Search

Mahubiri

Somo la 11: Maskani

[11-4] Sababu Iliyomfanya Mungu Amuite Musa Kwenda Katika Mlima Sinai (Kutoka 19:1-6)

Sababu Iliyomfanya Mungu Amuite Musa Kwenda Katika Mlima Sinai
(Kutoka 19:1-6)
“Katika mwezi wa tatu baada ya waisraeli kutoka katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai. Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa, Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita toka mlima ule, akisema, ‘utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli maneno haya: ‘Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu. Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu.’ Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.’”
 


Kwa Nini Mungu Aliwachagua Watu wa Israeli?

 
Kifungu kikuu cha maandiko kinatoka katika Kutoka 19:1-6. Japokuwa kifungu hiki cha maandiko si kirefu, nina mambo mengi ya kuzungumza kuhusu kifungu hiki. Kutoka katika kifungu hiki, nitapenda pia kuzungumzia juu ya ukweli uliofunuliwa katika sura ya 19 na ile ya 25 katika kitabu cha Kutoka. Ilikuwa imeshapita miezi mitatu tangu watu wa Israeli walipotoroka kutoka Misri na kufika katika jangwa la Sinai. Mungu aliwafanya waweke kambi zao mbele ya Mlima Sinai, na kisha akamwita Musa kwenda juu mlimani.
Baada ya kuwa amemwamuru Musa, Mungu alizungumza maneno yake kwa waisraeli, “Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu. Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.” Sababu iliyomfanya Mungu kuwaita na kuwakuza watu wa Israeli ilikuwa ni kuwafanya waisraeli kuwa tunu maalum na kuwathibitisha kuwa makuhani wa Ufalme wake.
Hili lilikuwa ndilo lengo ambalo kwa hilo Mungu aliwaokomboa watu wa Israeli toka Misri. Njia ambayo Mungu angeitumia ili kuwafanya Israeli kuwa tunu yake maalum ilikuwa ni kwa kuwapatia Sheria na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania ili kuwaokoa toka katika dhambi zao, ambapo angewasafisha dhambi zao, na kuwafanya kuwa watu wake binafsi, na kuanzisha juu yao taifa la makuhani. Kwa hakika, waisraeli ni lazima walitambue hili vizuri, na ni lazima wairudishe imani yao ambayo Mungu anaihitaji toka kwao. Ili kulifanya taifa lao kuwa Ufalme wa Makuhani wa Mungu, Mungu, kwa upande mmoja aliwapatia Sheria iliyoundwa na amri 613, na kwa upande mwingine, aliwafanya walijenge Hema Takatifu la Kukutania.
Kwa hiyo, ikiwa waisraeli hawamwamini Yesu Kristo aliyekuja kama Masihi wao, ni lazima watubu na kumwamini yeye kwa mioyo yao yote. Yesu, ambaye ndiye kiini halisi cha sadaka ya dhambi ya utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania, amezisafisha dhambi zao zote kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana na damu yake Msalabani. Kwa hakika, watu wa Israeli ni lazima waukubali ukweli kuwa Mungu amewafanya wao kuwa watu wake mwenyewe kwa kuwaleta wazawa wa Ibrahimu toka Misri; na kwa kuziosha kabisa dhambi zao zote kupitia sadaka katika Hema Takatifu la Kukutania. Kwa wakati ule, kwa sababu waisraeli walishindwa kuifuata Sheria ya Mungu, walitakiwa kusamehewa dhambi zao kwa kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa uliowekwa na Mungu. Sadaka hizi za kuteketezwa zilikuwa ni kivuli cha Yesu Kristo, Mwokozi ambaye sasa amewaokoa wanadamu toka katika dhambi zao.
Hata sasa, Waisraeli wanashikilia kuwa Musa ndiye nabii mkuu kuliko wote. Katika hili wako sahihi. Hata hivyo, kwa sababu hawamwamini Yesu Kristo kuwa ni Masihi aliyewaokoa toka katika dhambi zao zote, basi na wao pia hawalitambui Agano Jipya kuwa ni Neno la Mungu, na badala yake wanalitambua Agano la Kale tu kuwa ni Neno la Mungu. Lakini ni lazima tukumbuke kuwa Yesu si ni nabii mkuu tu kuliko Musa, bali ni Kuhani Mkuu wa Ufalme wa Mbinguni, Masihi ambaye waisraeli wamekuwa wakimtarajia na kumsubiri. Waisraeli wanatakiwa kutambua kwa imani kuwa kitu kikuu kilichokuwepo katika sadaka ya kuteketezwa ya Hema Takatifu la Kukutani kilikuwa ni Masihi mwenyewe.
 

