Search

خطبات

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 14] Msihukumiane

Warumi 14:1 inasema, “Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake.”
Paulo aliwaonya watakatifu huko Rumi kwamba wasihukumiane wala kubishania imani za wao kwa wao. Kwa wakati huo, kwa kuwa kulikuwa na watu ambao walikuwa ni waaminifu sana na wale ambao hawakuwa waaminifu sana katika kanisa la Rumi, basi hali hiyo ilisababisha kulaumiana na kubishania imani kati ya wao kwa wao. Ikiwa jambo hili litatokea kwako basi unapaswa kuheshimu imani ya mtu mwingine na jitahidi kuepuka mabishano yoyote na watumishi wa Mungu. Kwa kweli suala la kuwainua na kuwajenga watumishi wake si kazi yetu bali ni kazi ya Mungu mwenyewe. 
Hata ndani ya Kanisa la Mungu, kuna matatizo mengi ambayo yanajitokea kati ya waamini. Ikiwa tutaziangalia imani zao basi tunaweza kuzipata aina mbalimbali za imani. Baadhi walikuwa wamefungwa kwenye Sheria kabla ya kukombolewa kwao na kwa sababu hiyo bado wanayo ile harufu ya maisha yao ya kwanza ya kisheria katika imani yao. 
Baadhi ya Wakristo wanaweka mkazo mkubwa katika kuchagua aina ya vyakula. Kwa mfano, watu wa jinsi hiyo wanaweza kuamini kuwa hawapaswi kula nguruwe. Baadhi wanaweza kuamini kuwa wanapaswa kuishika na kuitunza Sabato katika hali yoyote ile. Lakini tunapaswa kuzitatua tofauti hizi za kiimani katika haki ya Mungu na kutolaumiana sisi kwa kwa sisi juu ya mambo madogo kama hayo. Huu ndio mkazo ambao Paulo alikuwa akiuzungumzia. 
Paulo anafundisha katika sura ya 14 kuwa hatupaswi kuwalaumu waamini wenzetu kutokana na udhaifu wao ili mradi wanayo imani katika haki ya Mungu. Kwa nini tusiwalaumu? Kwa sababu hata kama ni wadhaifu, wao pia wanaamini katika haki ya Mungu.
Biblia inawachukulia wote waliokombolewa toka katika dhambi zao kwa kuiamini haki ya Mungu kuwa ni watu wa thamani wa Mungu. Ijapokuwa wanaweza kuonana wao kwa wao kuwa wana mapungufu, lakini ukweli unabaki kuwa Mungu ametuamuru sisi kutolaumiana na kwa msingi wa imani ya kila mwamini. Hii ni kwa sababu hata kama waamini hao watakuwa na mapungufu ya mwilini, bado waamini hao wamefanyika kuwa watoto wa Mungu kwa imani. 
 

Imani ya Kila Mmoja Inatofautiana na Imani ya Mwingine 
 
Aya za 2-3 zinasema, “Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali.”
Kunaweza kuwa na tofauti kati ya watumishi wa Mungu katika kuiamini haki yake na kumfuata Mungu. Imani katika wokovu ni moja lakini kiwango cha imani katika Neno lake kinaweza kutofautiana. 
Ikiwa mtu mmoja amekuwa akiishi maisha ya kisheria kabla ya kuzaliwa upya katika injili ya haki ya Mungu, basi mtu wa jinsi hiyo atahitaji muda ili aweze kuachana na hiyo haki yake binafsi kwa kuamini kikamilifu katika haki ya Mungu. Watu wa jinsi hii wanaweza kuweka mkazo mkubwa katika kuishika Sabato, lakini usiwalaumu kwa sababu hata wao wanaiamini haki ya Mungu. 
Mungu anaridhishwa na imani ya wale wanaofahamu na kuamini katika haki ya Mungu. Mungu amewachukulia kuwa ni watu wake. Kwa hiyo, wale wanaoamini kwa kweli katika haki ya Mungu ni lazima wafanye kila jitihada ili kuwatia nguvu waamini wenzao kwa kutumia haki ya Mungu badala ya kuwalaumu kwa sababu ya udhaifu wa imani zao. 
 

