Search

Khotbah-Khotbah

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[18-2] “Tokeni Kwake, Enyi Watu Wangu, Wala Msipokee Mapigo Yake” (Ufunuo 18:1-24)

(Ufunuo 18:1-24) 
 
Katika sura ya 18 Mungu anatueleza kwamba atauangamiza mji ule mkubwa wa Babeli kwa mapigo yake makuu. Hii ni kwa sababu zitakapofikia nyakati za mwisho ulimwengu huu utakuwa umegeuka na kuwa mchafu na wenye dhambi sana mbele ya macho ya Mungu, na kwa kuwa Mungu hatakuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kuuangamiza ulimwengu pamoja na kuwa aliuumba yeye mwenyewe, basi Mungu atayaruhusu mapigo makubwa ambayo yatauhitimisha ulimwengu. Hivyo, ulimwengu huu utafanywa ukiwa hadi pale utakapokuwa umeharibiwa kabisa. 
Sababu halisi itakayomfanya Mungu kuuharibu ulimwengu huu huu ni kwa kuwa atakuwa ameiona damu ya manabii na watakatifu wake. Na kwa kuwa ulimwengu huu utakuwa umefanya dhambi nyingi na kubwa kwa kupitia vitu ambavyo Mungu aliupatia, basi ni hakika kuwa ulimwengu huu utakuwa ni mchafu sana kiasi kuwa Mungu hataweza kuvumilia. Kati ya sayari ambazo Mungu ameziumba, dunia ndio sayari nzuri zaidi kuliko zote. Hii ni kwa sababu Mungu aliuumba ulimwengu huu kwa uangalifu mkubwa sana, pia ni kwa sababu dunia ni mahali ambapo mipango ya Mungu ya kuwaokoa wenye dhambi katika Yesu Kristo imetimizwa. 
Hivyo, Mungu amekwishapanga jinsi atakavyouangamiza ulimwengu huu na jinsi atakavyoufanya Ufalme wa Kristo kuja. Wakati ulimwengu huu utakapokuwa umejawa na kila aina ya uchafu, basi Mungu atauharibu kwa kupitia malaika zake kwa mapigo ya mabakuli saba. Kisha atayafanya yote kuwa mapya na kuwafanya watakatifu wake kutawala katika ulimwengu mpya. 
 

Babeli Mji Ulio Anguka!
 
