Search

শিক্ষা

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 12] Zifanye Upya Akili Zako Mbele za Mungu

“Basi, ndugu zangu, nawasishi, kwa huruma zake Mungu itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Warumi 12:1).
“Ibada yenye maana” ni kitu gani? Imetafsiriwa kama “tendo la kiroho la ibada” katika Biblia ya Kiingereza ya (NIV), imetafsiriwa kama ambayo tunapaswa kumpatia Mungu. Kumpatia Mungu ibada yenye maana kuna maanisha ni kuitoa miili yetu kwa Mungu katika kuifanya kazi yake ya haki. Kwa kuwa tumeokolewa, basi tunahitaji kuitoa miili yetu na kukubaliwa na Mungu katika kuieneza injili ya haki. Ibada yenye maana ambayo tunapaswa kumpatia Mungu ni kuitoa miili yetu katika utakatifu na kumpatia Mungu. 
Katika sura ya 12 Paulo anazungumzia juu ya ibada yetu ya kiroho ilivyo. Haipaswi kuifuatisha namna ya dunia hii bali ibadilishwe kwa kufanywa upya akili zetu ili kwamba tuweze kuyathibitisha mapenzi ya Mungu yalivyo mema, ya kuridhisha na makamilifu. 
Ibada yenye maana ni kuitoa miili yetu yote na mioyo kwa Mungu. Sasa, inawezekanaje kwa wenye haki kuishi maisha kama hayo mbele za Mungu? Paulo anasema kuwa hatupaswi kuifuatisha namna ya dunia hii bali tugeuzwa kwa kufanywa upya akili zetu na kwamba tuitoe miili yetu kwa ajili ya kazi za Mungu za haki. Kuiamini haki ya Mungu hali tukiwa tumeitoa mioyo na miili yetu pia ni ibada yenye maana kwa Mungu. 
Kifungu hiki cha maandiko ni cha muhimu sana kwa sababu kinatueleza kuwa hatupaswi kuifuatisha namna ya dunia hii na badala yake tunapaswa kuzitumikia kazi za Mungu na kugeuzwa kwa kufanywa upya nia zetu. 
Hatuwezi kutoa ibada ya kiroho ikiwa hatujaigeuza mioyo yetu. Hata wenye haki hawawezi kuitoa miili yao au mioyo yao kwa Mungu ikiwa wataacha kuamini katika haki ya Mungu. 
Tunaweza kushawishiwa na kizazi hiki, kama ilivyotokea katika kizazi cha Paulo. Kwa kuwa tunaishi katikati ya mtiririko wa kizazi hiki chenye dhambi, kama ingekuwa hatujaamini katika haki ya Mungu bila shaka tungekuwa tunaufuata mkondo wa kizazi hiki. Hata wenye haki wanaoamini katika haki ya Mungu wanapokuwa wakiishi pamoja na watu wa kidunia hawawezi kabisa kukwepa kushawishiwa na mkondo huu wa kidunia. Hii ndio sababu Biblia inatueleza kuwa tusiifuatishe namna ya dunia hii. 
Inawezekanaje basi kwa wenye haki kutoa ibada yenye maana, ambayo ni sadaka takatifu kwa Mungu kwa mioyo na miili yao yote wakati bado wapo katika ulimwengu huu? Hii inawezakana tu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho inayozifanya upya akili zetu bila kuacha. Wenye haki wanaweza kufahamu na kuyafuata mapenzi makamilifu ya Mungu wanapozifanya upya akili zao na wanapogeuzwa na haki ya Mungu. 
Paulo hasemi hivi ati kwa sababu ya ujinga wake kuhusiana na masuala ya kidunia. Wala hatoi fundisho la kidini kwa waamini kwa kusema, “hebu tuwe wema,” hali akiwa hafahamu mazingira yao na uwezo wao. Sababu inayomfanya Paulo atutie moyo katika kuifanya upya mioyo yetu ili kumtumikia Mungu ni kwa sababu anafahamu kuwa waamini pia wanaweza kusombwa na namna za dunia hii. 
Kwamba tumezaliwa upya au la, miili yetu haitofautiani sana. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya wale ambao wamezaliwa tena upya na wale ambao hawajazaliwa tena upya—hii ndiyo imani katika haki ya Mungu. Ni wenye haki tu ndio wanaoweza kumfuata Bwana kwa kuzifanya upya akili zao hali wakiwa wanaamini katika injili ya maji na Roho. 
