Search

خطبے

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[3-4] Watumishi na Watakatifu wa Mungu Wanaoufurahisha Moyo Wake (Ufunuo 3:7-13)

(Ufunuo 3:7-13)
 
 
Bado Kuna Makanisa Katika Ulimwengu Huu Ambayo Yako Kama Kanisa la Filadelfia
 
Mungu anatueleza hapa kuwa Kanisa la Filadelfia lilikuwa ni kanisa lililosifiwa na kupendwa sana na Bwana miongoni mwa yale makanisa saba ya Asia.
Katika wakati wa sasa, tunaweza kuona kuwa, Mungu aliyeongea kwa yale makanisa saba ya Asia anataka makanisa yake kuwa kama Kanisa la Filadelfia ili aweze kufanya kazi kwa kupitia makanisa hayo na aweze kufurahishwa. Hata katika wakati wa sasa, makanisa ambayo yanasifiwa na Mungu ni yale yanayoihubiri injili ya maji na Roho.
Kama ilivyokuwa wakati ule, watakatifu ambao ni waaminifu kwa Mungu, hata kama uwezo wao ni mdogo, ukweli ni kuwa watakatifu hao wapo upande wa makanisa yanayoieneza injili ya maji na Roho. Mungu anafurahishwa na wafanyakazi kama hao. Kati yao hakuna anayeweza kuyafukuza mapepo kwa kuwawekea mikono wala hakuna anayeweza kutoa unabii. Pia hakuna aliyepewa karama ya kunena kwa lugha wala hakuna aliyepewa nguvu ya ushawishi. Kitu pekee wanachokifanya ni kwamba wanaamini na kuhubiri kuwa Yesu pekee ndiye aliyezisafisha dhambi zetu zote mara moja na kwa wote kwa kuzichukua dhambi za mwamandamu katika mwili wake kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana, na kwamba hukumu yetu yote ya dhambi ilihamishiwa kwa Kristo kwa damu yake Msalabani.
Wafanyakazi hawa si wengine bali ni waamini wanaomfuata Bwana, wanaomwabudu, na wanaoyatii mapenzi yake kwa imani yao katika injili ya maji na Roho. Wale wanaoihubiri injili ya maji na Roho si matajiri kifedha. Wala hawana karama nyingine yoyote ile. Kitu pekee walichonacho ni imani yao na hamu ya kuihubiri injili ya maji na Roho. Wao huamini kuwa kuifanya kazi ya kuieneza injili ndio kitu pekee kinachoufurahisha moyo wa Bwana, kwa kuwa Bwana alibatizwa na Yohana, akasubuliwa Msalabani, na kisha akafufuka tena toka kwa wafu ili kuzifanya dhambi zetu zote kutoweka. Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wanamshukuru na kumfuata Bwana peke yake.
Kitu tunachokitaka ni kuona kuwa injili hii ya maji na Roho inaenezwa kwa kila mtu, na pia tunapenda kila mmoja aweze kukombolewa toka katika dhambi zake zote. Katika hali ya kushangaza, Mungu ameturuhusu kuihuburi injili ya maji na Roho ulimwenguni kote, na ametubariki ili kwamba matunda mengi yaweze kuzaliwa. Pia ametupatia imani ambayo kwa hiyo tunaweza kukubali kuuawa kwa kuifia-dini katika nyakati za mwisho, na ametupatia baraka ya kunyakuliwa na kuishi katika Ufalme wa Milenia. Mungu ameturuhusu kuuawa kwa kuifia-dini, na ameturuhusu kushiriki katika ufufuo wa kwanza na kisha kufunikwa utukufu wa Mbinguni.
Wale wenzetu ambao sasa wamejitoa katika kuihubiri injili ya maji na Roho ni sehemu ya kanisa la Mungu linalopendwa.
Hebu tufikirie jinsi tunavyoweza kuieneza injili ya maji na Roho ulimwenguni kote. Mungu aliliambia kanisa lake kuwa mlango wa kuihubiri injili umekwisha funguliwa. Kwa kuwa hakuna mtu anayeweza kuzuia kile ambacho Mungu amepanga, basi ni hakika kuwa Mungu atatimiza kila kitu.
Mungu ameturuhusu sisi tunaoamini katika injili ya maji na Roho kuihubiri injili hii ya ubatizo wake kwa ulimwengu mzima. Hata leo hii, makanisa ya Mungu bado yamebarikiwa katika kufanya kazi ya kuieneza injili ya maji na Roho hapa duniani. Tunapoangalia juu ya uwezo wao binafsi, watu kama hao wanaweza kuoenekana wakiwa na mapungufu mengi. Lakini kwa kuwa ndani ya mioyo yao kuna ule upendo wa injili ya maji na Roho, basi Mungu anawashikilia kwa nguvu na anafanya kazi kupitia wao.
Kule kusema kuwa kuna makanisa yaliyo kama hivi hivi kunaleta tumaini kubwa kwa ulimwengu. Mungu ameyakabidhi makanisa kama hayo kazi ya kuieneza injili ya maji na Roho, na pia amehakikisha kuwa hakuna anayeweza kuzuia kile wanachokifanya. Wao wanaihubiri injili ya maji na Roho mahali pote ulimwenguni, na kwa sababu hiyo injili hii inaenezwa ulimwenguni mwote. Mungu anawatia nguvu, anawalinda, na anafanya kazi pamoja nao. Hivi punde tunaweza kuona kuwa Mungu atawabariki kimwili na kiroho wale wote wanaojiunga katika kazi hii na kuieneza injili ya maji na Roho katika mataifa yote ulimwenguni.
Sisi tunaieneza injili ya maji na Roho katika kila kona ya ya ulimwengu huu kwa kupitia vitabu vyetu vya karatasi na kwa kupitia vitabu-pepe. Tunafanya hivi hadi mwisho wa ulimwengu huu, na Bwana ataendelea kufanya kazi kupitia kwetu hadi Ufalme wa Kristo utakapotimizwa hapa duniani. Mungu atatuwezesha kuihubiri injili ya maji na Roho kwa watu bilioni 6.5 waliopo ulimwenguni kwa kupitia maandiko yetu. Mungu atubariki sote!
Ili tuweze kuifanya kazi inayompendeza Mungu, basi ni lazima tujiandae kwa vita ya kiroho. Kwa hiyo, ninamwomba Mungu ili kwamba awashikilie kwa nguvu na kuwabariki watumishi wake. Hakuna hata mmoja aliye mwaminifu kama Bwana wetu. Ninaamini kuwa hakuna ukweli wowote ule katika ulimwengu huu unaoweza kutuletea wokovu mkamilifu na wa wazi kama ule ambao injili ya maji na Roho ambayo tunaiamini imetuletea.
 

