuru?” Jibu letu ni nini? “Ndiyo, ninakushukuru, Bwana wangu!” Kisha anatuuliza tena, “Je, utanifuata?: Tunalijibuje swali hili?” “Ndiyo tutakufuata.”
Je, unapenda kumfuata Mungu? Kwa kweli tunataka kumfuata Bwana kwa sababu amezichukua dhambi zetu zote. Ikiwa Bwana angekuwa amezichukua asilimia 90% ya dhambi zetu basi tusingeweza kumfuata. Ungeweza kumlalamikia Mungu ukisema “ungelipaswa kuchukua asimilia 10% ya dhambi zangu zilizobakia! Ninawezaje kushungulikia tatizo la dhambi hizi mimi peke yangu? Ninawezaje kukufuata wakati ninatakiwa kuuosha uchafu wangu?” Basi kwa sababu ya dhambi hizi tengefikia hatua ya kuacha kumfuata Mungu. 
Hata hivyo, sasa tunapenda kumfuata Bwana kwa hiari kwa sababu ametuokoa kikamilifu toka katika dhambi zetu zote. “Ndiyo, umenikoa mimi kikamilifu. Sasa ninaweza kukufuata tangu sasa na kuendelea! Ninakushukuru Bwana! Ninakusifu. Ninakutukuza. Ninakupenda!” Tunafikia hatua ya kujitoa sisi wenyewe ili kumtumikia Bwana kwa sababu tunampenda na tunahitaji kumfuata. Tunataka kumfuata Bwana toka katika vina vya mioyo yetu kwa sababu ametuokoa toka katika dhambi zetu zote na kwa sababu tumeguswa na upendo wake. 
Hali hiyo hiyo inajitokeza kuhusiana na kuhudhuria kanisani. Kuhudhuria ibada za kila Jumapili ni kitu rahisi ikiwa tutapenda kufanya hivyo; ikiwa tunajifikiria kuwa hatupendi kuhudhuria kanisani kwa sababu kadhaa, basi hata kwenda kanisa mara moja kwa wiki linakuwa ni jambo zito kwetu. Ikiwa utayasikiliza maneno ya kuhuzunisha katika kila ibada kama yafuatayo—“Mabibi na mabwana, tubuni dhambi zenu zote mlizozifanya wiki iliyopita,”—basi baada ya miaka kadhaa utaacha kwenda kanisani. Wale ambao wana nia zenye nguvu wanaweza kudumu zaidi pengine kwa miaka kumi au au ishirini lakini hatimaye nao wanaliacha kanisa. Manabii wengi wa uongo wanawalazimisha watu wanaoteseka toka katika dhambi zao kutubu. Hii ndiyo sababu watu wengi wanaacha kwenda kanisani wakifikiri kuwa ni vigumu sana kumwamini Yesu. 
Sisi tunamfuata Bwana hali tukiwa tumevutiwa na upendo wake. Hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kumsifu Bwana tukiimba, “♪Ninampenda Yesu! Siwezi kumbadilisha Yesu na kitu chochote ulimwenguni ♪” Tunamfuata Yesu kwa sababu tunampenda sana. 
Wokovu wa Yesu ni wa kushangaza sana jinsi ulivyo. Bwana alituwezesha kumtumikia yeye pasipo kuwa na hata chembe ndogo ya dhambi. “Sasa, basi hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti” (Warumi 8:1-2). Mungu anatubariki ili tuweze wakati wote kumshukuru na kumsifu. Bwana anataka sisi tufurahi na kumfuata yeye wakati wote. Yeye alituokoa. Je, unaamini hivi? 