Ni nini basi kinachoweza kuifanya upya mioyo yetu? Imani katika Neno la injili ambalo linautangaza ukombozi wetu mkamilifu toka katika dhambi ndilo linaloweza kuifanya upya mioyo yetu. Bwana amezisamehe dhambi zote ambazo tulizitenda kwa miili yetu na kwa akili zetu katika ule udhaifu na mapungufu yetu ya mwili. Akili za mwenye haki zinaweza kufanywa upya kwa sababu Bwana wetu amezisamehe dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake na damu yake Msalabani. Kwa maneno mengine, akili zetu zimefanywa upya kwa sababu tunaamini katika haki ya Mungu. 
Sasa, tunahitaji kuwa na uelewa sahihi wa kile tunachokifanya mbele za Mungu. Ni lazima tutambue jinsi mapenzi yake makamilifu yalivyo, na yale ambayo Mungu anayataka kutoka kwetu, na utume aliotupatia, na yale ambayo wenye haki waliozaliwa tena upya wanapaswa kuyafanya. Ni lazima tuifanye upya mioyo yetu katika maeneo haya na tumtumikie Mungu. Mapenzi ya Mungu yanatutaka sisi kuitoa miili yetu na akili zetu, kujitoa sisi wenyewe kama dhabihu takatifu kwa Mungu. Tunaweza kujitoa sisi wenyewe kama dhabihu kwa Mungu pale tunapozifanya upya akili zetu. Kuzifanya upya akili zetu kunakuja kwa kuamini kuwa Mungu amezichukulia mbali dhambi zetu zote. 
Kuna tofauti kati ya wale waliozaliwa tena upya na wale ambao bado hawajazaliwa tena upya. Ni wenye haki tu ndio wanaoweza kuzifanya upya akili zao kwa uamini katika haki ya Mungu. Sisi wenye haki tunaweza kufanya mambo yanayompendeza Mungu katika imani kwa kuisafisha na kuifanya upya mioyo yetu na kuikana tamaa ya kidunia ya mwili wakati wote. Wenye haki wanatofautiana na wenye dhambi kwa sababu wanaweza kuifanya upya mioyo yao na kumtumikia Bwana wakati wote. 
 

Ni Lazima Uufanye Upya Moyo Wako Kwa Imani 
 
Kuna watu mashuhuri wengi sana katika Televisheni. Watu wa dunia hii wanahangaika kujaribu kuigiza mitindo ya watu hawa mashuhuri. Tunaweza kuona mwenendo mpya au mtindo mpya kwa kuangalia katika Televisheni. Tunaweza kuufungua ulimwengu kwa kutumia rimoti ya Televisheni. Je, maisha yako hayaifuatishi namna ya dunia hii? 
Mimi ninaona kuwa ulimwengu huu unabadilika kwa haraka sana. Pamoja na kuwa kwa sasa tunabeba fedha, nafikiri baadaye tutabeba fedha zilizo katika mfumo wa umeme na kadi zake. Ikiwa kuzipoteza kadi hizi litakuwa ni jambo lenye maudhi huenda basi tukapewa namba za siri katika mikono yetu au katika vipaji vya nyuso ili kuepuka usumbufu. Pia ninafikiria kuwa kutakuwa na majanga mengi ya asili kwa wakati huo. Hebu tuielekeze mioyo yetu katika kuzifanya upya akili zetu na kuieneza injili ya Mungu kabla ya wakati huo haujafika ili kwamba sisi wenye haki tusiifuatishe namna ya dunia hii. 
Kila ninapotembea ninafikiria juu ya namna ya kumtumikia Mungu. Ninapenda kuieneza injili iliyo na haki ya Mungu kwa juhudi kwa kuwa haitakuwa rahisi kuieneza injili hiyo wakati utakapowadia wa kuziweka namba za siri katika mikono yetu na vipaji vya nyuso zetu. Ninafanya kazi bila kuchoka wala kukata tamaa katika kuyafuata mapenzi ya Mungu. Pengine ninaweza kupumzika siku ile ambapo nitakuwa siwezi kufanya kazi tena. Wakati huo ukifika ninaweza hata kutoa kila nilicho nacho kwa ajili ya wenye shida na uhitaji. 
