Search

Проповіді

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 7-1] Utangulizi Kwa Sura ya 7

Kwa kuutambua ukweli kuwa kabla ya ukombozi wake mwili wake ulikuwa umehukumiwa kifo na Sheria ya Mungu, basi ndio maana Mtume Paulo alilifanya ungamo lake kwa kuamini kuwa alikuwa ameifia dhambi katika Yesu Kristo. Kabla hatujakutana na haki ya Mungu—yaani kabla hatujazaliwa upya—sisi ambao tunamwamini Kristo tulizoea kuishi chini ya himaya na laana ya Sheria. Hivyo, ikiwa tusingekutana na Yesu ambaye ametuletea haki ya Mungu basi Sheria ingeendelea kututawala. 
Paulo aliongelea juu ya mambo ya kiroho ambayo hayawezi kueleweka kirahisi katika hali ya mwili—yaani, wale ambao wameifia dhambi hawapo tena chini ya himaya ya dhambi kama ambavyo mwanamke aliyefiwa na mume wake jinsi alivyo huru toka katika majukumu yake kwa mumewe. Kifungu hiki kinaweza kuonekana kuwa ni rahisi lakini ni kifungu muhimu sana cha kiroho. Kina maanisha kuwa wale ambao hawajakutana na haki ya Mungu, kwamba wanapenda au hawapendi, basi ukweli ni kuwa watu hao wana bahati mbaya ya kuishi chini ya laana ya Sheria. Hii ni kwa sababu watu hao hawajalitatua tatizo la dhambi zao. 
Warumi 6:23 inatueleza kuwa “mshahara wa dhambi ni mauti,” kifungu hiki kinaamisha kuwa dhambi itapotea pale tu mshahara wake utakapokuwa umelipwa. Ikiwa mtu anamwamini Yesu lakini bado haifahamu haki ya Mungu iliyotolewa na Yesu, basi mtu wa jinsi hiyo bado anaishi katika dhambi na ni lazima aulipe mshahara wa dhambi. Hii ndio sababu tunapaswa kukutana na haki ya Mungu kwa kupitia Yesu Kristo. Ni kwa kuipokea haki ya Mungu tu ndipo tunapoweza kuwa wafu kwa dhambi zetu, kuwekwa huru toka katika Sheria, na kisha kuolewa na Bwana harusi wetu mpya Kristo Yesu. 
Tunaweza kuipata haki ya Mungu kwa kupitia Yesu Kristo, lakini pasipo kuamini katika haki hii ya Mungu basi hakuna mtu anayeweza kuwekwa huru toka katika Sheria. Njia pekee ya kujitoa toka katika laana ya Sheria ni kufahamu na kuamini katika haki ya Mungu. Je, umeipata haki hii ya Mungu kupitia kwa Yesu? Ikiwa bado haujaipata, basi sasa ni wakati wako wa kuiacha haki yako binafsi na kisha kurudi kwa unyenyekevu katika Neno la Mungu. 
 

