Search

Проповіді

Somo la 11: Maskani

[11-3] Yahwe Mungu Aliye Hai (Kutoka 34:1-8)

Yahwe Mungu Aliye Hai
(Kutoka 34:1-8)
“Kisha BWANA akamwambia Musa, ‘chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza ulizozivunja. Nawe uwe tayari asubuhi, na asubuhi ukwee juu katika Mlima wa Sinai, nawe hudhurisha nafsi yako kwangu huko katika kilele cha mlima. Asikwee mtu pamoja nawe, wala asionekane mtu awaye yote katika huo mlima; wala kondoo na ng’ombe wasilishe mbele ya huo mlima.’ Naye akachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza. Kisha Musa akainuka mapema asubuhi naye akakwea katika Mlima Sinai kama BWANA alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake. BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita mbele yake, akatangaza, ‘BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mweye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe, mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.’ Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu.”
 

Tunahitaji Kuchunguza Juu ya Mungu Tunayemwamini
 
Hebu tuanze kwa kuangalia Kutoka 3:13-16: “Musa akamwambia Mungu, ‘Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli na kuwaambia, ‘Mungu wa baba zenu amenituma kwenu,’ nao wakaniuliza ‘jina lake ni nani?’ Niwaambie nini?’Mungu akamwambia Musa, ‘MIMI NIKO AMBAYE NIKO;’akasema, ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli, ‘MIMI NIKO amenituma kwenu.’’ Tena Mungu akamwambia Musa, ‘Waambie wana wa Israeli maneno haya: ‘BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.’ Enenda ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, ‘BWANA Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, ‘Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri.’”
 


Mungu Yahwe Ni Nani?

 
Jina la Bwana katika Kiebrania ni Yahwe au Yhwh, na kwa desturi jina hili pia huitwa Yehova, jina Yahwe linamaanisha Yeye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe. Kwa maneno mengine, Mungu si sehemu ya uumbaji, bali ni yeye anayeishi kwa uweza wake mwenyewe, ndiye Muumbaji aliyeumba ulimwengu wote na vyote viujazavyo.
Hebu tuangalie Kutoka 6:2-7: “Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, ‘Mimi ni BWANA. Nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu BWANA sikujulikana kwao. Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. Na zaidi ya hayo nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. Basi waambie wana wa Israeli: ‘Mimi ni BWANA, nami nitawatoa ninyi mtoke nchi ya mizigo ya wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa, na kwa hukumu kubwa. Nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu kwenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke nchi ya mizigo ya wamisri.’”
