Search

Sermões

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-13] Ni Nani Atakayewatenga Wenye Haki na Upendo wa Kristo? (Warumi 8:35-39)

(Warumi 8:35-39)
“Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, 
‘Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; 
Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.
Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
 

Aya ya 35 inasema, “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?” Ni nani anayeweza kututenga na upendo wa Kristo uliotolewa kwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho ambayo ina haki ya Mungu ndani yake? Je, mateso na matatizo vinaweza kutukata toka katika upendo huo? Je, yale mapigo makuu ya miaka saba yanaweza kututenga na upendo huo wa Yesu? Kwa kweli hapana!
Hakuna mapigo au mahangaiko katika ulimwengu yanayoweza kututenganisha na upendo wa Bwana wetu ambao umetuokoa toka katika dhambi zetu. Hata pale ambapo tunatamani kuachwa peke yetu kwa sababu ya uchovu, halafu mtu moja akatuuliza ikiwa Yesu ametuokoa toka katika dhambi zetu au la, kwa hakika sisi sote tutajibu dhahiri kuwa kwa hakika Yesu ametuokoa na kwamba hatuna dhambi. Haijalishi jinsi mioyo yetu inavyoweza kuwa imechoka na kudhoofika, ukweli unabakia kuwa Yesu ametuokoa na bado ni mwokozi wetu wa milele. Hata kama tutakuwa tumechoka sana au tunaumwa sana kiasi kuwa hatuwezi hata kuimudu miili yetu, bado tutaendelea kukiri na kutoa shukrani zetu kwa haki ya Mungu. Hakuna kuchoka kwa namna yoyote ile kunakoweza kututenganisha na haki ya Mungu ambayo imetuokomboa toka katika dhambi zetu zote. 
Si mateso, wala njaa, wala uchi, wala adha, wala upanga unaoweza kututenga na haki ya Mungu. Wakati mwingine tunakutana na mateso toka kwa watu wa dini ambao wanatudhalilisha na kutusema vibaya. Mateso yetu yanawahusisha pia rafiki zetu, majirani, jamaa, na hata baadhi ya wanafamilia hasa pale wanapotuacha kutokana na madai kuwa sisi ni wazushi. Je, mateso haya yanaweza kutugenga na wokovu wa Yesu Kristo? Kwa hakika hapana!
Bila kujali jinsi ambavyo tunateswa kwa ukaidi, ukweli ni kuwa mateso hayo hayawezi kututenga na haki ya Mungu ambayo imetuokoa. Kwa kuwa haki ya Mungu imetufanya sisi kuwa tusio na dhambi, na kwa kuwa huu ni ukweli usiobadilika, basi hakuna mtu au kitu kinachoweza kututenga na upendo wa Mungu. 
Njaa, iwe ya kiroho au ya kimwili haiwezi kututenga na upendo wa Mungu. Kwa kuwa tunaamini katika injili ya maji na Roho basi kile kinachobakia katika mioyo yetu ni haki ya Mungu—ambayo ni imani katika Bwana wetu kuwa ametufanya sisi kuwa tusio na dhambi kwa injili ya maji na Roho. Imani hii ni imani itokanayo na baraka za kuamini katika haki ya Mungu. “Kwa kuwa Bwana amezifanya dhambi zangu zote kutoweka, basi mimi sina dhambi! Mungu amenifanya mimi kuwa mwenye haki na nisiye na dhambi, hali akinifunika sawasawa katika haki yake!” Hii ndiyo sababu imani yetu katika haki ya Mungu haiwezi kupotea hata kama njaa itakuwa kali kiasi gani. 
 

Haki ya Mungu Kwa Injili ya Maji na Roho
 
Mtu yeyote atakuwa na dhambi katika moyo wake hadi pale atakapoamini katika injili ya maji na Roho ndipo dhambi hizo zitakapoondolewa. Lakini yule anayeamini katika haki ya Mungu hana dhambi. Hii ndio sababu Bwana wetu alisema kuwa tunaweza kuutambua mti kwa matunda yake. Wale wasio amini katika haki ya Mungu wanaiacha imani yao katika Yesu mara wanapokutana na tatizo dogo, au njaa, mateso, au mapigo. 
