Search

Maswali ya kila mara juu ya Imani ya Kikristo

Somo la 3: Ufunuo

3-14. Ninaamini kwamba watakatifu watanyakuliwa kabla ya Dhiki Kuu. Lakini Biblia inaeleza mara nyingi juu ya watakatifu watakaokuwa wamebakia hapa duniani wakati wa Dhiki Kuu. Je, hao ndio wale waliokubaliana na ulimwengu, na ambao imani yao iligeuka na kuwa ya vuguvugu?

Kwanza kabisa, unapaswa kutambua kwamba nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki unayoimani ni mafundisho ya uongo. Hii ndio sehemu ambayo Wakristo wengi wameielewa vibaya. Wanafikiri kwamba kwa kuwa watakatifu watakuwa wamekwisha nyakuliwa kabla ya Dhiki Kuu, basi wakati huo utakapowadia utawakuta wenye dhambi peke yao hapa duniani. Hata hivyo, tatizo ni kwamba Biblia inataja mara nyingi juu ya watakatifu ambao, walipokuwa hapa duniani wakati wa Dhiki Kuu, waliyashinda mateso kwa uvumilivu na kisha kuuawa kama wafia-dini. 
Hivyo, watu wengi wanafikiri kimakosa kwamba watakatifu hawa ambao wameachwa duniani na kisha kuteswa wakati wa Dhiki ndio wale ambao walikubaliana na ulimwengu na ambao imani yao ilikuwa ya vuguvugu. 
Watu wanaoshikilia mtazamo huu wanaishi katika hali ya kuchanganyikiwa kwa kuwa hawaufahamu wakati maalum wa unyakuo kama unavyoelezwa katika Neno la Mungu. Sasa, wakati hasa wa unyakuo ni lini? Paulo katika 2 Wathesalonike 2:1-4 anazungumza nasi kuhusu jambo hili kama ifuatavyo: “Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.”
“Mtu wa kuasi… mwana wa uharibifu” maana yake ni Mpinga Kristo ambaye atatokea katikati ya Dhiki Kuu. Kwa maneno mengine, Mpinga Kristo atatokea hapa ulimwenguni kabla ya unyakuo na atajiinua kana kwamba ni Mungu. Hivyo atafanyika sanamu yake na kuwalazimisha watu waiabudu na kumtumikia yeye. Ili kumfanya kila mtu kuwa chini ya utawala wake, basi Mpinga Kristo atawafanya watu kuipokea alama au jina la Mnyama katika mikono yao ya kuume au katika vipaji vya nyuso zao, na atamzuia yeyote asiyekuwa na alama hii kutonunua au kuuza chochote. 
Wakati Mnyama huyu atakapoonekana hapa ulimwenguni, watu wa ulimwengu huu watalazimishwa kuipokea alama iliyotengenezwa kwa jina lake au kwa namba ya jina lake. Kwa hiyo, yeyote ambaye jina lake halijaandikwa katika Kitabu cha Uzima tangu uumbaji ataishia kuipokea alama na kumwabudu Mnyama. 
Hata hivyo, kwa kuwa watakatifu ambao wamefanyika kuwa watu wa Mungu wana Roho Mtakatifu ndani ya mioyo yao, wao hawataweza kumwabudu kiumbe yeyote yule mbali ya Bwana Mungu wao kana kwamba ni Mungu. Hivyo, Roho Mtakatifu anayekaa ndani yao atawapa nguvu ya kupinga shuruti za Shetani na za Mpinga Kristo na nguvu ya kuilinda imani yao kwa kuwa wafia-dini. Pia Roho Mtakatifu atawapatia maneno ambayo kwa hayo wanaweza kusimama kinyume na maadui zao. 
Ufunuo 17:12-13 inatueleza kwamba, “Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.” Mpinga Kristo atapokea mamlaka ya kuwatesa watakatifu na kuyatawala mataifa ya ulimwenguni kwa kipindi kifupi tu. Hivyo, madai ya Mpinga Kristo ya kuipokea alama yake yatafuatiwa muda si mrefu na mauaji ya watakatifu ya kuwa wafia-dini. 
Kwa upande mwingine, Ufunuo 11:11-12, inatueleza kwamba, “Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.” Kutokana na ukweli huu, kwamba mashahidi wawili waliouawa kama wafia-dini walifufuliwa na kunyakuliwa baada ya siku tatu na nusu, basi tunaweza kuona kwamba kipindi kati ya mauaji yetu ya kuwa wafia-dini na kunyakuliwa kwetu si mbali sana pia. Mashahidi hawa wawili walinyakuliwa mara walipofufuliwa. Wakati Bwana atakaporudi, watakatifu waliouawa kama wafia-dini na watakatifu watakaokuwa hai ambao hawakuipokea alama ya Mnyama watafufuliwa wote, watanyakuliwa angani, kisha watamlaki Bwana angani. 
Hivyo, tunaweza kutambua kwamba kuonekana kwa Mpinga Kristo, mauaji ya watakatifu ya kufia-dini na kufufuliwa kwao, na unyakuo, vyote hivyo vinahusiana. Paulo na Yohana walituelezea kwa kina juu ya wakati wa unyakuo wa watakatifu. Watakatifu wote watakipitia kipindi cha miaka mitatu na nusu ya kwanza katika ile Dhiki Kuu. Kwa maneno mengine, watakatifu watakuwepo hapa duniani hadi mapigo ya matarumbeta saba yatakapoisha. 
Baada ya kuonekana kwa Mpinga Kristo, watakatifu wataingia katika kipindi cha pili cha miaka mitatu na nusu katika ile miaka ya Dhiki Kuu, na watakuwepo hapa duniani hadi pale watakapouawa na kuwa wafia-dini kwa kukataa kuipokea alama ya Mnyama. Hali tukilitambua hili, basi sisi sote tunapaswa kupokea malezi ya imani katika Kanisa la Mungu, yaani wakati huu wa sasa.