Lakini kwa sasa, ninayafuata mapenzi ya Mungu, nimejitenga na siifuatishi namna ya dunia hii. Baada ya muda kupitia, wenye haki wengi huko Roma ambao walikuwa wameokolewa kwa injili iliyohubiriwa na Paulo walianza kuifuatisha namna ya dunia hii na kumwacha Bwana. Tunapaswa kuwa makini ili tusizifuate nyayo zao. 
Paulo aliandika kifungu hiki akiwa na mashaka kuwa waamini wa Roma walikuwa wakiifuatisha namna ya dunia hii. “Miili yenu inaifuatisha namna ya dunia hii, lakini kuna kitu kimoja cha thamani ambacho mnaweza kukifanya. Zifanyeni upya akili zenu. Je, Bwana hajawakomboa ninyi toka katika dhambi zenu zote? Ikumbeni injili ya haki ya Mungu na mfikirie yale ambayo yanampendeza. Zifanyeni upya akili zenu na mtende matendo mema na yanayokubalika kwa kuishi kiroho na si kimwili.” Hivi ndivyo Paulo alivyowaonya waamini wa Roma na kwetu leo hii. 
Ingawa kwa nje tunajifanya kutoifuatisha namna ya dunia hii, kwa kweli tunaifuatisha namna ya dunia hii. Hata hivyo, bado tunaweza kumtumikia Bwana wetu kwa kuzifanya upya akili zetu. Ingawa katika udhaifu wetu tunaona kuwa ni vigumu sana kutoifuatisha namna ya dunia hii, ukweli unabaki kuwa sisi bado tunaamini kuwa Bwana wetu amezichukulia mbali dhambi zetu zote kwa haki ya Mungu. Hivi ndivyo tunavyoweza wakati wote kuzitumikia kazi za Mungu za haki kwa imani yetu katika haki yake. Tunaweza kuyafuata mapenzi mema na makamilifu ya Mungu kwa kumwamini Mungu. 
Ni lazima tuzifanye upya akili zetu kila wakati. Kwa kuwa wenye haki ambao wameufia ulimwengu huu ni wasafi kulio watu wa dunia basi wao wanakutana na jaribu kubwa zaidi la kutaka kuyarudia mawazo potofu na akili za kidunia kuliko watu wa kidunia. Hii ndio sababu tunapaswa kuitunza mioyo yetu kwa imani yetu katika haki ya Mungu. 
Kwa kuwa Kristo amezichukulia mbali dhambi zetu zote, basi tunachohitaji ni kusimama imara katika imani hali tukijihakikishia wenyewe ule ukweli kuwa imani yetu imefanyika kuwa kamilifu. Je, unaamini kuwa Bwana wetu amezichukulia mbali dhambi zetu zote kwa haki ya Mungu? Ikiwa unaamini hivyo basi unaweza kuzifanya kazi za Bwana wetu kwa imani bila kujali juu ya mapungufu yako ya zamani kwa kuwa Bwana alikwaichukulia mbali hukumu na adhabu ya dhambi zako. 
Ni lazima tuzifanye upya akili zetu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Hii ni muhimu sana. Ikiwa hatuzifanya upya akili zetu kwa kuamini katika injili ya maj na Roho katika wakati huu basi sisi sote hatimaye tutaliacha kanisa na kufa. 
Kuishi maisha ya kufanywa upya kunakoendelea ni sawa na kupanda mlima ukiwa unaendesha baiskeli. Kutozifanya upya akili zetu ni sawa na kusimama ukiwa njiani kilimani na kuacha kukanyaga pedali, katika hali kama hiyo si kwamba utasimama tu bali utarudi nyuma na kuanguka chini ya kilima. 
Kanuni kama iyo hiyo inafanya kazi katika imani yetu katika haki ya Mungu. Sisi tunapandisha kilima tukiwa tunaendesha baiskeli. Kwa kweli ni vigumu kukifikia kilele kwa akili zetu na nia zetu. Tunahitaji kuishikilia haki ya Mungu kwa nguvu kwa kuwa sisi bado tupo katika miili yetu. Hakuna muda unaopita pasipo kuwa na mawazo ya kimwili. 
