Search

សេចក្តីអធិប្បាយ

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[15-2] Kituo cha Kugawa Hatma ya Milele (Ufunuo 15:1-8)

(Ufunuo 15:1-8)
 
Sura ya 15 inaeleza juu ya mapigo ya mabakuli saba, ambayo yatamiminwa mara baada ya kunyakuliwa kwa watakatifu, mapigo hayo yatamiminwa juu ya wale ambao watakuwa wamesimama kama maadui wa Mungu. Namba “saba” ambayo inajitokeza sana katika kitabu cha Ufunuo, kama vile mihuri saba, matarumbeta saba, na mabakuli saba, inasimama kumaanisha ukamilifu wa Mungu na nguvu zake kuu. Yesu Kristo ni Mungu mwenye nguvu na anayejua yote. Kule kusema kuwa Yesu ni Mungu mwenye nguvu na anayejua yote kuna maanisha kuwa Bwana wetu ni Mungu Mwenyezi ambaye kwake yeye hakuna kisichowezekana. Bwana wetu ni Mungu Mwenyewe ambaye amepanga vitu vyote na ambaye ana nguvu na mamlaka ya kuvitumiza vyote. 
Hivyo, watakatifu wanapaswa kumsifu Bwana kwa uwezo wake mkuu na unaoweza yote ambao umedhihirika kupitia mapigo ya mabakuli saba ambayo atayamimina katika ulimwengu huu. Tunamshukuru Bwana wetu kutokana na ukweli kuwa hukumu ya jinsi hiyo imefanywa iwezekane kwa kupitia uwezo na nguvu zake. Ule ukweli kuwa Bwana atalipiza kisasi kwa ajili ya watakatifu kwa maadui wake kwa mapigo ya mabakuli saba na mateso ya milele kuzimu, basi ni jambo ambalo watakatifu wanapaswa kushukuru kwa kuwa ukweli huo ni sahihi kabisa. Hivyo, watakatifu hawawezi kufanya lolote zaidi ya kumsifu Bwana. Haleluya!
Mapigo ya mabakuli saba yatawasili mara baada ya watakatifu kunyakuliwa baada ya kuipita miaka mitatu na nusu katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu. Kutokana na mapigo ya mabakuli haya saba, mioyo ya maadui wa Mungu itahuzunishwa, kwa kuwa watagundua kuwa Bwana wetu ni Mungu Mwenyezi, na hivyo watamhofia na kumwogopa Mungu. 
Ile “ishara kubwa mbinguni, na ya ajabu” inayoelezwa katika aya ya 1 ina maanisha ni mapigo ya mwisho ambayo yatamwagwa katika ulimwengu huu—yaani, mapigo ya mabakuli saba. Kwa upande mwingine, ule msemo unaosema “kubwa na ya ajabu” unatueleza katika namna tatu: kwanza, watakatifu, kwa kupitia Neno la unabii wanafahamu kila kitu kuhusu mapigo ambayo yataujilia ulimwengu huu; pili, watakatifu wataondolewa toka katika mapigo ya mabakuli saba; na tatu, nguvu ya haya mapigo ya mabakuli saba yatakayoletwa na Bwana yatakuwa katika ulimwengu mzima na yatakuwa yenye maangamizi ya kifo. 
Kwa upande mwingine, watakatifu waliokombolewa na kunyakuliwa wataimba “wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-kondoo” wakiwa angani. Msingi wa wimbo huu, kama unavyoonekana katika kitabu cha Kutoka 15:1-8, ni wimbo wa Waisraeli, ambao walikuwa wakimtukuza Bwana kwa nguvu na mamlaka yake baada ya kuvuka Bahari ya Shamu wakiongozwa na Musa. Hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kumsifu na kumtukuza Mungu kwa kuwaokoa kwa nguvu na mamlaka yake toka katika hali tete ya kufuatiwa na jeshi la Wamisri. 
