Search

Mahubiri

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 10-2] Imani ya Kweli Huja Kwa Kusikia (Warumi 10:16-21)

(Warumi 10:16-21)
“Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia: 
‘Sauti yao imeenea duniani mwote, 
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.’ 
Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena: 
‘Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, 
Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhabisha.’ 
Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema: 
‘Nalipatikana nao wasionitafuta; 
Nalidhihirika kwao wasioniulizia.’ 
Lakini kwa Israeli asema: 
‘Mchana kutwa naliwanyoshea mikono 
Watu wasiotii na wakaidi.’”
 

Aya ya 17 inasema, “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Je, imani inayomwokoa mtu katika dhambi zake zote inatoka wapi? Imani ya kweli inakuja kwa kulisikia Neno la Mungu. 
Ninapenda kuendelea kuishuhudia injili ya haki ya Mungu kwa kupitia Neno lake. Hebu tuanze kuangalia Warumi 3:10-20:
“Kama ilivyoandikwa ya kwamba: ‘Hakuna mwenye haki hata mmoja; 
Hakuna afahamuye; 
Hakuna amtafutaye Mungu. 
Wote wamepotoka; 
Wameoza wote pia; 
Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.’ 
‘Koo lao ni kaburi wazi; 
Kwa ndimi zao wametumia hila’; 
‘Sumu ya fira i chini ya midomo yao’; 
‘Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.’ 
‘Miguu yao ina mbio kumwaga damu; 
Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. 
Wala njia ya amani hawakuijua.’
‘Kumcha Mungu hakupo machoni pao.’ 
Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.”
Tunawezaje kukifahamu na kukiamini kifungu hiki ili tuweze kupokea wokovu? Tangu mwanzo, hakukuwa na mwenye haki au aliyemtafuta Mungu, bali wote walikuwa ni wenye dhambi. Makoo yao yalikuwa ni makaburi yaliyo wazi; ndimi zao zilikuwa kama za fira, zikiwa zimejaa hila na uchungu. Miguu yao ilikuwa myepesi katika kuimwaga damu. Hawakuifahamu njia ya amani na wala hakuwa na hofu ya Mungu katika macho yao, na walikuwa wakitembea katika njia ya uharibifu wao na mashaka. Kabla ya kuifahamu na kuiamini haki ya Mungu kila mtu alikuwa ni mwenye dhambi, na njia iliyosaidia kutambua kuwa walikuwa ni wenye dhambi ni kwa kupitia sheria. 
Tungeliwezaje kuzifahamu dhambi zetu pasipo sheria? Tungeliwezaje kumfahamu Mungu? Je, tuliwahi hata siku moja kumwogopa Mungu? Warumi 3:18 inasema, “Kumcha Mungu hakupo machoni pao.” Je, macho yetu ya kimwili yamewahi kumwona Mungu? Pengine tunaweza kuwa tunafahamu juu ya uwepo wa Mungu, lakini hatujawahi kumwona wala kumwogopa Yeye. Sasa, tuliwezaje kutambua kuwa tulikuwa ni wenye dhambi? Tulifikia hatua ya kuufahamu uwepo wa Mungu kwa kusikia Neno lake lililoandikwa. Hii ndiyo sababu kusikia huja kwa Neno la Mungu. 
Tunafahamu kuwa Mungu aliiumba ulimwengu kwa sababu imeandikwa katika Maandiko, “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” (Mwanzo 1:1). Ni kwa kulisikia Neno la hili la Mungu ndipo tulifikia hatua ya kuufahamu na kuuamini uwepo wake, na pia kuamini kuwa Mungu ndiye muumba wa ulimwengu mzima. Kama isingekuwa kwa ajili ya Neno la Mungu, basi kwa hakika kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angelikuwa anamfahamu wala kumcha Mungu. Pasipo Neno la Mungu hata sisi tusingeliweza kuzitambua dhambi zetu. 