Mungu Aliwafanya Waisraeli Wamshikilie Musa Kwa Heshima na Unyenyekevu, Lakini…
 
Kwa nini Mungu alimwinua sana Musa mbele ya Waisraeli? Ilikuwa ni kuwafanya waweze kukubali na kuamini maneno yote ya Mungu yaliyotamkwa kupitia Musa. Kwa maneno mengine, ilikuwa ni kuwafanya waisraeli waamini kuwa yale ambayo Musa aliyaongea kwao lilikuwa ni Neno la Mungu mwenyewe. Mungu alimwita Musa juu katika Mlima wa Sinai ili aweze kuinuliwa juu mbele ya watu wa Israeli. Hii iliwafanya waisraeli wamwogope Musa na Mungu, na kuona kuwa Musa alikuwa akiongea na Mungu, basi waisraeli walimwamini Mungu kwani Mungu aliongea na Musa kana kwamba alikuwa ni rafiki yake.
Kwa hakika, Neno la Mungu ambalo Musa alilitoa kwa watu wa Israeli liliaminiwa lote na waisraeli kuwa ni Neno halisi na ambalo Mungu amesema nao. Hata hivyo, kwa kumchukulia Musa kuwa ni mtu wa hali ya juu sana, watu wa Israeli walifanya makosa makubwa sana ya kutomkubali Yesu Kristo Masihi katika mioyo yao kuwa ni Mwokozi wao. Mwishowe, waisraeli walishindwa kumtambua Masihi wao vizuri, na kwa hiyo wameishia kuukataa upendo wake wa wokovu. Kwa sasa wanalo jukumu kuu mbele yao—ambalo ni kumkubali Yesu Kristo katika mioyo yao kuwa ni mwokozi wao, ambaye alikuwa ni nabii mkuu kuliko hata Musa.
 


Mungu Aliwaamuru Watu wa Israeli Kulitengeneza Hema lake Takatifu la Kukutania na Kumtolea Sadaka za Kuteketezwa

 
Kupitia Musa, Mungu alizitoa Sheria na amri zake kwa watu wa Israeli, na pia aliwaeleza kulijenga Hema Takatifu la Kukutania. Katika Hema Takatifu la Kukutania, Upendo wa Mungu wa huruma ambao kweli ndio ulioziondoa dhambi za waisraeli ulifunuliwa kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa. Kwa kupitia utaratibu huu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu amewapatia pia ondoleo la dhambi kwa wazawa wa kiroho wa Ibrahimu, na ameziosha dhambi zao zote ili wasipungukiwe na kitu ili kufanyika watu wa Mungu mwenyewe.
Mungu aliwapatia watu wa Israeli mbao mbili za mawe zilizokuwa na amri zake kumi zilizoandikwa juu yake. Amri kumi ziliundwa na amri kuu nne za mwanzo ambazo zilipaswa kufuatwa kati ya Mungu na mwanadamu, na amri sita za chini zilipaswa kufuatwa kwa ajili ya uhusiano wa wanadamu. Mbali na hizi amri kumi, Mungu aliwapatia pia watu wa Isareli mamia ya amri ambazo walipaswa kuzifuata katika maisha yao ya kila siku.
Sababu iliyomfanya Mungu awapatie waisraeli amri na sheria nyingi hivyo ilikuwa ni kutaka kuwaonyesha katika mioyo yao kuwa ni Mungu tu ndiye ambaye ni mkamilifu. Kwa watu wa kiroho wa Israeli—ambao ni wale wanaomwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao—kwa wao hakuna yeyote zaidi ya Mungu. Ili kuwafundisha vizuri watu wa Israeli kabla ya kuingia katika nchi ya Kanaani juu ya ukweli kuwa yeye ni Yehova; Mungu aliongea na Musa katika Mlima Sinai ili kuwapatia Sheria yake. Na aliwafanyia utaratibu kuwa pale wanapofanya dhambi kwa kuzivunja amri za Mungu waweze kusamehewa dhambi zao zote kwa kutoa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa aliokuwa ameuanzisha.
 