Ni Lazima Tusiwahukumu Watumishi wa Mungu
 
Aya ya 4 inasema, “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.”
Ni lazima tuwatambue watumishi wa Mungu ambao Mungu amewathibitisha pamoja na imani zao. Je, wewe unawalaumu na kuwahukumu watumishi wa Mungu hali ukiwa unaishi maisha yako ya Kikristo? Basi kama ni hivyo, Mungu ataikemea hiyo imani yako zaidi na zaidi. Ikiwa utazihukumu imani za wale ambao amewathibitisha na kuwakubali ati kwa sababu tu huwapendi, basi tambua kuwa wewe unapanda katika kiti cha hukumu cha Mungu na kutoa hukumu kwa watumishi wa Mungu. Kwa kweli kufanya hivyo si sahihi. Bali unapaswa kuwapokea watumishi hao wa Mungu unaowachukia kwa shukrani na kisha kutii ushauri na maelekezo yao wanapokuwa wakiinua haki ya Mungu. 
Ni lazima Mungu azithibitishe imani yetu. Ni lazima tuwe na imani ya kweli ambayo inatii maagizo ya Mungu. Kwa kuwa Mungu ameturuhusu sisi kuyatoa maisha yetu kwa Yesu Kristo, basi tunamshukuru Mungu kwa haki yake. Ni lazima tuwathibitishe na kuwakubali wale ambao Mungu amewathibitisha na kuwakubali, na pia ni lazima tusiwathibitishe na kuwakataa wale ambao Mungu hajawathibitisha na kuwakataa. Ninaamini kuwa utamtukuza Mungu kwa kuwa na imani katika haki yake badala ya kuiinua haki yako binafsi. Ninaamini kuwa Mungu ataithibitisha imani yako. Kisha utainuliwa kwa sababu ya imani yako katika haki yake. 
 

Ikiwa na Wao Pia Wanaamini Katika Haki ya Mungu...
 
“Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu.” (Warumi 14:5-6).
Miongoni mwa Wayahudi kulikuwa na wale ambao waliokolewa kwa kumwamini Kristo, ambaye ni Bwana wetu wa injili ya maji na Roho. Pamoja na kuwa wengi wao walimwamini Yesu, bado wengi wao walikuwa bado wamefungwa na Sheria. Lakini bado walikuwa ni watumishi wa haki ya Mungu kwa kuwa lolote walilolifanya katika kuishika Sheria walikuwa wakiineza haki ya Mungu. 
Hii ndiyo sababu Paulo alisema, “Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria) ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria” (1 Wakorintho 9:20-21).
Kwa kweli hatupaswi kuzidharau wala kuzikataa imani za wale wanaoamini katika haki ya Mungu. Ikiwa wanaamini katika haki ya Mungu na ikiwa wanamtumikia Mungu, basi ni lazima tuwakubali na kuwatambua wao kuwa ni watumishi wa Mungu. 
 