Kuelekea Kwa Kristo Baada ya Kuifia Dhambi 
 
Paulo aliwaambia wapendwa huko Rumi kuwa, “Ninyi pia mmefanyika wafu kwa ile sheria kwa kupitia mwili wa Kristo.” Ni lazima uwe na ufahamu sahihi juu ya lile neno lisemalo ‘mmefanyika wafu kwa ile sheria kwa kupitia mwili wa Kristo.’ Hakuna yeyote anayeweza kwenda kwa Kristo pasipo kuwa mfu kwa dhambi kwa kupitia mwili wa Kristo. Kwa maneno mengine, dhambi zetu ni lazima zife pamoja na mwili wa Yesu Kristo. Hii inawezekana tu wakati mtu anapoamini katika ubatizo wa Yesu alioupata kwa Yohana pamoja na kifo chake Msalabani. 
Tunaweza kuifia dhambi pamoja na Kristo kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu alioupokea toka kwa Yohana. Kwa sababu Yesu alikufa hali akiwa amebeba dhambi zote za mwanadamu zilizokuwa zimepitishwa kwake kwa ubatizo aliokuwa ameupokea toka kwa Yohana basi dhambi zetu pia zimekufa pamoja na Kristo hasa tunapoamini katika hili. Kule kusema kuwa dhambi zote za ulimwengu zilipitishwa kwa Yesu kwa kupitia ubatizo wake toka kwa Yohana basi huo ndio ukweli. Ukweli huu haupaswi tu kutambuliwa bali unapaswa pia kuwekwa katika mioyo yetu kwa imani. Ni lazima tuitunze imani hii hadi tutakapoingia katika Ufalme wa Mungu. Hii ndio maana Paulo alisema kuwa tulifanyika wafu kwa ile Sheria kwa kupitia mwili wa Kristo. Kwa hiyo, wale wanaoamini katika ukweli huu wanaweza kwenda mbele za Yesu Kristo, wakaishi pamoja naye na kisha wanaweza kuzaa matunda ya haki kwa Mungu. 
Sisi hatupaswi kuamini kwa kutegemea ule ukale wa waraka bali tunapaswa kuamini katika ukweli wa Roho. Kwa kweli wenye dhambi wanafanya dhambi nyingi zaidi kwa sababu ya Sheria. Hii ni kwa sababu Sheria inazifunua dhambi nyingi zaidi ambazo zimefichwa ndani yao na hivyo kuwafanya kuwa na ule ufahamu wa dhambi zao na kuwaruhusu kufanya dhambi zaidi. Moja ya kazi za Sheria ni kutufanya sisi kuzitambua dhambi zetu, na pia Sheria inafanya kazi ya kuifunua zaidi asili ya dhambi na kutufanya sisi kufanya dhambi zaidi. Pasipokuwepo kwa ile Sheria ambayo Mungu alitupatia tusingeweza kutambua kiasi kikubwa cha dhambi kilichofichika ndani yetu. Lakini Mungu alitupatia Sheria yake, na Sheria hii sio tu inazifanya dhambi kuwa wazi zaidi bali pia inatufanya sisi kutenda dhambi zaidi na zaidi. 
Kwa hiyo, Paulo anasema kuwa kwa kuwa tumekuwa wafu kwa dhambi kwa kupitia mwili wa Kristo, basi sasa tunapaswa kumtumikia Bwana kwa imani ya kuamini katika haki ya Mungu. Paulo anatueleza sisi kumtumikia Bwana kwa msaada wa Roho na karama ya wokovu iliyotolewa kwetu kwa imani iliyo ndani ya vina vya mioyo yetu na wala si kumtumikia Mungu kwa imani inayojengwa katika waraka wa Neno. Kama Biblia inavyotueleza kuwa “kwa kuwa andiko huua, bali Roho ndiye atoaye uzima,” ni lazima tumfuate Bwana kwa kutambua maana halisi ya injili ya maji na Roho ambayo ndiyo haki ya Mungu. Kwa maneno mengine, tunapoamini katika Neno la Mungu basi ni lazima tutambue na kuamini katika maana ya kweli iliyofichika katika Neno lililoandikwa. 
 

Je, Sheria ni dhambi? Kwa Hakika ni Hapana! 
 
