Search

Maswali ya kila mara juu ya Imani ya Kikristo

Somo la 3: Ufunuo

3-9. Lipi ni Sahihi: Kunyakuliwa Kabla ya Dhiki, au Kunyakuliwa Baada ya Dhiki? Je, Watakatifu Watakuwepo Hapa Duniani Wakati wa Dhiki Kuu?

Tukiangalia historia ya Ukristo, tunaweza kuona kwamba idadi kubwa ya waongo wamekuwa wakiinuka hadi wakati huu wa sasa. Huku wakikifafanua Ktiabu cha Ufunuo na huku wakipigia hesabu muda wa unyakuo kwa kutumia mbinu yao binafsi, waongo hawa wamepanga tarehe maalumu ya unyakuo na wamekuwa wakifundisha kwamba Bwana atarudi na watakatifu watanyakuliwa siku hii ya kuchaguliwa kwao. 
Hata hivyo, madai hayo yote yaliishia kuwa ni uongo. Tabia moja ambayo inafanana sana miongoni mwao wote ni kwamba wanaitetea nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Wanawaeleza wafuasi wao kwamba mali walizo nazo hazitakuwa na maana yoyote ile kwa kuwa watanyakuliwa na kuinuliwa angani kabla ya Dhiki Kuu, hawa waongo waliwadanganya watu wengi na hivyo kuwaibia mali na vitu vyao. 
Tunapaswa kutambua kwamba hii ni mbinu ya Shetani, akijaribu kuwadanganya watu wote wa ulimwengu huu ili kuwageuza wawe wafuasi wake kwa kupitia uongo huu. 
Jambo muhimu zaidi kwa watakatifu, na jambo ambalo watakatifu wengi wanajiuliza, ni swali kwamba unyakuo wa watakatifu utatokea lini. Ufunuo 10:7 inatueleza kwamba, “isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Je, aya hii inaposema kwamba, “siri ya Mungu itakapotimizwa” ina maanisha nini? “Siri ya Mungu” si kitu kingine bali ina maanisha ni unyakuo wa watakatifu. 
Baada ya mapigo sita kati yale mapigo ya matarumbeta saba ya Mungu kuisha, Mpinga Kristo atatokea hapa duniani, atautawala ulimwengu, na atamtaka kila mtu kuipokea alama ya Mnyama. Watakatifu watauawa na kuwa wafia-dini kutokana na mateso yake. Hii itafuatiwa mara na mlio wa tarumbeta la saba, ambapo watakatifu waliouawa kama wafia-dini pamoja watakatifu walio hai walioilinda imani yao watafufuliwa na kunyakuliwa. 
Wakati tarumbeta la saba litakapolia, Mungu hataleta pigo hapa duniani; bali, huu ni wakati ambapo unyakuo wa watakatifu utatokea. Baada ya unyakuo, basi Mungu ataendelea kuyamimina mapigo yake ya mabakuli saba hapa duniani. Kwa hiyo, kuwadia wakati wa mapigo ya mabakuli saba, watakatifu hawatakuwepo hapa duniani, bali watakuwa angani pamoja na Bwana. Sisi sote tunapaswa kutambua kwamba unyakuo wa watakatifu utakuja wakati malaika wa saba atakapolipiga tarumbeta la mwisho. 
Hata hivyo, hata sasa Wakristo wengi bado wanaendelea kuamini katika nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Kwa kuwa imani yao haijajiandaa kwa ujio wa majanga ya kiasili na kutokea kwa Mpinga Kristo, basi hatimaye watashindwa vita yao ya kiroho dhidi ya Shetani na Mpinga Kristo, watageuka na kuwa watumishi wake, kisha wataangamizwa pamoja na ulimwengu. 
Miaka mitatu na nusu ya kwanza katika ile miaka ya saba ya Dhiki Kuu ni wakati wa mapigo ya matarumbeta saba, wakati ambapo dunia itaharibiwa na majanga ya kiasili. Theluthi ya jua na theluthi ya nyota zitatiwa giza; theluthi ya misitu ya hapa duniani itaunguzwa; theluthi ya bahari itageuka na kuwa damu, huku ikiua theluthi ya viumbe hai ndani yake; vimwondo vitaanguka toka angani, na kuyageuza theluthi ya maji kuwa pakanga; na kama matokeo ya hayo, watu wengi sana watakufa. Ulimwengu utaangukia katika machafuko kutokana na mapigo haya, huku mataifa yakiinuka ili yapigane na mataifa mengine, huku falme zikipigana na falme, huku vita ikitokea sehemu mbalimbali. 
Kwa hiyo, wakati Mpinga Kristo atakapotokea na kuyatatua matatizo hayo yote katika hali yenye machafuko kama hiyo, basi watu wengi sana watamfuata, na kwa sababu hiyo watayaleta mapigo ya kutisha zaidi hapa duniani. 