Kwa maneno mengine, kimsingi, sisi tulikuwa hatuna ule ufahamu wa Mungu hali tukiabudu vitu visivyo na maana na tulikuwa hatuzifahamu dhambi zetu. Lakini Mungu alitupatia sheria, na hivi ndivyo tulivyoweza kuzitambua dhambi zetu mbele za Mungu. Tulifikia hatu ya kuyafahamu mapungufu yetu na dhambi zetu baada ya kulisikia Neno la Mungu la sheria ya Amri Kumi na zile amri 613.
Hakuna mtu anayeweza kuzitambua dhambi za mtu fulani pasipo uwepo wa Neno la sheria. Karibu kila mtuhumiwa awapo kifungoni hudai kuwa halifahamu kosa lake, au kuwa ni kwa nini amefungwa. Wengi wao hudai kuwa wao hawana hatia; na kwamba walipelekwa jela kwa makosa na pasipo haki. Pasipo kuifahamu sheria ya Mungu hatuwezi kuzifahamu dhambi zetu binafsi. Wakati mwingine twaweza kusema, “Nimekuwa nikifanya hivi wakati wote. Na kila mtu anatenda hivyo. Inawezekanaje kufanya hivi ikawa dhambi?”
Ni kwa kusikia na kuiona sheria ya Mungu ndipo tumeweza kuzitambua dhambi zetu. Pia tulifikia hatua ya kufahamu kuwa kuabudu miungu mingine, kulitaja bure jina la Mungu, kushindwa kuitunza kuifuata Sabato, kuua, kuzini, kuiba, kuongopa, wivu, na kushindwa kuishi kwa kulifuata Neno la Mungu ni dhambi kwa kuwa sheria ya Mungu imesema hivyo. Hivi ndivyo tulivyotambua jinsi tulivyokuwa wenye dhambi mbele za Mungu kwa Neno la sheria. Kabla ya ya sheria hii tulikuwa hatuzijui kabisa dhambi zetu.
Baada ya kutambua kuwa sisi ni wenye dhambi, sasa tufanye nini mbele za Mungu? Tunahitaji kujiuliza jinsi ambavyo dhambi zetu zinavyoweza kusamehewa. Ni kwa kulisikia Neno la Mungu ndipo tunapoweza kuzifahamu dhambi zetu na kisha kutambua hitaji la wokovu. Kama ambavyo wenye njaa wanavyojisikia haja ya kupata chakula, wale wanaotambua kuwa wameivunja sheria ya Mungu na wanaotambua kuwa wao ni wenye dhambi wakubwa wanalitambua hitaji lao la wokovu. Hivi ndivyo tulivyofikia hatua ya kumtambua Mungu na kutambua hitaji letu la kuamini katika haki yake kwa kupitia Yesu Kristo ambaye Mungu alimtuma kwa ajili yetu. Kama ambavyo “imani huja kwa kusikia,” sisi pia tunazifahamu dhambi zetu kwa kulisikia Neno la Mungu. 
 

Sasa Tunatambua Kuwa Sisi ni Wenye Dhambi. Sasa Tufanye Nini Ili Tuweze Kukombolewa Toka Katika Dhambi Zetu?
 
Wokovu huja kwa imani katika Neno la Mungu ambalo linasimama katikati ya mioyo yetu kama tunavyozitambua dhambi zetu kwa kusikia na kujifunza Neno la Mungu. Kama Warumi 3:21-22 inavyosema, “Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio.”
Mungu, kwa kutupatia sheria yake, ametufanya sisi tuweze kutambua kuwa ni wenye dhambi mbele zake kwa kuwa tumeshindwa kuishi kwa kufuata Neno lake. Kimsingi, sisi tuna mahitaji mawili: tunapenda kuishi kwa kuifuata sheria, lakini kwa wakati huo huo tunauhitaji wokovu wetu toka katika dhambi. Lakini kwa kuwa “…haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria,” wale ambao watakombolewa toka katika dhambi zao ni lazima wautafute wokovu kwa imani yao katika haki hii ya Mungu na si katika sheria. Tunatambua kuwa ukombozi huu hauji kwa kuitii sheria ya Mungu, bali kwa kuamini wokovu ambao umetolewa na Mungu katika ile haki ya Mungu ambayo imetuokoa kwa kupitia Yesu Kristo. 
