Search

တရားဟောချက်များ

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-1] Utangulizi Kwa Sura ya 8

Pengine sura ya 8 inaweza kuelezewa kuwa ni sura muhimu sana miongoni mwa sura kadhaa za kitabu hiki cha Warumi. Paulo anatufunulia jinsi ambavyo haki ya Mungu ilivyo ya kushangaza kwa kupitia mada mbalimbali ambazo zinapatikana katika kitabu hiki. 
Mada ya kwanza ni: “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu” (Warumi 8:1). Hii inamaanisha kuwa bila kujali jinsi ambavyo tunaweza kuwa waovu na wasio na thamani katika mwili, ukweli ni kuwa haki ya Mungu imetuweka huru mbali na dhambi zote. 
Mada ya pili ni: “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili” (Warumi 8:3). Hii ina maanisha kuwa kwa kuwa watu katika hali ya mwili hawakuweza kuifuata Sheria iliyokuwa imetolewa na Mungu, basi Yesu Kristo, kwa kuzichukua dhambi zote katika mwili wake kwa ubatizo wake na kifo chake Msalabani aliwaokoa watu wote toka katika dhambi na hukumu zao. Yesu alikuja hapa duniani na akazichukua dhambi zote za mwanadamu mara moja kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana na ndio maana Yesu aliweza kuzibeba dhambi zote za ulimwengu katika Msalaba wake, akasulubiwa, kisha akafufuka ili kuwaokoa wote wanaoamini katika ukweli huu. Kazi hizi zote za Bwana wetu zililengwa kuitimiza haki ya Mungu ya kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zao kwa unyenyekevu na kwa mapenzi ya Mungu Baba. 
Mada ya tatu ni: “Kwa maana wale waufutao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya Roho.” (Warumi 8:5). Hii ina maanisha kuwa wakati tunapoamua kumwamini Mungu, basi tunapaswa kumwamini Mungu kwa kutofuata mawazo yetu binafsi bali tulifuate Neno la Mungu. 
Mada ya nne ni: “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata Roho.” (Warumi 8:9). Wale wanaoamini katika haki ya Mungu wamempokea Roho Mtakatifu katika mioyo yao na wamefanyika kuwa wana wa Mungu. Hii pia ina maanisha kuwa huwezi kufanyika mwana wa Mungu ati kwa sababu tu unahudhuria kanisani kwa juhudi. 
Mada ya tano ni: “Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili” (Warumi 8:12). Mada hii inatueleza sisi kuwa wale walio okolewa toka katika dhambi zao zote kwa kuamini katika injili ya Bwana wetu ambayo imeitimiza haki ya Mungu hawawezi kuwa wadeni na watumwa wa miili yao. 
Mada ya sita ni: “Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani Baba” (Warumi 8:15). Kwa sababu wale wanaoamini katika Mungu wamempokea Roho Mtakatifu, ndio maana sasa wanamwita Mungu “Aba, yaani Baba.”
Mada ya saba ni: “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, yakuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo” (Warumi 8:16-17). Wale wanaoamini katika haki ya Mungu ni wale waliopokea Roho Mtakatifu, na wale waliopokea Roho Mtakatifu ndio wale ambao watakuwa warithi wa Ufalme wa Mbinguni pamoja na Kristo. 
Mada ya nane ni: “Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja navyo vina utungu pamoja hata sasa” (Warumi 8:22). Hii inatueleza sisi kuwa hata waamini katika haki ya Mungu wanakutana na mateso katika ulimwengu huu pamoja na viumbe vingine vyote, pia mada hii inatueleza sisi kuwa katika ulimwengu ujao hakutakuwa na manung’uniko wala maumivu. 
Mada ya tisa ni: “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza” (Warumi 8:30). Hii inatueleza sisi kuwa Mungu amewaita wenye dhambi katika Mwana wake Yesu Kristo, na kwamba amewafanya kuwa watoto wake kwa kuziondolea mbali dhambi zao zote mara moja kwa haki yake. 
Mada ya kumi na ya mwisho: “Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki” (Warumi 8:33). Hakuna anayeweza kuwahukumu watoto wa Mungu ambao wamempokea Roho Mtakatifu kuwa ni karama yao kwa ukombozi toka katika dhambi kwa kuamini katika haki ya Mungu. 
Mada hizi kumi ni mihutasari ya msingi ya kitabu cha Warumi sura ya 8. Sasa tutageukia ili tuweze kuzichunguza mada hizo kwa kina katika mjadala wetu mkuu.