Search

Проповіді

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-10] Mafundisho ya Kidini Yenye Makosa (Warumi 8:29-30)

(Warumi 8:29-30)
“Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”
 

Vifungu hivyo vinatueleza sisi kuwa Mungu alichagua tangu asili ili kuwaokoa watu katika Yesu Kristo. Ili kufanya hivyo, Mungu amewaita wao katika Kristo, amewahesabia haki wale aliowaita, na amewatukuza wale aliowahesabia haki. Misingi yote ya maandiko imepangwa na kutekelezwa kwa kupitia Yesu Kristo. Hivi ndivyo kitabu cha Warumi kinavyotueleza, lakini wanatheolojia wengi na watumishi wa uongo wameubadilisha ukweli huu ulio wa wazi kuwa katika fundisho la kawaida la dini hali likiwa na mawazo na matakwa yao binafsi na wanalieneza fundisho hilo kwa nguvu. Sasa tunageukia kuchunguza jinsi watu wengi wanavyouelewa vibaya ukweli huu. 
Baadhi ya watheolojia wanatoa mafundisho makuu matano ya kidini toka katika kifungu hiki: 1) sayansi-asili, 2) kuchaguliwa-asili, 3) wito makini, 4) kuhesabiwa haki, na 5) kutukuzwa. Mafundisho haya matano ya dini yanafahamika kama “Mnyororo wa Wokovu wa Dhahabu” na yamekuwa yakifundishwa kuwa ni ukweli kwa waamini na wasio waamini pia. Lakini madai yao yamejaa udanganyifu na upotovu mwingi. 
Mafundisho yote matano yanazungumzia juu ya kile ambacho Mungu amekifanya—ambacho ni, “Mungu alikwisha fahamu, alikwisha chagua, alikwisha ita, aliwahesabia haki, na akamtukuza mtu fulani.” Lakini Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili ni fundisho linalodai kuwa Mungu pasipo kujali hali alikwisha kuwachagua wale ambao atawaokoa hata kabla ya kuzaliwa kwao. Hata hivyo ukweli wa kibiblia kuhusu Kuchaguliwa Tangu Asili unafundisha kuwa Mungu amewafanya wenye dhambi kuwa watoto wake kwa kuwamwagia upendo wake juu yao. Na baada ya kuwachagua Mungu amewaita, amewahesabia haki, na amewatukuza. 
 

Kosa la Theolojia za Kuchaguliwa Tangu Asili na Kuteuliwa
 
Katika theolojia ya Kikristo, tunaweza kuyapata mafundisho “makuu matano ya kidini” ya Ukalvin uliokuwa ukienezwa na John Kalvin. Miongoni mwa mafundisho hayo ni Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili na Fundisho la Kuteuliwa. Katika mjadala unaofuata, nitaonyesha makosa katika mafundisho haya kwa mujibu wa Biblia na kisha nitatoa ushuhuda kwa injili ya maji na Roho. 
Fundisho la Kuteuliwa lilianzia kwa mwanatheolojia aliyeitwa John Kalvin. Kwa kweli Mungu anazungumzia juu ya kuteuliwa katika Yesu Kristo muda mrefu hata kabla ya kipindi cha Kalvin, lakini Fundisho lake la Kuteuliwa limewafanya watu wengi kuingia katika matatizo. Fundisho hili la uongo limeuwekea mipaka upendo wa Mungu na linauelezea upendo huo kana kwamba ni wa kibaguzi na usio na haki sawa. Tukiongea kimsingi, kwa kweli hakuna mipaka wala ukomo katika upendo wa Mungu, na kwa hiyo Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili ambalo linaleta ukomo huo juu ya upendo wa Mungu haliwezi kuwa kitu chochote zaidi ya kuwa ni uongo. Hata hivyo ukweli ni kuwa waamini wengi katika Yesu wamelipokea fundisho hili kuwa ni la asili na lenye majaliwa. 
