Mashahidi wawili wanaoonekana katika sura ya 11 ni watumishi wawili wa Mungu ambao Mungu atawainua kipekee ili kuwaokoa Waisraeli katika nyakati za mwisho. Ili kuitimiza ahadi yake aliyoifanya kwa Ibrahimu, basi Mungu atawafanya manabii hawa wawili, ambao wametumwa kuwakomboa Waisraeli toka katika dhambi, kufanya ishara na miujiza, na kisha kuwafanya Waisraeli huku wakiongozwa na wao kumrudia Yesu Kristo na kisha kumwamini Yesu kuwa Mwokozi wao. Hawa mashahidi wawili watawalisha Neno la Mungu watu wa Israeli kwa siku 1,260—yaani miaka mitatu na nusu ya kwanza katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu. Kwa kuieneza injili ya maji na Roho kwa Waisraeli na kwa kuwafanya waiamini injili hii kwa kupitia mashahidi hawa wawili, basi hapo Mungu atawapatia Waisraeli wokovu ule ule ambao amewapatia Wamataifa, yaani ni kama vile Wamataifa walivyookolewa toka katika dhambi zao kwa imani.
Ufunuo 11:4 inasema, “Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.” Kuna mafafanuzi tofauti kuhusu mizeituni hiyo miwili; baadhi ya watu wanadiriki kusema kwamba wao ndio ile mizeituni miwili. Lakini mizeituni hii miwili inawamaanisha wale waliotiwa mafuta. Katika nyakati za Agano la Kale, mtu alitiwa mafuta wakati alipofanywa kuwa nabii, mfalme, au kuhani. Wakati mtu alipowekwa mafuta Roho Mtakatifu alishuka juu yake. Kwa hiyo, mti wa mzeituni una maanisha ni Yesu Kristo ambaye alitungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Warumi 11:17).
Hata hivyo, tukiangalia Ufunuo 11:1—“Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo.”—tunapaswa kutambua kwamba lengo la sura ya 11 ni juu ya wokovu wa watu wa Israeli. Kwa maneno mengine, kuanzia wakati huo itaanza kazi ya kuieneza injili ya maji na Roho kwa Waisraeli, yaani juu ya ukombozi toka katika dhambi zao zote kwa kupitia neema ya wokovu iliyotolewa na Yesu Kristo, na kwa wao kufanyika watu wa Mungu wa kweli. Hivyo, mashahidi wawili ni manabii wawili wa Mungu ambao watainuka katika nyakati za mwisho ili kuwaokoa watu wa Israeli.
Katika Biblia, kinara cha taa kina maanisha ni Kanisa la Mungu. Kwa hiyo, vinara viwili vya taa vina maanisha ni Kanisa la Mungu miongoni mwa Wamataifa na Kanisa lililoruhusiwa miongoni mwa Waisraeli. Mungu si Mungu wa Waisraeli tu, bali pia ni Mungu wa Wamataifa, kwa kuwa Yeye ni Mungu wa kila mtu. Kwa hiyo, Mungu amelianzisha Kanisa lake miongoni mwa Waisraeli na Wamataifa pia, na Mungu anafanya kazi ya kuziokoa nafsi za watu toka katika dhambi hadi siku ya mwisho kwa kupitia Kanisa lake.
Kuanzia wakati wa Agano la Kale, Waisraeli walikuwa na manabii waliowekwa kwa Sheria ya Mungu, na kwa kupitia manabii hao Waisraeli walilisikia Neno la Mungu. Waisraeli wanayo Sheria ya Musa na Manabii. Kwa hiyo, wanafahamu kila kitu kuhusu utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa na unabii wa Agano la Kale, na hii ndio sababu wanahitaji manabii wa Mungu waliochaguliwa toka katika watu wao wenyewe.
Pia wanaamini kwamba wao ni watu wa Mungu waliochaguliwa, hivyo huwa hawazingatii wala kuwekea mkazo wanapoelezwa Neno la Mungu na Wamataifa. Hivyo, ni hadi pale manabii wanaoamini katika injili ya maji na Roho wanapokuwa wamechaguliwa na Mungu toka miongoni mwa Waisraeli, hapo ndipo Waisraeli wanapoweza kumkubali na kumwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao.
Hii ndio sababu Mungu mwenyewe atawaleta manabii wawili toka katika watu wa Israeli na kisha kuwatuma kwa Waisraeli. Kwa kweli manabii hawa watafanya maajabu mengi ambayo watumishi wa Mungu wanaofahamika katika Angalo la Kale wameyafanya. Ufunuo 11:5-6 inatueleza kwamba, “Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa. Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo.”
Pasipo hawa watumishi wa Mungu kuwa na nguvu na mamlaka kama hayo, watu wa Israeli wasingeliweza kutubu, hivyo Mungu atawavika mashahidi hawa wawili kwa nguvu zake. Mungu atawapatia mashahidi hawa wawili nguvu zake maalumu, ili waweze kulihubiri Neno la unabii kwa Waisraeli, na kuwashuhudia na kuwafanya waweze kuamini kwamba Yesu Kristo ndiye Masihi waliyemngojea kwa muda mrefu. Baada ya kuyaona maajabu yakifanywa na hawa mashahidi wawili, basi hapo ndipo Waisraeli watakapowasikia na kisha kumrudia Yesu Kristo.
Baada ya mashahidi wawili kuikamilisha kazi yao ya kuieneza injili kwa Waisraeli, Mpinga Kristo atatokea katika ulimwengu huu, atasimama kinyume na kazi yao kuihubiri injili, kisha atawafanya wawe wafia-dini. Ufunuo 11:8 inatueleza kuwa, “Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa.”
Baada ya kuwa wameihubiri injili kwa Waisraeli woe na hivyo kuitimiza kazi ya wito wao, mashahidi wawili watauawa mahali ambapo Yesu alisulubiwa hapo zamani. Ukweli huu unakazia ufafanuzi kwamba hawa mashahidi wawili ni kutoka miongoni mwa Waisraeli. Kwa kuwa wao ni watumishi wa Mungu wa watu wa Israeli.
Kwa kuhitimisha, Mungu atawainua watumishi wake wawili ili kuwashuhudia Waisraeli, ambao wamekataa kumwamini Yesu Kristo, na ambao kiroho ni kama vile Sodoma na Misri, kwamba kwa hakika Yesu ni Masihi wao waliyemsubiri kwa muda mrefu, na kwa kupitia mashahidi hawa wawili waliovikwa nguvu za Mungu, basi Mungu atawafanya Waisraeli wamwamini Yesu.