 

Watu wa Israeli Walipokea Sheria na Amri toka kwa Mungu. 

 
Hebu tuangalie Kutoka 24:3-8: “Basi Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, ‘Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda.’ Kisha Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli. Akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha Agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, ‘Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii.’ Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyuzia watu, akasema, ‘Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote.’”
Mungu alilifanya agano kwa damu alipowapatia Sheria watu wa Israeli kupitia Musa. Kwa kifupi, hii ilimaanisha kuwa Sheria ya Mungu ilikuwa ni Sheria ya Uzima. Mungu aliongea juu ya Sheria yake ya Uzima kwa waisraeli na watu wa Israeli walipaswa kuamini Maneno ya Mungu.
Kwa jinsi hiyo, Musa aliwaambia waisraeli kuleta damu ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani. Mungu alimfanya Musa kuwakusanya watu wake pamoja, akawasomea Sheria na amri ambazo ni agano la Mungu. Kisha Musa akawauliza, “Je, mtatii yale ambayo Mungu amewaamuru ninyi?” Kisha waisraeli wakamjibu kwa sauti moja kuwa wote watamtii.
“Nitakulinda na kukufanya kuwa ufalme wa kikuhani,” Kisha Mungu aliwaahidi waisraeli kupitia Musa. Kisha Musa akawanyunyuzia damu ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani. Hii inaonyesha kuwa mtu anapozini, mtu huyo anapaswa kusamehewa kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa. Ni lazima tukubali kuwa Mungu aliongea kama Neno la Uzima. Musa aliichukua damu ya sadaka, akawanyunyuzia watu wake, na akawaambia, “Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote.” Hii inatueleza kuwa kwa sababu Neno la Mungu ni Neno la Uzima, kama hatulifuati, basi ni lazima tuzipeleke dhambi zetu katika sadaka ya kuteketezwa kwa kuiweka mikono yetu juu ya kichwa cha mwanasadaka, na kumchinja, na kisha kuitoa damu yake kwa Mungu kwa ajili ya dhambi zetu.
Tunachopaswa kutambua ni kuwa katika Sheria hii ya Mungu, kuna adhabu kwa ajili ya dhambi zetu, lakini pia kuna utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa unaoziosha kabisa dhambi zetu zote. Kwa hiyo, tunaposhughulika na Sheria ya Mungu na amri zake, ni lazima tuzikubali katika mioyo yetu hali tukitambua kuwa katika Sheria hizi na amri kunapatikana sadaka inayotupatia ondoleo la dhambi zetu. Imani hii ni ya muhimu sana. Kwa sababu tunabarikiwa pale tunapoifuata Sheria ya Mungu na tunalaaniwa pale tunaposhindwa kuifuata. Ni lazima tuamini kwamba tunatakiwa kuziosha dhambi zetu mara kwa mara kwa sadaka zetu za kuteketezwa. Kwa hakika, wale waliofanya dhambi wanapaswa kupokea ondoleo la dhambi kwa kuzipeleka dhambi zao katika sadaka ya kuteketezwa kwa kuilaza mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka, na kwa kuchukua damu ya mwanasadaka na kuitoa kwa Mungu. Ni lazima sote tutambue na tuamini kwamba Sheria na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ni Sheria ya Uzima, ambayo kwa hiyo tunaweza kupokea maisha mapya toka kwa Mungu.
Kwa hiyo, wakati Sheria ya Mungu inatufundisha kuhusu dhambi zetu, injili ya maji na ya Roho inatuonyesha kinyume chake kuwa dhambi zetu zote zimeondolewa kupitia ubatizo ambao Yesu Kristo aliupokea toka kwa Yohana na kwa damu yake Msalabani—ambayo ni kweli imetuokoa toka katika dhambi zote za ulimwengu.