Sasa, je, hii haki ya Mungu na wokovu wake ni kitu gani? Hii ni injili ya maji na Roho ambayo imezungumzwa katika Agano la Kale na Agano Jipya. Injili ya maji na Roho inaonekana katika Agano la Kale kuwa ni wokovu kwa imani katika utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, na katika Agano Jipya kama imani katika ubatizo wa Yesu na Msalaba wake. Warumi 3:21-22 inasema, “...inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio.” 
Sasa tunawezaje kuipokea haki ya Mungu? Tunaweza kuipokea haki ya Mungu kwa kufahamu kupitia Neno la Mungu linaloshuhudiwa na torati na manabii kuwa Yesu ni Mungu na Mwokozi wetu, na kwamba tunaokolewa toka katika dhambi zetu zote kwa imani katika yeye Yesu Kristo. 
Kwa maneno mengine, tunaipokea haki ya Mungu kwa kuliamini Neno lake, ambalo limeshuhudiwa na torati na manabii wa Agano la Kale. Kule kusema kuwa sheria au torati na manabii vinalishuhudia Neno la Mungu kunaonyeshwa pia katika sura za kwanza za vitabu vya Waebrania na Warumi. 
Kule kusema kuwa Yesu alikuja ili kutukomboa ni wokovu ambao umeahidiwa kwetu na Mungu. Ahadi hii ya kuwaokoa wenye dhambi waliokuwa chini ya sheria na waliokuwa wamefungwa kwa ajili ya uharibifu wao ilitolewa na Mungu maelfu ya miaka iliyopita. Mungu aliendelea kuirudia ahadi hii na akafunua jinsi ambavyo aliendelea kuishikilia ahadi hiyo kwa kupitia watumishi wengi mbalimbali ambao walikuja kabla yetu. 
Kwa mfano hebu tukiangalie kifungu hiki. Mambo ya Walawi 16:21 inasema, “Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.” Kifungu toka kwa Warumi 3:21-22, kuwa haki ya Mungu ilishuhudiwa na torati na manabii kina maanisha kuwa wokovu mkamilifu wa Yesu ulifunuliwa kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa ya Hema Takatifu la Kukutania katika Agano la Kale kwa kupitia manabii kama vile Isaya, Ezekieli, Yeremia, na Danieli. 
Kwa maneno mengine, Mungu alikwishajifunua kwa kupitia Neno la Agano la Kale jinsi ambavyo ataitunza ahadi yake ya wokovu—kwamba atafanya hivyo kwa kumtuma Yesu Kristo na kumfanya kuzichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake, kwa kufa Msalabani badala yetu, na hivyo kulipa mshahara wa dhambi zetu zote kwa mwili wake, yote haya kwa ajili ya ukombozi toka katika dhambi zetu kwa kupitia haki ya Mungu. Hivyo, wokovu wetu si kwa sheria bali ni kwa imani yetu katika haki ya Mungu, ambaye ni Yesu Kristo mwenyewe kama anavyoshuhudiwa na torati na manabii. 
Mungu anatueleza kuwa tunaokolewa toka katika dhambi zetu kwa kuamini katika haki ya Mungu ambayo ilitimizwa na Yesu Kristo. Imani yetu inakuja kwa kulisikia Neno la Mungu, ambalo ni Neno la Yesu Kristo. Tunawezaje kufahamu na kuamini kuwa Yesu ni Mwokozi wetu? Tunafahamu na kuamini kuwa Yesu ni Mwokozi wetu kwa kulisikia Neno la Mungu lililozungumzwa kwa watumishi wake, kwamba Mungu aliahidi kutuokoa kwa mujibu wa mpango wake, na kwamba Yesu alikuja kutuokoa kwa mujibu wa ahadi na mpango huo. Kama ilivyoandikwa katika Danieli 9:24, “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu.”