Kitabu cha Ufunuo Ni Neno la Mungu Lililobarikiwa Linalotolewa Kwa Wale Wanaoshinda
 
Mungu alitueleza kuwa “yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima.” Ukweli huu una maanisha kuwa Mungu atawaruhusu watu kama hao kuishi katika Ufalme wa Milenia. Maneno haya“Yeye ashindaye” yana maanisha ni wale wanaoilinda imani yao dhidi ya Mpinga Kristo kwa ukweli hadi mwisho wa nyakati, na kwa wakati wa sasa tulio nao ni wale wanaopambana na kuwashinda wafuasi wa injili ya uongo kwa kutumia imani yao katika Neno la kweli. Ni lazima tuushinde uovu kwa wema kwa kuihubiri injili ya maji na Roho kwa ulimwengu mzima. Ni lazima tupambane na kuwashinda waongo wote na mafundisho yao ya kiimani kwa kutumia imani yetu katika Neno la maji na Roho.
Ili tuweze kupambana na kuwashinda waongo, basi ni lazima tujikumbushe sana juu ya Neno la injili ya maji na Roho. Kama tungekuwa tumeamini katika injili ya maji na Roho sasa na kisha tukasafishwa dhambi zetu zote, basi ni hakika kuwa mapambano yetu dhidi ya waongo yangelikuwa yameanza wakati ule ule tulipoamini. Wale wanaoamini katika injili ya kweli wanapambana na kuwashinda wale walio na injili ya uongo.
Ni lazima tuihubiri injili ya maji na Roho wakati wote kwa wale wanaoifuata injili ya uongo. Kwa nini? Kwa sababu nguvu ya injili ya maji na Roho inaweza kuharibu imani yao potofu na kisha ikawaletea maisha mapya. Biblia inatueleza kuushinda ubaya kwa wema. Kwa hiyo, hatupaswi kukata tamaa katika mapambano yetu mema ya kiroho yanayoziokoa nafsi hizi toka katika dhambi zao.
Katika vita vyetu vya kiroho kunapatikana baraka ya wokovu wa roho. Sisi tunaweza kumpatia Mungu matunda yote ya uzima wa milele kwa kupambana na kuwashinda waongo kwa imani yetu katika injili ya maji na Roho.
 