Katika kipindi cha kale, wakati makabila yalipowekeana ahadi, mara nyingi walileta aina fulani ya sadaka ya kuteketezwa. Walileta kondoo, mbuzi, au mafahari ya ng’ombe, na walithibitisha makubaliano yao kwa damu iliyopatikana toka katika wanyama wao wa sadaka kwa kuwachinja makoo yao. Hii ilikuwa ndio msingi wa hadidu za rejea, kwa maana ilimaanisha kuwa, “Ikiwa hutalifuata agano ambalo umeliweka nami, basi kwa hakika utakufa kama mnyama huyu alivyokufa.” Kwa kifupi, waliyathibitisha makubaliano yao kwa damu.
Kama hivyo, Mungu ameithibitisha Sheria yake kwa damu. Kwa maneno mengine alituambia kuwa, ikiwa tutashindwa kuzifuata sheria zote 613 na amri, basi tutauawa kwa sababu ya dhambi. Lakini kwa wakati huo huo, pia ametueleza kulipokea ondoleo la dhambi zetu kwa kumpatia yeye sadaka ya dhambi kwa imani kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania.
Ikiwa tusingelichukulia Neno la Mungu la Sheria kwa nia, tusingeweza kamwe kuikwepa hasira toka kwa Mungu kwa sababu ya dhambi zetu. Lakini ikiwa tutampatia sadaka ya kuteketezwa aliyoiandaa kwa ajili yetu, basi Mungu atazipokea sadaka hizi za kuteketezwa na atatusamehe dhambi zetu zote. Ni lazima sisi sote tuiamini Sheria hii ya Uzima, Sheria hii ya wokovu inayotueleza kuwa Mungu atazisamehe dhambi za watu wote wa Israeli kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ya Hema Takatifu la Kukutania, na kwamba tutapokea ondoleo la dhambi zetu katika mioyo yetu. Yeyote anayeidharau Sheria ya Mungu ametengwa kutoka katika upendo wa Mungu wa huruma, na kwa hiyo, sisi sote inatupasa kuiamini Sheria na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa kuwa ni ukweli wa wokovu katika maisha yetu.
Hii ndiyo sababu iliyomfanya Musa kulisoma agano lililofanywa kwa damu, na kwa damu hii aliwanyunyuzia watu wa Israeli, na wakaweka ahadi zao kwa Mungu kwa damu. Kwa hiyo basi, tukitambua kuwa sote tunatakiwa kufa ikiwa hatutaitii Sheria hii iliyothibitishwa kwa damu, sisi sote ni lazima tupokee ondoleo la dhambi zetu zote kwa kuamini pamoja na Sheria katika Yesu Kristo, ambaye ndiye sadaka yetu halisi ya kuteketezwa na sadaka ya amani kwa Mungu.
Sisi sote ni lazima tutambue na kuamini katika ukweli kwamba tunaweza kusamehewa dhambi zetu zote kwa kumpatia Mungu sadaka zetu za kuteketezwa kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania. Kupitia nyuzi zake za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, Mungu ametufundisha kwa wazi juu ya ondoleo la dhambi kwa wanadamu wote. Ili waweze kusamehewa dhambi zao zote, inabidi dhambi zao zote zipelekwe kwenye sadaka ya kuteketezwa kwa kuweka mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka wa kuteketezwa, kisha mwanasadaka huyu atatakiwa kuimwaga damu yake ambayo itawekwa katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na damu inayosalia itamwagwa ardhini.
Hii ilikuwa ni sadaka ya kutoa ambayo ilihitajika kwa mujibu wa sheria ya kifo na dhambi. Kwa hiyo, kwa imani yetu, ni lazima sisi sote tupokee ondoleo la dhambi lililoahidiwa kwa sadaka ya kuteketezwa inayoziondoa kabisa dhambi zetu. Kwa kutupatia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu ametupatia sisi sheria ya wokovu, ili tuweze kuliamini Neno la Mungu na kisha tusamehewe dhambi zetu zote. Ni lazima sisi sote tupokee baraka ya ondoleo la dhambi iliyotolewa na Mungu kwa kukubali katika mioyo yetu sheria mbili ambazo Mungu amewapatia wanadamu: Sheria yenyewe na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania.
 


