Search

Bài giảng

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[12-1] Kanisa la Mungu Ambalo Litadhuriwa Sana Hapo Baadaye (Ufunuo 12:1-17)

(Ufunuo 12:1-17)
“Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili. Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa. Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake. Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi. Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini. Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake akatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu. Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume. Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo. Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule. Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake. Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.”
Hii inatueleza juu ya Kanisa la Mungu likimpatia Mungu utukufu kwa kupitia kifo cha kuifia-dini. “Mwanamke aliyevikwa jua” ana maanisha ni Kanisa la Mungu hapa duniani, na ule msemo “na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake” una maanisha kuwa Kanisa bado lipo chini ya utawala wa ulimwengu. Na kwa upande mwingine, msemo unaosema “na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili,” una maanisha Kanisa la Mungu litayashinda mateso na vitisho vya Shetani kwa kuuawa na kuifia-dini.
Aya hii inaelezea juu ya Kanisa la Mungu likiwa katikati ya Dhiki Kuu. Katika nyakati za mwisho Kanisa la Mungu litateseka sana na kudhuriwa na Shetani na wengi watauawa na kuifia-dini, lakini hata hivyo litamshinda Shetani kwa imani yake na kisha litatukuzwa na Mungu. Hata katika wakati wa Dhiki, watakatifu wa Kanisa la Mungu watamshinda Mpinga Kristo na kisha kuibuka washindi kwa kuifia-dini kwa kuamini katika injili ya maji na Roho.
Ni hakika kuwa wana wa Mungu ambao wamezaliwa tena upya kwa maji na Roho wauawa na kuifia-dini katika nyakati za mwisho. Wale ambao watakuwa wamekwisha amini na kumtumia Mungu kabla ya kuja kwa Dhiki, na wale ambao wataiamini injili na kisha kuinuka kama uyoga katikati ya Dhiki, wote hao watakuwa na imani ya kuweza kuifia-dini imani inayowawezesha kusimama kinyume na kumshinda Mpinga Kristo.
Wale ambao watakuwa wameondolewa katika kuifia-dini kwa sababu ya kumkana Mungu pia wataondolewa Mbinguni, kisha wataangukia kuzimu wakiwa pamoja na Shetani. Tunapaswa kujiandaa kupokea kuuawa kwa ajili ya kuifia-dini hali tukiwa na imani thabiti ili kwamba tusije tukaikosa baraka ya milele tuliyoandaliwa. Pia tunapaswa kufahamu kwamba wale wote waliozaliwa tena upya watakutana na vitisho vya Shetani. Mauaji ya wafia-dini yatakuwa ni ya muda tu, na mara baada ya mauaji haya kuisha, basi Ufalme wa Mileni na ule wa Mbinguni vitakuwa ni mali yetu.
Hivyo, tunapaswa kuishi katika wakati huu hali tukifahamu kwamba nyakati za mwisho zitakapokuja, tutauawa na kuifia-dini kwa imani na kupitia Roho Mtakatifu. Wakati huo Roho Mtakatifu atatupatia maneno ya kuongea wakati wa mauaji hayo, hali akituwezesha kuyashinda mateso yetu kwa ujasiri na kisha kupokea kuuawa kwa kuifia-dini kwa hiari pasipo kuikana imani yetu.
Hata katikati ya Dhiki ya kutisha, Kanisa la Mungu litapigana dhidi ya Shetani na kumshinda kwa kuuawa na kuifia-dini. Ni wazi kwamba Kanisa litapokea thawabu toka kwa Mungu kwa kumshinda Mpinga Kristo kwa kuifia-dini, na kwa kuamini katika Neno la Bwana hata katika kipindi cha mwisho cha Shetani.
 