Bwana Alituambia Kujifunza Toka Katika Mfano wa Mti wa Mtini
 
Mti wa mtini ni ishara ya taifa la Israeli. Kama kila taifa lilivyo na ua lake au mti wake wa kitaifa, basi mti wa mtini ni alama ya utaifa ya taifa la Isareli. Ni lazima utambue kuwa wakati matawi ya Israeli yanapozidi kuwa manene, basi ni hakika kuwa nyakati za mwisho zitakuwa zimekaribia sana ulimwenguni. Biblia inatueleza kuwa Bwana atarudi wakati taifa la Israeli litakapokuwa likijengwa upya hapa duniani na kuwa lenye nguvu.
Siku hizi katika magazeti kuna habari nyingi zilizojaa kuhusu mgogoro kati ya Waisraeli na Wapalestina. Kwa sasa Israeli inamiliki eneo lake lote la kihistoria na limekuwa ni taifa lenye nguvu sana. Kwa sasa hali ya baadaye ya Israeli inamtegemea sana Mungu. Kuanguka au kuinuka kwa Israeli kutatokana na mujibu wa Neno la Mungu. Na wakati Israeli itakapopotea katika ulimwengu huu, basi ni lazima utambue kuwa hapo ndipo kurudi tena kwa Bwana mara ya pili duniani kutakapotimizwa. Kama Biblia inavyosema kuwa Bwana atarudi wakati matawi ya mtini yatakapokuwa yamenenepa, Bwana anaeleza juu ya mwisho wa ulimwengu huu kwa kupitia kurudishwa na kufanikiwa kwa Israeli. Pia anabashiri kuwa katika nyakati za mwisho kutakuwa na matatizo yatakayoyapiga na kuharibu mazingira ya kiasili ulimwenguni.
Mungu alimweleza kila mtu kuwa na imani katika injili ya maji na Roho. Madhumuni yote ya Mungu yamelengwa katika imani juu ya injili ya maji na Roho. Kwa hiyo, wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wameokolewa toka katika dhambi zao zote. Bwana alituambia kuwa, “Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu” (Luka 21:36). Sisi hatuwezi kuikwepa Dhiki itakayokuja kwa nguvu zetu binafsi. Lakini kwa kuliamini Neno la Mungu, ni hakika kuwa tunaweza kuishinda Dhiki hiyo. Hivi sasa tupo katika hali ambayo inatulazima kuiandaa imani yetu katika kuuawa na kuifia-dini kwa maana wakati wa Dhiki unatukaribia.
Ikiwa Wakristo wanafikiri kuwa hawatakuwepo katika kipindi cha Dhiki Kuu wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, basi ni dhahiri kuwa imani yao hiyo ina makosa makubwa. Hatupaswi kuyaamini mafundisho ya kiimani ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Fundisho hili la kiimani lipo kinyume na ukweli wa Biblia, kwa kuwa Maandiko, na hasa Kitabu cha Ufunuo yanatueleza kuwa kuuawa na kufia-dini kwa watakatifu kutatokea baada ya kupita ile miaka mitatu na nusu kati ya ile miaka saba ya Dhiki. Hivyo, kitendo cha watakatifu kufikiri kuwa hawataingia katika kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu kitawaongoza katika imani iliyopotoshwa na ambayo ni hatari. Ni lazima utambue kuwa wale wanaomwamini Yesu watakuwa katikati ya Dhiki Kuu.
Kwa mujibu wa Neno la Mungu, je, wenye haki watabakia katika ulimwengu huu kwa muda gani? Watabakia katika ulimwengu huu hadi pale Shetani atakapowataka wenye dhambi kupokea alama yake, yaani wakati ambapo watakatifu watauawa kwa kuifia-dini na majeshi ya Mpinga Kristo. Huu ndio ukweli uliodhihirishwa na Mungu, na hii ndiyo imani sahihi.
 