Kuna watu wanaofikiri kuwa “ingawa Yesu alihukumiwa Msalabani kwa niaba yangu kwa ajili ya dhambi zangu, basi ni dhambi ile ya asili tu ndiyo iliyoondolewa na kwamba ninapaswa kuendelea kuomba msamaha kwa ajili ya dhambi nyingine ninazozitenda kila siku.” Wale walio na aina hii ya imani kwa kweli wanatenda dhambi dhidi ya Mungu kwa kutokuamini kuwa Yesu alizichukulia mbali dhambi zao zote, na kwamba kwa sababu ya kutokuamini kwako wao wenyewe wanajihukumia adhabu na kujiharibu. Watu hao ndio wale hasa wanaomkana Yesu na wasioiamini haki ya Mungu. 
Lakini wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho ndio wale wanaoamini katika haki ya Mungu, na bila kujali mazingira wanayokutana nayo bado watendelea kuishikila imani yako hali wakisema, “kwa hakika Mungu ameniokoa mimi toka katika dhambi za ulimwengu. Sina dhambi!” Hata kama tutakutana na kifo katika siku za mwisho za njaa yetu ya kiroho, kwa hakika hatutaweza kamwe kumkana Mungu kuwa ametufanya sisi tusio na dhambi na kwamba tumefanyika kuwa watu wake. Haki ya Mungu iliyozichukulia mbali dhambi zetu zote inabakia katika mioyo yetu kama imani yetu. Injili ya maji na Roho ni kubwa sana na ina nguvu. Haijalishi kuwa ni aina ipi ya mapigo tunakutana nayo katika maisha yetu, kwa kuwa haki ya Mungu imo ndani ya Kristo, basi sisi hatutaweza kamwe kutengwa na upendo wa Kristo. 
Katika kifungu hicho hapo juu, kule kusema “uchi” kuna maanisha nini? Hilo neno lina maanisha ni kupoteza mali zetu zote. Hadi kufikia kipindi cha kati, kulipojitokeza tatizo katika kijiji au taifa hasa katika nchi za Ulaya, mara nyingi watu walijihusisha katika kuwasaka wachawi hali wakitumia mbuzi wa kizingizio ili kumletea mbuzi huyo matatizo yao yote; hivyo watu walichukua kila kitu toka kwa wachawi hao na wakawalaumu kuwa ni wazushi. Hii ndio sababu Paulo alitumia neno “uchi” katika kuongelea jambo hili. 
Katika nyakati hizo, iliwezekana kabisa kumtuhumu mtu kuwa ni mzushi, pia iliwezekana kutumia mashahidi wawili au mmoja katika kumhukumu adhabu mtuhumiwa ili achomwe hadharani, afilisiwe mali zake zote, na kuifutilia mbali heshima yake yote. 
Hata kama tunasukumwa kwenda katika hali hiyo ya uchi kwa namna hiyo, tukapoteza kila kitu tulicho nacho na kisha tukauawa, basi ile haki ya Mungu ambayo kutokana na upendo wake imo ndani yetu, na ambayo imezichukulia dhambi zetu zote, basi haitaweza kamwe kutoweka kamwe toka kwetu—hivi ndivyo injili ya maji na Roho ilivyo kamilifu. 
Si adha au upanga vinavyoweza kututenganisha na upendo wa Kristo. Hata kama tutawekwa chini ya upanga na kuuawa, ukweli utabakia kuwa sisi tulioamini hatuna dhambi. Wakristo wengi katika Kanisa la Mwanzo walishutumiwa uongo kwamba walichoma moto mji wa Roma na kwa sababu hiyo waliuawa hadharani kwa miili yao kulishwa simba. Hata walipokuwa wakifa bado waliendelea kumtukuza Bwana ambaye amewaokoa. Waliweza kuendelea kusifu kwa kuwa walikuwa ni waamini wa injili ya maji na Roho. Wale ambao wamekombolewa kwa kuamini katika ukweli kuwa Mungu amewapenda na amezichukulia mbali dhambi zao zote wanaweza kumsifu Bwana hata wakati wanapouawa na kuliwa na simba. 
Ujasiri huu unatokana na imani katika haki ya Mungu ambayo imezichukulia mbali dhambi zetu zote na pia ujasiri huu unatoka katika upendo wake. Ujasiri wa jinsi hiyo unaweza kupatikana ndani yetu kwa kuwa Mungu yupo ndani yetu, anazungumza nasi, anatulinda, anatupatia nguvu, na anatufariji. Si adha wala upanga, wala utisho, wala kuuawa kwa imani kunakoweza kututenga na upendo wa Mungu. 
Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho ni wale ambao wanaamini pia katika haki ya Mungu na ambao ni watu wa Kristo. Wale wanaoamini katika haki ya Mungu ni wale ambao wanapendwa na Kristo. Lakini baadhi ya watu wanaubadilisha upendo mkamilifu wa Kristo kuwa katika upendo wa kawaida wa kihisia hali wakikiangalia kifo chake tu Msalabani, hali wakihuzunishwa na kulia kwa sababu ya mateso ya Yesu. Lakini hisia za kibinadamu zinaweza kubadilika kwa usiku mmoja. 