Mara nyingi tunapoishiwa nguvu tunakata tamaa kwa urahisi. “Siwezi kufanya hivi. Siwezi kuamua kufanya hivi. Nguvu ya dhamira yangu ni dhaifu sana lakini dhamira ya yule ndugu yangu ni kubwa sana. Mimi sina nguvu lakini dada yule ana nguvu sana. Kwa kweli mimi ni dhaifu sana ukinilinganisha na akina kaka na akina dada wale. Wao wanaonekana kuwa wanafaa zaidi na wana nguvu ya kumtumikia Mungu lakini mimi sina nguvu hiyo.” Yeyote asiyeamini na kuishikilia haki ya Mungu anaweza kufikia hatua ya kuacha kupiga pedali na kisha akaanguka chini ya mlima. 
Je, hali hii inawahusu watu wachache? Kwa kweli hapana. Hali hii inawahusu watu wote. Mwendesha baiskeli mzuri anaweza kupanda mlima akiwa na baiskeli kwa urahisi, lakini mtu dhaifu atakuwa na wakati mgumu kuupanda mlima huo. Hata hivyo, tatizo kwa wenye haki halipo katika nguvu zao za kimwili—bali tatizo lao linahusiana na kule kuishikilia imani yao katika injili ya maji na Roho. Haiwezekani kukifikia kilele cha kiroho kwa kutumia nguvu za kimwili. Kuwa dhaifu kimwili au kuwa na nguvu kimwili hakuhusiani chochote na masuala haya ya kiroho. 
Kumbuka kuwa hakuna anayeweza kuishi maisha ya kiimani kwa sababu ya nguvu au nia yenye nguvu aliyonayo. Hupaswi kujilinganisha na wengine na kukatishwa tamaa. Wewe shikilia haki ya Mungu tu. Bwana atatuvusha ikiwa tutaendelea kuzifanya upya akili zetu kwa imani katika haki ya Mungu. Injili ya wokovu ambayo tuliipokea itapandwa katika mioyo yetu na Bwana atatushikilia ikiwa tutaendelea kuichunguza mioyo yetu kila siku. Ni lazima tuyasafishe mawazo yetu mabaya kwa kuamini katika haki ya Mungu na kuifanya kazi ya Bwana. 
Ninamshukuru Bwana wetu kwa neema yake ambayo imetufanya sisi kumtumikia Mungu kwa kuzifanya upya akili zetu. Mungu wetu ameturuhusu kukimbia mbele zake kwa imani yetu kwa kutufanya sisi tuzifanye upya akili zetu. 
 

Nafahamu ya Kuwa Hakuna Jema Likaalo Ndani Yangu 
 
Katika Warumi 7:18 Paulo anasema, “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.” Paulo alifahamu vizuri kuwa hakukuwa na kitu chema katika mwili wake. Kule kusema hakuna kitu chema kinachoweza kukaa katika mwili ndio kanuni. 
Paulo alikiri kuwa hakuna chema kilichokuwa kikikaa ndani ya mwili wake. Alifahamu kuwa haijalishi jinsi alivyokuwa ameipenda Sheria na jinsi alivyokuwa amejitahidi kuishi kwa kuifuata Sheria hiyo, bado alifahamu kuwa hakuweza kuishi kwa kuifuata Sheria hiyo kikamilifu. Moyo unapenda kujifanya upya ili kumfuata Bwana, lakini mwili unapenda bila kukoma kuachana na vita ya kiroho. 
Hivi ndivyo Paulo alivyoomboleza katika Warumi 7:21-24, “Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” 
Je, Paulo aliuelezeaje mwili wake? Aliuelezea kuwa ni “mwili wa mauti.” Je, ni vipi basi kuhusu miili yetu? Je, si miili ya mauti pia? Kwa kweli ni miili ya mauti! Mwili pekee ni mwili wa mauti. Mwili unapenda kutenda dhambi nakwenda mahali ambapo kuna dhambi. Paulo alisema, “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” Na hii ndiyo sababu Paulo alisema, “Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” (Warumi 7:25).
Paulo anaonyesha wazi kuwa kuna sheria mbili. Ya kwanza ni sheria ya mwili. Ni sheria ambayo inatafuta kutimiza na kufuata tamaa za mwili na inadumu katika fikra zamwili ambazo zinapingana na yale ambayo yanamfurahisha Mungu. 