Vita Kubwa ya Kiroho Itakayokuja Katika Nyakati za Mwisho
 
Matokeo ya imani ya wenye haki yanaelezwa kwa wazi kabisa katika Dhiki Kuu iliyoruhusiwa na Mungu. Ni lazima utambue kuwa pasipo imani yako katika injili ya maji na Roho, basi huwezi kupata ushindi wa kweli katika vita yako dhidi ya Shetani katika nyakati za mwisho. Lakini kwa wakati ule ule, ni lazima pia utambue kuwa ushindi wa mwisho utakuwa ni kwa wenye haki, maana kwa imani yao katika injili ya maji na Roho watakuwa washindi halisi hata pale mwisho wa dunia utakapokuwa unakaribia. Kwa hiyo, ni lazima tuikamilishe kazi ya kuihubiri injili ya maji na Roho katika ulimwengu wote kabla ya kuja kwa nyakati za mwisho.
Ni lazima tumfurahishe Bwana wetu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Sisi tunayo injili ya maji na Roho, ambayo ni Neno la imani inayoweza kutupatia ushindi wa mwisho. Mungu anaueleza ulimwengu kwa wazi juu ya mwisho wake. Pia ni lazima tutambue kuwa wakati huo Bwana atarudi, na kwamba atawainua watakatifu kwenda mbinguni, na kwamba ataleta mapigo makuu kwa wale watakaokuwa wamebakia hapa ulimwengu hadi wakati huo. Kwa hiyo, ni lazima tuzipokee nyakati za mwisho kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, hali tukiwa tumevishwa imani ya kweli. Mungu amewaeleza wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho kuusubiria Ufalme wa Milenia kwa imani kama alivyosema katika wakati wa Nuhu kwamba mwisho wa ulimwengu ulifika wakati watu wakila na kunywa. 
Kwa kweli watu hawawezi kuyatatua matatizo yote ya nyakati za mwisho ikiwa hawataamini katika injili ya maji na Roho. Ni lazima tuamini katika injili ya maji na Roho kwa namna zote. Wale wasioamini katika injili hii ya maji na Roho ni hakika kuwa hawawezi kuvumiliwa na Mungu kabisa. Mungu atayaleta mapigo ya kutisha zaidi kwa ulimwengu huu katika hatua za mwisho za nyakati za mwisho. Kwa kuwa wale wasioamini katika injili ya maji na Roho hawawezi kuikwepa hukumu ya haki ya Mungu, basi ni lazima waiamini injili hii sasa.
Hivyo, ili kuikwepa hukumu ya Mungu, basi ni muhimu kwa kila mtu kujifunza juu ya injili ya maji na Roho na kuiamini kwa moyo wake wote. Ukweli wa wokovu ambao upo kwa kila mtu ni injili ya maji na Roho. Hakuna injili nyingine ya kweli mbele za Mungu zaidi ya injili ya maji na Roho. Kwa kweli ulimwengu huu kwa sasa unaihitaji sana injili ya maji na Roho kwa kuwa unaishi katika kina cha dhambi ukiwa na desturi ya dhambi.
Kwa kuwa hakuna dhamana ya mambo ya baadaye kwa wakati huu tuliopo, basi ndio sababu watu wanaishi wakifanya dhambi huku wakizifuata starehe zao binafsi. Tumaini la kweli la mwanadamu linapatikana katika Neno la injili ya maji na Roho, na ni Neno hili tu ndilo linaloweza kutupatia tumaini la kweli. Hata hivyo, ulimwengu huu ni ulimwengu ambao haumtafuti Mungu. Hivyo ni lazima uamini kwa moyo wako wote katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu Kristo kwa kuwa wewe ni mwenye dhambi na hivi punde utahukumiwa na Mungu kwa sababu ya dhambi zako. Kisha, utaweza kukombolewa toka katika hukumu ya Mungu ya kutisha. Biblia inamtia moyo kila mtu kuzitubu dhambi zake, kurudi kwa Mungu, na kuipokea injili ya maji na Roho.
Mwisho wa dunia ni wakati ambapo baada ya kuwa wamekula na kulala katika dhambi, watajikuta wakiingia katika ziwa la moto pasipo hata kutambua.
Watu ni lazima waupokee wokovu wao unaotolewa na Mungu, lakini pasipo kuifahamu injili ya maji na Roho watawezaje kukombolewa toka katika dhambi zao? Kila mtu ni lazima atambue kuwa ataipokea hukumu ya Mungu ya kutisha kwa sababu ya dhambi zake, na pia ni vema kila mtu atambue kuwa injili ya maji na Roho ni ukweli wa wokovu na Neno la baraka.
Biblia haijatueleza siku wala saa kamili ambapo mwisho wa dunia utatokea. Kitendo cha Mungu kuificha saa ambapo ulimwengu utafikia mwisho ni kitendo cha hekima ya Mungu. Ikiwa Mungu angelitufunulia saa ya siku ya mwisho, basi ni hakika kuwa kutufunulia huko kungeleta matatizo sana. Hii ndiyo sababu Mungu aliwaficha watu wasiijue siku ya hukumu. Lakini nyakati zilizopangwa na Mungu zitakapowadia, basi atakitimiza kila kitu, na hapo ndipo ulimwengu mpya utakapoanza.
Katika kifungu cha maandiko mwanzoni mwa sura hii, Mungu alisema, “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.” Hili Neno ni ahadi ya Mungu kwamba atawakomboa wenye haki toka katika yale mapigo saba ambayo yataujia ulimwengu huu baada ya kuuawa na kuifia-dini. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa atawaepusha watakatifu ili wasiuawe kwa kuifia-dini au kuteswa na Mpinga Kristo katika nyakati za mwisho. Idadi kubwa ya watu watakabiliana na hukumu ya kutisha ya Mungu kwa sababu ya kutoiamini injili ya maji na Roho na kwa kutopokea ondoleo la dhambi zao. Kwa matokeo hayo, roho zao zilizojaa dhambi zitangukia kuzimu. Lakini Mungu ataruhusu mauaji ya kufia-dini kwa watakatifu, kwa kuwa mauaji haya ndiyo yatakayowakomboa toka katika mapigo ya kutisha.
 