Ingawa hisia zetu zinabadilika kila asubuhi na kila usiku, ule upendo ambao kwa huo Bwana wetu ametuokoa hauwezi kubadilika wala kurekebishwa na chochote. Upendo wake ni wa milele na haubadiliki. Hivi ndiyo injili ya maji na Roho ilivyo na nguvu, na hivi ndivyo haki ya Mungu ilivyo kuu. Hakuna anayeweza kututenga na Bwana wetu ambaye amefanya sisi kuwa wakamilifu na aliyetufunika katika upendo wake mkamilifu. Hii ndiyo nguvu ya injili ya maji na Roho na pia ni nguvu ya imani yetu katika haki ya Mungu. 
Neno la Kiyunani linalomaanisha “injili” linaitwa “euaggelion,” na lilisemekana kuwa lina “dunamis”—neno hili la Kiyunani lina maanisha nguvu, ujasiri, au uwezo, neno hilo ndilo lililofanya kuwepo kwa neno “nguvu” —ya Mungu. Nguvu kidogo ya dainamoo inaweza kuiangusha nyumba nzima na kuitawanya. Bomu la Tomahawk lililotupwa toka katika meli ya kivita linaweza kuharibu jengo kubwa imara na kulifanya kuwa kifuu. Haijalishi jinsi jengo hilo linavyoweza kuwa limeimarishwa, ukweli ni kuwa jengo hilo haliwezi kulinganishwa na nguvu ya bomu la maangamizi. 
Ndege mbili za kiraia ziliweza kuliangusha ghorofa pacha la Kituo cha Biashara Ulimwenguni huko New York. Nini kilitokea wakati zile ndege zilipoligonga jengo hilo? Jengo lililipuliwa kwa mlipuko wa ndege hizi kisha moto ukakolea zaidi kutokana na mafuta ya ndege hizo kiasi kuwa kila kitu kiliyeyuka. Kwa kuwa zile nguzo vya vyumba zinazoshikilia jengo pia ziliyeyuka, basi muda si mrefu jengo zima nalo lilianguka likianzia ghorafa moja hadi nyingine. Jengo zima lilianguka baada ya dakika chache kutokana na mihili yake yote kushindwa kuhimili uzito wa jengo baada ya kuwa mihili hiyo imeyeyuka. 
Nguvu ya injili ya Mungu ni ile ya injili ya maji na Roho. Pia ni nguvu ambayo ina haki ya Mungu ndani yake. Pengine si vizuri kutumia jambo hili kuielezea haki ya Mungu, lakini nguvu ya injili ya maji na Roho iliyotolewa na haki ya Mungu ni kama dainamoo maana inaweza kuziondoleo mbali dhambi zote. Haki ya Mungu ni kuwa Bwana wetu ametuokoa sisi kwa kuzichukulia mbali dhambi zetu zote wakati ule alipokuja hapa duniani, akabatizwa, akafa Msalabani, na kufufuka toka kwa wafu. 
Injili ya maji na Roho ni haki ya Mungu ambayo kwa hiyo Yesu amezichukulia mbali dhambi zote ambazo mwanadamu alikuwa amezitenda tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu hadi mwisho wake. Hii ndiyo sababu kuwa hakuna kitu kinachoweza kumtenga Mungu na wale ambao anawapenda kwa kupitia ukombozi wao kwa imani katika injili ya haki ya Mungu. Pia imani ya Paulo, ilikuwa ni ile iliyokuwa ikiamini katika haki ya Mungu. 
Sasa je, tunaweza kuipokea haki ya Mungu kwa injili ya damu ya Msalaba tu? Kwa kweli hatuwezi. Kuiamini injili ya damu ya Msalaba pekee haiwezi kutupatia haki ya Mungu. Wale wanaofikiria hivi watajikuta wakiiacha imani yao katika Yesu mara wapatwapo na tatizo dogo. 
Kwa mfano, wakati mali zao za kidunia zinapokuwa zimechukuliwa, au kwa mfano wanapokutana na matatizo kazini kwa sababu ya masuala yao ya kidini, watu wa jinsi hiyo wanaweza kukubali kuikana imani yao. Haya ni matokeo ambayo hayakwepeki kwa Wakristo wengi. Wale ambao hawana Roho Mtakatifu katika mioyo yao kwa kutoamini katika injili ya maji na Roho hawajakombolewa toka katika dhambi zao na wamefungwa ili kujiuzuru na kurudi nyuma mara wapatwapo utisho mdogo. 