Wafalme wa dunia wamezini na vitu vya ulimwenguni na wakaishi katika anasa zake, wakati wafanya biashara wamekazana katika kuuza na kununua kila kitu ambacho Mungu amewapatia, na kwa sababu hiyo wamempoteza Mungu kwa kuzifuata tamaa zao. Mungu ataharibu kila kitu yaani—majengo, dini, bidhaa zote zinazopatikana katika dini, watu waliojitajirisha kupitia dini, wafalme, wanasiasa, watu walioelemewa na tamaa ya kumiliki vitu na mali, na zaidi—haya yote yataharibiwa na Mungu. 
Mungu atalitikisa kila jengo duniani na kuliangusha chini na hataacha hata jengo moja likiwa limesimama, na ataharibu vitu vyote kwa moto, kuanzia watu hadi misitu na miti. Wakati kila kitu katika ulimwengu huu kitakapoanguka, watu wataomboleza na kulia. Hasahasa, Mungu atahakikisha kuwa anawaangamiza wale wote waliojitajirisha kupitia dini. Ni muhimu kufahamu mapema kwamba Mungu atauangamiza ulimwengu huu mzuri ambao aliuumba yeye Mwenyewe. 
Wakati huu, Mungu atawaruhusu watakatifu waliozaliwa tena upya na walioshiriki katika ufufuo wa kwanza wa Yesu Kristo kutawala hapa duniani kwa miaka elfu moja. Mungu atawafidia watakatifu kwa kazi ya kuitumikia injili ya maji na Roho na kwa kuuawa na kuifia-dini katika kuilinda imani yao walipokuwa hapa duniani ambapo atawapatia Ufalme wa Mungu. Mungu atawapatia mamlaka juu ya miji kumi, juu ya miji mitano, na juu ya miji miwili na atawafanya kutawala kwa miaka elfu moja, na baada ya hayo, atawapatia Mbingu na Nchi Mpya ili waishi humo milele. 
Kwa nini basi Mungu anakwenda kuiangamiza dunia, ambayo ni sayari nzuri zaidi ulimwenguni? Hii ni sayari pekee ambapo samaki wanaweza kuogelea katika mito, wanyama wa porini wanaweza kuzunguka misituni, na mwanadamu anaweza kuishi ndani yake. Lakini kwa kuwa Mungu hataweza tena kuuvumilia ulimwengu ambao dhambi imekuwa nyingi sana, basi Mungu ataufanya ulimwengu huu kwa mapigo yake kuwa mabaki. Mungu ameamua kuuangamiza ulimwengu. 
Kila mtu anayeishi katika dunia hii, isipokuwa tu kwa wale waliookoka, wataangamizwa kwa mapigo ya mabakuli saba. Kwa kuwa wenye haki wote wa nyakati za mwisho watauawa kuifia-dini, watateswa na kunyanyaswa na ulimwengu huu, basi Mungu ataukanyaga ulimwengu ili kulipiza kisasi kwa matendo maovu ya ulimwengu huu. Wakati huu utakapowadia, viongozi wa kidini na wafanya biashara waliokuwa wakizifanyia biashara nafsi za watu wataangamizwa wote. Mungu hatawaua wale tu waliokuwa wakijifanya ni viongozi wa kidini ilhali hawajazaliwa tena upya, bali pia atawatupa viongozi hao pamoja na Ibilisi katika ziwa la moto na kibiriti. 
Ni hakika kuwa Mungu atauangamiza ulimwengu huu. Hivyo, ni lazima tutambue na kuamini pasipo shaka kuwa ulimwengu huu utakuja angamizwa. Mungu atawaua wafanya biashara wanaojisifia kwa sababu ya vitu vyote vikubwa na wanaozifanyia biashara nafsi za watu katika dini zao. Hata hivyo, pamoja na kuwa mapigo ya Mungu yanakaribia, bado kuna watu ambapo hawafahamu chochote huku wakiwa na ujasiri binafsi. Hebu jaribu kuwaangalia viongozi wa kidini wa dunia hii. Je, si watu wenye majivuno, kana kwamba wanatenda mambo sahihi mbele za Mungu? Je, ni kweli kuwa Mungu atawakubali watu wa jinsi hiyo? 
Ikiwa Mungu amesema kuwa atauangamiza ulimwengu huu kwa sababu ya dhambi za watu, basi tunapaswa kuamini hivyo, hii ni kwa sababu mambo yote yatakuja kufanyika sawasawa kabisa na jinsi Mungu alivyosema. Pia ni lazima tuilinde imani yetu. Mimi sisemi hivi kama mmoja wa viongozi wa vikundi-dini ambao wanaunda nadharia zao za mafundisho ya kidini na kisha kuzungumzia juu ya unabii wa kiapokaliptik utakaokuja, bali mimi nasema tunapaswa kuamini kile ambacho Mungu ametuambia katika Maandiko —yaani, ni hakika kwamba Mungu aliyehai atauangamiza ulimwengu huu kwa mapigo makubwa ya mabakuli saba. 
 

