Search

उपदेश

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[9-1] Pigo Toka Shimo Lisilo na Mwisho (Ufunuo 9:1-21)

(Ufunuo 9:1-21) 
“Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni. Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi. Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wowote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao. Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu. Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia. Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu. Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani. Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao. Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni. Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili zinakuja baadaye. Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu, ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue hao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati. Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu. Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi; nilisikia hesabu yao. Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoa moto na moshi na kiberiti. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao. Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo. Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda. Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu.
Kile kitendo cha Mungu kumpatia malaika ufunguo wa shimo la kuzimu lisilo na mwisho maana yake ni kwamba aliamua kuleta pigo la kutisha kama kuzimu kwa mwanadamu.
Shimo lisilo na mwisho linafahamika kuwa ni kuzimu, maana yake ni sehemu ya kina kisicho na mwisho. Mungu atalifungua shimo hili la kuzimu ili kuleta mateso kwa Mpinga Kristo atakayekuwa akiishi duniani pamoja na wafuasi wake, na kwa wale wote wanaosimama kinyume dhidi ya wenye haki. Malaika wa tano alipewa ufunguo wa kulifungua shimo hili la kuzimu. Hili ni pigo la kutisha sana ambalo linatisha kama kuzimu inavyotisha.
 
Aya ya 2: Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni.
Wakati Mungu aliporuhusu kufunguliwa kwa shimo lisilo na mwisho, ulimwengu mzima ulijazwa na vumbi kama majivu ya volkano, na hivyo kulileta pigo la giza. Pigo hili la giza limehifadhiwa kwa ajili ya wale wanaopenda giza. Mungu ni Mungu wa nuru anayetuangazia, akitupatia injili ya maji na Roho kwa kila mtu. Kwa wale wanaouamini ukweli huu, Mungu amewapatia neema ya wokovu na amewaruhusu kuishi katika nuru yake angavu. Lakini wale wasioupokea ukweli wanakabiliana na ghadhabu ya haki ya Mungu, kwa kuwa Mungu atawaletea pigo la giza na hukumu yake ya haki.
Kimsingi, wanadamu wanazaliwa wakiwa wenye dhambi, na wanapendelea giza kuliko nuru katika maisha yao. Hivyo wanastahili kupokea pigo la giza toka kwa Mungu kwa kuikataa na kutoiamini injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana.
 
Aya ya 3: Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi.
Mungu atawatuma nzige katika ulimwengu huu na kisha kuziadhibu dhambi za wale wanaoupinga ukweli wa Mungu katika mawazo yao ya kiasili. Pigo hili la nzige linaweza kuleta maumivu ya kutesa kama yale ya kuumwa na nge. Hivyo, wenye dhambi wote wa ulimwengu huu wanapaswa kuuamini upendo wa kweli wa Mungu. Na wale wasiouamini upendo huo wa Mungu, basi watapata uzoefu wa kuona jinsi maumivu ya ya kuukataa upendo wa Mungu ulivyo.
Mungu aliwatuma nzige hapa duniani na akawafanya watu kulipa mshahara wa dhambi zao kwa kusimama kinyume na Mungu wa kweli kwa mawazo yao ya kiasili. Gharama hii dhambi ni mateso toka katika pigo la nzige.
 
Aya ya 4: Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wowote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.
Wakati Mungu atakapolileta pigo la kutisha la nzige, hatasahau kuonyesha huruma yake kwa wale watakaokuwa wametiwa muhuri yake. Pia anawaamuru nzige wasiidhuru nchi na miti.
 
Aya ya 5: Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu.
Katika kitabu cha Wimbo Ulio Bora 8:6, Mungu anazungumzia juu ya upendo wake na hasira yake, anasema, “Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, na wivu ni mkali kama ahera; mwako wake ni mwako wa moto, na miali yake ni miali ya Yahu.” Vivyo hivyo, pigo hili linatueleza jinsi adhabu ya Mungu ilivyo kali kwa wale wanaoukataa upendo wa Mungu ulioonyeshwa kupitia injili ya maji na Roho. Pigo hili litawatesa watu kwa miezi mitano.
 
Aya ya 6: Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.
Pigo la nzige litaleta mateso makubwa sana kiasi kwamba watu watatamani kufa kuliko kuishi kwa mateso hayo, lakini bado hawataweza kufa hata kama watakuwa wakitamani kufa. Pigo hili limekuja kwa sababu watu walimdharau Mungu. Wakidhani kuwa mwisho wa maisha ya kimwili ndio mwisho wa yote, wanamdharau Mungu, ambaye anatawala juu ya uzima na mauti. Lakini kwa kupitia pigo hili la nzige, Mungu anatuonyesha kuwa hata kifo hakiwezi kuja pasipo kibali cha Mungu.
 
Aya ya 7-12: Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu. Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani. Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao. Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni. Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili zinakuja baadaye.
Mikia ya nzige toka katika shimo lisilo na mwisho wana nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. Pamoja na kwamba mwonekano wa nzige hao ni kama wanawake, nzige hawa ni viumbe jasiri na katili sana. Hii inaonyesha dhambi kubwa ambayo wanaume wameifanya kwa kuwafuata wanawake kuliko kumfuata Mungu. Tusisahau kwamba Shetani anataka kutufanya tuanguke katika dhambi ya uasherati na kisha kutunyakulia mbali toka kwa Mungu, anafanya hivyo kwa kuleta dhambi ya tamaa ya mwili katika maisha yetu.
 
Aya ya 13-15: Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu, ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue hao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati. Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.
Hukumu ya Mungu ya dhambi, ambayo ameingojea kwa muda mrefu kwa ajili ya mwanadamu itakuwa imeanza. Sasa ni pigo la vita ambalo litaua theluthi ya wanadamu katika Mto Frati.
 
Aya ya 16: Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi; nilisikia hesabu yao.
Hapa, idadi ya jeshi la wapanda farasi imeelezwa. Vita hii inaonyesha juu ya vita ya kisasa inayotumia umeme. Pamoja na kuwa theluthi ya wanadamu itauawa katika vita hivi, bado wale watakaokuwa wamebaki wataendelea kuabudu miungu na kusimama kinyume na Mungu, na watakataa kuzitubia dhambi zao. Hii inaonyesha jinsi ambavyo moyo wa kila mtu utakavyokuwa umefanywa mgumu kutokana na dhambi zake katika nyakati za mwisho.
 
Aya ya 17: Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoa moto na moshi na kiberiti.
Alichokiona Mtume Yohana ilikuwa ni silaha ya maangamizi ya kutisha ya karne ya 21, kama vile vifaru, ndege za kivita, pamoja na silaha nyingine za kisasa.
 
Aya ya 18-19: Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao. Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo.
Vita kubwa inayotumia silaha za kisasa itakuja katika nyakati za mwisho. Na theluthi ya wanadamu watakufa kutokana na pigo la moto na moshi na kiberiti vitakavyotoka katika silaha hizo.
 
Aya ya 20: Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda.
Pamoja na mapigo haya, wale waliosalia baada ya vita hiyo wataendelea kuabudu na kuziinamia sanamu zaidi, kwa kuwa watu hawa watakuwa wameandaliwa ili kuangamizwa.

Aya ya 21: Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao.
Hii inatuonyesha kuwa nyakati za mwisho, mwanadamu hatazitubia dhambi zake mbele za Mungu. Hivyo, Mungu atawahukumu wenye dhambi, lakini atauruhusu ulimwengu mpya na ulio barikiwa kwa wenye haki.