Je, Ni Aina Ipi ya Alama Ambayo Watu Wataipokea Katika Nyakati za Mwisho za Dhiki Kuu? 
 
Biblia inatueleza kuwa watu wataipokea alama yenye jina la Mpinga Kristo. Lakini Neno la Ufunuo linatueleza pia kuwa wale wanaoipokea alama ya Mpinga Kristo katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono yao ya kuume watatupwa katika ziwa la moto. Maana kwa kuipokea alama ya huyu Mpinga Kristo watakuwa wamegeuka na kuwa watumishi wa Shetani milele. Ziwa la moto limeandaliwa kwa wale walio na dhambi.
Kipindi cha neema ambapo watu wanaweza kuokolewa toka katika dhambi zao ndicho hiki kinachopita sasa. Biblia inasema kuwa idadi kubwa ya wafia-dini itainuka katika nyakati za mwisho. Kwa kuwa majina ya hawa wafia-dini yameandikwa katika Kitabu cha Uzima, basi wao wataweza kuikataa alama ya Mpinga Kristo na jina lake.
Mungu anatueleza kuwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wataangamia wote wakati huo. Watauawa kwa kuifia-dini kwa sababu ya kukataa kuipokea alama ya Shetani. Wale waliofanyika kuwa wenye haki hawapaswi kuyaogopa mauaji ya kuifia-dini ya nyakati za mwisho, bali wanapaswa kumshukuru Mungu kwa ajili ya Ufalme wa Milenia unaowangojea baada ya mauaji yao ya kuifia-dini.
Kwa kuwa kupokea alama ya Mpinga Kristo ni tendo la usaliti linalomkana Bwana, basi tunapaswa kulikataa tendo hilo. Sisi sote tunaweza kuinuka na kuwa wafia-dini kwa kuitunza imani yetu katika Mungu ili tuweze kumpatia Mungu utukufu. Bwana wetu ametueleza kuwa atawapatia wenye haki nguvu ya kuyashinda magumu.
 