Paulo aliielezea Sheria ya Mungu kwa kusisitiza juu ya kazi zake. Hii inaonyesha jinsi ilivyo muhimu kuamini hali ukiwa na ufahamu sahihi wa kazi ya Sheria. Hapo kabla Paulo aliziangalia dhambi zake kwa njia yake mwenyewe, na kwa sababu ya jambo hili hakuweza kuzifahamu dhambi zake binafsi, lakini kwa kupitia Sheria ya Mungu Paulo aliweza kutambua kuwa alikuwa na moyo wenye tamaa ndani yake. 
Ninatumaini kuwa waamini katika Yesu katika wakati wa leo wanaweza pia kuufikia ufahamu kama huo ambao Paulo aliufikia kuhusiana na Sheria. Kuna watu wengi sana ambao hali hawajautambua ukweli wa Sheria, bado wanajitahidi sana kuyaishi maisha yao kwa kuifuata Sheria. Wanakwenda kanisani hali wakifikiri kuwa ikiwa watajaribu kwa nguvu zaidi basi wanaweza kuyafuata yote yaliyo katika Sheria. Lakini ukweli ni kwamba, watu hawa hawataweza kabisa kuipata haki ya Mungu. 
Hawajaitambua maana ya kina ya Sheria iliyotolewa na Mungu na kwa hiyo wamefanyika kuwa wanasheria. Wao ni wanafiki vipofu ambao hawawezi kuiona mioyo yao wenyewe, na hawafahmu kuwa wanasimama kinyume na haki ya Mungu katika jumuiya ya Kikristo. Siku hizi kuna watu wengi sana wa jinsi hiyo katika Ukristo wa sasa. Wale ambao hawaifamu kwa kweli haki ya Mungu na wamempokea Yesu kuwa ni Mwokozi wao wa mazoea katika imani ya kisheria basi watu hao hawataweza kuepushiwa adhabu ya mauti ya milele. 
Paulo alieleza kuwa kwa kupitia amri za Mungu alifikia hatua ya kuifahamu hila iliyokuwamo ndani ya moyo wake. Alipozitambua dhambi zake kwa kupitia amri hizo, Paulo aliendelea kuwa mwanasheria ambaye alifikiria kuwa alipaswa kuitunza na kuifuata Sheria ya Mungu. Amri za Mungu ziliifunua hila iliyokuwemo katika moyo wa Paulo na ilimfanya Paulo aendelee kutenda dhambi zaidi. Hivi ndivyo Paulo alivyokuja kutambua kuwa hakuwa chochote zaidi ya kuwa kama mwenye dhambi mkubwa. 
Kuna asili kumi na mbili za dhambi katika mawazo ya mwanadamu. Wakati Paulo alipokuwa hafahamu kuhusu kazi halisi ya Sheria alijifikiria yeye mwenyewe kuwa ni mtu safi pasipo kutambua jinsi alivyokuwa ni mwenye dhambi. Lakini matokeo ya juhudi yake ya kuishi kwa kufuata amri za Mungu yalimwonyesha kuwa alikuwa mbali na asiyeweza kuzifuata na kuzitunza amri na kwamba amri hizi zilizifunua dhambi zake zaidi na zaidi. 
Je, watu wakoje wanapomwamini Yesu? Ulipoanza kuamini katika Yesu kwa mara ya kwanza bila shaka ulikuwa umeamshwa sana na ile imani yako, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda bila shaka ulianza kuziona dhambi nyingi ambazo kimsingi zipo ndani yako. Je, uliweza kuzitambua dhambi hizo kwa kupitia kitu gani? Ni kwa kupitia Sheria iliyoandikiwa na amri zake ndipo tumeweza kuiona mioyo yetu ikiwa imejazwa na aina kumi na mbili za dhambi. Na tunajikunyata mara tunapoziona nafsi zetu mbele ya Sheria. Hii ni kwa sababu kwa kupitia Sheria tunajiona jinsi tulivyo wenye dhambi wakubwa. 
Hii ndiyo sababu baadhi ya watu waliliunda fundisho la Kuhesabiwa Haki kwa Imani ili kujifariji wao wenyewe. Fundisho hili linadai kuwa ingawa tuna dhambi katika mioyo yetu, na kwa kuwa tunamwamini Yesu, basi Mungu atatuhesabia sisi kuwa ni wenye haki. Hili ni fundisho tu lililoundwa na mwanadamu. Watu waliliunda na kuliamini fundisho hilo ili kuweza kuzificha dhambi zao hali wakijitahidi kuishi na kuridhika kutokana na fundisho hili. Lakini kwa sababu bado wanafunuliwa kuwa ni wenye dhambi mbele ya Sheria, basi dhambi zao zinaendelea kuwa nzito zaidi na zaidi katika mawazo yao. Ili tuweze kuwekwa huru toka katika dhambi zetu zote basi hatuna chaguo jingine zaidi ya kuamini katika injili ambayo ina haki ya Mungu ndani yake. Hii ndiyo njia pekee ya kuweza kukombolewa toka katika dhambi zetu zote. 
Kama Paulo alivyofikiria kuwa Mungu alimpatia amri ili aweza kuzifuata, bila shaka Paulo alilifikiria jambo hilo kikawaida kuwa angaliweza kujaribu na kufanya kila awezalo kuifuata na kuitunza Sheria. Lakini kinyume na hivyo, Paulo alikuja kutambua kuwa amri hizi zilikuwa zikiipeleka nafsi yake katika kifo kwa sababu ya dhambi. Mwishowe Paulo alitambua kuwa alikuwa amezielewa na kuziamini vibaya zile amri za Mungu. 
Kila mtu ana zile aina kumi na mbili za dhambi zinazotajwa katika Marko 7:21-23. “Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.” 