Mawazo au hoja za Fundisho hili la Kuchaguliwa Tangu Asili yameweza kuyatawala mawazo mengi, kwa kuwa fundisho hili linafaa sana kwa watu ambao wanapenda kufanya falsafa, na kwa sababu hiyo fundisho hili limeyatawala mawazo na fikra zao hali likiwafanya waamini. Fundisho hili linadai kuwa hata kabla ya uumbaji, Mungu bila kujali hali aliwachagua asili na kuwateua baadhi na kwamba wengine walichaguliwa ili kuachwa nje ya kule kuteuliwa. Ikiwa fundisho hili lingekuwa ni la kweli basi zile nafsi ambazo zilichaguliwa kuachwa zingekuwa na msingi wa kuweza kumlalamikia Mungu na angeonekana kuwa ni Mungu asiyefanya haki. 
Kwa sababu ya mafundisho haya, Ukristo wa leo umeangukia katika machafuko makubwa. Kama matokeo ya jambo hilo, Wakristo wengi wanateseka hali wakiwa wanatangatanga kwa kusema, “Je, nimeteuliwa? Ikiwa Mungu alinikataa mimi tangu kabla ya uumbaji basi kuna maana gani ya kumwamini Yesu?” Basi wanaishia kutafuta kujua ikiwa walijumuishwa au walitolewa katika ule uteuzi wa Mungu. Hii ndiyo sababu Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili lilivyozalisha machafuko mengi miongoni mwa waamini wanaomwamini Yesu kwa kuwa wanawekea sana umakini katika suala la kuchaguliwa kuliko injili ya kweli ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu. 
Fundisho hili limeugeuza ukweli wa Ukristo kuwa kama moja ya dini nyingine za ulimwenguni. Lakini sasa ni wakati wa sisi kuyakanusha mafundisho haya potofu toka ndani ya himaya ya Ukristo kwa kutumia injili ambayo inabeba ushahidi wa haki ya Mungu. Kwa hiyo, ni lazima kwanza ujionee wewe mwenyewe ikiwa Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili ni sahihi au hapana halafu ukombolewe toka katika dhambi zako zote kwa kufahamu na kuamini katika injili ya maji na Roho. Wale ambao wamechaguliwa na Mungu kikwelikweli ni wale ambao wanafahamu na kuamini katika haki yake. 
 

Kuchaguliwa Tangu Asili na Kuteuliwa Zinazungumziwa na Ukweli 
 
Waefeso 1:3-5 inasema, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.” Kuchaguliwa Tangu Asili kunakozungumzwa katika kifungu hiki cha Waefeso ni kuchaguliwa kwa wateule “katika Yeye (Kristo) kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu” (Waefeso 1:4). Pia kifungu hiki kinatueleza kuwa Yesu Kristo hajamtenga mtu awaye yote toka katika neema ya wokovu toka katika dhambi. 
Kutoka katika kifungu hiki ni lazima tutambue kile ambacho ni kosa katika Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili. Kosa la msingi katika fundisho hili ni kuwa linaleta upendeleo dhidi ya vigezo vya uteuzi wa Mungu–ambayo ni sawa na kusema kuwa kuokolewa kwa mtu au kutookolewa hakutegemeani na Neno la Mungu na badala yake kutegemea maamuzi ambayo hana uamuzi wake. 
Ikiwa tungeliiweka imani yetu katika Yesu kwa kuangalia ufahamu wa Kuchaguliwa Tangu Asili na kuteuliwa, tungeliwezaje basi kumwamini Yesu katika hali ya hasira kwa sababu ya mashaka na kutokuwa na hakika? Ukalvin unafundisha fundisho la dini la uongo ambalo linamgeuza Mungu mwenye haki kuwa Mungu asiye na haki na mwenye upendeleo. Sababu iliyomfanya Kalvin akafanya makosa hayo ni kwa sababu aliliacha lile neno “katika Yesu Kristo” toka katika uchaguzi asili wa Mungu na kosa hilo limekuwa ni shimo kubwa la kuwachanganya na kuwapotosha wengi. Lakini andiko linatueleza wazi kuwa, “Mungu anatuchagua sisi katika Mwana wake Yesu Kristo” (Waefeso 1:4).
Ikiwa kama wakalvin wanavyodai kuwa Mungu aliwachagua baadhi bila kanuni yoyote ili awe Mungu wao hali akiwaacha wengine pasipo sababu yoyote basi ni jambo gani litakalokuwa baya kama hili? Kalvin alimgeuza Mungu kuwa ni Mungu asiye wa haki katika mawazo ya watu wengi. Lakini katika Warumi 3:29 Biblia inatueleza sisi kuwa, “Au je! Mungu ni Mungu wa Wahayhudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia.” Mungu ni Mungu kila moja na Mwokozi wa wote. 