Aya ya 2: “Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa.”
Aya hii inatueleza juu ya Kanisa la Mungu likiwa katika Dhiki. Inatueleza juu ya Kanisa lote likivumilia katika mateso na dhiki za nyakati za mwisho zilizoletwa na Shetani. Kanisa la Mungu litapita katika Dhiki Kuu, yaani wakati wa kupambana dhidi ya Mpinga Kristo. Hivyo, watakatifu watamwita Mungu tu wakati watakapokuwa wakipita katika hiyo Dhiki. Wataomba hivi, “Mungu, tunaomba utupatie neema yako ili kwamba tuweze kupita kwa haraka katika dhiki hizi zote. Utusaidie kwa kuzikomesha dhiki hizi zote. Uturuhusu kuzishinda hizi dhiki. Tufanye tuweze kumshinda Shetani!”
 
Aya ya 3: “Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.”
Wakati Shetani atakapoonekana duniani hapo baadaye, atatenda kana kwamba yeye ni Mungu, na kwamba atayakusanya mataifa yote ya ulimwenguni na atayatumia kama zana yake ya kuyatimiza madhumuni yake. Pia ni hakika kuwa atawaua watakatifu na kisha kuutawala ulimwengu kama Mungu na mfalme.
Msemo unaosema, “Na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba,” unaonyesha kuwa Shetani, mvunja-amani, atawakokota wafalme saba na mataifa saba kama mali yake. Aya hii inatueleza kuwa, kimsingi, Shetani katika uwepo wake, anasimama kinyume na Mungu.
 
Aya ya 4: “Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.”
Aya hii inatueleza kile ambacho Shetani anakifanya. Joka aligeuka na kuwa kinyume na Mungu Mbinguni na alitupwa kutoka mbinguni. Yule Joka aliwavuta theluthi ya malaika wa Mbinguni katika mkia wake na akawaongoza kwenda katika maangamizi yao pamoja na maangamizi yake. Hivyo alivurumishwa atoke katika uwepo wa Mungu. Lakini hata akiwapo hapa duniani, anajaribu kuisimamisha kazi ya injili ya Mungu kwa kuwatesa wale wanaoiamini injili.
 
Aya ya 5: “Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.”
Hii inatueleza kuwa Kanisa la Mungu, kwa kuwa linauawa kwa kuifia-dini na kwa kumwamini Yesu Kristo, basi Kanisa hilo litafufuliwa na Kristo na kunyakuliwa kwenda katika Ufalme wa Mbinguni.
 
Aya ya 6: “Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini.”
Aya hii inatueleza kuwa Mungu atawalisha watu wake kwa miaka mitatu na nusu katika ulimwengu huu. Kanisa la Mungu litalishwa na kulindwa na Mungu kwa siku 1,260 kabla ya ujio wa dhiki kuu kamilifu, na wakati utakapowadia, Kanisa litapigana dhidi ya Mpinga Kristo na kisha litauawa na kuifia-dini.
 
Aya ya 7-8: “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.”
Hii inazungumzia juu ya Shetani kufukuzwa na kuondolewa kikamilifu huko mbinguni.
Kabla ya kuja hapa ulimwenguni, Shetani atatupwa nje ya Mbingu moja kwa moja. Ibilisi hataweza tena kamwe kukaa Mbinguni. Shetani, aliye na mamlaka juu ya anga, anakaa angani na duniani na kwa sasa anavitawala vitu hivyo. Kwa kuwa atakuwa ameondolewa moja kwa moja toka Mbinguni, basi akiwa hapa duniani atawatesa watakatifu zaidi na zaidi hasa nyakati za mwisho zitakapowadia. Lakini, hatimaye Shetani atatolewa na kutupwa katika shimo lisilo na mwisho na kuzimu iliyoandaliwa na Mungu.
 
Aya ya 9: “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake akatupwa pamoja naye.”
Katika nyakati za mwisho, Shetani baada ya kuwa ameondolewa toka Mbinguni na kutupwa duniani, atawatesa na kuwaua watakatifu kwa mara ya mwisho. Watakatifu wengi watauawa na kuifia-dini katika mikono yake.
 