Je, Tunawezaje Kuokolewa Toka Katika Dhambi Zetu Zote?

 
Kwa kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ambao Mungu alimpatia Musa, aliwaonyesha watu wa Israeli kuwa wokovu wao toka katika dhambi zao zote unawezekana kwa imani yao tu katika ondoleo la dhambi zao kupitia sadaka ya kuteketezwa.
Tunapompatia Mungu imani yetu inayoamini juu ya sadaka ya kuteketezwa iliyowekwa na Mungu mwenyewe, basi Mungu ataipokea imani yetu na atatuokoa toka katika dhambi zetu zote. Kwa nini? Kwa sababu Mungu amekwisha kuwaokoa wanadamu wote toka katika dhambi zao, na kwa wale wanaoamini, anawapatia baraka yake ya kuwatakasa toka katika dhambi zao zote. Kwa kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa uliowekwa na yeye aliye mkamilifu, Mungu ametuwezesha kuifahamu sheria ya wokovu. Ikiwa mtu hafahamu au haamini katika ukweli kwamba Yesu Kristo amezisafisha dhambi zake milele kwa ubatizo wake na damu yake Msalabani, basi kwa hakika mtu huyo atahukumiwa. Inatulazimu sisi sote kuuamini upendo wa Mungu wa huruma.
Mungu ametuokoa sisi kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania, utaratibu ambao njia yake ya wokovu ilikuwa ni kwa kuzipitisha dhambi zetu katika mnyama wa sadaka kwa kuilaza mikono yetu juu ya kichwa cha mnyama huyo. Kwa hiyo, ni lazima sisi sote tuiamini injili ya rehema ambayo imewaruhusu wote wanaoamini katika ukweli huu kusafishwa dhambi zao. Wale ambao hawaitambui Sheria na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa mbele za Mungu hawawezi kamwe kupokea ondoleo la dhambi zao milele, lakini wale wanaoamini katika injili ya rehema za Mungu wanaweza wote kupokea ondoleo la dhambi zao milele.
Mungu hakutuambia kuwa tusifanye dhambi tu, bali alitufundisha kuwa sisi ni viumbe wenye dhambi ambao tungeendelea kutenda dhambi kila siku. Kwa hiyo, alitueleza kumpatia yeye sadaka zetu za kuteketezwa ili tuweze kupokea ondoleo la dhambi hizi. Na hii ndiyo sababu Mungu alisema, wakati mwenye dhambi atakapokuwa akitoa sadaka ya kuteketezwa, “Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng’ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia” (Kutoka 20:24).
Sadaka za dhambi ambazo waisraeli walizitoa kwa Mungu zilichukua muundo wa kuiweka mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka wa kuteketezwa, ambapo dhambi zao zilipitishwa kwenda kwa mwanasadaka huyo, kwa kuikinga damu yake na kuiweka katika pembe za madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, na kwa kuiweka nyama ya mwanasadaka juu ya madhabahu na kuichoma kwa moto. Kuiamini kwa moyo wote sheria ya wokovu iliyotolewa na Mungu kulihitajika sana kila wakati walipotoa sadaka za jinsi hiyo. Sadaka ambazo Mungu alizitaka hazikuwa zile za kidini, bali zilikuwa ni zile za haki ambazo zilipitisha dhambi zao katika sadaka za kuteketezwa katika imani, hali wakiamini kuwa kama si kwa neema ya Mungu walistahili kwenda kuzimu.
Bwana wetu alibatizwa na Yohana na akamwaga damu yake Msalabani ili kuzifanya dhambi zetu zitoweke. Aliamua kuziondoa dhambi zetu kwa njia ile ile ya sadaka za dhambi. Sadaka hii ya imani ilikuwa ni kivuli cha sadaka ya wokovu wa Agano Jipya iliyotimizwa na Yesu Kristo—ambayo ni kusema, Kristo alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi za ulimwengu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana, alikufa Msalabani, na kwa hiyo amewaokoa wanadamu wote toka katika dhambi zao. Ni kwa kuuamini ukweli huu kwa mioyo yetu yote ndipo tunapofanyika wana wa Mungu.
 