Hivyo, ulimwengu huu utashuhudia kuinuka kwa asasi zenye mafungamano ya kisiasa ya kimataifa, utaratibu wa kiutawala ambao unashughulikia maslahi ya jumla ya mataifa yote. Muungano huu wa mataifa duniani utaangukia katika mikono ya Shetani huku Mpinga Kristo akitokea, kisha muungano huo utageuzwa kua ni muungano unaosimama kinyume na Mungu na watakatifu wake. Mtawala wa muungano huu wa kimataifa atayatawala mataifa yote, kisha atatenda kama Mpinga Kristo. Yeye, anayefanya kazi kwa kutumia nguvu za Shetani ni adui wa Mungu na ni mtumishi wa Ibilisi. 
Wakati huo, Mpinga Kristo atazionyesha rangi zake halisi, huku akiwazuia watu kutomwamini Mungu a kweli na kuwalazimisha wamwabudu yeye kana kwamba ni Mungu. Na ili kulitimiza hili, atafanya ishara nyingi mbele yao, atatatua matatizo mengi ya hapa ulimwenguni huku akitumia nguvu za Shetani, na kwa sababu hiyo ataukamata moyo wa kila mtu. 
Mwishoni, Mpinga Kristo atatengeneza sanamu yake na kuwataka watu wote waiabudu kana kwamba ni Mungu. Na ili kumweka kila mtu chini ya uongozi wake wakati huo wa dhiki, basi Mpinga Kristo atawalazimisha watu kuipokea alama yake katika mikono yao ya kulia au katika vipaji vya nyuso zao, na kisha atawazuia wote wasio na alama hii kufanya biashara yoyote ile. Pia atawaua wale wote ambao watakataa kumwabudu yeye, atawaua bila kujalisha idadi yao. Kwa hiyo, yeyote ambaye jina lake halijaandikwa katika Kitabu cha Uzima ataishia kuipoka alama hii na kisha kumwabudu Mnyama. 
Hata hivyo, watakatifu hawatasalimu amri kwa Mpinga Kristo wala kuipokea alama yake. Kwa kuwa Roho Mtakatifu anakaa katika mioyo yao, basi hakuna mwingine yeyote zaidi ya Mungu Mwenyezi wanayeweza kumwabudu kwa kuwa ni Bwana wao. Hivyo, watakatifu watakataa kumwabudu Shetani na Mpinga Kristo na kuwa watumishi wao, bali watauawa na kuwa wafia-dini kwa imani yao, na kwa sababu hiyo watawashinda Shetani na Mpinga Kristo. 
Kama vile Ufunuo 13:10 inavyotueleza, “Mtu akichukua mateka, atachukuliwa mateka. Mtu akiua kwa upanga, atauawa kwa upanga. Hapa ndipo penye subira na imani ya watakatifu.” Wakati Mpinga Kristo atakapoonekana na kisha kuwalazimisha watu kuipokea alama yake, wakati huo miaka mitatu na nusu ya Dhiki Kuu itakuwa imeshapita, na kipindi cha miaka mingine mitatu na nusu kitakuwa kimeanza. Wakati huu watakatifu watateswa na Mpinga Kristo na kisha kuuawa kama wafia-dini. 
Lakini kitendo cha Mpinga Kristo kutwaa madarakana kuwatesa watakatifu ni mambo yaliyoruhusiwa na Mungu kwa kipindi cha muda mfupi tu, kwa kuwa Bwana atakifupisha kipindi cha Dhiki kwa watakatifu wake. Wakati huo, watakatifu watampatia Mungu utukufu kwa kupambana na Mpinga Kristo ili kuilinda imani yao na kisha kumshinda kwa wao kuwa wafia-dini. 
Baada ya kukipitia kipindi cha kwanza cha miaka mitatu na nusu katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu, watakatifu waliozaliwa tena upya watakuwepo hapa duniani hadi watakapouawa na kuwa wafia-dini wakati ambapo kipindi cha pili dhiki kitakapokuwa kimeanza. Hivyo, watakatifu ni lazima wapambane na Shetani na Mpinga Kristo na kuwashinda kwa imani yao. Hii ndio sababu Ufunuo inatueleza kwamba Mungu atawapatia Mbingu wale watakaoshinda. Kwa hiyo, kabla ya kupita kwa miaka mitatu na nusu ya ile Dhiki Kuu na kabla ya kuonekana kwa Mpinga Kristo, basi imani ya watakatifu itatunzwa katika Kanisa la Mungu, yaani chini ya ulinzi na uongozi wa Bwana wetu. 
Hivyo, watu wanapaswa kuwekwa huru toka katika haya mafundisho mabaya ya kidini ambayo Shetani ameyaeneza katika jumuia za Kikristo, mafundisho hayo ni nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, pia wanapaswa kupokea ondoleo la dhambi zao zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho na kisha kujiunga katika Kanisa la Mungu. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo imani yao inapoweza kujengwa kwa kupitia Kanisa la Mungu kwa miaka mitatu na nusu ya kwanza katika ile miaka ya Dhiki Kuu, na ni hapo ndipo wanapoweza kuwa imani inayoweza kupambana dhidi ya Mpinga Kristo na kisha kuyapokea mauaji yao wa kuwa wafia-dini utakapowadia wakati mgumu wa dhiki.