Ya pili ni sheria ya Roho wa uzima. Sheria ya Roho inataka kutuongoza kwenda katika njia sahihi ambayo Mungu anataka tuifuate. Sheria ya Roho inayatamani yale yaliyo kinyume na sheria ya mwili. Sisi Wakristo tunabanwa kati ya sheria hizo mbili hali tukijitahidi kuamua kuwa ni wapi tuelekee. 
Wakati fulani tunaendelea kufuata yale ambao mwili wetu unayataka, lakini tunapozifanya upya akili zetu, basi tutazifuata kazi za Mungu zinazopendwa na Roho. Sababu inayotufanya kuitoa miili yetu kama dhabihu kwa Mungu halafu mara tukatenda mambo ya mwili—ni kwa sababu sisi sote tuna mwili. Kwa hiyo, ni lazima tuzifanye upya akili zetu kwa Roho Mtakatifu. 
Ingawa tumeokolewa, mara nyingi tunaifuatisha namna ya dunia hii kwa sababu tupo katika mwili. Kwa kuwa kila mmoja katika ulimwengu huu anaishi maisha yake hali akiwa anaufuatisha ulimwengu, basi mara nyingi tunashawishiwa kuwafuata hao. Kwa hiyo, kuna njia moja pekee tu ambayo tunaweza kuitumia katika kumfuata Mungu, na njia hiyo ni ile ya kuzifanya upya akili zetu. Tunaweza kuishi hali tukizifanya upya akili zetu katika imani. Hivi ndivyo tunavyoweza kumfuata Bwana wakati wote hadi atakaporudi tena. 
Tukiingalia miili yetu tu, basi hakuna hata mmoja anayeweza kuzifuata kazi za haki za Bwana na sisi sote tumepangiwa kuishia katika maangamizi. Lakini tunaweza kumfauta Bwana kwa kuzifanya upya akili zetu na kuishikilia haki yake kwa mioyo yetu yote. Ni lazima tuzifanye upya akili zetu na kumfuata Mungu. Hii ndiyo sababu katika Warumi 8:2 Paulo alisema kuwa, “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” 
Kwa kupitia haki ya Mungu, Kristo amekifanya kile ambacho Sheria haikuweza kukifanya kwa jinsi ilivyokuwa dhaifu kwa kupitia mwili. Kama Warumi 8:3 inavyosema, “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili.”
Mungu alimtuma Mwanawe pekee Yesu Kristo kuja hapa ulimwenguni na akaihukumu dhambi katika mwili wake. Kule kusema “Aliihukumu dhambi katika mwili” maana yake ni kuwa dhambi zetu zote zilichukuliwa mbali na kwa hivyo tulifanywa kuwa tusio na dhambi. Tulikombolewa toka katika dhambi zetu kwa kuamini katika haki ya Mungu. Ili kuyatimiza masharti ya Sheria ya haki, Mungu alimtuma Mwanawe kuzichukulia mbali dhambi zetu zote kwa kupitia ubatizo wake na damu yake Msalabani na kisha kutuokoa toka katika dhambi zote za ulimwengu. 
Baada ya kuupokea wokovu huu, basi aina mbili za watu zinajitokeza: kwanza ni wale wanaoishi kwa jinsi ya mwili na wanaozielekeza akili zao katika mambo ya mwili, na pili ni wale wanaoishi kwa jinsi ya Roho na wanaozielekeza akili zao katika mambo ya Roho. Ni lazima ufahamu kuwa mawazo ya mwili yanamwongoza mtu kwenda katika mauti, bali mawazo ya Roho yanakuongoza kwenda katika uzima na amani. Mawazo ya kimwili yana uadui na yapo kinyume na Mungu. 
Hatuwezi kuitii Sheria ya Mungu na kamwe hatuwezi kufanya hivyo (Warumi 8:7). Hata wenye haki waliozaliwa tena upya ikiwa hawatazifanya upya akili zao, basi wakati fulani wataangukia katika mawazo ya mwili. Ikiwa hatuamini kuwa Mungu amezichukulia mbali dhambi zetu zote, halafu ikiwa hatutazifanya upya akili zetu, basi kwa hakika tunaweza kwa urahisi kabisa kuangukia katika matendo ya mwili na hatuwezi kumfuata Bwana. Hii ndiyo sababu tunapaswa kuzifanya upya akili zetu mara kwa mara. 