Je, Kanisa la Mungu Liendelee Kuihubiri Injili ya Maji na Roho Hadi Lini? 
 
Je, Mungu ameturuhusu kuieneza injili ya maji na Roho kwa muda gani? Jibu ni hadi wakati tutakapouawa kwa kuifia-dini katika wakati wa Dhiki Kuu. Mungu ameufungua mlango kwa wenye haki ili kwamba waweze kuihubiri injili ya maji na Roho hadi wakati huo. Wenye haki wataendelea kuihubiri injili ya maji na Roho hadi wakati wa kuifia-dini utakapowafikia. Baada ya kuifia-dini hapo ndipo ulimwengu utakapofikiwa na mapigo ya kutisha.
Kwa sasa, wenye haki na wenye dhambi wanaishi wakiwa wamezungukwa na uoto mzuri wa asili uliotolewa na Bwana. Baada ya kuwa wameishaihubiri injili ya maji na Roho, basi wenye haki ni lazima waitunze imani yao ikiwa safi huku wakimsubiri Bwana hadi wakati wa Dhiki utakapowadia. Wenye haki wanatakiwa kulipalilia shamba la injili.
Katika nyakati za mwisho, yaani wakati tutakapokuwa tukilazimishwa kuipokea alama ya Mnyama, ni lazima tupambane na kuushinda ulimwengu kwa kutumia imani yetu katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Tunapouawa na Mpinga Kristo na kuifia-dini katika nyakati za mwisho, basi imani yetu itakuwa imeshinda. Maisha yote ya wenye haki yanamtegemea Bwana. Ikiwa wenye haki wanaamini katika Neno la Mungu, kwamba atawalinda katika saa ya kujaribiwa, na kisha wakaendelea kuihubiri injili hadi mwisho wa ulimwengu, basi ni hakika kuwa Mungu atawapatia maisha ya ushindi. Wenye haki ni lazima waihubiri injili ya wokovu wa kweli kila mahali leo hii na kesho.
Sisi sote ni lazima tukungojee kurudi kwa Bwana wetu na kisha tuwe waaminifu kwake maana thawabu ya Ufalme wa Milenia tunayoingojea inaletwa kwetu. Wakati Bwana atakaporudi hapa duniani, basi Ufalme wa Milenia utatolewa kwa wenye haki. Kisha wenye haki watavikwa utukufu wa Mungu pamoja na Bwana.
Lakini kwa sasa, ni lazima tuendelee kuihubiri injili ya maji na Roho tunapokuwa hapa duniani hadi wakati wa mwisho tutakaposhindwa kufanya hivyo. Injili inayowaokoa wenye dhambi, yaani injili ya maji na Roho ndiyo injili ya ukombozi wa kweli wa dhambi.
Baada ya kuwa wameishi hadi mwisho wa ulimwengu hali wakiihubiri injili ya maji na Roho, basi wenye haki watakutana na Bwana, watatawala kwa miaka elfu moja, na baada ya kuisha katika Ufalme wa Milenia, wataingia katika Ufalme wa Mungu na kuishi na Bwana milele. Ninamshukuru Bwana katika imani. Ni lazima tumshukuru sana Bwana kwa kutupatia tumaini hili.
 
 
Kanisa la Filadelfia Lilikuwa ni Kanisa Maalum Lililopendwa na Bwana, Ambalo Pamoja na Kuwa na Nguvu Kidogo Halikulikana Jina la Yesu na Lilifuata Mapenzi ya Mungu
 