Wenye Haki Wataishi Kwa Ajili ya Bwana 
 
Aya za 7-9 zinasema, “Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.”
Sisi tunaishi pamoja na Kristo na tunakufa pamoja naye kwa sababu tumeokolewa toka katika dhambi zetu zote na tumepokea maisha mapya kwa kuamini katika haki ya Mungu iliyofunuliwa katika injili. Mambo yote ya kale yamepita katika Kristo na tumefanyika kuwa viumbe vipya. Kuamini kwa kweli katika haki ya Mungu maana yake ni kufahamu na kuuamini ukweli kuwa wewe ni wa Kristo. Hivyo, wale wanaoamini katika haki ya Mungu hawana lolote zaidi la kufanya na ulimwengu huu na badala yake wamefanyika kuwa watumishi wa Mungu. 
Ikiwa unafanyika kuwa mtumishi wa Mungu, basi kwa hakika utamwinua Mungu, utampenda, utaishi kwa ajili ya utukufu wake, na kisha utamshukuru kwa kukuruhusu wewe kuishi maisha yako kwa namna hii. 
Je, ni kweli kuwa wewe ni mali ya Kristo? Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wamesulubiwa pamoja na Kristo na wamerudishwa tena katika maisha pamoja naye. Kwamba tukiishi au tukifa sisi tu mali ya Kristo kwa kupitia haki ya Mungu. Bwana anafanyika kuwa ni Bwana wa waliookolewa. 
 

Hatupaswi Kuwahukumu Waamini Wenzetu
 
Imeandikwa katika Aya ya 10-12, “Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa kama niishivyo, anena Bwana kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.”
Kwa sababu Kristo Mungu wetu anaishi, basi ni hakika kuwa siku moja tutapiga magoti mbele zake na kukiri kila kitu. Hivyo ni lazima tusikae katika kiti cha hukumu na kisha kuwahukumu kaka na dada zetu bali tunapaswa kusimama mbele za Mungu kwa unyenyekevu. Ni muhimu sana kuishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu zaidi ya kuhukumiana na kulaumiana katika Kanisa lake. Ikiwa tutawahukumu na kuwalaumu kaka na dada zetu kutokana na udhaifu wao, basi na sisi pia tutahukumiwa kwa udhaifu wetu mbele za Mungu. Hii ndiyo sababu tunapaswa kutambua jinsi ilivyo vema kuishi kwa ajili ya mapenzi ya Mungu kwa pamoja katika kanisa lake. 
Imani ya kweli inawatia nguvu waamini wa kweli na inaifuatia haki ya Mungu. Kumbuka kuwa imani isiyo ya kweli itaiacha haki ya Mungu na kuijenga haki yake yenyewe. Vipi kuhusu wewe? Je, unaifuata haki ya Mungu kwa imani? Au unaifuata haki ya mwili wako binafsi? 
 

Ni Lazima Tuimarishane Katika Imani 
 
Aya za 13-14, zinasema, “Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.”
Kwa kuwa kuna tofauti katika kiwango cha imani miongoni mwa wale wanaoamini katika haki ya Mungu, basi tunapaswa kufanya kazi ya kujengana katika imani zetu kwa kutiana moyo. Jambo hili linaleta ukuaji kwa waamini wa haki ya Mungu. Ikiwa kweli tutaishi kwa ajili ya Mungu na haki yake basi sisi tutakuwa watu wake. 
Ikiwa wewe ni Mkristo unayeamini katika haki ya Mungu unaweza kufanya lolote kwa imani yako katika Neno la Mungu. Ikiwa hauwezi, basi ni kwa sababu wewe unaifuata haki yako binafsi badala ya kuifuata haki ya Mungu. Kuifuata haki yako binafsi mbele ya haki ya Mungu ni sawa na kuufuata ulimwengu na kuwa na imani potofu. 
Wale wanaoitafuta haki yao binafsi pamoja na kuwa wameokoka kwa kuamini katika haki ya Mungu, basi watu hao wanaishi kama maadui wa Mungu. Mungu anawapenda wale waliookoka kwa kuamini katika haki yake kuendelea kuifuata haki yake katika maisha yao yote. 
 