Paulo alisema kuwa, sisi, tuliozaliwa tena upya tunaweza ama kuangukia katika mwili kwa kuyafuata mawazo ya mwili, au tunaweza kuyafuata mawazo ya Roho kwa kuzifanya upya akili zetu. Sisi tunaelea kati ya mambo hayo mawili. Lakini bado Paulo alisema, “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata Roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake” (Warumi 8:9). 
Sisi ni watu wa kiroho wa Mungu. Kwa maneno mengine, sisi ni watu wake. Pamoja na kuwa tunazifuata tamaa za dunia na kuzifuatisha katika udhaifu wetu, ukweli unabakia kuwa sisi ni wale tuliozaliwa tena upya. Mara nyingi tunaangukia katika mwili pale tunapokuwa tumezielekeza akili zetu katika mambo ya mwili, lakini kwa kuwa tuna Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu, basi ukweli unabakia kuwa sisi ni watu wa Kristo. Pia unaweza kusema kuwa sisi ni watu wa Mungu tuliofanyika wenye haki. 
Paulo alisema, “miili yetu imekufa pamoja na Kristo.” Halafu akaongezea, “Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki” (Warumi 8:10). Mawazo yetu ya kiroho ni lazima yaamshwe. Sisi bado tu dhaifu, na miili yetu inaweza kwenda kinyume kwa urahisi hadi wakati wa kifo chetu. Lakini akili zetu na mawazo ni lazima yafanywe kuwa upya kwa kuamini katika haki ya Mungu. 
Kila tunapotambua kuwa ndani yetu kuna tamaa ya dhambi basi hebu tuyaelekeza macho yetu juu ya haki ya Mungu. Hapo tunaweza kutambua kuwa haki ya Bwana imezichukulia mbali dhambi zetu zote. Itazame haki ya Mungu na uiamini. Mshukuru Mungu kwa kuzichukulia mbali dhambi zetu zote na kisha fikiria juu ya matendo na kazi za Mungu zinazompendeza. Ukifanya hivyo basi akili zako zitafanywa kuwa upya. 
Ni lazima tuzifanye upya akili zetu kwa imani na kisha tuzielekeze akili zetu katika mambo ambayo yanampendeza Mungu. Hivi ndivyo wenye haki wanavyopaswa kuishi. Ni kwa kufanya hivi ndipo tunapoweza kumfuata Bwana hadi atakaporudi tena. Ninafahamu kuwa sisi sote tumechoshwa na maisha yetu ya kila siku. Ni vigumu kufanya kazi na ni vigumu pia kuja kanisani. Kila mtu anakutana na magumu. Wakati mwingine huwa ninamwonea wivu Yesu pale alipokuwa akilia wakati wa kifo chake na kusema, “imekwisha.” Nina ujasiri kuwa sisi pia tutaweza kusema “imekwisha,” na kisha tukawa huru kutokana na magumu haya yote. 
Kuja kwa Bwana wetu mara ya pili kunakaribia. Basi hebu tuzifanye upya akili zetu hadi wakati huo pasipo kuifuatisha namna ya dunia hii. Kwa kuwa ili kumfuata Bwana, mioyo yetu inahitaji kuishikilia haki ya Mungu, basi ni lazima akili zetu zifanywe upya kila mara. Hivi ndivyo tunavyoweza kumfuata Bwana hadi atakaporudi tena. Wakati umekaribia sana. 
Hivi karibuni nilisoma makala moja katika gazeti ambayo iliripoti kuwa shimo la ukanda wa ozoni katika ncha ya Antaktika limekuwa kubwa mara tatu ya bara zima la Amerika Kaskazini. Pia nilisoma makala nyingine kuhusiana na mpango wa makombora ya kujihami. Mpango huu unalenga katika kuyalenga na kuyapiga makombora ya masafa ya kati na kwamba utafiti wa msingi unaonyesha kuwa kuna mafanikio. Maana ya maendeleo haya ipo wazi: mazingira yataendelea kuharibiwa zaidi hasa pale ambapo nguvu za kijeshi zinazidi kuzidishwa mara kadhaa. 