Yesu ni Mwokozi wa wote. Alitoa ukombozi kwa kima mtu kwa kuzichukua dhambi za kila mwanadamu katika mwili wake kwa ubatizo alioupokea toka kwa Yohana na damu yake Msalabani (Mathayo 3:15). Maandiko yanatueleza kuwa Kristo alimwokoa kila mwenye dhambi kwa kuzibeba dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake na akazibeba dhambi hizi hadi Msalabani kwa niaba yetu (Yohana 1:29), na akahukumiwa kwa ajili ya dhambi hizi badala yetu (Yohana 19). Pia Yohana 3:16 inatueleza kuwa, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yesu Kristo alizichukua katika mwili wake dhambi za kila mtu kwa ubatizo wake, akafa Msalabani, na akafufuka toka kwa wafu kwa ajili ya wanadamu wote katika haki ya Mungu. 
Uelewa wetu kuhusu ni akina nani ambao Mungu amewaita ni lazima ujengwe katika Neno lake. Ili kufanya hivyo hebu tuangalie katika kifungu toka kwa Warumi 9:10-11. “Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo bali kwa sababu ya nia yake aitaye).”
Neno linasema hapa kwamba ili lisimame kusudi la Mungu “kwa nia yake aitaye.”. Ni akina nani basi ambao Mungu amewaita katika Yesu Kristo? Kwa hakika ni wenye dhambi ambao ndio Mungu amewaita. Kati ya Esau na Yakobo ni nani aliyependwa na Mungu? Mungu alimpenda Yakobo. Mungu hawapendi watu kama Esau ambaye alikuwa amejaa haki yake mwenyewe, bali aliwaita wenye dhambi kama Yakobo na akawaruhusu kuzaliwa tena upya kwa kupitia injili ya maji na Roho. Haya yalikuwa ndiyo mapenzi halisi ya haki ya Mungu ambayo yaliwachagua wenye dhambi kama Yakobo kuwapenda na kuwaita kwa kupitia Yesu Kristo. 
Kwa sababu Adamu alikuwa ndiye baba wa kale wa kila mtu, basi wote walizaliwa kama watoto wa mwenye dhambi. Katika Zaburi 51, Daudi anasema kuwa alitungwa mimba katika hali ya dhambi tangu alipokuwa katika tumbo la mama yake. Kwa kuwa watu wanazaliwa wakiwa wenye dhambi basi wanatenda dhambi pasipo kujali nia zao. Katika maisha yao yote wanaendelea kuzaa matunda ya dhambi hadi mwisho wao kabisa. Marko 7:21-23 inatueleza sisi kuwa kama ambavyo mti wa matufaha unavyozaa matufaha na mti wa mapeazi unavyozaa mapeazi, wanadamu wamefungwa kuishi katika dhambi katika maisha yao yote kwa sababu walizaliwa na dhambi. 
Bila shaka umeshakutana na uzoefu wa kutenda dhambi kinyume na matakwa yako. Hii ni kwa sababu ulizaliwa ukiwa ni mwenye dhambi tangu mwanzo kabisa. Watu wanazaliwa wakiwa na mawazo maovu yakiwemo uzinifu, ukahaba, uuaji, wizi, ufisadi, uovu, umalaya, na dhambi nyingine kama hivyo katika mawazo yao. Hii ndio sababu kila mtu anaishi maisha yake katika dhambi. Dhambi inarithiwa. Kwa kuwa tulizaliwa na dhambi ambazo wazazi wetu waliotutangulia walizileta kwetu, basi kimsingi tuliwekewa ile nia ya kuishi katika dhambi. Hii ndio sababu inayotufanya tuhitaji kumwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wetu na kisha kuamini katika haki ya Mungu. 
Je, hii ina maanisha kuwa kazi ya kwanza ya Mungu ya kumuumba Adamu iliishia katika kushindwa? Hapana, haimaanishi hivyo. Mungu aliamua kuwafanya wanadamu kuwa watoto wake, hivyo aliamuru mtu wa kwanza kuanguka katika dhambi. Kimsingi, Mungu alituruhusu sisi kuwa wenye dhambi ili Mungu aweze kutuokoa na kutufanya sisi watoto wake kwa ubatizo wa Yesu Kristo na damu yake. Hivyo, ni lazima tutambue kuwa sisi tulizaliwa tukiwa ni wenye dhambi pasipo kukwepa. 