Aya ya 3 hapo juu inasema, “Nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.” Katika toleo la Biblia ya Mfalme Yakobo, ibara isemayo “kwa jina langu BWANA” imeandikwa hivi “kwa jina langu YEHOVA.” Neno la kiebrania YEHOVA linamaanisha “yeye aliye hai” au “jina sahihi la Mungu mmoja wa kweli.” Hapo kabla Mungu alilifanya jina lake Yehova lisifahamike kwa wanadamu. Hivyo, watu kwa wakati huo walimuita Mungu tu. Lakini sasa, ili kuwaokoa watu wa Israeli, Mungu alipenda jina lake Yehova kujulikana kwa watu wote wa ulimwengu huu. “Mimi ni Yehova. Mimi ni Yahwe. Mimi niko ambaye niko, mimi ndiye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe.” Hivyo Mungu alipenda aweze kufahamika.
Mungu ni yeye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe, “Mungu wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo.” Amekuwepo akiishi hata kabla ya zama za kale, hata kabla ya mwanzo wa kila kitu. Kwa maneno mengine, Mungu anaishi na uwepo wake ni wa milele. Mungu aliruhusu kuwa watu wa Israeli, wana wa Ibrahimu, wafanywe watumwa huko Misri kwa miaka 430, kisha akaahidi kuwa atawakomboa toka katika utumwa na kuwaongoza katika nchi ya Kanaani. Kama alivyokuwa ameahidi, Mungu Yehova alionekana baada ya miaka 430 na akamwamuru Musa kuwakomboa wana wa Israeli toka katika mateso ya Farao. “Mimi ni Yehova. Mimi niko ambaye niko, Mungu wenu. Waruhusu watu wangu waende.” Ni kwa ajili ya watu wake, Mungu alijifunua mwenyewe kwa Musa, na akamwamuru Farao kuwaruhusu watu wake kuondoka, hii ni kwa sababu Yehova Mungu aliyafahamu mateso ya wana wa Israeli. Kwa sababu alifahamu kuwa watu wake walikuwa wakiugua chini ya mateso yao, Mungu akasema atawakomboa toka katika utumwa wao.
Baada ya miaka 430 tangu alipoitoa ahadi yake kwa Ibrahimu, Mungu alikuja kwa watu wa Israeli na akajidhihirisha kwao. “Mimi ni Yehova. Mimi ni Mungu. Nimekuja kuitimiza ahadi niliyomwapia Ibrahimu, baba yenu, ya kuwa nitawaongoza wana wake kutoka Misri kwenda katika nchi ya Kanaani. Pia ninayafahamu mateso yenu yote. Sasa nenda kwa Farao na umwambie hivyo.” Kuwa hivi ndivyo Mungu Yehova alivyosema.
Ni lazima tutambue kuwa kwa kweli Mungu ndiye Mungu wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo. Mungu pia ni Mungu wetu, Mungu wa mimi na wewe. Je, basi jina lake ni nani? Jina lake ni Yahwe, maana yake Yeye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe. Mungu amekuwepo hata kabla ya uumbaji wa ulimwengu, kama yeye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe, ambaye uwepo wake hautokani na mtu au kitu chochote, bali unaotokana na yeye mwenyewe.
 