 

Mungu Ameyaweka Majuma Sabini Kwa Ajili ya Watu Wetu 
 
Tunaendelea na kifungu hicho hapo juu toka katika kitabu cha Danieli. Kifungu kinaeleza juu ya anguko la Israeli kwa Babeli, wakati ambapo Mungu aliazimia kuwa Waisraeli wachukuliwe kwenda uhamishoni kama wafungwa na waishi huko kwa miaka sabini kama watumwa kwa sababu ya kuabudu miungu mingine. Kama Mungu alivyodhamiria, Israeli ilivamiwa na kuzidiwa nguvu na Babeli na uharibifu ulikuwa ni mkubwa sana kiasi kuwa Israeli walisalimu amri kwa majeshi ya wavamizi ambao waliwachukua waisraeli wengi kama wafungwa na wakawageuza kuwa watumwa wao. Miongoni mwa watumwa waliochukuliwa walikuwepo pia wenye busara kama vile Danieli ambaye alifanywa kuwa mshauri wa mfalme wa Babeli. 
Hivyo Mungu aliwaadhibu Waisraeli kwa namna hii kwa ajili ya dhambi zao, lakini kwa kuwa alikuwa ni mwenye rehema, hakuiacha ghadhabu yake idumu milele lakini badala yake alipanga kuwaweka huru katika wiki 70. 
Wakati Danieli alipokuwa akitubu mbele za Mungu kwa niaba ya watu wake, aliomba kwa ajili ya rehema za Mungu na ukombozi, Mungu akamtuma malaika ambaye alikizungumza kifungu hicho hapo juu: “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu.” Kifungu hiki ni ahadi ya Mungu kwa Danieli kuwa atazisamehe dhambi zote za watu wake kwa wiki 70 wakati ambapo makosa yao yatamalizika. Pia kifungu hicho kinatufunulia sisi ahadi ya ukombozi wa Mungu kwa kupitia Yesu Kristo. 
Kwa kuwa Waisareli walitenda dhambi nyingi, Mungu alipaswa kuwaadhibu, lakini pia Mungu alizisamehe dhambi zao zote zilizopita kwa gharama ya wiki 70 utumwani. Wakati makosa yatakapokuwa yamekombolewa na mwisho wa dhambi umefanyika, basi dhambi zote za Waisraeli zitakuwa hazipo tena. Wakati upatanisho kwa ajili ya makosa utakapokuwa umefanyika, wakati haki ya milele itakapokuwa imeletwa, na wakati maono ya unabii yatakapokuwa yamefungwa, basi maneno yote yaliyozungumzwa na Yeremia yatatimia. Katika kipindi chote za wiki 70 za utumwa, yote haya yatatokea na katika wiki la 70 Waisraeli watarudi katika nchi yao ya asili. 
Hivi ndivyo Mungu alivyomweleza Danieli kwa kupitia malaika wake. Ahadi hii ilikuwa ni ahadi ambayo ilitolewa kwa Waisraeli lakini pia ina maana ya kiroho—kama Mungu alivyopanga zile wiki 70 kwa watu wa Israeli na mji wao mtakatifu, Mungu ameuandaa mji wetu mtakatifu katika Ufalme wa Mbinguni kwa ajili yetu sisi sote tunaomwamini. 
Katika Warumi, inasemwa kuwa, “Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio.” Wakati Yesu alipokuja hapa duniani, alibatizwa na kufa Msalabani, maovu yetu yote yaliondolewa, dhambi zetu zote ziliisha, haki ya Mungu ilidhihirishwa, na maono ya unabii yalitiwa muhuri. Kifungu toka Danieli kinamalizia kwa kusema, “kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu” Je, hii ina maanisha nini? Yeye aliye Mtakatifu ni Yesu Kristo ambaye ndiye aliyekuja hapa duniani ili kutiwa mafuta. 
Je, kutiwa mafuta kuna maanisha nini? Maana yake ni kuwa Yesu atazichukua zile nafasi tatu za Mfalme, Kuhani Mkuu wa Ufalme wa Mungu, na Nabii. Kama Mfalme wetu, Kuhani Mkuu na Nabii, Yesu atayatimiza mapenzi ya Mungu ya kutukomboa toka katika dhambi zetu zote. Kama ilivyotabiriwa na malaika aliyezungumza na Danieli, Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake na akahukumiwa kwa niaba yetu kwa kuja hapa duniani na kubatizwa. 