Paulo pamoja na watu wengine wote hatimaye walifikia hatua ya kuzitambua dhambi zao kwa kupitia amri za Mungu. Kwa kutumia Sheria walizitambua dhambi zao na hivyo waliuawa, kisha waliigundua haki ya Mungu kwa kupitia Yesu Kristo na kisha wakaiamini. Je, una uelewa gani kuhusu haki ya Mungu? Je, bado unajaribu kuzitunza amri hali ukifikiria kuwa unaweza kuzitunza na kuzifuata zote kikamilifu? Kwa maneno mengine, Mungu alitupatia Sheria yake ili kwamba tuweze kuzitambua dhambi zetu na kisha turudi kwake—ili tuweze kukombolewa toka katika dhambi kwa kuamini katika haki ya Mungu. Ni lazima tuwe na ufahamu sahihi kuwa ni kwa nini Mungu alitupatia amri zake na kisha tuziamini kiusahihi. Mara utakapoufahamu ukweli huu, ndipo utakapoitambua thamani ya injili ya maji na Roho Mtakatifu. 
Wale wanaoamini katika amri za Mungu wanaweza kutambua jinsi walivyo wenye dhambi wakubwa mbele za Mungu. Watu ambao hawalifahamu jukumu la amri na hawaamini katika haki ya Mungu basi watu hao watakuja kukutana na magumu makubwa katika maisha yao ya kidini na hivyo hatimaye wataongozwa katika maangamizi yao. Hii ni kwa sababu ni vigumu sana kuishi mbali na dhambi hali tukiwa bado tunaishi katika ulimwengu ambao umejaa dhambi. Hii ndiyo sababu baadhi ya watu wanadiriki hata kujitenga kwenda kuishi katika maeneo ya upweke milimani na kujaribu kuishi maisha ya upweke na ya kitawa. Wanafikiria kuwa kwa kuishi milima na kwa kujitenga mbali na dhambi za ulimwengu basi angalau wanaweza kuepuka kutenda dhambi, lakini hali haiwi hivyo. 
Ni lazima tutambue kuwa, ingawa ni kweli kuwa kila mtu anatenda dhambi katika ulimwengu huu na kwamba kila mtu ana dhambi katika moyo wake, basi ukombozi toka katika dhambi kama hizo unaweza kupatikana kwa kuifahamu na kuamini katika haki ya Mungu. Hata kama tungeukwepa ulimwengu ili tuweza kuzikwepa dhambi zake bado tusingeweza kuzikwepa dhambi za mioyo yetu. Hii ni kwa sababu dhambi zinapatikana katika mioyo yetu. Ili tuweze kujiweka huru toka katika dhambi basi ni lazima tuamini katika injili ya maji na Roho. Sheria ya Mungu na amri zake inazifanya dhambi zetu kuwa na dhambi zaidi. Wale ambao wanafahamu madhara ya dhambi zao ni lazima wafahamu na kuamini katika haki ya Mungu iliyofunuliwa kwetu kwa kupitia injili ya maji na Roho. 
“Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti. Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua” (Warumi 7:10-11). Ni lazima tuwe na ufahamu sahihi wa Sheria. Wale ambao hawajailewa vizuri Sheria watautumia muda wao wote wa maisha hali wakiishi katika maisha ya kisheria hali wakijaribu kuikwepa Sheria hadi siku yao ya mwisho. Ni wale tu wanaolifahamu jukumu halisi la Sheria ndio wanaoweza kuipenda na kuamini katika haki ya Mungu iliyotimizwa na Yesu. Je, unaifahamu haki hii ya Mungu? 
Mtume Paulo alisema kuwa kwa kuwa hapo kabla alikuwa hajazaliwa tena upya, basi alikuwa ni mali ya mwili na aliyekuwa ameuzwa chini ya dhambi. Pia alikiri kuwa pamoja na kuwa alipenda kuishi kwa kuifuata Sheria ya Mungu, alijikuta akiishia kufanya yale ambayo alikuwa hapendi kuyafanya—yaani kutenda dhambi. Hii ni kwa sababu hakuwa na Roho Mtakatifu ndani yake kwa kuwa hakuwa na ile haki ya Mungu. Kisha Paulo alikiri kuwa sababu iliyomfanya atende dhambi kinyume na matakwa yake ni kwa sababu ya dhambi iliyokuwa ndani ya moyo wake kwa kuwa alikuwa bado hajaipata haki ya Mungu kwa wakati ule. 
Hata hivyo, Paulo aliitambua sheria moja na sheria hiyo ilikuwa ni sheria ya dhambi—ambao ni ukweli wa msingi kuwa mwanadamu aliye na dhambi katika moyo wake hawezi kukwepa kutenda dhambi. Pia alitambua kuwa nafsi ya ndani ya mwanadamu bado inatamani wakati wote kuishi kwa mujibu wa Sheria ya Mungu. Lakini Paulo alikiri kuwa kama ambavyo mti wa dhambi unavyozaa matunda ya dhambi, yeye alikuwa ni mwenye dhambi aliyeweza kuendelea kuishi katika dhambi kwa kuwa alikuwa bado hajakutana na Yesu na alikuwa bado hajapokea ukombozi wa dhambi zake. Kwa maneno mengine, ilikuwa ni sahihi kwake yeye kuuawa kwa sababu ya dhambi zake. 
Hii ndiyo sababu Paulo alikiri kuwa yeye alikuwa ni mtu mwenye huzuni hali akiomboleza, “Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” (Warumi 7:24) Haya yalikuwa ni masahihisho binafsi pale alipokuwa mwenye dhambi. Naomba utafakari juu ya kuitumia toba hii ya Paulo kwako wewe binafsi. Je, bado haujafungwa katika mwili huu wa mauti ambao hauwezi kuitunza na kuifuata Sheria? Ni lazima tuamini katika haki ya Mungu. Haki hii ya Mungu imefichika katika injili ya maji na Roho na tunaweza kuipata haki hii ya Mungu kwa kuamini katika injili hii. 
Paulo aliweza kuwekwa huru toka katika huzuni zake zote kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo na kifo chake Msalabani.