Sababu inayoufanya Ukristo wa leo kuwa dhaifu katika ulimwengu huu ni kwa sababu ya imani hii ambayo imefungwa katika damu ya Yesu tu Msalabani. Aina hii ya imani ni ile ambayo haijaipokea haki ya Mungu kwa kupitia injili ya maji na Roho. 
Mwamini mwenye haki ambaye amekombolewa toka katika dhambi zake zote kwa kuipokea haki ya Mungu anaweza kutenda kazi kwa ajili ya nafsi nyingi. Kwa kuwa mtu huyo anaamini katika injili ya maji na Roho na ana Roho Mtakatifu, na kwa kuwa Mungu yupo pamoja naye katika Neno lake, basi mtu huyo anaweza kufanya kazi nyingi za kiroho na kuzigeuza nafsi nyingi zilizopotea kumrudia Mungu. Hii ndiyo imani katika haki ya Mungu, yaani imani katika injili ya maji na Roho. Injili ya maji na Roho inatolewa na Mungu na wala haitokani na matendo yetu, na kwa sababu hiyo tunaweza kuifanya kazi yake kwa kupitia Mungu mwenyewe.
Aya ya 36 inasema, “Kama ilivyoandikwa: ‘Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.’” Kati ya wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wapo wale ambao wanafanyiwa hivi hapa duniani. Kwa kweli, mara nyingi waamini katika injili ya maji na Roho wanachukiwa na wengine, hasa na wale ambao imani yao ni potofu ambao wanajidai wao wenyewe kuwa ni Wakristo. 
Kwa maneno mengine, Wakristo waliozaliwa tena upya wanachukiwa zaidi na Wakristo wa mazoea kuliko hata na Mabudha. Kifungu hiki kisemacho, “kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa,” ni Neno la Mungu ambalo linasemwa kwa waamini wa injili ya maji na Roho. Hata Bwana wetu, hali akiyafuata mapenzi ya Mungu kwa ubatizo wake na damu yake Msalabani “alihesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.” Bwana alituokoa kwa kuja na kuishi hapa duniani katika maisha ya jinsi hiyo. 
 

Haki ya Mungu Imezishinda Dhambi Zote za Ulimwengu 
 
Aya ya 37 inasema, “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Tunawezaje kuyashinda mambo haya yote? Sisi tunautangaza ushindi wetu kwa nguvu ya imani yetu katika upendo wa Mungu. 
Yeye anayeamini katika injili ya maji na Roho ana nguvu ya Mungu. Lakini yeye asiyeamini katika injili ya maji na Roho ana dhambi tu katika moyo wake. Imani na wokovu wa wale walio na dhambi hauwezi kuwa imara bali utakuwa na milima na mabonde kwa sababu ya hisia zao, na kwa sababu hiyo hawana nguvu. Lakini wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wana nguvu. Hawana nguvu itokanayo na wao wenyewe bali wana nguvu ya injili iliyotolewa na Mungu, na kwa nguvu hii, wanaweza kuhimiri na kuyashinda mateso na mapigo yote. Wenye haki ni lazima washiriki katika vita ya kiroho dhidi ya wenye dhambi na waihubiri injili ya maji na Roho kwa wenye dhambi hao. Pia wenye haki ni lazima wavumilie kuishi na kuteswa kwa ajili ya injili kama sehemu ya maamuzi yao kiasili. Maamuzi yetu yanahusu maisha ya kuishi kwa ajili ya Bwana. 
Mithali ya kale inasema, “Ikiwa mtu angekosa kusoma kwa siku moja, angelizungumza maneno ya kuudhi.” Sasa, ni vipi kuhusu sisi? Sisi pia ikiwa tutairuhusu siku moja kuishi bila Mungu na injili yake, basi tutasukumwa kukimbilia katika ufisadi. Hivi ndivyo inavyotupasa kuishi maisha yetu hadi kifo chetu kitakapotokea. Lakini tukiishi kwa ajili ya Kristo, tukijitoa wenyewe kuwa dhabihu na kuteswa kwa ajili ya Mungu, na ikiwa tutapigana vita ya kiroho dhidi ya majeshi ya roho waovu, basi mioyo yetu itajazwa chakula cha kiroho ambapo tutaweza kupata nguvu mpya ya kusonga mbele. 