“Imani huja kwa kusikia.” Tunawezaje kusikia na kuiamini injili hii ya haki ya Mungu? Tunawezaje kuamini kuwa Yesu Kristo ni Mwokozi wetu? Tunaweza kusikia na kuamini kwa kutumia Neno la Mungu lililozungumzwa katika Agano la Kale na Agano Jipya, kwa maneno yaliyozungumzwa na manabii wa Mungu na watumishi wake. Hii ndiyo sababu Paulo alisema kuwa imani huja kwa kusikia, na imani hii huja kwa kulisikia Neno la Kristo. 
Manabii wa Agano la Kale, kama vile Danieli na Isaya walitabiri juu ya kuja kwa Yesu Kristo. Hasa Isaya, alitabiri kuwa, “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu...” na “...lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake” (Isaya 53:4,7). 
Ni nani kati ya waliokuwepo wakati wa Isaya ambaye angeliamini kuwa Yesu Kristo atazaliwa kwa bikira ili kuja hapa duniani kama mtu wa kawaida, akaishi kwa miaka 33, akabatizwa, akasulubiwa, akafufuka toka kwa wafu siku ya tatu? Lakini Isaya aliona na kutabiri mambo haya takribani miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu. Isaya alishuhudia kuwa Kristo atazibeba huzuni zetu na dhambi zetu zote. 
Hii ndio sababu Paulo alitumia Neno la Agano la Kale mara kwa mara alipokuwa akiandika kitabu cha Warumi katika kuelezea jinsi ambavyo watumishi wa Mungu walivyoshuhudia jinsi Yesu alivyofanyika kuwa Mwokozi wetu kwa kuja hapa duniani, kwa kuzichukulia mbali dhambi zetu zote, na kwa kutuokoa na haki ya Mungu. 
 

Kwa Kuwa Wote Wamefanya Dhambi
 
Warumi 3:23-24 inasema, “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.” Kwa kuwa tulizaliwa katika dhambi na kwamba sisi sote tumefanya dhambi mbele za Mungu, basi kwa sababu hiyo sisi sote tumepungukiwa utukufu wake. Lakini tulihesabiwa haki bure kwa neema ya Mungu kwa kupitia ukombozi katika Yesu Kristo. Kuhesabiwa kwetu haki kulikuwa ni bure pasipo gharama yoyote. Hatukupaswa kulipa mshahara wa dhambi zetu kwa kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake na akalipa mshahara wa dhambi hizo kwa kuyatoa maisha yake mweneywe Msalabani, alifanya haya yote ili kutukomboa sisi ambao tutamsikia na kumwamini. 
Tuna maanisha nini tunaposema juu ya wokovu toka katika dhambi? Kwa kweli tunaaminisha imani katika haki ya Mungu. Kuiamini haki ya Mungu hakuhusiani chochote na matendo, bali inahusiana na mioyo yetu. Tunahesabiwa haki kwa kulisikia Neno la Bwana na kuliamini kwa mioyo yetu yote. Ili kutuokoa toka katika dhambi zetu zote, Bwana wetu alikuja hapa duniani akafanyika kuwa Mwanakondoo wa Mungu, ambaye alizichukua dhambi zote za ulimwengu kwa kubatizwa na Yohana Mbatizaji, na kisha akafa Msalabani. Kisha akafufuka siku ya tatu na sasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba. 
Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake, akalipa gharama zote za adhabu ya dhambi zetu kwa kuutoa uhai wake na kisha akafufuka toka kwa wafu; Yesu alifanya haya yote ili kutuokoa toka katika mauti yetu. Tunaokolewa kwa kuamini hivi. Wokovu wetu unakuja kwa imani, na imani yetu huja kwa kulisikia Neno la Mungu lililoandikwa, na kusikia kwetu huja kwa Neno la Kristo. 