Hata hivyo, Mungu aliamua kumtuma Yesu Kristo kuja hapa duniani kabla ya uumbaji hali akijua kuwa wanadamu watakuwa wenye dhambi. Kisha Mungu akaziweka dhambi zote za ulimwengu juu ya Yesu kwa kupitia ubatizo alioupokea toka kwa Yohana na akamfanya kufa juu ya Msalabani. Kwa maneno mengine, Mungu aliamua kumpatia mtu yeyote aliyeamini baraka za ukombozi toka katika dhambi na baraka ya kufanyika watoto wa Mungu. Huu ni mpango wa Mungu na dhumuni lake la kumuumba mwanadamu. 
Baadhi ya watu wanaweza kuuliza katika kutokuelewa kwao, “mtazame Yakobo na Esau. Je, mmoja si alichaguliwa na mwingine aliachwa na Mungu?” Lakini Mungu hakuwachagua wale ambao wanasisitiza kuwa wameokolewa nje ya Yesu Kristo. Mungu alichagua kumfanya kila mtu kwa mtoto wake kupitia Yesu Kristo. Tukiendelea kutafakari juu ya Agano la Kale peke yake tunaweza kupata mtazamo kuwa Mungu aliuchagua upande mmoja, lakini katika Agano Jipya tunaweza kuona pasipo makosa kuwa Mungu alimteua mtu kama Yakobo ili aweze kuwaokoa wenye dhambi wengine wote kwa kupitia Yesu Kristo. Ni lazima tuwe na uelewa mzuri na kuamini katika wale ambao Mungu amewaita kwa Neno lake. 
Kati ya Esau na Yakobo ni nani ambaye Mungu alimpenda? Hakumwita mwingine yeyote zaidi ya Yakobo, mtu aliyekuwa na mapungufu mengi, mlaghai na asiye na haki, ili aweze kumpenda na kumwokoa katika haki ya Mungu. Wewe pia unapaswa kuamini katika ukweli huu kwamba Mungu Baba amekuita kwa kupitia Yesu Kristo katika haki yake. Pia ni lazima uamini katika ukweli kuwa injili ya maji na Roho katika Yesu Kristo ndiyo haki ya Mungu halisi. 
Kwa nini basi Mungu aliwachagua watu kama Yakobo? Mungu alimchagua Yakobo kwa sababu alikuwa ni mwakilishi wa wanadamu wote wasio na haki. Wito wa Mungu kwa Yakobo ulikuwa ni wito ambao uliendana na nia ya Mungu; yaani wito kwa mujibu wa Neno la Mungu kwamba “tulichaguliwa katika Yesu Kristo.” Wito huu pia unaendana vizuri na Neno la kweli kwamba “ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo bali kwa sababu ya nia yake aitaye”.
Njia ya kuwaokoa wenye dhambi kwa kupitia Yesu Kristo ilikuwa na lengo la kuitimiza haki ya Mungu kwa upendo wake. Hii ilikuwa ni sheria ya wokovu iliyokuwa imewekwa na haki ya Mungu kwa wenye dhambi. Mungu aliwaita watu kama Yakobo, ambaye hakuwa na haki yake binafsi kabisa ili kuwafunika katika haki yake kwa kupitia Yesu Kristo. 
Je, Mungu aliwaita wale ambao walikuwa na haki yao binafsi na ambao walionekana kuwa wako safi? Au je, aliwaita wale ambao hawakuwa na haki binafsi na waliokuwa na mapungufu mengi? Wale ambao Mungu aliwaita walikuwa ni watu kama Yakobo. Mungu aliwaita na kuwaokoa wenye dhambi waliokuwa wamefungwa kwenda kuzimu kwa sababu ya dhambi zao. Ni lazima utambue kuwa tangu kuzaliwa kwako wewe pia umekuwa ni mwenye dhambi ambaye umepungukiwa na utukufu wa Mungu, na kwa hiyo ulikuwa umefungwa kwenda kuzimu. Kwa maneno mengine, unahitaji kuifahamu hali yako binafsi ya kweli. Mungu aliwaita wenye dhambi wote kwa kupitia Yesu Kristo na akawaokoa katika haki yake. 