Ni Lazima Tufahamu Maana ya Jina la Mungu
 
Ni muhimu kwamba tufahamu na kuamini kuwa Mungu ndiye yeye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe, ambaye ndiye aliyetuumba, anayetutawala, na aliyetukomboa toka katika dhambi zetu. Ni lazima tumwamini Mungu Yahwe kuwa ni Mungu wetu sahihi, kwa sababu huyu Mungu Yahwe ndiye kweli aliyeumba ulimwengu wote, na anaendelea kuwepo hata sasa. 
Kama vile watu wa Israeli, wewe na mimi pia tunamwamini Mungu, na tumepokea pia maagizo yake mbele ya uwepo wake. Kama vile watu wa Israeli walivyoshindwa kuifuta Sheria yote, sisi nasi tulishindwa kuishi kwa Sheria. Kwa hiyo, kwa sababu ya dhambi zetu mbele za Mungu, tulikuwa ni viumbe ambao tusingeweza kuikwepa bali kuwa chini ya hukumu ya kutisha ya dhambi. Kwa maneno mengine, kwa sababu ya dhambi zetu tusingeweza kukwepa hukumu toka kwa Mungu kwa sababu ya dhambi zetu.
Na hii ndiyo sababu kuwa kila mmoja wetu ni lazima atoe mwanasadaka wa kuteketezwa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi. Ili tuweze kuokolewa toka katika dhambi zetu, tulipaswa kumpa Mungu Baba malipo ya upatanisho yaliyo sawa na uhai wetu binafsi, hali tukiwa na imani. Kwa hakika tungelipaswa kutoa sadaka ya kuteketezwa iliyo sawa na uhai wetu ili kuiridhisha hasira ya Mungu yenye haki na kuufunua upendo wa Mungu wenye huruma. Amani kati yetu wanadamu na Mungu inaweza kupatikana kwa kutoa upatanisho halisi wa uhai kwa dhambi zetu. Ni kwa imani tu ndipo tunapoweza kukombolewa toka katika dhambi zetu zote na adhabu.
Kwa kuwa hivi ndivyo ilivyo, basi kila tunapokwenda mbele za Mungu, tunapaswa tukiri kwa sababu ya dhambi tulizozifanya mbele yake, kiasi kwamba hatuwezi kukwepa bali kuhukumiwa kwa ajili ya dhambi hizi. Tunapomwamini Mungu kama Mwokozi wetu ni lazima tutambue na kukiri kuwa tumefungwa na kuzimu kwa sababu ya dhambi zetu, hivyo tunapaswa kumwamini Masihi aliyelipa malipo ya dhambi zetu na aliyetukomboa toka katika hukumu kama Mwokozi wetu. Tunapokwenda mbele za Mungu, ni lazima tuamini katika ubatizo na damu ya Yesu Kristo, ambaye ni sadaka ya kuteketezwa ya dhambi zetu, tumwamini kuwa ni Masihi, na tumtambue hivyo. Ni lazima tukiri kuwa sisi sote tumekuwa wenye dhambi mbele za Mungu kwa sababu ya kushindwa kwetu kuyatii maagizo yake, na ni lazima tuamini kuwa Yesu Kristo Masihi ametukomboa toka katika dhambi zetu.
Ni lazima tutambue kuwa hatuwezi kukwepa bali kuwa chini ya adhabu ya Mungu ya dhambi. Hivyo, kwa kuikiri hali yetu ya dhambi, tulistahili kupokea baraka ya ondoleo la dhambi ambayo Mungu ametupatia, na tuliweza kuujenga msingi wa imani inayoweza kuzikusanya rehema za Mungu na kupokea ondoleo la dhambi zake.
Ili kutufanya sisi kuwa watoto wake binafsi, Mungu alituumba sisi katika sura yake, lakini alituruhusu kuzaliwa katika udhaifu. Kama wazawa wa Adamu, sote tunazaliwa tukiwa wenye dhambi, lakini hii ni nafasi ya Mungu ya kina kutufanya sisi kuwa wana wake.
Tulikuwa ni viumbe ambao tusingeweza kukwepa bali kuhukumiwa kwa dhambi zetu, lakini ili kuyatimiza mapenzi yake, Mungu alimtuma Mwanawe kuja kwetu, na ametusamehe dhambi zetu zote. Yesu, Mwana wa Mungu, aliupokea ubatizo wake na akafa Msalabani kwa unyenyekevu kufuatana na mpango wa Mungu. Hivyo, Mungu Yehova ametupatia maisha mapya kwetu sisi tunaoamini kuwa dhambi zote za ulimwengu zilipitishwa kwa Mwanae kwa ubatizo toka kwa Yohana, na kwamba ametuokoa toka katika dhambi zetu zote kwa damu yake Msalabani, na kwamba alizibeba hukumu zote za dhambi zetu.
Ubatizo wa Yesu na damu yake vilikuwa ni sadaka ya kuteketezwa ambavyo vimetosha kuliko kawaida ili kuturuhusu sisi pale tunapoamini, kupokea maisha mapya, kuokolewa toka katika dhambi zetu zote, na kufanyika wana wa Mungu. Ni lazima tuokolewe toka katika dhambi zetu zote kwa kuamini na kwa imani yetu katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Ni lazima tuwe na aina ya imani inayoturuhusu kufanyika watu wa Mungu. Ni ukweli kamili, na ni hakika kuwa walio na imani ya jinsi hiyo ndio wanaoweza kufanyika watu wa Mungu.
 

Miungu Yote ya Dini za Ulimwengu Huu ni Viumbe Vilivyotengenezwa na Mwanadamu tu. 
 
