Ufunuo 4:6-9 inaelezea juu ya viumbe wanne wenye uhai kama ifuatavyo: “Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele,…. ”
Wale viumbe wanne wenye uhai waliokizunguka kiti cha enzi cha Mungu, pamoja na wale wazee 24, ni watumishi waaminifu wa Mungu ambao wanaoyatenda mapenzi yake na kisha kuutukuza utakatifu wake na utukufu. Wakati Mungu anapotenda kazi, hatendi peke yake, bali anatenda wakati wote kupitia watumishi wake. Viumbe wanne wenye uhai, ni watumishi walio karibu zaidi na Mungu, wamepokea uwezo wa kuyatenda mapenzi ya Mungu wakati wote.
Kila moja kati ya wale viumbe wanne wenye uhai ana umbo la peke yake, jambo linaloonyesha kwamba kila kiumbe hai anamtumikia Mungu kwa viwango tofauti. Viumbe hao wana macho pande zote ndani na nje, hii ina maanisha kwamba wakati wote wapo makini kuyaangalia madhumuni ya Mungu. Kwa hiyo, viumbe wanne wenye uhai ni watumishi waaminifu wa Mungu ambao wakati wote wanayatenda mapenzi yake.
Kwa nyongeza, viumbe wanne wenye uhai hawapumziki katika kuusifu utukufu wa Mungu na utakatifu wake, ni kama vile Mungu asivyolala. Wanausifu utakatifu wa Mungu Baba na Bwana Yesu, ambaye ni Mwana-kondoo wa Mungu, pia wanazisifia nguvu zake kuu. Kwa namna hii, wale viumbe wanne wenye uhai wanaosimama mbele ya kiti cha Mungu cha enzi wanamsifu Mungu toka katika mioyo yao yenye unyenyekevu, na hawafanyi hivyo kama sehemu ya kulazimishwa. Kwa nini? Kwa sababu ya kile ambacho Yesu Kristo amekifanya—yaani, kwa kitendo chake cha kujishusha katika umbile la kibinadamu na kwa kuzaliwa hapa ulimwenguni kwa kupitia mwili wa Bikira Mariamu; kwa kuzichukua dhambi zote za mwanadamu katika mwili wake kwa kuupokea ubatizo toka kwa Yohana; kwa kuzichukua dhambi hizo hadi Msalabani na kisha kufa juu yake; na kisha kuwakomboa wanadamu toka katika dhambi—sasa, Yesu ameketi katika kiti cha enzi cha Mungu, na kwa sababu ya matendo haya mema anastahili kupokea utukufu toka kwa viumbe hawa wenye uhai milele na milele.
Hivyo hawa viumbe wanne wenye uhai wakiwa pamoja na wazee 24 wanamwinua Mungu, kwa kumpatia sifa za kweli toka katika mioyo yao.