Wakati Wakristo wanapoanguka, basi ujue kuwa ni kwa sababu hawajaishi kwa ajili ya Bwana. Lakini tunapoishi kwa ajili ya Bwana, nguvu zetu za kiroho zinakua zaidi na zaidi na afya yetu ya kimwili na nguvu pia zinaongezeka zaidi. 
Aya za 38-39 zinasema, “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Paulo aliamini hivi kwa kuwa alikuwa ni mwamini katika injili ya maji na Roho. Ukweli huu unatuhusu pia sisi: wala mauti wala uzima havitaweza kututenga na Kristo. 
Katika zama za kale, mamlaka kuu za kidunia za wakati huo kama vile dola ya Rumi ilijaribu kuwashawishi Wakristo kuikana imani yao na kutoa habari za waamini wengine kwa mamlaka hiyo huku wakiwapatia aina zote za vivutio kama vile cheo katika ofisi za juu, wake, na mali ili kwamba tu waweze kuikana imani yao. Lakini waamini wa kweli katika injili ya maji hawakuyabali majaribu kama hayo ya mamlaka, mali na heshima. 
Imani si kitu kinachoweza kubadilishwa na vitu ambavyo ulimwengu unaweza kuvitoa. Ikiwa mtu angelituonyesha hundi iliyo wazi na kisha akatuambia, “nitakupatia hundi hii ikiwa utaacha kuihubiri injili,” bila shaka tutaweza kumjibu kuwa, kwa sababu ya tumaini letu la hapo baadaye na kwa sababu ya imani yetu yenye nguvu kwa Mungu, “basi uitumie wewe mwenyewe kwa kuwa unaihitaji; kwangu mimi hundi hiyo si kitu ni kama kipande cha karatasi tu.” 
 

Injili ya Maji na Roho Ndiyo Injili Pekee Iliyo na Haki ya Mungu
 
Kuna watu wengi ambao wameniambia mimi kuwa, “Ikiwa utakubali kuwa imani yetu katika damu ya Msalaba pia ni imani sahihi, basi sisi pia, tutaithibitisha imani yako. Si kwamba tutaacha kukuita wewe kuwa ni mzushi, bali tutakusaidia.” Hawa wanaoitwa kuwa ni viongozi wa kidini wamewahi kuyasema hayo kwangu. Lakini haki ya Mungu ni sahihi na yenye uhakika hasa inapopimwa kwa Neno lake. Kile ambacho si sahihi kitabakia kuwa si sahihi, na kile ambacho ni cha kweli kitabakia kuwa cha kweli. Kuitambua imani isiyo ya kweli ni tendo la uasi dhidi ya Mungu, na kwa sababu hiyo siyo tu kwamba siwezi kuithibitisha imani yao bali ninapaswa kukosoa makosa yaliyomo ndani ya imani hiyo bila kukoma. 
“Je, wewe unaamini katika damu ya Msalaba tu? Basi kama hivyo una dhambi katika moyo wako. Umefungwa ili kwenda kuzimu. Hata kama unafikiria kuwa ninasema kwa namna mbaya, ukweli utabaki kuwa ni ukweli.” Kutokana na maneo kama hayo, watu wengi wamekuwa wakijitenga nami—nikisema kwa usahihi kabisa watu wengi wanashindwa kuwa karibu na mimi. Watu wengi walizoea kunifuata wakifikiri kuwa mimi nipo kama wao. Lakini kila wakati waliponifuata niliwaambia kuwa, “Ninyi ni wachungaji wa uongo na matapeli mnaolifanyia biashara jina la Mungu ili mweze kuishi, ninyi ni kama wezi tu.” Ni nani ambaye angeniua kwa kusema maneno kama hayo? Lakini kile ambacho si cha kweli kitabakia kuwa hivyo, na hii ndio sababu nimekuwa imara na mwenye msimamo usioyumbishwa. 
Pia nimewahi kujaribiwa na wale wanaosema kuwa ikiwa nitaamini katika damu ya Yesu watanipatia hiki na kile na mamlaka. Lakini kama kifungu hicho hapo juu kinavyosema, “wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu.” sisi hatuhitaji mamlaka yoyote ile, hatuhitaji yaliyo juu au chini. Hatuhitaji nguvu ya uponyaji ambayo baadhi ya matapeli wanadai kuwa nayo. Sisi tuliozaliwa tena upya hatuhitaji mambo kama hayo na wala hatuyapendi. 
Pia kifungu hicho kinatueleza kuwa hakuna kitu kingine kilichoumbwa kinachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Yesu Kristo Bwana wetu. Hata kama kungekuwa na wageni wa ajabu katika ulimwengu, bado wasingeliweza kututenga na upendo wa Mungu ambao umetuokoa. 
