Search

उपदेश

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[17-2] Umakini Wetu Uzingatie Mapenzi ya Mungu (Ufunuo 17:1-8)

(Ufunuo 17:1-8) 
 
Ufunuo 17:1-5 inasema, “Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi, ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake. Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi. Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake. Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa: 
LA SIRI, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.”
Kahaba anayetajwa katika kifungu hicho hapo juu anasimama kumaanisha juu ya dini za ulimwengu huu, kifungu hiki kinatueleza kuwa wanadini hao walikuwa wamejiingiza katika anasa za kutupwa kwa vitu vya ulimwengu na kwa vitu vingi ambavyo Bwana alikuwa amevitoa. Walijikita katika aina zote za anasa, kwa kuvaa mikufu ya dhahabu, na heleni za almasi, na kwa kujipaka mafuta yenye manukato mbalimbali. Kifungu hiki kinatueleza kuwa yule mwanamke alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu mkononi mwake, ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na uchafu kwa sababu ya uasherati wake. Haya ndiyo ambavyo Mungu alimwonyesha Yohana. 
Kifungu hiki kinatueleza kuwa Shetani anafanya uhaini katika nafsi za watu na anatafuta kuwafanya wamtii yeye kwa kuwafanya walewe kwa vitu vya hapa ulimwenguni. Pia wafalme wote wa ulimwengu, wameleweshwa na Shetani kwa kutumia vitu vya hapa ulimwenguni. Hivyo, kila mtu hapa duniani ameleweshwa kwa mvinyo wa uasherati wa ulimwengu. 
Shetani anafikia malengo yake wakati watu wanapokuwa wameleweshwa na mawimbi ya ulimwengu huu, yaani starehe zake na tamaa ya vitu na mali. Ukweli ni kwamba lengo la Shetani ni kuwazuia watu ili wasimwangalie Mungu. Ili kufanya hivyo, basi Shetani anazifanya nafsi za watu kuleweshwa na vitu vya ulimwengu huu. Ni lazima tuutambue ukweli huu. 
Hakuna hata mmoja katika ulimwengu huu ambaye hawezi kuuangukia mtego wa tamaa ya vitu na mali. Kila mmoja anaangukia katika hali kupenda vitu na mali. Mielekeo yote ya mitindo ya kisasa hapa ulimwenguni inadhibitiwa na Shetani. Kila mmoja anafikiri kuwa ana mtindo wake wa kipekee. Lakini nyuma ya fikra kama hizo, yupo mmoja anayezitawala na kuziongoza, na huyo si mwingine bali ni Shetani. Hii ndio sababu kwamba hatupaswi kuishi maisha ya kuzama katika tamaa ya vitu na mali, badala yake tunapaswa kuishi kwa kulishika na kulimeza Neno la Mungu na kuzitenda kazi zake. 
Neno la Ufunuo ambalo Mungu analifunua kwetu kwa kupitia Mtume Yohana ni ukweli. Sasa, ni jambo gani basi ambalo Mungu anataka kutueleza kwa kupitia Neno hili? Bwana wetu anatueleza kuwa hatupaswi kujilowanisha pamoja na ulimwengu huu, bali tunapaswa kusimama kinyume na ulimwengu. Kwa maneno mengine, Mungu anatueleza sisi watakatifu kumfikiria na kumwamini Mungu kwa mioyo yetu yote. 
1 Yohana 2:15 inasema, “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.” Wakati mioyo yetu inapotokea kupenda vitu vya ulimwengu huu, basi ni hakika kuwa Mungu hawezi kukaa ndani ya mioyo yetu. Lakini wakati mioyo yetu inapotumbilia mbali vitu vya ulimwengu huu, basi hapo Mungu anaweza kukaa katika mioyo yetu. Hatupaswi kuishi maisha yetu hali tukiwa tumeloweshwa katika tamaa ya vitu vya ulimwengu. Tunaweza kuongozwa na mwongozo wa Mungu pale tu tutakapokuwa tukilitafakari Neno la Bwana wetu na dhumuni lake. 
Tunaweza kuyabadilisha mawazo yetu wakati wowote ule. Wakati tamaa ya vitu vya ulimwengu inapojaribu kuingia katika mioyo yetu, basi tunapaswa kuikataa tamaa hiyo. Hapo ndipo tunapoweza kuyasukumia mbali mambo yote ya machafu ya ulimwengu huu toka katika mioyo yetu. Ni kitu gani ambacho Bwana wetu anakitaka toka kwetu? Na ni jambo gani ambalo Mungu anatueleza kulifanya? Ni kuhakikisha kuwa mawazo ya kimungu yanachipua katika mioyo yetu, na kwamba ni lazima tuyafute mambo ya kidunia katika mioyo yetu. 
Mungu ametupatia baraka nyingi sana, na sasa tunatambua kuwa tunapaswa kuihubiri injili ya maji na Roho kwa watu wa ulimwengu mzima katika siku zetu zilizosalia. Hivyo, hatuuachi umakini wetu ili kuzingatia mapenzi ya Mungu. Tunaweza kuiondolea mbali tamaa ya vitu vya ulimwengu iliyo katika mioyo yetu kwa kuzifikiria kazi za kiroho. 
Sisi watakatifu ni lazima tuiondolee mbali tamaa ya vitu vya ulimwengu. Tunapaswa kuishi maisha ya Kikristo kwa imani hadi Bwana atakaporudi tena. Tunapaswa kufanya kile ambacho Bwana ametukabidhi katika maisha yetu yaliyosalia, yaani hadi siku ile tutakaposimama mbele za Mungu. Pia tunapaswa kumpenda Bwana, na kisha kuishi kwa imani, na kufanya kazi yoyote ambayo atakuwa ameturuhusu kuifanya.