Mungu alilipatia Kanisa hili la Filadelfia baraka zake maalum za kulindwa katika wakati wa majaribu. Baraka hii ni baraka ya ondoleo la dhambi, baraka ya kuishi katika Ufalme wa Milenia, na baraka ya kuwa warithi wa Ufalme wa Mungu milele. Wakristo wanaobakia kama wenye dhambi watafungiwa nje ya baraka za Mungu. Lakini wenye haki watatawala kwa miaka elfu moja.
Bwana atawainua watakatifu katika dunia hii kwa kupitia kuuawa kwao kwa kuifia-dini, na kisha atayashusha mapigo makubwa ya dhiki juu ya ulimwengu huu. Mungu atafanya hivyo ili kuweza kuwatambua wema kati ya waovu, na kisha awatahukumu na kuwaangamiza wenye dhambi. Mungu anawapenda wenye haki, hasa wale ambao wana nguvu kidogo lakini wanaendelea kuihubiri injili hadi mwisho wa ulimwengu. Watakatifu waliokuwa na imani kama hiyo na ambao ni sehemu ya makanisa ya jinsi hiyo, ni hakika kabisa kuwa walibarikiwa. Mungu alifurahishwa na watakatifu hawa wenye haki.
Mungu anasema kuwa atawapa thawabu wale wote wanaopambana na kumshinda Shetani kwa kuamini katika injili ya maji na Roho kwa mioyo yao yote.
Kuna Wakristo wengi hapa duniani wanaodai kumwamini Yesu lakini wakiwa bado wanadanganywa na Shetani. Kazi ya wokovu, iliyowakomboa wenye dhambi wote toka katika dhambi zao kwa kule kuja kwa Yesu hapa duniani ilitimizwa kwa matendo yake mawili ya haki. Imani katika matendo haya mawili ya wokovu inaamini kuwa Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake katika Mto Yordani, na kwamba aliikamilisha hii kazi ya wokovu kwa kuzibeba dhambi hizo hadi Msalabani, akahukumiwa kwa ajili ya dhambi hizi kwa damu yake binafsi. Hii ni injili ya wokovu, yaani injili ya ondoleo la dhambi ambayo imewaokoa wenye dhambi.
Wale wanaopungukiwa imani “ni wale wanaodai kuwa hawana dhambi pasipo kuamini katika ubatizo wa Yesu.” Imani ya jinsi hiyo ni ya uongo. Kwa upande mwingine, baadhi ya watu wanadai kuwa hakuna mtu yeyote anayempenda Yesu kama wao wanavyofanya lakini wakati huo huo wanajielezea wao wenyewe kuwa ni wenye dhambi. Lakini Bwana wetu hamruhusu yeyote zaidi ya wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho kuingia Mbinguni. Haandiki majina ya wenye dhambi katika Kitabu chake cha Uzima. Ni wale tu wanaoamini katika injili ya maji na Roho ndio ambao majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima.
Wokovu toka katika dhambi uliotolewa na Mungu haupatikana “kwa kile anachotenda mtu,” bali unapatikana kwa “kile mtu anachoamini.” Katika imani hii, suala la kwanza ni kuamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wetu, na pili ni kuamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani kama matendo makamilifu kwa ajili ya wokovu wetu. Pia ni lazima tuamini katika ufufuo wa Kristo na kuja kwake mara ya pili.
Mathayo 7:21-23 inasema, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” Kwa nini Yesu atawakana watu hawa? Kwa sababu wale walio na dhambi hawawezi kuandikwa majina yao katika Kitabu cha Uzima. Siku hizi, kuna watu wengi wanaodai kumwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao, lakini wengi wao hawaamini juu ya ule ubatizo ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana.