Hatupaswi Kujiendekeza Katika Ulimwengu Huu Ambao Utaangamizwa Hivi Punde
 
Hivyo, hatupaswi kushikilia tamaa ya kulimbikiza vitu na mali za ulimwengu huu ambao utaangamizwa hivi punde. Tunapaswa kuridhika na vitu ambavyo Mungu ametupatia, na kisha tuvitumie na kushiriki na wengine kama Mungu anavyotaka. Mali na vitu vya hapa ulimwenguni vinahitajika katika kumtumikia Mungu. Tunapaswa kuishi kama watumishi waaminifu ambao tunasimamia vile ambavyo Mungu ametupatia katika kuihubiri injili. Hatupaswi kujichanganya na kisha kutegwa na mali na vitu vya ulimwenguni, hii ni kwa sababu tunaamini kuwau Mungu atauangamiza ulimwengu huu. 
Hatupaswi kujidanganya kwa kufikiri kwamba utajiri na thamani za ulimwengu huu vitadumu milele. Hivyo tunapaswa kuishi tukiingojea siku ya kurudi Bwana hali tukifahamu kwamba Mungu atawakanyaga viongozi wa kidini na wafuasi wao pia. Tusipofanya hivyo, tutaishia kuanguka katika ulimwengu huu, ulimwengu ambapo utaangamizwa hivi punde. Kwa hiyo, ili tusiweze kuanguka katika ulimwengu huu unaokabiliwa na maangamizi yake, tunapaswa kuamini kwamba sayari hii ya dunia itaangamizwa kwa hakika. 
Hadi sasa Mungu yuko macho, na wakati utakapowadia, Mungu atayatimiza yale yote aliyoyasema. Pamoja na ukweli kwamba hata miongoni mwa wale waliozaliwa tena upya wapo baadhi ambao imani yao haijakomaa, tunachopaswa kukifanya sisi ni kuamini pasipo shaka. Pia sisi sote sote ni lazima tuwe macho tena na tena. Hatupaswi kukatishwa tamaa na ulimwengu huu ambao utaangamizwa hivi punde, na badala yake tunapaswa kuishi maisha yetu kwa kuiweka imani yetu katika Neno la Mungu. Kwa nyakati fulani mioyo yetu inaweza kudhoofika, lakini bado tunapaswa kuishi kwa imani thabiti. 
Ni jambo la kushangaza kwamba Mungu atayafanya mambo haya yote kwa ulimwengu huu. Ikiwa Mungu asingeliuharibu ulimwengu huu kisha akajenga Ufalme wa Kristo mahapa pake, basi ni hakika kuwa wenye haki wangelikatishwa tamaa sana. Hii ndio maana mpango wa Mungu ni wa ajabu sana na ndio maana unatoa tumaini kwa watakatifu wenye haki. 
Ikiwa wasioamini wangelibakia katika kiburi chao na kisha wakaendelea kuishi kwa furaha hali wakiwa hapa duniani na hata wakaweza kuingia Mbinguni baada yetu, basi ni hakika kwamba kwetu sisi ingelionekana kuwa ni jambo lisilo la haki ambalo Mungu ameliruhusu. Ahadi ya Mungu, kwamba awahukumu na kuwaangamiza wote wanaowatesa wenye haki, wanaowanyanyasa kwa uongo wao, na wanaoimwaga damu ya watakatifu, ni ahadi yenye haki na sahihi. 
Ikiwa kusingelikuwa na hukumu ya Mungu kwa wenye dhambi wa ulimwengu huu, je, si dhahiri kuwa isingelikuwa haki kwa wenye haki ambao wameishi maisha yote kwa ajili ya Bwana hali wakivumilia shida na magumu mbalimbali? Hivyo ni sahihi kabisa kwamba Mungu atauhukumu ulimwengu huu. Wakati ulimwengu huu utakapofikia hatua ya kuwa kama ulimwengu wa wakati wa Nuhu, basi ni hakika kabisa kwamba Mungu ataubinua ulimwengu huu na kuuangamiza. 
Kwa kuwa tunamwamini Bwana, ni hakika kuwa hatuwaonei tamaa watu wa ulimwengu huu kabisa. Hii ni kwa sababu, Bwana amesema kuwa atauhukumu ulimwengu huu na kisha kumtupa Shetani, Mpinga Kristo na wafuasi wake katika moto wa kuzimu, na kwa sababu hiyo sisi sote tunaweza kuvumilia na kungojea. 
Ulimwengu huu umebakiza dakika chache sana ili uangamizwe, hii ni kwa mujibu wa unabii wa Neno la Mungu. Katika ulimwengu mzima tumekwishaona dalili nyingi sana zinazoonyesha ujio wa mapigo ya nyakati za mwisho. 
Hali ya hewa isiyo ya kawaida kama vile El Nino na magonjwa mapya kama vile Kichaa cha Ng’ombe yanausumbua ulimwengu huu wa sasa. Magonjwa yasiyo na tiba ambayo mwanadamu hana uwezo wa kuyatatua yanaendelea kuugubika ulimwengu, vivyo hivyo majanga makubwa ambayo hayatarajiwi kama vile njaa kali na matetemeko ya ardhi ya kutisha yanaendelea kuipiga dunia. 
Mambo haya yote yanapotokea, tunapaswa kuamini kwamba Mungu yupo, na pia tunapaswa kuishi maisha yetu hali tukifahamu kuwa Mungu atawahukumu na kuwaangusha wale wote walioishi kwa matamanio yao hali wakijirundikia utajiri walipokuwa hapa ulimwenguni. Katika ulimwengu wa leo dhambi imetawanyika mahali pengi sana. Ulimwengu huu una matumizi ya ovyo sana kwa sababu ya starehe na anasa zake. Watu wametingwa kwa kuoana, kula na kunywa, na kujenga majumba yao pasipo kukumbuka juu ya hali yao ya kiroho. Ulimwengu wa leo ni mahali ambapo mwanamume anafanya dhambi ya zinaa na mwanamume mwenzie, na wanawake wengi pia wakifanya tamaa na kuzini na wanawake wenzao (Warumi 1:27). 
Je, wakati wa Nuhu ulimwengu haukuwa kama hivi? Unapaswa ufahamu vizuri juu ya maana ya neno ‘ufiraji.’ Wakati Sodoma na Gomora zilizopoangamizwa, hali na utamaduni wao ulikuwa kama ulivyo katika ulimwengu tunaoishi sasa. Ulimwengu huu umekuwa ni mchafu sana na wenye dhambi, kiasi kwamba Mungu ataleta moto na kuuchoma kuwa majivu, pia umegeuka na kuwa ulimwengu ambao unamilikiwa na mashetani. 
 