Vivyo hivyo, watakatifu wa Agano Jipya hawawezi kufanya lolote zaidi ya kumsifu Bwana kwa wokovu wao wa milele, ambao umekuja kwa kupitia ondoleo la dhambi lililotimizwa kwa ubatizo wa Yesu alioupokea toka kwa Yohana na kwa damu yake Msalabani. Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, watu wa Mungu watamsifu tena Bwana, wakimshukuru kwa kuifia-dini, kwa ufufuo, unyakuo na uzima wa milele, mambo hayo yatakuwa yamewezekana kwa kupitia Yesu Kristo aliyewakomboa toka kwa adui zao na toka katika dhambi zao zote. 
Kwa nyongeza, jambo la muhimu na la kipekee kwa wimbo huu ni kwamba unasifu nguvu za Bwana, uwezo wake, na haki yake. Wafia-dini hawataweza kufanya lolote zaidi ya kumsifu Bwana kwa nguvu zake, kwa neema ya wokovu toka katika dhambi, na baraka ya uzima wa milele. 
“Hekalu la hema takatifu la ushuhuda” katika aya ya 5 lina simama kumaanisha Hema Takatifu la Kukutania ambalo Mungu aliliruhusu kwa Waisraeli wakati walipoondoka Misri ili aweze kuwapatia baraka za kuandamana na Bwana. 
“Kitani” katika aya ya 6 ina simama kumaanisha haki ya Mungu. Inatueleza kuwa malaika watavikwa haki ya Mungu na kisha kupokea mamlaka toka kwa Mungu ya kutoa hukumu ambayo hakuna adui anayeweza kuikataa. 
Aya ya 8 inasema, “Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, hata yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba.” Hapa tunaweza kuzigundua maana tatu. Kwanza, aya hii inaonyesha jinsi hasira kamilifu ya Mungu ilivyo kwa adui zake. 
Pili, inatueleza kuwa hakuna anayeweza kuingia katika Hekalu la Bwana pasipo kuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo na damu yake, hii ni kwa kuwa wokovu wa Mungu kwa wenye dhambi ni mkamilifu sana. 
Tatu, inaonyesha kuwa hakuna wema wa mwanadamu unaoweza kumwezesha yeyote yule kuikwepa hukumu ya haki ya Mungu, na kwamba ni kuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo na damu yake ndipo mtu anapoweza kuikwepa hasira ya Mungu itakayomiminwa kwa kwenye dhambi. 
Hivyo, watakatifu ni lazima waishikilie injili na kuihubiri hadi wakati wa mwisho. Na wale ambao bado hawajapokea ondoleo la dhambi zao ni lazima watambue kuwa wamefungwa na watakabiliana na hukumu ya haki ya Mungu, hivyo ni lazima wairudie haraka iwezekanavyo injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Kifungu hiki kinatuonyesha kuwa, ile hukumu ambayo Mungu ataileta kwa maadui zake kwa mapigo ya mabakuli saba ni kamilifu mbele ya wote watakaoiona, na kwa sababu hiyo hakuna yeyote atakayeweza kuizuia hadi hukumu hii ya dhambi itakapokuwa imekamilika. 
Sura ya 15 katika kitabu cha Ufunuo inatuonyesha kuwa Mpinga Kristo, Shetani, mapepo, na wale wote wanaosimama kinyume na kutoiamini injili ya maji na Roho, ambayo imeletwa kwetu kwa upendo wa Kristo, ni maadui wa Bwana wetu. Nimsifu na kumshukuru Bwana kwa kuyaleta mapigo yake kwa maadui hawa wa Mungu ili kuwahukumu. Ni sahihi kabisa kwa watakatifu kumsifu Bwana kwa wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu, na kwa wimbo wa Mwana-kondoo. 
Hakuna anayeweza kutuzuia kuisifu haki ya Bwana, nguvu, uweza, na ukweli yake. Ninamsifu Bwana kwa kutupatia baraka kama hizo. Haleluya! 