Ukimuacha Yehova, Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu, miungu mingine yote ni miungu ya kidunia tu iliyotengenezwa na mwanadamu mwenyewe. Hakuna kitu chochote katika ulimwengu huu ambacho kimekuwepo au kuishi kwa uwezo wake binafsi, bali ni Mungu tu. Na hii ndiyo sababu Mungu Yahwe alisema, “Mimi niko ambaye Niko.”
Je, yupo kweli yeyote anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe? Budha alizaliwa toka katika tumbo la mama yake, na kwa jinsi hiyo yeye ni kiumbe tu wa Mungu. Ndivyo ilivyo kwa Konfusius, na pia kwa Muhammad, kwa kuwa wote walizaliwa na wazazi wao, na kwa hiyo nao ni viumbe tu walioumbwa na Mungu. Sanamu ya Budha ambayo imetengenezwa na kuundwa na wafuasi wake pia ni kitu kilichoumbwa na mwanadamu mwenyewe, sanamu hiyo imeundwa kwa mawe au metali ambazo Mungu mwenyewe aliziumba. Kila kitu kuanzia jua, mwezi, nyota, maji, hewa, na kundi la nyota na sayari za ulimwengu vyote viliumbwa na Mungu. Hakuna kitu chochote katika ulimwengu huu ambacho hakikuumbwa na Mungu. Pia hata malaika, na viumbe wa kiroho waliumbwa na Mungu.
Ni Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Yakobo tu, ambaye tunamwamini, ndiye Mungu Yahwe, ambaye anaishi kwa uwezo wake mwenyewe. Mungu Yahwe hakuumbwa na yeyote. Yeye tu ndiye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe, yeye tu ndiye muumbaji wa ulimwengu wote, ni yeye tu ndiye aliyetuumba mimi na wewe. Ni Mungu Yahwe tu aliyepanga katika mapenzi yake kutuokoa toka katika dhambi zetu na kutufanya kuwa watu wake mwenyewe.
Ni kwa sababu Mungu alipanga kwamba tuzaliwe hapa duniani hali tukilia na kurudi kwake tukiwa mikono mitupu, na ni kwa sababu ya mpango huu kwamba ameturuhusu kuteseka katika ulimwengu huu, ili tusiweze kuwa na namna ya kujisaidia zaidi ya kumtafuta na kukutana na Mungu.
Tunaposema kwamba tunamwamini Mungu, ni lazima tukiri kuwa sisi ni aina ya viumbe ambao, kwa sababu ya dhambi zetu na kushindwa kwetu kuzifuata sheria za Mungu, hatuwezi kukwepa bali tutakutana na adhabu ya kifo, kuzimu, na mateso ya kutisha mbele za Mungu. Kabla hatujamwamini Yesu Kristo Masihi kuwa Mwokozi wetu, ni lazima kwanza tujitambue kuwa sisi ni wenye dhambi ambao hatuwezi kukwepa bali kuikabili hukumu ya kutisha ya dhambi na kuwa tutatupwa kuzimu.
 


