Search

ስብከቶች፤

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[11-2] Wokovu wa Watu wa Israeli (Ufunuo 11:1-19)

(Ufunuo 11:1-19)
 
Kwa nini Mungu aliwatuma manabii wawili kwenda kwa watu wa Israeli? Mungu alifanya hivyo ili hasahasa kuwaokoa watu wa Israeli. Kifungu kikuu kinatueleza kwamba Mungu atawafanya mashahidi wake wawili kutabiri kwa siku 1,260. Hii inalenga kuwaokoa Waisraeli kwa mara ya mwisho. Kule kusema kwamba Mungu atawaokoa watu wa Israeli kuna maanisha pia kwamba wakati huo mwisho wa dunia utakuwa umefika.
Aya ya 2 inasema, “Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa mana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanganya mji mtakatifu miezi arobaini na miwili.” Hii ina maanisha kwamba wakati mapigo ya kutisha yatakapokuja kwa Wamataifa, wakati wa kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu kitakapoanza na kisha kuleta mkanganyiko mkuu na mapigo, na wakati ambapo miongoni mwa Wamataifa walioisikia na kuiamini injili watakapouawa na kuifia-dini, basi hapo ndipo Mungu atakapowainua manabii wawili kwa ajili ya watu wa Israeli, na atawafanya manabii hao kushuhudia kwamba Yesu ni Mungu na Mwokozi, na kwa sababu hiyo kuwaokoa Waisraeli. Kifungu hiki kinatueleza kwamba hizo ndizo kazi za Mungu ambazo zitakuja hapo baadaye.
Ni lazima tulifundishe hili Neno kwa wale ambao, hali wakiwa wamedanganywa na shetani, wanadai kwamba viongozi wa madhehebu yao ndio mizeituni miwili ya nyakati za mwisho, na kwamba mwanzilishi wa kikundi chao cha kidini ni Eliya aliyetabiriwa katika nyakati za mwisho. Kila mara makanisa ya kidunia yanapozungumza juu ya Ufunuo, yanakitumia kifungu hiki kinachozungumza juu ya mizeituni miwili mara nyingi. Kati ya watu wote waliodanganywa na vikundi-dini vya kizushi na ambao nimekutana nao katika maisha yangu ya kiimani hadi sasa, hakuna hata mmoja aliyeshindwa kudai kwamba kiongozi wa kikundi chake cha kidini ni mmoja kati ya ile mizeituni miwili inayotajwa katika kifungu hiki cha maandiko. Kila mzushi niliyekutana naye hatimaye ametoa madai ya jinsi hiyo.
Lakini mizeituni miwili na vinara vya taa viwili vya Ufunuo havina uhusiano na yale ambayo wazushi hawa wanadai. Kiukweli, mizeituni hii miwili ina maanisha ni manabii wawili ambao Mungu atawainua miongoni mwa Waisraeli ili kuweza kuwaokoa.
Sura ya 11 inatueleza kwa kina jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wa Israeli. Kama ilivyo kwa Kitabu cha Warumi, kila sura katika Kitabu cha Ufunuo ina wazo kuu linalojitegemea. Kwa kwa kulifahamu wazo kuu la sura hii ya 11, ndipo tunapoweza kufahamu kwamba kifungu hiki kinaeleza nini. Hali wakisoma kwamba Wamataifa wataukanyaga mji mtakatifu kwa mizei arobaini na mbili, basi baadhi ya watu wanadai hata pasipo kufahamu wazo kuu la sura hii, kwamba wakati huo kipindi cha watu wa Mataifa kitakuwa kimekwisha, na kwamba kipindi cha wokovu wa Waisraeli kitakuwa kimefunguliwa, na kwamba kuanzia hapo na kuendelea Waisraeli wataokolewa.
Lakini hoja hii ipo mbali kabisa na ukweli. Sura ya 7 inatueleza kwamba idadi kubwa isiyohesabika ya Wamataifa watatoka katika ile Dhiki na kukokolewa—yaani, Wamataifa na Waisraeli wote wataokolewa wakati wa Dhiki, na kwamba si Waisraeli peke yao. Hivyo, kile ambacho sura ya 11 inatueleza ni kwamba Mungu atawainua manabii wawili ili kuwaokoa watu wa Israeli katika nyakati za mwisho, ukweli huu hautuelezi kwamba Wamataifa hawataokolewa.