Manabii wa Uongo Watauawa
 
Mara nyingi manabii wa uongo wanatafuta kumiliki mali na vitu ili kujilimbikizia utajiri isivyo halali, hali wakiwa wamejificha katika tawala za taasisi zao za kidini. “Ikiwa unamwamini Yesu, utakuwa tajiri, utaishi vizuri, na utapona magonjwa yako”—ni lazima ufahamu kwamba nyuma ya uongo kama huo ipo nia ya kunyonya mali na vitu. 
Hata hapa Korea, sasa ni muda mrefu tangu Ukristo ulipopoteza imani yake ya msingi na kuharibiwa na kila aina ya nguvu za mapepo kwa kisingizio cha jina la Yesu. Huu ni ukweli wa Ukristo wa leo. Lakini kwa wale manabii wa uongo ambao wanaipima imani kwa kiwango cha umiliki wa mali na vitu vya ulimwenguni, na ambao wanafanya ushirikina pamoja na Neno la Mungu, basi ni hakika kuwa hukumu ya Mungu ya kutisha ya kuzimu na mapigo makubwa ya mabakuli saba vinawangojea. 
Mungu anatueleza kwamba wale wote wanaowadanganya watu na watu wanaodanganywa na manabii wa uongo wote kwa pamoja watapokea hukumu. Hatupaswi kuuangalia ulimwengu huu na kisha kuufuata. Badala yake tunapaswa kuamini kwamba kwa kuwa Mungu yupo hai, basi wale wote wasiomwamini Yesu na wanaosimama kinyume naye na kuwatesa wenye haki watahukumiwa na kuadhibiwa mauti ya milele. Pia ni lazima tuamini kwamba baada ya kuuhukumu ulimwengu, ni hakika kwamba Mungu atawakirimu watakatifu kwa mateso na maumivu yao yote waliyoyapata kwa ajili ya jina la Kristo.