Mungu Yahwe ni Mwenye Maarifa yote na ni Mwenyezi

 
Ni Mungu tu ambaye ni Mwenyezi na mwenye maarifa yote ambaye alituumba sisi na anayetawala ulimwengu wote. Baada ya kulitambua hili, basi ni lazima tukiri mbele za Mungu jinsi tulivyo wenye dhambi—hii ni kusema kuwa, ni lazima tukiri kwamba kwa sababu ya dhambi zetu hatuwezi kuikwepa bali tutaikabili hasira ya kutisha ya Mungu. Na ni lazima tuuamini ukweli kuwa kwa kumwamini Mwanakondoo wa Mungu aliyekuja kutukomboa toka katika dhambi zetu zote, na kuzipitisha dhambi zetu zote katika mwanasadaka huyu wa kuteketezwa kwa kuilaza mikono yetu katika kichwa chake, matatizo yetu yote ya dhambi yametatuliwa. Ni sisi ambao kwa kweli tunatakiwa kuhukumiwa na kufa kutokana na dhambi zetu, lakini kwa sababu mwanasadaka huyu wa kuteketezwa alizichukua dhambi zetu zote kwa ubatizo wake, dhambi zetu zimeoshwa kabisa. Ni lazima tuuamini ukweli huu. Ni lazima tutambue kuwa kupitia sadaka hii ya kuteketezwa, Mungu Mwenyezi, ambaye kwake hakuna kisichowezekana, kwa hakika ametuokoa sisi ambao tusingeweza kukwepa bali kufungwa kuzimu kutokana na dhambi zetu. Watu wanaoamini hivyo ni waamini wa kweli wa Yesu Kristo Masihi.
Kwa kweli ni makosa kumwamini Masihi pasipo ufahamu na utaratibu mzuri. Tunaposema kuwa tunamwamini Mungu, imani yetu ni lazima ithibitishwe katika msingi mzuri wa kibiblia. Na ni lazima tuufanye msingi wa kwanza na wenye nguvu wa ukweli juu ya Neno lake, linalosema, “Mimi niko ambaye niko. Mimi ni Yehova.”
Watu wa Israeli walishindwa kufuata Sheria ambayo Mungu aliwaamuru kuifuata. Amri ambazo Mungu aliwapatia waisraeli pia zilitolewa kwetu sisi tunaoishi katika zama za sasa. Ikiwa kweli unapenda kumwamini Mungu, na kama kweli unapenda kuwa mwana wa Ibrahimu kwa imani yako, ni lazima utambue kuwa Mungu amewapatia waisraeli sheria 613 na pia ametupatia na sisi pia sheria hizohizo. Pia ametoa sheria hizo kwa kila mmoja katika ulimwengu huu, na kwa ulimwengu mzima. Na ni lazima tutambue kuwa sisi pia tumeshindwa kuzifuata amri za Mungu, kama vile waisraeli walivyoshindwa, na kwa jinsi hiyo tumepangiwa kifo kwa kuwa “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23).
Ni lazima tuamini kuwa Mungu ametusamehe dhambi zetu kwa ukweli wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Ili kufanya hivyo, ni lazima tuutafute ukweli wa wokovu, ambao kwa huo Bwana wetu ametuokoa toka katika dhambi zetu na adhabu ya dhambi zetu.
Japokuwa tumeshindwa kuzifuata sheria makini za Mungu, ikiwa hatutambui kuwa sisi ni wenye dhambi wabaya, na ikiwa hatukiri kuwa tunastahili kuhukumiwa kwa dhambi zetu, basi hatutaweza kamwe kumwamini Masihi. Ikiwa watu wangekuwa wanaamini kuwa wanaweza kuingia mbinguni hata kama wakibaki kuwa ni wenye dhambi, ilhali Mungu amekwisha rekodi dhambi zao katika Kitabu cha Hukumu, basi watu wa jinsi hiyo wangekuwa wanazibadili Sheria za Mungu wao wenyewe, na kufanya dhambi ya kuliitia jina la Mungu bure. Watu wa jinsi hiyo hawawezi kamwe kuokolewa toka katika dhambi zao. Watahukumiwa milele kwa ajili ya dhambi zao, na wataadhibiwa kwa hukumu ya kuzimu, bila kujali kuwa wanamwamini Mungu au la, kwa maana hawajamtambua Mungu. Watu hawa ni lazima watubu mara moja na wabadilike toka katika hali ya kutokuamini.
Hata katika kipindi hiki, Mungu yupo katika mioyo yetu, na anaishi kwa uwezo wake mwenyewe katika maeneo haya yote. Na anafahamu kila kitu kutuhusu sisi.
Japokuwa Mungu anaishi, wapo watu ambao hawamwamini, na baadhi yao wanamdhihaki Mungu. Lakini sisi sote tunahitaji sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya dhambi zetu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Mungu kuwafanya waisrali kutoa sadaka ya upatanisho kwa sadaka zao za kuteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania, kwa mujibu wa njia ya wokovu ambavyo Mungu aliiratibu.
Kwa hakika Mungu ndiye anayeishi kwa uwezo wake mwenyewe. Ndiye aliyekuwepo tangu mwanzo, na ndiye aliyepo hata sasa. Ni Mungu aliye hai, aliyeonekana, na aliyeongea kwa baba zetu wa kiimani hapo kale, ndiye aliye hai, anayeonekana, na anayeongea nasi sasa, anafanya kazi miongoni mwetu, anatuongoza, na anayatawala maisha yetu.
 