Watu wa Mungu ni wale ambao wamehesabiwa haki kwa kuamini katika haki ya Mungu. Mungu alichagua tangu asili kuwaita wenye dhambi zote na kuwakomboa katika Yesu na alikitimiza kile alichokuwa amekichagua asili. Huu ndio uchaguzi asili na uteuzi wa kweli katika Yesu Kristo ambao Mungu anauzungumzia. Ili tuweze kuufahamu uteuzi wa kweli wa Mungu ni lazima kwanza tutambue msingi wa ukweli huu juu ya uteuzi kama unavyoelezwa katika Agano la Kale. 
 

Usuli (Maelezo ya Msingi) Kuhusu Uteuzi wa Mungu Toka Katika Agano la Kale
 
Mwanzo 25:21-26 inatueleza kuhusu habari ya Yakobo na Esau wakiwa bado katika tumbo la mama yao Rebeka. Kati ya hao wawili Mungu alimchagua Yakobo. Kalvin alijenga msingi wa Fundisho lake la Kuteuliwa toka katika kifungu hiki, lakini muda si mrefu tutagundua kuwa uelewa wake unatoka nje ya mapenzi ya Mungu. Kuliwa na sababu kwa nini Mungu alimpenda Yakobo kuliko Esau. Sababu hii ni kuwa watu kama Esau badala ya kuishi na kumtegemea Mungu wanazitegemea nguvu zao wenyewe, wakati watu kama Yakobo wanaishi hali wakiwa wanaitegemea haki ya Mungu. Biblia inaposema kuwa Mungu alimpenda Yakobo kuliko Esau ina maanisha kuwa Mungu anawapenda watu kama Yakobo. Hii ndiyo sababu sisi “tulichaguliwa katika Kristo” (Waefeso 1:4).
“Kuteuliwa pasipo sababu yoyote” pasipo Yesu na nje ya haki ya Mungu ni fundisho la uongo la Kikristo. Wazo hili linahusiana katika kuleta dhana ya kuamini katika Mungu wa majaliwa katika Ukristo. Lakini ukweli unatueleza sisi kuwa Mungu aliwachagua wenye dhambi wote katika Yesu. Kwa kuwa Mungu aliamua kuwaokoa wenye dhambi wote “katika Yesu Kristo,” basi kuteua kwake kulikuwa ni kwa haki. Ikiwa Mungu angelikuwa amemchagua Yakobo pasipo kanuni au sababu yoyote na kisha akamkataa Esau pasipo msingi wowote basi angelikuwa ni Mungu asiye na haki, lakini Mungu alituita sisi katika Yesu Kristo. Na ili kuwaokoa wale ambao alikuwa amewaita, Mungu alimtuma Yesu kuja hapa duniani ili kuzichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake ambao umeitimiza haki ya Mungu, na kisha kuimwaga damu yake ya thamani Msalabani. Hivi ndivyo Mungu alivyotuchagua na kutupenda kwa kupitia Kristo Yesu. 
Tunahitaji kuyatupilia mbali mawazo yetu binafsi ya kibinadamu na kisha kuamini katika Neno la Maandiko, na sio katika imani ya kimaandiko bali katika imani yetu ya kiroho. Kwa maneno mengine, Mungu Baba alituchagua sisi sote kupitia Yesu Kristo. Lakini Kalvin anakutumiaje ule uteuzi wa Mungu? Imani ya kweli inapatikana wakati mtu anapofahamu na kuamini katika haki ya Mungu. Kuamini katika mawazo ya wanadamu kuwa ni ya kweli ni sawa na kuamini sanamu badala ya Mungu. 
Kuamini katika haki ya Mungu kwa kupitia Yesu ni tofauti na kuamini katika Fundisho lenye makosa la Kuchaguliwa Tangu Asili. Kama tungekuwa hatufahamu na kuamini katika Yesu Kristo kwa mujibu wa Neno la Mungu lililoandikwa, basi tusingekuwa na tofauti yoyote na wanyama wengine ambao hawana utashi wa kufikiri. Sisi tumechaguliwa kama watoto wa Mungu kwa muhuri wa haki ya Mungu “katika Yesu Kristo.” Tunapaswa kuzichunguza imani zetu kwa msingi wa Neno la Maandiko. 