Baadhi wanaweza kuuliza hivi, “Waisraeli 144,000 si walikwisha okolewa, maana sura ya 7 inatueleza kwamba hii ni idadi ya Waisraeli ambao walikuwa wametiwa muhuri na Mungu?” Kutiwa muhuri si sawa na kuokolewa. Hakuna hata mmoja anayeweza kuokolewa pasipo kupitia Yesu Kristo. Wokovu unakuja kwa kuamini kwamba Yesu Kristo alifanyika kuwa Mwokozi wetu kwa kuja hapa duniani, kwa kubatizwa na kuzichukua dhambi zetu zote, kwa kuzichukua dhambi zote za ulimwengu na kwenda nazo Msalabani na kisha kufa Msalabani, na kisha kufufuka tena toka kwa wafu.
Pamoja na kuwa tunafahamu kwamba tumefungwa katika dhambi hadi tutakapokufa, ukweli ni kwamba tumeokolewa kwa kuamini kwamba Yesu Kristo alizifanya dhambi zetu zote kutoweka na hivyo amefanyika kuwa Mwokozi wetu. Ingawa Waisraeli 144,000 watatiwa muhuri, Mungu atawainua manabii wake wawili, na atawatumia manabii hao kuihubiri injili yake kwa Waisraeli. Kwa maneno mengine, Neno hili linatueleza kwamba manabii wawili wataihubiri injili kwa Waisraeli, na kwamba 114,000 wataokolewa.
Biblia haina ubabaishaji wala ubaguzi. Hakuna hata mmoja anayeweza kuokolewa pasipo kupitia Yesu Kristo. Pasipo kupitia Yesu Kristo Mungu anachoweza kukisema ni “Hujaokolewa.”
Manabii wawili, ambao ni miti miwili ya mizeituni iliyotajwa katika kifungu hiki, watauawa mahali panapoitwa Golgotha. Miili yao itaachwa pasipo kuzikwa, na wale wasiompokea wala kumwamini Yesu watafurahia kuuawa kwao na watatumiana zawadi. Lakini aya ya 11 na ile ya 12 inatueleza kwamba, “Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.”
Hii inatueleza moja kwa moja kwamba sisi—yaani, wewe na mimi ambao ni Wamataifa—tutauawa pia na kuifia-dini kwa imani wakati utakapowadia, na kwamba muda mfupi baada ya sisi kuuawa na kuifia-dini, ufufuo na unyakuo wetu vitafuata. Jambo hili linaendelea kuonekana katika sehemu mbalimbali za Kitabu cha Ufunuo. Pia kuna vifungu vinavyotueleza kwamba wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapokuwa yamemiminwa katika dunia hii, watakatifu walionyakuliwa watakuwa wakimsifu Mungu angani.
Sura ya 14 pia inazungumzia juu ya watu 144,000 waliookolewa, huku wakimsifu Mungu kwa wimbo ambao hakuna hata mmoja anayeweza kuuimba isipokuwa aliye malimbuko ya wokovu ndiye anayeweza kuimba. Hapa tunaelezwa kwamba baada ya watu wa Israeli kuokolewa, watauawa na kuifia-dini kila mahali, na mara baada ya kuuawa na kuifia-dini ufufuo na unyakuo wao utafuata.
Hili pia litawahusu pia Wamataifa. Katika nyakati za mwisho, wewe na mimi tutapitia magumu ya mapigo ya matarumbeta saba, lakini Mungu atatulinda na mapigo haya. Wakati Dhiki Kuu ya miaka saba itakapofikia kilele chake kwa kupita miaka mitatu na nusu, basi mateso ya watakatifu yatakuwa yamefikia kileleni. Lakini mateso haya ya kutisha yatadumu kwa muda mfupi tu. Watakatifu wengi na watumishi wa Mungu watauawa na kuifia-dini, na mara baada ya kuuawa na kuifia dini unyakuo wao utafuata.
Kwa nini? Kwa sababu Ufunuo imekuwa ikiandika mara kwa mara kwamba wakati mapigo ya mabakuli saba yatakapokuwa yakimiminwa hapa duniani, basi watakatifu watakuwa wapo mbinguni wakimsifu Mungu. Neno linautaja mchakato huu kuwa ni wa ajabu.
Ufunuo 10:7 inasema, “isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Siri ya Mungu iliyofichwa si kitu kingine chochote zaidi ya kunyakuliwa. Katika 1 Wathesalonike 4:16, Mtume Paulo anatueleza kwamba, “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.”