“Imani huja kwa kusikia.” Tunaamini kwa mioyo yetu. Akili zetu zinahusiana na ufahamu, wakati miili yetu ipo kwa ajili ya kufanya kazi, na tunaamini kwa kutumia mioyo yetu. Sasa, tunapaswa kuamini nini katika mioyo yetu na kivipi? Ni kwa kulisikia Neno la Mungu, tunaweza kuisikiliza injili, na kwa kuisikiliza injili tunaweza kuwa na imani, na kwa kuwa na imani tunaweza kuokolewa. Tunapoamini kwa kutumia Neno la Mungu—yaani kuamini katika Neno lililoandikwa linalotangaza kuwa Kristo alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, akazibeba, akafa Msalabani na kisha akafufuka tena toka kwa wafu. 
Kuwa na imani katika Neno la Mungu ni kuwa na imani katika haki yake. Hivyo, imani pasipo kulisikia Neno la Mungu ni jambo la ovyo na haina maana. Madai yasemayo kuwa Mungu alijifunua kwa kupitia ndoto za mtu fulani ni uongo kabisa. 
Tunaokolewa kwa imani na ni kwa imani tu. Hebu tusome tena kwa mara nyingine, Warumi 3:24-26: “Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminye Yesu.” Amina. Bwana wetu alifanyika kuwa kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. Sisi tulifanyika kuwa maadui wa Mungu kwa sababu ya dhambi zetu, lakini Yesu aliuanzisha upya uhusiano wetu na Mungu kwa kufanyika kuwa kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu kwa ubatizo wake, kifo chake, na ufufuo wake. 
Katikati ya kitabu cha Warumi 3:25 kuna kifungu kisemacho, “ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa.” Kifungu hiki kinatueleza kuwa Mungu alisubiri kwa uvumilivu kwa muda mrefu na kwamba ataendelea kusubiri hadi Siku ya Hukumu. Wale wanaomwamini Yesu Kristo, wale wanauamuni wokovu kwa kupitia maji na damu, wale wanaoamini katika wokovu wa Mwana wake, wale waliofanyika kuwa kipatanisho kwa Mungu baba—hao ndio ambao dhambi zao zote zimehamishiwa mbali na Mungu. ‘Kuzihamishia dhambi’ maana yake ni kuwa Mungu amezihamishia dhambi zao wale wote wanaosikia na kuamini katika Neno la Mungu na injili yake, yaani wale wanaoamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake kwenda Msalabani. 
Kwa baadhi ya nyakati tunaweza kujikuta tukisitasita katika maisha yetu, lakini hii ni kwa sababu ya udhaifu wa miili yetu na akili zetu, na kadri tusivyoukana wokovu wa Yesu basi Mungu hataziona dhambi hizi zote kuwa ni dhambi. Kwa maneno mengine, Mungu haziangalii dhambi za wale ambao wameokoka kwa kuamini katika maji na damu ya Yesu Kristo katika mioyo yao, bali Mungu huzipita juu yake. 
Kwa nini basi Mungu anazihamisha dhambi zetu na kuzipita? Inawezekanaje kwa Mungu kuzidharau dhambi kama hizo, wakati yeye ndiye Mungu pekee aliye wa haki? Hii ni kwa sababu Kristo alikuja hapa ulimwenguni na alibatizwa. Ni kwa sababu Yesu alizitoweshea mbali dhambi zetu zote kwa ubatizo wake na kusulubiwa kwake ambapo Mungu alizipitisha dhambi zetu zote tulizozifanya kwake. Je, zile dhambi tulizozifanya ina maanisha kuwa ni dhambi ya asili? Hapana, kwa kweli haimaanishi hivyo bali ni dhambi zote zilizopita. 
Kwa mtazamo wa umilele, wakati wote katika ulimwengu huu unaonekana kuwa ni wakati uliopita. Ulimwengu huu una mwanzo wake na mwisho wake, lakini Mungu ni wa milele, na kwa hiyo tunapolinganisha muda wake na muda wetu wa kidunia, basi dhambi zote za ulimwengu zinaonekana kuwa zimetendwa katika wakati uliopita mbele zake. “...ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa.” Hii ndiyo sababu Mungu haziangalii dhambi zetu. Hii si kwa sababu hana macho ya kuziangalia dhambi zetu bali hazioni kwa sababu Mwanawe Yesu Kristo amelipa mshahara wa dhambi zetu. Kwa kuwa ubatizo wa Kristo na kusulubiwa kwake kulizisafishilia mbali dhambi zetu, basi sisi tunasimama mbele za Mungu kama watu tusio na dhambi. 