Moja kati ya mafundisho matano ya Ukalvin inazungumzia juu ya “upatanisho wenye ukomo.” Fundisho hili linadai kuwa miongoni mwa watu wengi wa ulimwenguni, baadhi wameondolewa toka katika wokovu wa Mungu. Lakini upendo wa Mungu na haki yake haviwezi kuwa visivyo na haki kiasi hicho. Maandiko yanatueleza kuwa Mungu “hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli” (1 Timotheo 2:4). Ikiwa baraka ya wokovu ingekuwa ni baraka yenye ukomo na mpaka na inayotolewa kwa baadhi na kisha kuzuiliwa kwa wengine, basi kungekuwa na watu wengi sana ambao wangekuwa wameikatia tamaa imani yao katika Yesu. Wale wanaoamini katika mafundisho ya uongo kama hayo ni lazima warudi katika injili ya maji na Roho, waokolewe toka katika dhambi zao na kisha wapokee uzima wa milele na kufahamu na kuamini katika Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao. Mungu amemwokoa kila mtu kwa kupitia Yesu Kristo kwa haki yake. 
Ikiwa ni kweli kuwa Mungu aliwapenda baadhi na aliwachukia baadhi, basi watu wangemgeuzia Mungu migongo yao. Hebu tuchukulie kuwa Mungu anasimama hapa sasa hivi. Unadhani Mungu atawachagua wale waliosimama mkono wake wa kuume kwa ajili ya wokovu na wale waliosimama mkono wake wa kushoto kwenda kuzimu pasipo sababu yoyote, je hii itakuwa ni haki? Wale watakaokuwa katika mkono wake wa kushoto watakuwa hawana chaguo zaidi ya kugeuka na kuwa kinyume na Mungu. Ikiwa Mungu angekuwa yupo kama hivi, ni nani basi katika ulimwengu huu ambaye angemtumikia na kumwabudu yeye kuwa ni Mungu wa kweli? Wale wote ambao watakuwa wamechukiwa na Mungu pasipo sababu yoyote wangeasi na matokeo yake na wao pia wangelimchukia Mungu. Hata watenda maovu ya jinai katika ulimwengu huu wanasemekana kuwa na maadili yao na usawa wa haki zao wenyewe. Itawezekanaje basi kwa muumba wetu akawa si mwenye haki kiasi hicho, na ni nani anayeweza kumwamini Mungu asiye na haki kiasi hicho? 
Baba yetu aliamua kuwaokoa wenye dhambi wote kwa haki ya Mungu inayopatikana katika Mwanawe Yesu Kristo. Hii ndiyo sababu Fundisho la Wakalvin la Upatanisho Wenye Ukomo halina kitu cha kufanya kuhusiana na haki ya Mungu. Lakini kwa sababu ya mafundisho kama hayo yenye makosa, watu wengi bado wanapotoshwa na kwenda kinyume hali wakimwamini Mungu kimakosa au wakigeukia mbali toka kwa Mungu kwa sababu ya kutokuelewa kwao. 
 

Filamu Isiyo ya Kweli
 
Kitabu cha riwaya cha Stephen King kilichoandikwa “Msimamo,” miaka kadhaa iliyopita kilitengenezwa katika mfululizo wa vipindi vya televisheni, na kilisifiwa katika ulimwengu mzima. Habari ya riwaya hii inaweza kuelezewa kama hivi: Katika mwaka wa 1991, pigo liliipiga Marekani likawaacha watu wachache tu waliokuwa hai au ambao walikuwa wana “kinga” dhini ya ugonjwa ulioipiga nchi hiyo. Miongoni mwa waliosalia, wale wanaomtumikia Mungu kwa nguvu walikutana katika mji wa Boulder huko Colorado ilihali wale wanaomwabudu “Mtu Mweusi” walikutana Las Vegas, Nevada. Makundi haya mawili yalizijenga jamii zao kitofauti hadi jamii moja itakapoiharibu jamii nyingine. 
Miongoni mwa waliosalimika, kijana mmoja aliyeitwa Stuart aliendelea kuota ndoto zinazojirudia kuwa mwisho wa dunia umekuja, na mwanamke mzee aliyeitwa Abigail akamweleza katika ndoto zake kwenda mahali fulani, hali akimkumbusha kuwa Mungu alikuwa amekwisha mteua tayari. Katika mkanda huu wa filamu inaonekana kuwa Mungu alimwokoa kijana huyu kwa sababu alikuwa amemchagua tangu asili kabla ya uumbaji hata pale alipokuwa hamwamini Mungu au Yesu. 