Hata hivyo, kule kusema kwamba Bwana atashuka kutoka Mbinguni, hakumaanishi kwamba atashuka hapa duniani haraka. Bwana atashuka kutoka Mbinguni hadi angani, na wakati ufufuo wa kwanza utakaowafufua waliolala na kuwabadilisha wale waliozaliwa tena upya wakiwa hai utakapotokea, basi hapo ndipo unyakuo ambao kwa huo watakatifu watampokea Bwana utafuata. Baada ya chakula cha harusi ya Mwana-kondoo kufanyika angani na baada ya ulimwengu huu kuangamizwa kabisa kwa mapigo ya mabakuli saba, Bwana atashuka katika ulimwengu utakaokuwa umefanywa upya pamoja nasi na ataonekana mbele ya wale watakaokuwa wapo hai.
Kulitafsiri Neno la Ufunuo kwa kuzingatia mawazo binafsi ya mtu ni kuelekea katika njia ya maangamizi. Ni makosa kabisa kuamini katika nadharia tupo zinazopendekezwa na baadhi ya wanatheolojia, pia ni makosa kutetea nadharia hizo pasipo kulifahamu Neno.
Miongoni mwa watheolojia wanaoheshimwa sana katika jamii za Wakristo wahafidhina, yaani wanazuoni kama vile L. Berkhof na Abrahamu Kuyper waliotoa nadharia ya amilenia. Kati ya nadharia hizi, nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, kunyakuliwa baada ya dhiki, na amilenia, kuamini katika nadharia ya amilenia ni sawa na kutoiamini Biblia yenyewe.
Kipindi ambapo watu walikuwa wakiamini katika nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki kimeshapita, na katika kipindi hiki, wengi wanaamini katika nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Lakini nadharia hii pia haina uhalali wa kibiblia. Lakini bado kuna watu wengi wanaoipenda nadharia hiyo hasa wanapoelezwa juu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Kwa nini? Kwa sababu kwa mujibu wa nadharia hii ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, Wakristo hakuna watakachokihofia kuhusiana na kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu.
Hivyo, nadharia hiyo inawafanya waamini waikubali maana wanaishi maisha ambayo si baridi wala si moto, na kuyafanya makanisa kushughulika zaidi na ongezeko la idadi ya waumini wao. Hivyo, imani za watu zinakuwa na uzembe. Kwa kuwa wanafikiri kuwa hawana kitu cha kuhofia kuhusiana na kipindi cha Dhiki Kuu, hivyo imani yao inakuwa ni ya kizembe wakati ambapo imani yao inapaswa kuwa imara kufuatia ujio wa nyakati za mwisho. Hapo zamani za kale, watu walikuwa wakiiamini nadharia ya amilenia, kisha wakaiamini nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki kwa muda, na sasa wanaamini juu ya nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki.
Mwaka 1830, Mchungaji Scofield, aliyekuwa profesa katika Taasisi ya Biblia ya Moody, alianza kuandika Biblia ya marejeo. Huyu Scofield alikuwa ameshawishiwa sana na mwanatheolojia mashuhuri aliyeitwa Darby.
Darby, mwalimu wa kiroho wa Scofield, ambaye hapo awali alikuwa ni kasisi wa Kikatoliki alikuwa na akili sana na mwenye ufahamu wa juu. Yeye aliliacha Kanisa Katoliki baada ya kuzitambua nadharia zake za uongo, kisha akajiunga na asasi ndogo ya Kikristo na akawa kiongozi wake. Pamoja na kwamba Darby alisoma Biblia mara kwa mara, hakuweza kuelewa kikamilifu ikiwa unyakuo utatokea kabla au baada ya Dhiki Kuu. Hivyo aliamua kusafiri ili kutafuta ushahidi wa wazi kuhusiana na jambo hili.
Katika safari hii, alikutana na binti wa kike aliyekuwa kiongozi wa elimu ya kiroho. Huyu binti alidai kwamba ameona katika maono kwamba kunyakuliwa kutatokea kabla ya Dhiki Kuu. Hali akiamini hilo kwamba unyakuo utatokea kabla ya Dhiki, Darby alihitimisha masomo yake ya kibiblia kwa nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki.
Hata hivyo, kwa kuwa watu wa wakati huo walikuwa wameamini zaidi katika nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki, hiyo nadharia ya Darby ya kunyakuliwa kabla ya dhiki haikupokelewa vizuri.