Usikatishwe tamaa na udhaifu wako binafsi. Bwana alizichukulia mbali dhambi zote za wale ambao hasira zao hazitawaliki. Pia alizichukulia mbali dhambi zote za watu ambao wana asili ya uasherati na ufisadi. Je, jambo hili halikufanyi wewe upende kumfuata Bwana? Hii ndio sababu tunampenda Bwana wetu. Bwana wetu hatulazimishi kumfuata wala hatushurutishi kumwabudu yeye. Mungu ametubariki sisi. Amefanyika kuwa Baba yetu na tumefanyika kuwa watoto wake na Mungu anatueleza sisi kumfuata yeye. Mungu anawaambia watumishi wake kumtumikia Yesu. 
Wale wote ambao wameokolewa na Mungu ni watumishi wake. Mungu anawabariki watenda kazi wake wote na anawaeleza kumfuata Yesu. Bwana hatuiti sisi kwa sababu ya matendo yetu. Bwana anatueleza sisi kuwa, “nilikuokoa kikamilifu toka katika dhambi zako zote. Hasira yako haivumiliki. Una tabia ya uasherati na ufisadi. Maelezo yako yanapita hali ya kawaida ya kueleza. Wewe ni mjinga. Unastahili kulaaniwa kwa sababu ya dhambi za baba zako. Lakini nilikuona na sijali kuhusu mambo mengine. Huwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea kutenda dhambi maisha yako yote, hata hivyo nilizichukua dhambi zako zote. Niliteseka kwa ajili yako na kisha kufufuka tena toka kwa wafu ili kuzitoweshea mbali dhambi zako zote. Nilifanya mambo haya kwa sababu ninakupenda. Ninakupenda. Je, wanipenda?” Jibu lako ni nini? “Ndiyo, ninakupenda Bwana wangu. Unatambua kuwa mimi pia ninakupenda. Asante sana Bwana!”
“Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” “Amini nawaambieni, yeye aniaminiye Mimi, atazifanya kazi ninazozifanya pia; kazi kubwa kuliko hata hizi, kwa sababu naenda kwa Baba yangu,” Maneno haya aliyasema Bwana. Je, unaamini hivi? Je, asili zetu zina uovu kiasi gani! Ni dhambi ngapi ambazo tumezifanya mbele za Mungu? Usijifanye kutofanya dhambi. 
Tunafanya dhambi mara nyingi katika maisha yetu ya kila siku. Lakini Bwana amezichukulia mbali dhambi zetu hata pale zinapokuwa nyingi kama nyota za angani. Bwana Yesu alizichukulia mbali dhambi zetu kwa usahihi na kwa ukamilifu. 
 

Mungu Alitufanya Sisi kuwa Wafanyakazi Wake kwa Kutuvika katika Haki Yake
 
Kwa nyakati fulani tunaweza kufikiria kuwa hatuwezi kumfuata Mungu hasa pale tunapojichunguza sisi wenyewe. Wakati mwingine mioyo yetu inaonekana kuwa ni miangavu kama siku yenye jua lakini wakati mwingine mioyo yetu inakuwa na uzito na giza. Na katika nyakati mbalimbali tunajikuta sisi wenyewe tukiwa katika giza hali tukiwa tunamfuata Bwana baada ya kuwa tumezaliwa upya. Tunabadilika kana kwamba tunaifuata ile misimu minne. Mungu alimpatia Nuhu aina nane ya misimu wakati Nuhu alipotoka katika ile safina. Mungu akasema, “Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma” (Mwanzo 8:22).
Milima na mabonde ya imani yetu hayataisha. Baadhi ya siku tunamsifu Yesu kwa furaha, lakini tunabadilika na kukasirika mara tunapokutana na magumu. 
“Ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.” Hivi ndivyo Bwana alivyosema (Waebrania 10:17-18). 
Mwili hauwezi kufanya lolote zaidi ya kuendelea kufanya dhambi hadi utakapokufa. Hiyo ni sheria ya mwili. Mwili unaitumikia sheria ya dhambi. Hii inamaanisha kuwa mwili unachoweza kufanya ni kutenda dhambi tu. Lakini Mungu aliwafanya wale ambao wanaweza kutenda dhambi tu kuwa watumishi wake. Je, Mungu anatufanyaje sisi kuwa watumishi wake? Kwa hakika hawezi kuwafanya wale walio na dhambi kuwa watumishi wake. 