Ukweli Ambao Ni Lazima Tusiusahau
 
Pamoja na kuwa tumeokolewa, kuna kitu kimoja ambacho ni lazima tusikisahau. Ni kwamba, japokuwa tusingeweza kukwepa bali tungehukumiwa milele, kwa ubatizo wake na kwa kuimwaga damu yake Msalabani, Bwana wetu ametukomboa sote toka katika hukumu ya jinsi hiyo ya dhambi zetu. Hadi siku ile tutakaposimama mbele za Bwana wetu, kwa kweli tusiusahau kamwe ukweli huu na wakati wote tuuamini katika mioyo yetu. Ni lazima tuuamini hata pale tutakapokuwa katika Ufalme wa Mungu tukimsifu Mungu. Ni lazima tumshukuru Mungu kwa kuturuhusu sisi ambao tusingeweza kukwepa laana ya milele na kuhukumiwa kwa ajili ya dhambi zetu, kumwamini Bwana wetu kuwa ni Mwokozi na kwa kutupatia uzima wa milele.
Ni lazima tuitambue injili ya maji na Roho milele. Kitu gani kitatokea ikiwa hatutakiri kuwa tunastahili kufungwa katika hukumu ya milele kwa ajili ya dhambi zetu? Hakutakuwa na sababu ya sisi kumsifu Mungu. Kwa kweli Mungu ametuokoa sisi, viumbe wadhaifu, ambao tusingeweza kukwepa hukumu ya Mungu milele kwa ajili ya dhambi zetu. Hii ndiyo sababu ni kwa nini tunalazimika kumwamini na kumsifu Bwana—kwa sababu Bwana wetu aliupokea ubatizo na akamwaga damu yake kwa ajili yetu. Na hii ndiyo sababu kuwa wewe nawe unapaswa kuamini, pia hii ndiyo sababu kuwa sisi sote tunapaswa kuihubiri injili ya maji na Roho. Wote wanaoamini katika ubatizo ambao Yesu aliupokea na damu ambayo aliimwaga kwa ajili ya dhambi zao wana mioyo ambayo inamsifu Mungu. Kwa sababu Bwana amewaokoa toka katika dhambi zao na kifo, wao nao wanamsifu Mungu kila siku kwa imani yao.
Tatizo ni kuwa baadhi ya watu wamemuelewa vibaya Yesu. Ufahamu wao juu ya Yesu upo upande mmoja na nusu yake hauna kitu. Hawa ni aina ya watu ambao dhamiri zao zimeharibika, watu ambao hawatambui kuwa wanafanya dhambi hata pale ambapo wamezungukwa na aina zote za dhambi. Wale wote wanaotenda dhambi lakini bado hawatambui kuwa hiyo ni dhambi—basi watu wa jinsi hiyo ni wenye dhambi.
Japokuwa sisi ni viumbe dhaifu ambao hatuwezi kujisaidia bali tunatenda dhambi, ni lazima tuzikiri dhambi zetu kila wakati tunapozifanya, na ni lazima tuuthibitishe ubatizo wa Bwana wetu na damu yake Msalabani—na hii ndiyo injili ya maji na Roho. Hivyo kwa kweli tunakiri kuwa sisi hatuwezi na ni wenye dhambi mbele za Mungu. Na kwa kuiamini injili ya maji na Roho tunaweza kupumua kwa ahueni. Kwa hakika, kwa kuiamini injili ya maji na Roho, tumepata amani katika mawazo yetu.
Ninapozungumzia juu ya kutokuwa na dhambi, haimaanishi kuwa hatuwezi kuzitambua dhambi zetu hata pale tunapozitenda. Haimaanishi kuwa wale wanaoiamini injili ya maji na Roho hawahitaji kuzitambua dhambi zao kuwa ni dhambi. Japokuwa kwa hakika tumeokolewa toka katika dhambi zetu zote, bado tunazitambua dhambi ambazo tunazifanya jinsi zilivyo—kuwa ni dhambi zetu. Kitu ambacho hatupaswi kusahau ni kuwa pamoja na kuwa tusingeweza kukwepa hukumu ya milele kwa sababu ya dhambi zetu, Bwana wetu ametuokoa sisi toka katika dhambi zetu zote na adhabu ya dhambi kwa ubatizo wake, damu yake Msalabani, na kwa ufufuko wake. Tusisahau kamwe kuwa, Bwana wetu ametuokoa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, na tunapaswa kuamini na kumtukuza Mungu kwa hilo. Ni lazima tukumbuke jinsi ambavyo tulikuwa hapo mwanzo. Kumbuka kuwa wakati mmoja tulikuwa viumbe dhaifu ambao tusingeweza kukwepa hukumu ya milele kwa sababu ya dhambi zetu. Na ni lazima tuutukuze wokovu wa ondoleo la dhambi ulitolewa na Mungu, na tumshukuru kila siku kwa neema yake kuu ya wokovu. Hii ndiyo imani ya mwamini yeyote wa injili ya maji na Roho.
 


