Search

Maswali ya kila mara juu ya Imani ya Kikristo

Somo la 3: Ufunuo

3-10. Unaposema kwamba unyakuo utakuja baada ya malaika wa saba kulipiga tarumbeta lake, je, hujichanganyi kutokana na kile ambacho Bwana amekisema, kwamba hakuna mtu anayeijua siku wala saa ya unyakuo, akiwamo Bwana Mwenyewe?

Hapana kabisa! Alichotueleza Bwana wetu si juu ya siku na saa ambapo watakatifu watanyakuliwa, bali ametueleza juu ya habari za utangulizi na ishara ambazo zitapelekea kutokea kwa tukio hili muhimu. Ni kwa kufahamu hivyo ndipo watakatifu wanaompenda Bwana wanapoweza kuiandaa imani yao, na hapo ndipo wanapoweza kushiriki katiak unyakuo kwa kupambana dhidi ya Mpinga Kristo na kuyapokea mauaji yao ya kuwa wafia-dini wakati utakapowadia. 
Kwa kupitia ufunuo wake, Mungu alimwonyesha Mtume Yohana, aliyekuwa uhamishoni katika Kisiwa cha Patmo mambo yote ambayo yatakuja kutokea nyakati za mwisho za ulimwengu huu. Vivyo hivyo, Mungu anapopanga na kuzitimiza kazi zake, basi huwa anahakikisha kuwa watumishi wake wanafahamu. 
Katika Neno la Mungu lote, Kitabu cha Ufunuo ndio kinachoongoza kwa kuandikwa kwa lugha ya picha. Kwa sababu hii, ni watumishi wa Mungu tu ambao wameokolewa toka katika dhambi zao zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho na hivyo kuwa na Roho Mtakatifu ndani ya mioyo yao ndio wanaoweza kuzielezea vizuri lugha hizo za picha kwa watu. Neno la Ufunuo linawafunulia kwa kina watumishi wa Mungu na watakatifu wake kuhusu mapigo ya matarumbeta saba, kuonekana kwa Mpinga Kristo, watakatifu kufia-dini, kufufuka na kunyakuliwa kwa wataktaifu, Ufalme wa Kristo wa Milenia, na Mbingu na Nchi Mpya. 
Kunyakuliwa kwa watakatifu kunahusiana kwa karibu kabisa na vifo vya wafia-dini. Ufunuo 11:10-12 inatueleza kuhusu kifo cha manabii wawili, na juu ya ufufuo na kunyakuliwa kwao kwa muda wa siku tatu na nusu. Mashahidi hawa wawili watauawa na Mpinga Kristo kisha baada ya siku tatu na nusu watafufuliwa toka mauti. Tunachoweza kukiona katika maelezo haya ni kwamba wakati Mpinga Kristo atakapoonekana hapa duniani na kisha kuwafanya watu wamwabudu Mnyama kwa kuipokea alama yake katika mikono yao ya kuume au katika vipaji vya nyuso zao, basi watakatifu watapambana dhidi ya Mpinga Kristo na kisha kuuawa na kuwa wafia-dini kwa imani yao, lakini kufuatia kurudi kwa Bwana muda mfupi baada ya kuuawa kwao na kuwa wafia-dini, watashiriki katika ufufuo wa kwanza na kisha kunyakuliwa. 
Pia Paulo alizungumzia juu ya unyakuo katika 1 Wathesalonike 4:16-17: “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.”
Wakati utawala wa Mpinga Kristo utakapoanza katika ulimwengu huu, wakati atakapojaribu kutulazimisha ili tuipokee alama yake, na wakati atakapodai aabudiwe kana kwamba ni Mungu, basi sisi watakatifu ni lazima tutambue kwamba wakati wa kuuawa kwetu na kuwa wafia-dini umewadia, pia ni lazima tuamini kwamba mara baada ya kuuawa kama wafia-dini utafuatia ufufuo na unyakuo wetu. Hatufahamu kuwa ni mwezi upi na ni siku ipi mambo haya yatatokea. Lakini tunachofahamu ni kwamba unyakuo wa watakatifu utakuja baada ya malaika wa saba kulipiga tarumbeta lake. Watakatifu wote ni lazima wajiandae kuipokea Siku ya Bwana kwa kuuamini ukweli huu.