Mungu amekufanya wewe kuwa mtumishi wake kwa kuzichukulia mbali dhambi zote ambazo mwili wako unazitenda hadi siku yako ya mwisho na kisha alilipa kikamilifu mshahara wa dhambi zako ili kukufanya wewe kuwa mkamilifu. Aliwatakasa na kuwaita ili mfanyike kuwa watumishi wake watakatifu. Mungu alitufanya sisi kuwa watumishi wake. Ingawa sisi tu wadhaifu, lakini sasa tuna nguvu. Unaweza kuuliza kuwa ni “nguvu gani? Sisi tuna nguvu ya haki yake. Tuna nguvu kamilifu kwa kujivika katika haki ya Mungu. Kwa maneno mengine, sisi tumefanyika kuwa wakamilifu. Ingawa tu wadhaifu katika mwili, sisi tuna nguvu katika Roho. 
 

Ni Nani Anayeweza Kumtumikia Bwana?
 
“Kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote” (2 Wakorintho 6:10). Sisi tuna dhambi japokuwa tunaonekana kuwa ni wenye dhambi. Sisi hatuna dhambi ingawa tunatenda dhambi. Kwa hiyo tunaweza kuwasaidia watu wengi kuokolewa kwa injili ya maji na Roho. Hili ni fumbo la Kristo na siri ya Ufalme wa Mbinguni. 
Ninamsifu Bwana ambaye ametuokoa sisi kikamilifu. Ni nani anayeweza kumtumikia Bwana? Wale wanaopenda kumtumikia Bwana kwa kujaribu kutofanya dhambi au wale wanaoamini kuwa Bwana alizichukulia mbali dhambi zao ambazo wanazifanya katika kipindi chote cha maisha yao? Ni hawa wa pili ndio wanaoweza kumtumikia Bwana na kumfurahisha. Ni wale tu wanaoamini kuwa Bwana alizioshelea mbali dhambi zao kikamilifu ndio wanaoweza kumtumikia. Wanajitoa kwa hiari yao kwa Bwana na kisha wanawekeza vyote walivyonavyo katika kazi ya Bwana. Wanajisikia fahari kuwa wafanyakazi wa Bwana kwamba wanaweza kufanya angalau kitu kidogo kwa ajili ya Bwana. 
Baadhi ya watu wanaiogopa haki yao wenyewe kuwa inaweza kuvunjika, kwa hiyo hawakasiriki hata katika mazingira ambayo yangaliwafanya kukasirika. Haki yao binafsi inapaswa kuvunjwa. Ni lazima tutupilie mbali haki zetu katika shimo la takataka kama tunavyoutupa uchafu kwenda mbali. Haki yetu binafsi ni lazima ivunjwe. Ni lazima tuiwekee muhuri na kuikata na kisha kuitupa katika shimo la takataka. Tunaweza kumshukuru Bwana na kisha kuiinua haki yake pale tunapokuwa tumeiweka kando haki yetu binafsi. 
Watu wa jinsi hiyo wanaweza kumsifu na kumshukuru Bwana hali wakiimba, “Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake” (Zaburi 100:4). Wale walio na haki yao binafsi, ingawa wanaweza kuokolewa, watu hao hawawezi kumtumikia na kumpenda Bwana hadi mwisho. Wale wanaotambua kuwa mwili unaitumikia dhambi tu katika kipindi chote cha maisha yao na wanaoamini kuwa Bwana alizichukulia mbali dhambi zao zote zikiwemo dhambi zitakazokuja wanapenda kumtumikia na kumpenda Bwana kwa uvumilivu. Katika mioyo yao kunapatikana ile nia ya kumpenda Bwana. 