Kuna baadhi ya Wakristo ambao wanaamini juu ya uwepo wa viumbe hai waishio nje ya dunia. Kuna baadhi ya hata wachungaji ambao wanaamini juu ya uwepo wa viumbe hao. Lakini ukweli ni kuwa hakuna viumbe kama hao. Nilipokuwa nikisoma katika seminari moja, profesa wangu mmoja ambaye alikuwa akifundisha Kiyunani alikuwa akiamini juu ya uwepo wa viumbe hao. Basi nikamuuliza, “je unaweza kuthibitisha imani yako kwa ushahidi wowote toka katika maandiko?” Kwa kweli hakuweza kuwa na jibu lolote kuhusiana na hoja yangu. Kwa kweli hakuna viumbe kama hao waishio nje ya dunia tuliyonayo. Mungu aliupenda sana ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee. Kama kweli kungekuwa na hao viumbe waishio nje ya dunia basi kusingekuwa na haja ya Yesu kuzaliwa katika ulimwengu huu tu. 
Baada ya kuwekeza fedha nyingi katika utafiti, tumeweza kuufikia mwezi tu na baadhi ya vyombo vyetu vimeifikia hata sayari ya Mars, lakini hatujaweza kuthibitisha kuwa kuna maisha hai nje ya dunia tunayoishi. Hata kama uwezo wa mwanadamu kisayansi na kiteknolojia ni mkubwa kiasi gani, ninaweza kusema kwa ujasiri kuwa, kwa kufuata msingi wa maandiko hatutaweza kamwe kuviona viumbe vingine vilivyo nje ya dunia. Biblia inatueleza kuwa hakuna viumbe vingine vilivyoumbwa vinavyoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Yesu Kristo Bwana wetu. Sasa, upendo huu wa Mungu ni kitu gani? Huu si mwingine zaidi ya injili ya maji na Roho. Huu ndio upendo wa Mungu. Wokovu ambao umetuokoa na kutufanya sisi kuwa tusio na dhambi kwa injili ya maji na Roho ndio upendo wa Mungu, na hakuna kitu kinachoweza kututenga na upendo huu. 
Katika sura ya 9, Paulo anazungumzia tena kuhusu imani, lakini katika sura hii anafanya majumlisho ya yale aliyoyaongea katika sura ya 8 ambapo kilele cha imani kimefikiwa. Sura ya 1 hadi ya 8 ya kitabu cha Warumi kinatengeneza mada nzima ambapo katika sura ya 8 ndio kama kilele cha imani kinafikiwa. Kama ambavyo Neno la Mungu linavyotuonyesha katika sura ya 8, wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho ndio wanaoweza kutotenganishwa na upendo wa Mungu. 
Hata hivyo, wale wasioamini hawataweza kuwa kama wale wanaoamini. Pengine wanaweza kuishi kwa ajili ya Bwana kwa muda tu, lakini kusema kweli hawataweza kuilinda imani yao na kuishi katika imani hiyo hadi watakapokufa. Wanaweza kuishi maisha ya kidini kwa miaka 10, au 20, lakini hatimaye imani yao itapungua na kuharibika na kufa kabisa hali ikiwaacha wakiwa wametengwa na Mungu kikamilifu. Si kwamba matendo yao yana upungufu, bali ule upendo wao kwa Kristo utapotea ndani yao. Kwa kuwa hawana Roho Mtakatifu katika akili zao, basi watu hao watajikuta hawana upendo wa kumpenda Bwana katika mioyo yao. Kwa kifupi, ndani ya mioyo yao kuna dhambi badala ya upendo. 
Kadri siku zinavyozidi kwenda, ninatambua zaidi na zaidi jinsi ambavyo upendo wa wokovu ulivyo mkamilifu, ambao kwa huo Bwana wetu ametuokoa kwa kupitia injili ya maji na Roho. Nilipokutana na Bwana kwa mara ya kwanza, shukrani zangu za kina kwa upendo wa Yesu zilikuwa ni za kimyakimya kama ambavyo jiwe dogo linavyoweza kutengeneza wimbi dogo baada ya kutupwa katika ziwa. Mwitikio wangu ulikuwa ni kuutambua ule ukweli kimya kimya kuwa Yesu alizichukua dhambi zangu zote na kwamba kwa sababu hiyo mimi nimefanyika kuwa nisiye na dhambi. Lakini wakati nikiishi maisha ya kuihubiri injili tangu wakati huo, basi mawimbi katika moyo wangu yamekua na kuwa makubwa na yenye kina kana kwamba moyo wangu umepigwa bomu. 