Inawezekanaje kwa Mungu kuziona dhambi zetu wakati Yesu Kristo ambaye ndiye utimilifu wa haki ya Mungu amewakomboa wote wanaoiamini haki ya Mungu na kuzichukulia mbali dhambi toka kwetu? Hivi ndivyo Mungu anavyoionyesha haki yake sasa kwa kuzipita dhambi zetu ambazo tulizilifanya hapo zamani, yaani dhambi ambazo zimekwishalipiwa na Yesu Kristo. 
Imani katika haki ya Mungu inakuja kwa Neno la Kristo kwa sababu Neno la Kristo lenyewe lina ile haki ya Mungu halisi. Kwa kuionyesha haki yake, si kwamba Mungu aliionyesha haki yake tu, bali pia haki ya wale wanaoamini katika Yesu Kristo. Mungu ameziondoa dhambi zetu zote na sisi pia tunaamini katika mioyo yetu kuwa Yesu amezichukulia mbali dhambi zetu zote. Hii ndiyo sababu tumefanyika kuwa tusio na dhambi na tuliohesabiwa haki kwa kuwa tumeivaa haki ile ile ya Kristo (Wagalatia 3:27). Kwa kuwa sisi pamoja na Mungu sote tu wenye haki, basi sisi toe ni familia moja na mimi na wewe ni watoto wake. Je, unaziamini hizi habari za kupendeza? 
Je, hii ina maanisha kuwa tuna kitu chochote ambacho twaweza kujivunia? Kwa kweli hapana! Tunaweza kujivunia kitu gani wakati wokovu wetu unawezekana kwa kusikia tu na kuliamini Neno la Kristo? Je, tuliokolewa kwa matendo yetu wenyewe? Kuna nini cha kujivunia? Hakuna! Je uliokolewa kwa kuwa umehudhuria sala za mapema asubuhi katika Kanisa lako? Uliokolewa kwa sababu hujawahi kukosa hata ibada moja ya Jumapili kanisani? Je, uliokolewa kwa sababu ya uhakika kuwa hutakosa kulipa zaka? Kwa kweli hapana. 
Matendo haya yote, na imani zinazojengwa katika matendo ni imani potofu. Sisi tuliokolewa toka katika dhambi zetu kwa kuiamini haki ya Mungu katika mioyo yetu. Imani huja kwa kusikia, na wokovu huja kwa imani katika Neno la Kristo. 
Kujaribu kupokea ondoleo la dhambi kwa kupitia sala za toba baada ya kumwamini Yesu pia ni imani isiyo sahihi, hii ni kwa sababu imani ya kweli huja kwa kuamini katika haki ya Mungu na si kwa matendo ya sheria. Kama Neno la Mungu linavyosema, “Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani. Basi twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria. Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia.” (Warumi 10:27-29)
Wokovu unakuja kwa Waisraeli na Wamataifa pia, kwa kusikia na kuamini katika mioyo yao kuwa Yesu Kristo amewaokoa kwa maji na damu yake. Tunaokolewa toka katika dhambi zetu pale tunapoamini katika haki ya Mungu. Tunapoiamini haki hii ambayo ni Yesu Kristo, basi tunaokolewa toka katika dhambi zetu zote. Mungu anafanyika kuwa Baba yetu na sisi tunafanyika kuwa watoto wake. Huu ndio wokovu kwa imani katika haki ya Mungu, unaopatikana kwa kusikia na kuamini katika Neno la Kristo. Imani yetu inakuja kwa kuamini katika haki ya Mungu. 
Wokovu wetu unakuja kwa imani yetu katika Neno la Kristo. Je, unaamini kuwa Kristo alikuja hapa duniani kama Mwokozi wako, na kwamba alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake na kuwa kipatanisho kwa Mungu? Na kwamba alikufa Msalabani, akafufuka siku ya tatu toka kwa wafu, na kwamba ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba? Je, unauamini kweli wokovu huu na katika upatanisho wa Bwana wetu Yesu Kristo? 