Ni Lazima Tuziachilie Mbali Imani za Mafundisho ya Dini.
 
Kutoka 20:25-26 inasema, “Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi. Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.” Ni lazima tutazame kwa makini juu ya jambo ambalo Mungu ameliongea katika aya hii. Mungu aliwaambia waisraeli kuwa katika kuifanya madhabahu, ikiwa wataijenga madhabahu ya mawe, wasiijenge kwa mawe yaliyokatwa au kuchongwa, bali waijenge kwa mawe ambayo yapo katika muundo na umbile lake la asili. Je, hii inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa Mungu anafurahia kuipokea imani yetu katika wokovu wake, ambayo haiwezi kuongezewa au kubadilishwa na mawazo ya mwanadamu.
Mungu anatuonya sisi kwa kauli hii, “Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake,” ili tusimwabudu yeye kwa imani za kidini zilizotengenezwa na mwanadamu. Kila dini iliyopo hapa ulimwenguni ni bure tu kwa maana ni mfumo wa imani uliotengenezwa na wanadamu. Wanajiwekea kanuni za msingi katika dini zao zinazowaeleza watu kujaribu kuwa watakatifu hatua kwa hatua hali wakiishi maisha ya kidini ya uaminifu. Hata wakristo wa kidini wanadai kuwa wanaweza kutakaswa kwa kuongezewa utakaso kidogokidogo wakati wanapoishi maisha mazuri kulingana na Sheria ya Mungu.
Lakini, ni kweli? Kwa hakika ni hapana! Wanadamu waliozaliwa kama wazawa wa Adamu hawawezi kuifuata Sheria ya Mungu kwa sababu ya dhambi zao, na hawawezi kukwepa kifo bali watakikabili kwa sababu ya dhambi hizi. Kwa hiyo, ili kuwaokoa watu wote wa jinsi hiyo toka katika dhambi za ulimwengu, Mungu alianzisha utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania, na kwa hakika amewaokoa wote.
Kwa hiyo, ni lazima sisi sote tuikubali injili ya rehema ya ondoleo la dhambi zetu, injili ya wokovu wetu kwamba Mungu ametuwekea sisi kwa nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa iliyodhihirishwa katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Ni lazima tuamini kama ilivyoandikwa katika Neno la Biblia, kwamba Yesu Kristo alikuja hapa duniani kama Mungu wa Neno, kuwa alizifanya kazi zake kama alivyoelezwa na nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilizodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania, na kwa hakika ametuokomboa toka katika dhambi zetu zote.
Je, itakuwaje kwa watu ambao wana imani na mafundisho ya kidini tu? Je, wanafanyaje ili waweze kusamehewa kutokana na dhambi za kila siku? Watu wa jinsi hiyo wanajaribu kupokea ondoleo la dhambi kwa kutoa maombi yao ya toba, hali wakijaribu baadae kuwa wenye haki kwa kupitia mafundisho ya kuongezewa utakaso taratibu. Mafundisho ya jinsi hii ni ya upotofu, na ni mafundisho ya kiimani yaliyotengenezwa na mwanadamu mwenyewe. Kujaribu kumfikia Mungu kwa jitihada za mtu binafsi kunaonyesha kiburi, na ni jambo la wazi linaloonyesha uovu wa kidini wa mtu binafsi.
Watu ni lazima wakiri kuwa hakuna kitu ambacho wao wenyewe wanaweza kufanya ili kuzifanya dhambi zao kutoweka mbele za Mungu. Tulipozaliwa katika ulimwengu huu, wote tulizaliwa kama aina ya viumbe ambavyo haviwezi kujisaidia zaidi ya kuendelea kutenda dhambi zetu binafsi, na hii ndiyo sababu tunatenda dhambi nyingi sana mara kwa mara. Haijalishi ni mara ngapi Mungu anatueleza tusitende dhambi katika Sheria yake, bado tunajikuta tukiivunja Sheria yote na kutenda dhambi maradufu mbele za Mungu. Kwa hiyo, ni lazima tukiri mbele ya Sheria ya Mungu kwamba sisi tu wenye dhambi. Na ni lazima tuamini kwa mioyo yetu juu ya ukweli wa wokovu kuwa Mungu ametuokoa toka katika dhambi zetu zote kupitia kazi za Bwana wetu Yesu kama zilivyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa.
Hakuna njia nyingine zaidi ya kulimini Neno la Mungu, kwamba ili kutokoa sisi toka katika dhambi zote za ulimwengu, Bwana mwenyewe alifanyika kuwa sadaka yetu ya kuteketezwa kwa kupitia ubatizo wake, na kwamba kwa jinsi hiyo ametuokoa toka katika dhambi za ulimwengu. Biblia inatueleza kuwa hakuna mungu mwingine zaidi ya Yehova, na kwamba hakuna anayeweza kwenda kwa Baba pasipo kupitia kwa Kristo (Yohana 14:6). Kwa kulitambua na kuliamini Neno la Mungu la Sheria, sisi tunakuwa ni wenye dhambi, na kwa kuiamini injili ya maji na Roho, sisi tumeokolewa toka katika dhambi zetu. Huu ndio ukweli na imani yetu halisi katika Mungu.
Kwa hiyo, ni lazima tuuamini wokovu wake kwa mujibu wa sheria ya ondoleo la dhambi ambayo Bwana wetu ameiweka kwa ajili yetu ili kutuokoa sisi toka katika dhambi zetu zote. Ukristo si kama moja ya dini zingine za ulimwengu, bali ni ukweli wa wokovu uliojengwa katika msingi wa imani yetu inayomwamini Yesu Kristo aliyeonekana katika nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa.
 

