Search

Maswali ya kila mara juu ya Imani ya Kikristo

Somo la 3: Ufunuo

3-7. Alama au Chapa ya Mnyama ni Kitu Gani?

Wakati wa Dhiki Kuu, ili kumfanya kila mtu awe chini ya mamlaka yake, basi Mpinga Kristo atawalazimisha watu wote kuipokea alama au chapa yake katika mikono yao ya kuume au katika vipaji vya nyuso zao. Alama hii ni alama ya Mnyama. Mpinga Kristo atawataka watu kuipokea alama yake ili aweze kumfanya kila mtu kuwa mtumishi wake. Mpinga Kristo ataendelea na mipango yake ya kisiasa huku akitumia maisha ya watu kama nguvu yake. Ikiwa watu hawana alama inayoonyesha kuwa wao wapo upande wa Mnyama, basi atawazuia wasiweze kununua au kuuza chochote kile. Alama hii ni namba au jina la Mnyama. Wakati Mnyama atakapoonekana hapa ulimwenguni, watu walazimishwa kuipokea alama hii itakayokuwa imeundwa ama kwa jina lake au kwa namba yake. 
Ikihesabiwa, basi namba ya Mnyama katika alama hii ni 666. Hii ina maanisha kwamba Mnyama, ambaye ni Mpinga Kristo, anajitangaza kuwa yeye ni Mungu. Kwa maneno mengine, inaonyesha kiburi cha mwanadamu cha kujaribu kuwa kama Mungu. Kwa hiyo, yeyote atakayeipokea alama hii katika mkono wake wa kuume au katika kipaji cha uso wake atakuwa akimtumikia na kumwabudu Mpinga Kristo Mnyama kama ni Mungu. 
Wakati ulimwengu unapokabiliana na magumu mengi toka katika mapigo ya matarumbeta saba, Mpinga Kristo, hali akitiwa nguvu na Shetani, ataufanya ulimwengu wote kuwa chini ya utawala wake kwa nguvu kuu. Huku akijitibu jeraha lake la mauti na kufanya miujiza mingi ikiwemo kuleta moto toka angani, basi atawafanya watu wengi wa ulimwengu huu kumfuata. Kama vile mashujaa wanavyotokea wakati wa shida, Mpinga Kristo, mtu aliyepokea nguvu toka kwa Shetani, atayatatua matatizo magumu ambayo ulimwengu utakuwa ukikabiliana nayo kwa mamlaka makuu, na kwa sababu hiyo ataheshimiwa na watu wote wa ulimwengu kana kwamba ni Mungu. Kwa kuwa Shetani atawafanya watu wengi wamtumikie Mpinga Kristo kana kwamba ni Mungu, basi watu wengi wataishia kumwabudu kana kwamba ni Mungu. 
Hatimaye, Mpinga Kristo ataifanya kazi yake ya mwisho kwa msaada wa mnyama mwingine atakayetoka katika nchi. Mnyama wa pili atawalazimisha watu kutengeneza sanamu ya Mnyama, ambaye ni Mpinga Kristo; ataipatia sanamu hiyo pumzi kwa nguvu za Shetani na kuifanya iweze kuongea; na atamuua kila ambaye hataiabudu sanamu ya huyo Mnyama. Atamfanya kila mtu kuipokea alama au chapa ya huyu Mnyama katika mikono yao ya kuume au katika vipaji vya nyuso zao, na atamzuia yeyote yule asiye na alama hiyo kununua wala kuuza chochote. 
Kupokea alama ya Mnyama maana yake ni kusalimu amri na kuwa mtumishi wa mnyama huyo. Alama hiyo haitapokelewa kwa kulazimishwa kimwili, bali kwa kuwafanya watu wafanye maamuzi binafsi kuipokea. Lakini, kwa kuwa pasipo kuwa na alama hii hakuna anayeweza kukunua au kuuza kitu chochote kile, basi watu wote hapa ulimwenguni ambao hawajapokea ondoleo la dhambi watasimama upande wa Mnyama na wataishia kusalimu amri mbele zake. 
Hivyo, wale watakaosalimu amri kwa Mnyama na kisha kuipokea alama yake watatupwa pamoja na Ibilisi, katika ziwa liwakalo kwa moto na kibiriti. Wakristo wa mazoea ambao hawajazaliwa tena upya, na kwa kuwa mioyo yao haina Roho Mtakatifu, hatimaye watasalimu amri mbele ya Shetani, wataipokea alama katika mikono yao ya kuume au katika vipaji vya nyuso zao, kisha watamwabudu huyu Shetani kana kwamba ni Mungu. Wakati huo, ni wale tu waliopokea ondoleo la dhambi na walio na Roho Mtakatifu katika mioyo yao ndio watakaoweza kuyapinga matakwa ya kuipokea alama ya Mnyama, kisha watapambana na kumshinda Mpinga Kristo kwa imani.