Mungu Yahwe Yuko Hai Hata Sasa

 
Kama vile Mungu alivyokuwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo, ndivyo alivyo sasa Mungu wangu na Mungu wako. “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali ni Mungu wa amani” (1 Wakorintho 14:33). Yeye si Mungu wa wakristo wenye matendo ya kujifanya na kujionyesha, lakini yeye ni Mungu wa wao wanaoamini katika injili ya maji na Roho. Sisi tunayo imani inayoamini katika Neno la Mungu na tunamtii Mungu kwa kusema “ndiyo.” Mungu ni Mungu wetu. Pale anapotueleza, “Umepangiwa kuzimu,” sisi tunamwambia, “Ndiyo, uko sahihi.” Pale anapotuambia, “Utaendelea kufanya dhambi hadi siku ile utakapokufa,” basi tunamwambia tena, “Ndiyo, uko sahihi.” Na anapotuambia, “Lakini kwa kweli nimewaokoa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa,” bado tunaweza kusema pia, “Ndiyo, uko sahihi.” Hivyo basi, kwa kweli tumefanyika wana wa Mungu ambao tunamtii kila wakati kwa kusema “ndiyo.” Ninamshukuru Mungu wetu kwa neema yake kwamba ametuokoa kwa injili ya maji na Roho.
Ni lazima tuamini na kutambua katika mioyo yetu kuwa Bwana wetu kwa hakika ametuokoa toka katika dhambi zetu zote kupitia maji, damu, na Roho, na kwa hiyo ametufanya sisi kuwa watu wa Ufalme wa Mungu. Mpe Bwana shukrani kwa kuamini kuwa injili ya maji na Roho ni zawadi ya wokovu ambayo Mungu amekupatia.
Ninamsifu Mungu daima kwa imani yangu kwa kuniokoa milele, mimi ambaye nisingeweza kukwepa kifungo cha milele huko kuzimu kwa sababu ya dhambi zangu, ameniokoa kwa injili ya maji na Roho. Hali tukikumbuka kuwa sisi sote tulikuwa watu wa shaba—maana yake, tusingeliweza kuikwepa hukumu ya Mungu—hivyo hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kumsifu Mungu kwa ukombozi wetu toka katika dhambi, kwa kutuokoa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Na ni lazima tumshukuru Mungu kwa kuuamini ukweli wa injili uliofichika katika nyuzi hizi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa.
Ni Mungu Yahwe tu ambaye ndiye Mungu wa wanadamu wote. Na amefanyika Mungu mwokozi wa wanadamu wa kabila zote. Sisi sote ni lazima tumwamini Mungu Yahwe kuwa ni Mungu wetu.