Kwa Kupitia Kifungu Kikuu cha Maandiko Hapo Juu, Ni Lazima Sisi Sote Tutambue Kuwa Ni Kwa Nini Mungu Ametuita
 
Ni lazima sote tutambue ukweli kuwa Mungu ametuita mimi na wewe ili kutufanya kuwa tunu yake maalum. Mimi na wewe hatuwezi kuwa watu wa Mungu kwa matendo na juhudi zetu. Bali, wewe na mimi tumefanyika wana wa Mungu kwa sababu tumeuamini ukweli kuwa Yesu Kristo alikuja hapa duniani kutukomboa toka katika laana ya Sheria na adhabu na uharibifu wa kuzimu. Kwa kubatizwa na Yohana na kumwaga damu yake Msalabani, kwa hakika ametuokoa kikamilifu sisi tunaoamini. Masihi, Mwana wa Mungu, alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, akazichukua dhambi zote za mwanadamu kwa ubatizo wake mara moja, akazibeba dhambi hizi za ulimwengu Msalabani, akajitoa mwenyewe kwa ajili yetu kulipa malipo ya dhambi zetu kwa kusulubiwa, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo amefanyika Mwokozi kwa wale wanaomwamini kwa mioyo yao yote.
Mungu anatueleza kuwa amewapatia wanadamu ondoleo sahihi la dhambi kwa kupitia nyuzi zake za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Bwana wetu anatuuliza sisi, “Je, unaziamini kazi zangu, kwa yale niliyoyafanya kwa ondoleo la dhambi zako, kwamba nilikuja hapa duniani na kubatizwa na Yohana na kumwaga damu yangu Msalabani?” Tunachoweza kusema mbele za Mungu ni “ndiyo.” Ili sisi tuweze kuokolewa hakuna njia nyingine zaidi ya kuamini katika onndoleo la dhambi ambalo Mungu ametupatia. Sio tu kwa waisraeli wa zama za Agano la Kale, bali kwetu sisi wa leo—kwa hakika, watu wote wa ulimwengu mzima—ni lazima wafahamu kwa nini Mungu alimuita Musa katika Mlima Sinai na kumwambia Neno hili katika kifungu hiki cha maandiko. 
Mungu aliwapatia waisraeli amri kumi, na kisha akawaambia kujenga madhabahu ya mavumbi kwa imani ili kupokea ondoleo la dhambi zao (Kutoka 20:24). Vivyo hivyo, kwa kupitia imani yetu katika injili ya maji na Roho iliyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ambayo Mungu alitupatia, ni lazima pia tukombolewe toka katika dhambi zetu zote.
Je, jina la Mungu mwenyewe ni lipi? Jina lake ni “Yahwe.” Maana yake, “MIMI NIKO AMBAYE NIKO,” ambayo ina maanisha kuwa, Mungu ndiye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe. Ilikuwaje basi akaja kwetu? Alikuja kwetu kupitia maji na Roho (Yohana 3:5). Bwana wetu alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, alizichukua dhambi zote za wanadamu kwa kubatizwa na Yohana, na alifanywa kafara kwa niaba yetu kwa kusulubiwa hadi kifo. Ni kwa sababu ya ukweli huu, na ni kwa sababu tunatakiwa kuamini hivyo, kwamba Mungu alitueleza kuwa na imani ambayo ilidhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilizotumika katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Imani ya kweli inakuja pale tunapoyakana mawazo yetu binafsi na kutambua ondoleo la dhambi lililotolewa na Mungu. Hatuwezi kumshukuru vya kutosha kwa yeye Mungu kutupatia upendo usio na masharti kama huo, kwani hakuna kinachoweza kutufanya tuwe na majivuno mbele za Mungu.
Ni lazima tuujenge msingi wetu wa imani katika maarifa sahihi ya Mungu ya kibiblia. Mungu alizungumza juu ya msingi huu wa imani kwa watu wa Israeli, na alizungumza nasi pia. Hata sasa, mnapaswa wote kutambua na kuamini katika ukweli uliodhihirishwa katika rangi za lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania, rangi ambazo zinaunda msingi huu wa imani. Ni lazima tumwamini Mungu wa kweli. Ili kutuokoa mimi na wewe toka katika dhambi zetu, Mungu mwenyewe alizichukua dhambi zetu zote kwa ubatizo wake na akamwaga damu yake Msalabani.
Ninyi, ambao pia mnataka kuwa watu wa kiroho wa Israeli, ni lazima muiamini injili ya maji na Roho ili muweze kuokolewa toka katika dhambi zenu zote kwa kuuanzisha upya utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ulioharibiwa na Ukristo wa kidini. Wewe na Mimi ni lazima tuifahamu injili hii ya maji na Roho iliyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, na pia kwa mara nyingine tuweke msingi wa imani yetu ya ondoleo la dhambi ili msingi huo ubakie kuwa imara.
Ni lazima tumshukuru Yesu kwa imani yetu. Ili kutuokoa sisi ambao tusingeweza kukwepa kifungo huko kuzimu, Mungu Baba alitutumia Yesu Kristo, aliyekuja kama nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, kupitia Neno lake la kweli. Kwa kuuamini ukweli huu kwa moyo wote kuwa Bwana wetu ametuokoa toka katika dhambi zetu zote kwa huduma zake nne zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa, na kwa kuuamini upendo wake wa rehema, basi ndipo tunampatia shukrani zote Mungu. Ni pale tu tunapofahamu vizuri sababu iliyomfanya Mungu kumuita Musa katika Mlima Sinai ndipo tutakapokuwa miongoni mwa wale waliojenga msingi wao wa imani katika ondoleo sahihi la dhambi. Mimi na wewe ni lazima tutambue sababu iliyomfanya Mungu kumuita Musa katika Mlima Sinai, na kisha tuiamini: ilikuwa kwa lengo la kutusamehe dhambi zetu zote kupitia sadaka ya kuteketezwa na kutufanya sisi kuwa wana wake mwenyewe.
Kutoka katika ukweli uliodhihirishwa katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania, ndipo unapoweza kukutana zaidi na upendo wa rehema za Mungu. Ni matumaini yangu na maombi kuwa nyote mtauamini upendo huu wa rehema za Mungu na kuupokea katika mioyo yenu.