Je, una moyo unaopenda na kutaka kumtumikia Bwana? Je, una moyo ambao unamshukuru Bwana? 
 

Bwana Anatuwezesha Kuishi Maisha ya Furaha Pasipo Dhambi
 
Sisi watumishi wa Mungu, tunaishi katika mafanikio na furaha zaidi kuliko wale wanaopata mamilioni ya dola kwa mwaka. Tunakula matikiti wakati wa kiangazi na tunakula mapeazi na zabibu wakati wa majira yake. Tunaweza kula kitu chochote tunachopenda. Sisi si maskini. Je, umewahi kuishi kimaskini baada ya kuwa umekombolewa? Sisi tumekuwa tukiishi katika mafanikio. 
Tunaweza kuishi kwa mafanikio ikiwa tutatembea pamoja na Bwana. Yeye atembeaye na Bwana hatakuwa na uhitaji. Je, unaamini hivi? Ingawa sisi si matajiri kwa kuangalia vigezo vya kiulimwengu ukweli ni kuwa bado tunaishi pasipo kuwa na mapungufu. Je, unaamini hivi? Je, una mahitaji na matamanio ambayo bado hayajafikiwa hata baada ya kukutana na Bwana? Kwa kweli hatuna kitu tunachopungukiwa. Kwa kweli kwa sasa tunaishi maisha ya kitajiri kuliko ilivyokuwa hapo awali. Nimeishi na kulala vizuri sasa hivi kuliko ilivyokuwa hapo zamani. 
Bwana wetu ametuokoa sisi kikamilifu. Hatuna maneno ya kutosha kuelezea baraka hii. Bwana wetu ametuokoa kikamilifu na amekuwezesha wewe na mimi kumshukuru Mungu kwa kupitia Yesu. Hii ni neema kubwa! 
“Ole wangu maskini mimi!” Paulo alisema maneno haya alipokuwa akiuangalia mwili wake. “Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” Tunafanya dhambi katika kipindi chote cha maisha yetu. Ni nani aliyetuokoa toka katika dhambi ambazo tunazitenda kwa miili yetu? Ni Yesu Kristo ndiye aliyetuokoa. Kama Paulo alivyofanya, mimi pia ninafanya vivyo hivyo, ninamshukuru Mungu kwa kupitia Yesu Kristo Bwana wetu. Asante Bwana wangu kwa kuzichukulia mbali dhambi zangu zote. 
Baada ya kuwa ameipokea haki ya Mungu, Mtume Paulo hakuishi kwa kutegemea haki yake binafsi. Alikiri mara nyingi kuwa mwili wake ulikuwa umeuzwa chini ya dhambi. Baadhi ya watu wanadai kuwa Paulo aliandika sura ya 7 kabla hajaokolewa na sura ya 8 baada ya kuokolewa. Kwa hiyo si sahihi. 
Neno la Mungu linatumika kwa wale wote walio okoka na wale ambao hawaja okoka. Linatumika kwa kila mtu. Wanatheolojia wengi, hali wakiwa hawalifahamu Neno la Mungu wanaujasiri wa kutenganisha kati ya ura ya 7 na sura ya 8 kisha wakitumia sura ya 7 kwa wale ambao hawajaokoka na sura ya 8 kwa wale waliookoka. Wanalitenganisha Neno la Mungu kwa ibara ingawa hawajui namna ya kuzitenganisha ibara hizo. Kuna watu wengi ambao wapo safi na wengine wenye uongo katika kada hii. 
Bwana amezichukulia mbali dhambi zetu zote kikamilifu. Ninataka wewe uishi kwa imani kwa kumshukuru Mungu. Ninapenda uzitoe chunusi katika sura yako. Bwana amezichukulia mbali dhambi zako zote nyeusi toka katika moyo wako. Ninamshukuru Bwana ambaye ametuokoa toka katika dhambi zote za mwili.