Aya ya 10: “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”
Shetani hatapatikana kamwe katika Ufalme wa Mbinguni. Wakati nyakati za mwisho zitakapokuwa zikiishia, hataweza kukaa Mbinguni tena. Hii ndio sababu Kitabu cha Ufunuo 21:27 kwamba hakuna watenda maovu wala waongo wanaopatikana Mbinguni.
 
Aya ya 11: “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”
Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, watakatifu watauawa na kuifia-dini ili kuilinda imani yao. Yeyote aliye mtakatifu ataufikia ushindi wa imani kwa kupitia kifo chake cha kuifia-dini kwa imani. Kwa maneno mengine, wafia-dini wanaomwamini Bwana, watashinda viti dhidi ya nafsi zao.
 
Aya ya 12: “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”
Baada ya Shetani kutupwa toka Mbinguni, basi atakapokuja hapa duniani atakuwa na nguvu za muda dhidi ya ulimwengu, atawanyanyasa na kuwatesa watakatifu katika hali ya kutisha. Lakini kwa watakatifu watakaokuwa wameifia-dini na kunyakuliwa angani, watakuwa wakiingojea furaha ya ajabu. Baada ya kunyakuliwa, Mungu atayaleta mapigo ya mabakuli saba katika dunia yote na bahari.
 
Aya ya 13: “Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.”
Aya hii inazungumzia juu ya mateso ya watakatifu yatakayokuja katika wakati wa Dhiki Kuu. Watakatifu na watumishi wa Mungu watakufa wakati huo kwa kuifia-dini, lakini mauaji ya kuifia-dini yatakuwa ni ushindi mkubwa kwao wa kiimani. Hakutakuwa na kifo tena, mateso, wala laana kwao. Kitakachokuwa kimebakia kwao ni kumsifu Mungu na kutukuzwa milele wakiwa Mbinguni.
 
Aya ya 14: “Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.”
Biblia inatueleza kuwa kunyakuliwa kutatokea baada ya kupita kwa miaka mitatu na nusu katika ile Dhiki Kuu. Neno hili linatueleza kuwa Mungu atawapatia watakatifu ulinzi maalumu na kuwatia moyo katikati ya mapigo ya kiasili ya Dhiki Kuu. Mungu atatustawisha sisi sote tunaoilinda imani yetu ili kwamba tuweze kupigana na kumshinda Shetani kwa imani hii.
Kule kusema sasa tunaishi kwa ajili ya injili ya maji na Roho basi injili hiyo inafanywa kuwa chakula chetu cha kiroho, pia kuihubiri injili hii kunafanywa kuwa chakula cha kiroho. Tutaendelea kuishi maisha yetu tukiihubiri injili hadi mapigo ya matarumbeta saba yatakaposhuka hapa duniani. Kwa nini? Kwa sababu kama hatuihubiri injili hadi nyakati za mwisho za kuuawa kwetu kwa kuifia-dini, basi ni hakika kuwa nafsi nyingi zitapotelea na kwenda kuzimu. Hakuna wakati mwingine wa kuihubiri injili zaidi ya sasa.
 
Aya ya 15-17: “Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule. Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake. Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.”
Hapo kabla, Shetani aliwaua watakatifu kwa kuwatesa na kuwafanya waende mbali na injili. Lakini siku hizi, wakati ambapo injili imeenezwa sana kwa kupitia njia mbalimbali, Shetani anajaribu kuwaua watakatifu kwa kuimimina dhambi na kuwafanya wazame kwa mmiminiko wa hizo dhambi. Hivyo, Shetani amejaribu kuleta kifo kwa watakatifu wengi kwa kuumwaga mto wa dhambi na kuwafanya wanywe toka katika mto huo. Kwa kuwa watakatifu wameweza kuishi na kutouawa na jitihada hizo za Shetani, basi Shetani atakuja na mbinu nyingine ili kuwaua watakatifu kikamilifu kama inavyoonyeshwa katika sura ya 13.