Tembea Katika Upendo 
 
Aya za 15-18 zinasema, “Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya. Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu tena hukubaliwa na wanadamu.” 
Wale waliookolewa kwa kuamini katika haki ya Mungu wanaishi ili kuieneza haki hiyo ya Mungu na wala hawawadharau watu wake kwa sababu ya chakula. Wakati mwingine tunaleta chakula ili kushirikiana na wengine kwa upendo. Lakini Paulo anatuonya sisi kuhusiana na kuwatenga ndugu maskini na akina dada maskini na kushirikiana na matajiri kwa sababu jambo hilo litamfanya Mkristo kujikwaa. 
Baraka ambazo Mungu amewapatia wale wanaoamini katika haki ya Mungu zinaturuhusu kuifuata haki ya Mungu, zinatupatia amani ya akili tunayoipata katika injili ya maji na Roho, na zinatuwezesha kumtumikia Bwana kwa pamoja hali tukishirikishana furaha zetu ambazo Mungu ametupatia. Hivyo wale ambao ni matajiri ni lazima watambue kuwa utajiri wao wote unatoka kwa Mungu na kwamba wanapaswa kuushirikisha utajiri wao pamoja na wengine hali wakiitumika injili na kuifuata haki ya Mungu kwa pamoja. Mungu anafurahishwa na watu wa jinsi hiyo na anawapenda sana wanapoishi maisha kama hayo. 
 

Tafuta Kuwajenga Wengine 
 
Aya za 19-21 zinasema, “Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana. Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza. Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lolote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa.”
Hapo zamani katika miji kama Rumi na Korintho, kwa nyakati fulani watu waliuza vyakula vilivyokuwa vimetolewa sadaka kwa miungu. Baadhi ya waamini katika haki ya Mungu walizoea kununua vyakula vya jinsi hiyo na kuvila. Kisha baadhi ya waamini waliokuwa na imani dhaifu katika kanisa la Mungu walifikiri kuwa kula vyakula vya jinsi hiyo ilikuwa ni dhambi. Hii ndiyo sababu Paulo alisema, “Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu” (aya ya 20).
Hoja hiyo hiyo pia inatumika katika kuzungumzia suala la mvinyo. Kulikuwa na waamini baadhi ambao hawakujali sana kuhusu kunywa pombe. Lakini Paulo alitoa maelekezo kuwa ikiwa tabia kama hizo za unywaji wa pombe itazifanya imani za waamini kuwa dhaifu basi itakuwa vema ikiwa wataacha kunywa pombe ili kutowakwaza waamini wenzao. Jambo hili pia linatokea miongoni mwetu. Kwa hiyo, ni lazima tuishi maisha yetu ya Kikristo katika namna ambayo inawajenga wengine na kisha tuitafute haki ya Mungu. Kuna mambo ambayo yanaweza kujitokeza leo hii kuhusiana na vyakula vilivyotolewa kafara kwa mababu waliokufa zamani, basi katika hali kama hiyo ni vizuri kutokula vyakula kama hivyo kwa ajili ya wale ambao ni wadhaifu katika imani. 
 

Uwe na Imani Katika Haki ya Mungu
 
Aya za 22-23 zinasema, “Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali. Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.”
Wale wanaoamini katika haki ya Mungu ndio wale walio na imani sahihi. Imani katika haki ya Mungu ni imani itolewayo na Mungu inayoweza kuzisafishilia mbali dhambi zetu zote. Hivyo, Wakristo ni lazima waamini katika haki ya Mungu na wawe na uhakika wa imani yao katika haki ya Mungu. 
Maandiko yanatueleza sisi kuwa kumfuata Mungu pasipo kuamini katika haki yake ni dhambi. Kitu chochote kinachotendwa pasipo kuwa na imani ni dhambi. Ni lazima tuwe na imani zaidi katika haki ya Mungu hali tukifahamu kuwa kitu chochote kinachotendwa pasipokuwa na imani ni dhambi. 
Biblia inasema, “Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia.” Kila kitu ni safi ikiwa utakula kwa imani katika haki ya Mungu kwa kuwa Mungu aliumba kila mmea na mnyama. 
Ni lazima tufahamu jinsi ilivyo muhimu kwetu kufahamu na kuamini katika haki ya Mungu. Ni lazima pia tuwajenge waamini wenzetu waliozaliwa upya na kisha kuziheshimu imani zao.