Kwa sababu hiyo, majina yao hayajaandikwa katika Kitabu cha Uzima. Hata hivyo, wenye dhambi hawa wanajaribu kuingia katika Ufalme wa Bwana hali wakiwa wamebeba dhambi zao. Hivyo hawawezi kuingia katika ufalme huo. Baadhi ya watu ni majasiri sana kiasi kuwa wanaamini kuwa wanaweza kuingia Mbinguni hata kama wana dhambi. Watu wa jinsi hiyo hawaamini juu ya wokovu uliotolewa na Mungu, bali wanaamini katika toleo lao binafsi la kiimani lililoundwa kwa majivuno. Wale ambao imani yao ni potofu hawaamini kuwa Yesu ni Mungu, wala hawauamini ukweli kuwa Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake, pia hawaamini kuwa Yesu alizibeba dhambi hizi zote kwenda Msalabani. Watu hawa wanamchukulia na kumwamini Yesu kama miongoni mwa wenye hekima wakuu wanne ulimwenguni. Watu wa jinsi hiyo ni wenye dhambi hata kama watamwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao. Hata hivyo, Bwana ana kitu cha kuweza kuwapatia wenye dhambi hawa. Bila shaka unaweza kujiuliza kuwa “ni kitu gani hicho?” Kwa kweli ni kuzimu inayowangojea!
Sisi wenye haki, ambao dhambi zetu zimesamehewa, ni lazima tupambane na kuwashinda waongo kwa kutumia injili ya maji na Roho hadi mwisho wa ulimwengu. Kile ambacho wenye haki wanakiamini si ukweli unaoweza kuharibika. Haijalishi mtu anavyotusema, sisi hatuwezi kukata tamaa kuhusiana na imani yetu juu ya injili ya kweli ambayo kwa hiyo tunamwamini Bwana hadi siku ile Bwana atakaporudi. Neno la kweli ambalo wenye haki wanaliamini limepokelewa toka kwa Mungu mwenyewe. Limeshuhudiwa na Neno la Mungu. Mungu mwenyewe alilisema Neno hilo. Mungu mwenyewe aliahidi ondoleo la dhambi zetu. Wenye haki waliokolewa toka katika dhambi zao zote na wakafanyika kuwa wakamilifu kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu na Msalaba wake. Je, kuna jambo lolote la maana au la muhimu ambalo wenye dhambi wanasema kuhusu sisi? Hakuna kabisa! Wenye haki ni lazima waitunze imani yao katika injili ya maji na Roho kwa kuamini katika Neno la Mungu.
Sasa ni wakati wa majanga ya kiasili, na si muda mrefu vita ya nyuklia itakuja hapa duniani. Na majanga ya kiasili yamepangwa ili kujitokeza kwa ukubwa zaidi. Watumishi wa Mungu ni lazima waone vizuri kile kinachoujia ulimwengu huu na kisha wahubiri juu ya hicho. Ni lazima utambue kuwa mwisho wa ulimwengu unaweza ukatokea kwa kushtukiza mara moja. Wakati vita ya nyuklia itakapoanza hapa ulimwenguni, basi majanga ya kiasili yatafikia kiwango cha juu kisichotazamiwa, na alama ya Mnyama itakuwa ikisukumwa kwetu—yaani wakati ambapo kuuawa kwetu kwa kuifia-dini na ufufuo, na kujengwa Ufalme wa Milenia utakapokuja—huu ndio wakati ambapo Kristo atarudi hapa duniani. Mambo yote yanatokea na yanatimizwa na Bwana.
Bila kujalisha anachosema mtu, sisi ni lazima tuamini katika Neno la Mungu hadi mwisho wa ulimwengu na kisha tuitunze imani hii. Bila kujali magumu yaliyopo, tunapomfuata Bwana ni lazima tuitunze na kuieneza imani yetu katika injili ya maji na Roho.
Hebu tuishi maisha yetu hali tukiitumainia Siku ya Bwana. Hebu tuwaandae wenye dhambi kwa ajili ya msamaha wao wa dhambi kwa injili ya maji na Roho! Ninaamini kuwa Bwana wetu amekwishaandaa baraka zote za Mbinguni zilizohifadhiwa kwa ajili ya wenye haki na anatusubiri. Ni lazima tujiandae kabla ya siku ya ufufuo wa wafu na ya kubadilishwa kwa watakatifu haijafika. Acha kujilaumu jinsi maisha yako yalivyo matupu, na badala yake amini katika injili ya maji na Roho.
Unapokuwa umeufahamu ukweli wa injili, inawezekanaje basi ukachagua kuishia kuzimu kwa kukataa kuuamini ukweli huo? Badala ya kuangukia katika kukata tamaa kwa sababu ya utupu wa maisha, ni lazima tujiandae kwa ajili ya Ufalme wa Milenia kwa kukombolewa toka katika dhambi zetu zote kwa kupitia imani katika injili ya maji na Roho. Baada ya kuyaishi maisha yetu hali tukiwa na imani kama ile ya Kanisa la Filadelfia iliyopongezwa na Mungu, basi ni hakika kuwa tutakutana na Bwana wetu mawinguni! Halleluya!