Je, ni kweli kuwa Mungu anawaokoa hata wale ambao hawamwamini Yesu? Kwa kweli hapana. Mungu amekwisha mchangua kila mtu tangu asili katika Yesu Kristo ili kuwaokoa wale wanaoamini katika haki yake toka katika dhambi zao. 
Mstari mama wa filamu hii unajengwa katika Mafundisho ya Kalvin ya Kuchaguliwa Tangu Asili na Kuteuliwa. Filamu hii ni hadithi tu ambayo inaelezea sehemu tu ya fundisho la mtheolojia fulani. Inawezekanaje pasipo sababu Mungu akaamua kuwatuma baadhi ya watu kwenda kuzimu na kisha kuwateua wengine kupata wokovu? Kwa kuwa Mungu ni mwenye haki, basi Mungu amemchagua kila mmoja tangu asili na kumteua kila mtu kwa kupitia Yesu Kristo, na hakuna hata mmoja ambaye anazuiwa katika wokovu wa haki yake. Kuchaguliwa Tangu Asili na kuteuliwa na Mungu pasipo Yesu Kristo ni jambo lisilo na maana kibiblia. Ni bahati mbaya kuwa wanatheolojia wengi wanaendelea kudai kuwa Mungu aliteua baadhi na kisha akawazuia baadhi. 
Hata kabla ya hajauumba ulimwengu, Mungu alipanga kuwaokoa wenye dhambi wote na kuwafanya kuwa watoto wake kwa haki yake kwa kupitia Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, Mungu aliwateua wenye dhambi wote kwa kupitia injili ya Yesu. Je, wewe unaamini vipi? 
Je, unaamini kuwa watawa wa Kibudha wanapotafakari kwa kina katika milima basi wameachwa katika uteuzi wa Mungu? Ikiwa Kuchaguliwa Tangu Asili na Kuteuliwa kwa Mungu kungekuwa hakuna kanuni pasipo Yesu Kristo, basi kwa hakika kusingekuwa na haja ya sisi kulihubiri Neno lake wala kuliamini. Ikiwa pasipo Mwokozi Yesu Kristo baadhi ya watu walichaguliwa kuokolewa na wengine kutookolewa, basi kwa hakika kungekuwa hakuna sababu kwa wenye dhambi kumwamini Yesu. Mwishowe hata kule kusema kuwa Yesu ametuokoa sisi toka katika dhambi zetu kwa kupitia ubatizo na dhamu yake Msalabani kusingekuwa na maana. Lakini katika haki ya Mungu inayopatikana katika Yesu Kristo, Mungu aliruhusu wokovu hata kwa hawa watawa wa Kibudha ambao hawamwamini Yesu ikiwa tu watatubu na kuyageuzia mawazo yao kwa Mungu. 
Kuna watu wengi katika ulimwengu huu ambao wanaishi maisha yao hali wakiwa wanaamini katika Yesu. Je, tungalipaswa kuwagawa katika makundi, kundi moja lingekuwa la wale ambao wapo kama Esau na jingine la wale ambao wangekuwa ni kama Yakobo. Watu kama Yakobo wanajitambulisha wenyewe kama wenye dhambi ambao wamefungwa kwenda kuzimu, na kwa hiyo wanaokolewa toka katika dhambi zao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu. Kundi jingine limeundwa na watu kama Esau ambao wanajaribu kuingia katika malango ya mbinguni kwa kuongezea juhudi zao binafsi katika imani zao kwa Yesu. 
Je, wewe upo kama nani? Yakobo au Esau? Je, unaamini katika haki ya Mungu? Au je, unaamini katika Mafundisho ya Kidini yenye makosa ya Kuchaguliwa Tangu Asili? Chaguo lako kati ya mambo haya mawili ndilo litakaloamua hapo mwishoni mahali utakapokuwapo–mbinguni au kuzimu. Ni lazima uyaondolee mbali mafundisho haya yenye makosa na kisha upokee haki ya Mungu ili uweze kufanya amani pamoja na Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho inayotamkwa na haki ya Mungu. Ni imani hii tu ndiyo inayotupatia sisi ukombozi sahihi na mkamilifu toka katika dhambi zetu na misha ya milele.