Ni nani aliyesema kuwa tunapaswa kuamini katika damu ya Msalaba tu? Je, Paulo alisema hivi? Katika kitabu cha Warumi, Paulo alizingumzia kwa wazi na bila kubabaika juu ya injili ya maji na Roho: “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima” (Warumi 6:3-4).
Je, injili hii ya maji na Roho si sahihi na kamilifu? Haijalishi jinsi imani ya mtu fulani inavyoweza kuwa ndogo, ikiwa mtu huyo anaamini katika injili ya maji na Roho, basi mtu huyo ameokolewa toka katika dhambi zake zote. Haijalishi kuwa una mapungufu kiasi gani, imani yako imefanywa kuwa kamilifu kwa injili ya maji na Roho. Haijalishi kwamba wewe ni dhaifu kiasi gani, unaokolewa kwa imani yako katika injili ya maji na Roho. Ingawa sisi binafsi hatuna nguvu, lakini ikiwa tutaishi kwa ajili ya Mungu, basi ule uchafu wote utaondolewa toka katika mioyo yetu. 
Hata kama watu wameisikia injili hii na kisha wakaishi kwa kuifuata kwa miaka 10, ukweli ni kuwa wale wasioamini tangu mwanzoni watageuka mwishoni na kuwa kinyume na Mungu na kumwacha Mungu. Wale ambao wameamua kutoutazama wala kuusikia ukweli wa Mungu kwa kuyafunga macho yao na kuyafunga masikio yao basi watu hao ni wajinga sana kwa kuwa wanaikataa baraka ya Mungu kwa mikono yao wenyewe na wanaelekea kwenda katika maangamizi yakifo chao. Watu hao ndio wale wanaomsulubisha Kristo kila siku kwa dhambi zao ingawa ukweli ni kuwa bila ubatizo wa Yesu kusingekuwa na kifo cha Yesu Msalabani. 
Kila siku inayopita ninazidi kutambua jinsi ambavyo injili hii ni kuu na kamilifu—kadri ninavyozidi kuwa dhaifu, ndipo ninapozidi kutambua jinsi upendo wa Bwana wetu ulivyo mkamilifu na wa kushangaza kama unavyoonyeshwa na injili hii, na hapo ndipo ninapomshukuru Mungu zaidi na zaidi. Kadri ninavyozidi kuihubiri injili hii, ndivyo ninavyozidi kupaza sauti; kadri ninavyozidi kuihubiri injili hii, ndivyo ninavyozidi kuwa na nguvu zaidi, na kadri ninavyozidi kuihubiri injili hii ya kweli, ndivyo ninavyozidi kushawishika. 
Hata kama umezaliwa tena upya, ikiwa haulisikilizi Neno la Mungu na haumtumikii, basi magugu yataanza kukua katika akili zako, na kwa sababu ya magugu haya akili zako zitakuwa na huzuni na upweke. Hali hii itakapotokea, imba nyimbo zako za kusifu tena na na tena na kisha mfikirie Yehova. Akili zako zitasafishwa na utaweza kuiinua roho yako tena kwa kumwimbia Mungu nyimbo za sifa. 
Ni lazima uzichangamshe akili zako ili kuondokana na mambo yote ambayo si safi na kisha uufanye moyo wako kuwa mpya kwa kuujaza Neno la Mungu. Mioyo yetu imekwisha safishwa lakini wakati uchafu wa dunia unapoingia katika akili zetu na kujaribu kutuchanganya na kutufanya kutokuwa wazingatiaji, basi tunaweza kumwabudu Mungu na kumwomba tena kwa kuimba nyimbo za sifa za Bwana, na katika hali hiyo tutakuwa tukiinua na kuifanya mioyo yetu kuwa mipya. 
Haijalishi kuwa ni watu tunaweza kuwepo, kwa kweli kumsifu Mungu ni uzoefu wenye kupendeza na kutia moyo. Hakuna dhambi ndani ya wale waliokombolewa na kwa hiyo kusifu na kufurahi kunajitokeza kwenyewe toka katika akili zao. Nyimbo za kusifu zitokazo katika mioyo yetu yenye furaha zinaweza kuyafanya magugu yanayokua katika akili zetu kutoweka. 