Ikiwa nchi inaongeza nguvu zake za kijeshi, je, maadui au wapinzani wake nao hawataongeza nguvu hizo ili kulingana na ongezeko hilo? Mataifa yote ya ulimwenguni hayataweza kukaa kimya na kuiona nchi moja ikikua na kuwa na nguvu za kivita. Je, nini kitatokea ikiwa mataifa haya yataingia katika vita? 
Wakati baadhi ya mataifa yalipojaribu kutengeneza silaha za Nyuklia yale mataifa yenye nguvu kubwa yalijaribu kwa nguvu zote kuwazuia ili wasiwe na uwezo huo wa kinyuklia. Lakini hebu tuseme kuwa mbinu hizo za kuwazuia zimeshindikana na nchi husika imefaulu kuwa na silaha hizo za maangamizi makubwa na halafu ikatishia kuzitumia. Basi kwa hakika mataifa mengine yaliyosalia yatajitahidi kutengeneza silaha mpya ili kukabiliana na hali hiyo. 
Silaha hizo mpya zitaiangamiza dunia hii, silaha ambao zina nguvu zaidi kuliko silaha za nyuklia. Kwa sasa vita havipiganwi kwa bunduki kama ilivyokuwa hapo zamani. Hakutakuwa na suala la kuwaua wanadamu, bali mji mzima au nchi nzima inaweza kufutwa kwa dakika chake. Vita ya nyuklia haitaweza kufanywa kuwa ya kawaida bali itasababisha vita nyingine ya dunia. Baada ya kuwa tumeharibiwa na vita hivyo, sasa maangamizi makubwa yatatujia kutokana na majanga ya kiasili. Ukanda wa ozoni utaharibiwa kwa haraka zaidi na kwa sababu hiyo mawimbi na dhoruba yatainuka kutokana na uharibifu wa mazingira. Kisha hapo Mpinga-Kristo atatokea kwa nguvu kubwa na kuushinda ulimwengu huu. 
Unaweza kusema kuwa ninakielezea kisa hiki kupita zaidi, lakini ukweli ni kuwa kimsingi, asili ya mwanadamu ni yenye uovu. Mataifa yanazidi kuimarisha majeshi na yanaunda silaha mpya ambazo haziwezi kutumika kamwe kwa madhumuni mazuri. Silaha za nyuklia zinaweza kulinganishwa na aina moja ya silaha za maangamizi ya halaiki. Nchi zitapigana ili kwamba ziweze kusalimika. Nchi nyingine zitajitahidi kujiunga na nchi fulani ambayo inataka kuutawala ulimwengu. Lakini haijalishi kuwa silaha hizo zina mipango gani, ukweli unabaki kuwa silaha za nyuklia na uwezo wa kijeshi vinaweza kutumika kwa ajili ya madhumuni mabaya. 
Hapo zamani, Paulo aliwaambia waamini huko Roma kutoifuatisha namna ya dunia hii bali wamfuate Bwana kwa kuifanya upya mioyo yao. Kwa kweli hiki ni kifungu kizuri sana kwetu sisi ambao tunaishi katika kipindi hiki. Katika siku hizi za mwisho, ni lazima tutambue mapenzi ya Mungu jinsi yalivyo mema na yanayofurahisha na kisha tumfuate Bwana wetu kwa imani. 
Ingawa tuna mapungufu mengi, Bwana wetu ni Mungu Mwenyezi mwenye nguvu. Mungu Mwenyezi anakaa ndani yetu kama Roho Mtakatifu. Ingawa miili yetu inaweza kuwa na udhaifu, Roho Mtakatifu aliye ndani yetu ana nguvu sana. Huyu Roho Mtakatifu anazifanya upya akili zetu kwa imani katika Neno ili kwamba tuweze kumfuata Bwana. 
Hebu sisi sote tuzitegemee nguvu za Roho Mtakatifu, tuzifanye upya akili zetu na tumtumikie Bwana. Ikiwa Bwana atarudi hali tukiwa tunamtumikia, basi itakuwa vema kama tutaenda naye. Tutaishi tukiendelea kuieneza haki ya Mungu hadi siku ile ambayo Kristo atarudi. Zifanye upya akili zako kwa kuamini katika haki ya Mungu.