Kuna watu wengi wanaomwomba Mungu kutokea katika ndoto zao, wanaosema kuwa wataamini ikiwa wataweza kumwona Mungu angalau mara moja kwa macho yao. Baadhi wanadai kuwa wamewahi kumwona Yesu katika ndoto zao, na kwamba aliwaambia kufanya mambo haya na yale kama vile kujenga kanisa hapa, kujenga kituo cha maombi, n.k., lakini mara nyingi hutaja vitu ambavyo vinahitaji fedha na kwa sababu ya madai hayo ya uongo kuna idadi kubwa ya watu ambao wamepotoshwa. Kuna matukio mengi ya kusikitisha katika ulimwengu wa Kikristo. Ni lazima utambue kuwa mambo hayo yote si kazi za Bwna wetu bali ni mambo ya Ibilisi mwenyewe. 
Ikitokea kuwa umemwona Yesu katika ndoto zako, basi usilichukulie jambo hilo kwa undani sana. Ndoto ni ndoto tu. Yesu si yule anayeweza kukutokea wewe kwa namna kama hiyo la sivyo kungekuwa hakuna haja ya kuwa na Biblia. Ikiwa Yesu anaweza kututokea angalau mara moja, basi tunapaswa kuifunga Biblia kwa kuwa tutakuwa hatuihitaji tena. Lakini jambo kama hilo la kutegemea ndoto linaweza kuleta madhara makubwa katika kazi ya Kristo ya wokovu. 
Ikiwa tungalimwamini Yesu pasipokuwa na Biblia, basi angelipaswa kuonekana kwa kila mtu. Lakini hakuna haja ya jambo kama hilo kwa kuwa Bwana wetu amekwishayatimiza mahitaji yote ya wokovu. Hii ndiyo sababu imani huja kwa kusikia na kuamini katika Neno la Kristo. Je, ni kweli kuwa watu wote wamesikia kuhusu Yesu Kristo? Wanaweza kuwa wamelisikia jina la Yesu Kristo, lakini si wote ambao wameisikia injili ya kweli. Hii ndiyo sababu Paulo aliuliza, “Tena wamsikieje pasipo mhubiri?” (Warumi 10:14)
Hivyo, ni lazima tuihubiri injili hii ambayo ina haki ya Mungu. Lakini kwa njia gani na kivipi? Lakini swala la kwa njia gani injili inahubiriwa si la muhimu; njia zote za kuhubiri habari njema kama vile kwa kuongea maneno au kwa maandiko yaliyoandikwa zinaweza kutumika. Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo. Maandiko yaliyochapishwa ambayo yanaihubiri injili yanaweza pia kuwaongoza wasomaji kwenye imani ya kweli. Ni lazima ukumbuke kuwa imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa kuihubiri habari njema, hivyo haijalishi unatumia mbinu gani katika kuihubiri injili cha muhimu ni kuihubiri habari njema. 
Ikiwa kweli una imani katika Neno la Mungu, basi utatambua ya kuwa wewe ni Mkristo wa kweli. Ninatumaini kuwa unalifahamu jambo hili; kwamba umeokolewa toka katika dhambi zako. Pia ninatumaini na kuomba kuwa utaendelea kulishikilia Neno la maji na Roho kwa wema. Hebu sasa tumalizie mjadala wetu kwa kusoma pamoja toka Warumi 10:17. 
“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Amina. Wale wanaoamini katika mioyo yao kwa kulisikia Neno hili la Mungu lilioandikwa ndio wale walio na imani ya kweli. Je, unayo imani hii ya kweli? Bwana wetu ametukomboa toka katika dhambi zetu zote. 
Tunashukuru na kufurahi kuwa Bwana wetu amezichulia mbali dhambi zetu zote! Pasipo injili, basi mara zote watu wanakatishwa tamaa, lakini kwa kule kusikia kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, basi mioyo yetu inajazwa na furaha na imani yetu inaanza na kuzidi kukua. 
Ninamshukuru Bwana kwa kutuokoa.