Kwa baadhi ya nyakati, udhaifu wetu hufunuliwa. Kwa kuwa mawazo yetu na hisia zetu zinaweza kubadilika katika mazingira tofauti, ingawa tunaweza kuwa na furaha na hisia nzuri tunapokuwa na ndugu zetu katika Kristo, basi tunaweza pia kujikuta tukiwa na mawazo machafu hasa wakati tunapokuwa peke yetu. Hii ndiyo sababu Paulo alipokuwa akiungalia mwili wake alilia akisema, “Ole wangu maskini mimi mwenye dhambi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa Mauti? Namshukuru Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo!” (Warumi 7:24-25)
Pamoja na kuwa Paulo alikuwa dhaifu katika mwili wake, ukweli ni kuwa Paulo alifanyika kuwa mkamilifu kwa kuokolewa na injili ya maji na Roho. Je, ni Paulo peke yake aliyekuwa kama hivi? Mimi pia nipo kama Paulo. Je, wewe pia haupo kama Paulo? 
Wakati watu wa kidunia wanapowakusanya watu pamoja, basi mara nyingi wanaume hupenda kunywa hali wakizungumzia kuhusu kazi zao na kuhusu waliopanda vyeo na wale ambao hawajapanda vyeo na mambo kama hayo, wakati wanawake huwa wanatumia muda mwingi kujisifia waume zao, watoto wao, nyumba zao, na mambo kama hayo. Lakini majadiliano kati ya wenye haki kwa kweli yapo tofauti kabisa kiviwango ukilinganisha na yale ya watu wa kidunia. Hata pale ambapo tunaushiriki mkate pamoja, mara nyingi tunazungumzia kuhusu nafsi ambazo zimeokolewa katika ulimwengu mzima: India, Japani, Ulaya, Afrika, Marekani, na kadhalika, hali tukimsifu Mungu na kuwa na faragha ya pamoja ya akili zetu. 
Tunapokisoma Kitabu cha Warumi, tunaweza kuiona imani ya Paulo hivyo kuushirikisha uzoefu wake katika mioyo yetu. Pia tunaweza kuona jinsi ambavyo wokovu wa Mungu ulivyo mkuu. Pia tunaweza kuihisi hali ya injili ilivyo ya kushangaza. Tunaweza kukifahamu kifungu na kutambua maana iliyofichika katika maandiko. Kwa kuwa tunatambua jinsi wokovu wa Bwana wetu ulivyo sahihi na mkamilifu, basi sisi hatuna jambo lolote la kufanya zaidi ya kuisifu haki ya Mungu. 
Hata kama ulimwengu mzima ungegeuka sasa hivi, ukweli ni kuwa injili ya maji na Roho ambayo imetuokoa sisi toka katika dhambi itabakia kama ilivyo na haitabadilika. Kwa kuwa upendo wa Kristo umetuokoa, na kwa kuwa upendo huu haujatuacha kamwe na bado umo ndani yetu, basi tunachotakiwa kufanya ni kuigeuza mioyo yetu kutoielekea dunia na kumwelekea Mungu. Sisi ni wadhaifu, na kwa sababu ya udhaifu huu, kuna nyakati ambazo tunajikuta tukizifuata njia au namna za kidunia, lakini hali hii inapojitokeza kila wakati, basi tunachopaswa kukifanya ni kuzigeuza akili zetu ili zimwelekee Mungu na kuamini katika ule ukweli kuwa Bwana wetu ametuokoa. Miili yetu bado haijabailika na bado inaishi chini ya sheria ya dhambi. Hivyo ni lazima kwa utashi kabisa kuikana miili yetu na kisha kuishi maisha yetu hali tukiwa na mawazo ya kiroho. Ili tuweze kuyazuia magugu kukua katika mioyo yetu, basi tunapaswa kumrudia Mungu kila mara na kuisifu haki yake. 
Je, sasa unatambua jinsi injili hii ya maji na Roho ilivyo na nguvu? Kwa kuwa kitabu kizima cha Warumi kimejengwa katika injili ya maji na Roho, basi ukweli ni kuwa hatuwezi kulifungua neno la Mungu vizuri pasipo kwanza kuiamini injili hii. 
Ninamshukuru Bwana kwa kuturuhusu kuzifungua na kuziona siri za Neno lake. Hakuna anayeweza kututenga na haki ya Mungu ambayo imo katika upendo wa Kristo. Ikiwa unapenda kuiamini haki ya Mungu, basi amini katika ubatizo wa Yesu alioupokea toka kwa Yohana na damu yake Msalabani kuwa ndio ukombozi na wokovu wako. Basi hapo ndipo wewe nawe utaipokea haki ya Mungu. 
Baraka za haki ya Mungu na ziwe juu yako.