Darby alidai kwamba kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Ufunuo ni wokovu wa watu wa Isareli, na kwamba haisemi chochote kuhusu wokovu wa Wamataifa. Na kuhusu lile neno linalosema “Imekupasa kutoa unabii tena (10:11),” alilitafsiri kuwa ni injili ya Ufalme ambayo inatangaza ujio wa ufalme huo badala ya ukweli kwamba ni kuihubiri injili ya maji na Roho.
Scofield, ambaye aliikubali nadharia hiyo ya Darby kama ilivyo na hivyo akaiweka nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki katika Biblia yake ya marejeo, kisha akatengeneza nadharia yake juu ya nyakati saba. Madai kama hayo ya Scofield yalitimiza matakwa ya wakati wake na yakaendana vizuri sana na hali yake, na hivyo madai hayo yalileta mjadala mkubwa wa kidini ulimwenguni kote na hatimaye yakakubaliwa katika sehemu nyingi.
Lakini Mungu anasema nini katika Biblia? Katika maandiko tunamwona Yesu akilipokea na kulifungua gombo lililokuwa limetiwa mihuri saba mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, yaani Yesu aliyeigawa historia katika vipindi saba kwa mihuri saba.
Kipindi cha kwanza ni kipindi cha farasi mweupe. Hiki ni kipindi cha wokovu, kipindi ambacho Mungu aliamua kutuokoa tangu wakati ule alipouumba ulimwengu huu na alipomuumba mwanadamu, na ni hakika kwamba Mungu ametuokoa. Kama vile Ufunuo 6:2 inavyotueleza, “Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda,” Bwana ameshinda na ataendelea kushinda. Hata kabla ya uumbaji, injili ilikuwepo na wokovu ulikuwa umekwisha anza.
Kipindi cha pili ni kipindi cha farasi mwekundu, yaani wakati wa Shetani. Hiki ni kipindi cha Ibilisi ambapo ataipora amani toka kwa wanadamu, na kuwafanya kupigana vita dhidi yao, kuchukiana, na kushiriki katika machafuko ya kidini. 
Kipindi cha tatu ni kipindi cha farasi mweusi, ambacho ni kipindi cha njaa ya kimwili na kiroho, na kipindi cha nne ni kipindi cha farasi wa kijivujivu, yaani kipindi cha mauaji ya kuifia-dini. Kipindi cha tano ni kipindi cha unyakuo—Mungu amepanga unyakuo wa watakatifu kama moja ya nyakati zake. Kipindi cha sita ni kile cha mabakuli saba, kikiwa kimehusisha maangamizi ya ulimwengu huu, na kipindi kinachofuatia ni kile cha Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya. Hivyo, Mungu ameupanga ulimwengu huu katika nyakati saba, ndani ya gombo lilitiwa mihuri saba.
Maoni ya Scofield juu ya nyakati saba yalijengwa katika msingi wa maono na mawazo yake binafsi. Kinyume na mawazo hayo, nyakati saba zilizotabiriwa katika Ufunuo 6 kwa kupitia mihuri sita katika lile gombo lililoshikiliwa na Mungu ni nyakati zilizopangwa na Mungu Mwenyewe. Hata hivyo bado watu wanazizungumzia nadharia zilizotengenezwa na watu, yaani nadhari ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, na kwa sababu hiyo wale wanaoiamini nadharia hiyo wanafikia hitimisho kwamba hawana sababu yoyote ya kumwamini Bwana kwa nguvu.
Wanaoamini hivyo wameamua katika mioyo yao kwamba, “Kwa kuwa tutanyakuliwa kabla ya Dhiki Kuu, tutakuwa tayari tupo katika uwepo wa Mungu wakati miaka saba ya Dhiki Kuu itakapowadia. Hivyo hatuna cha kuhofia!” Kama Neno la Mungu lingekuwa limetuambia kwa hakika kwamba tutanyakuliwa kabla ya ile Dhiki, basi kusingelikuwa na sababu ya kuiandaa imani yetu, na kwamba kuhudhuria Kanisani mara moja au mbili kwa mwaka kungekuwa kunatosha. Lakini Mungu hajatueleza hivi.
“Nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini.” “Nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili.” Neno la Mungu kama hilo linatueleza kwamba Wamataifa pia wataokolewa katika kipindi cha Dhiki. Mungu atawainua manabii wake wawili ili kuieneza injili ya maji na Roho. Hakuna hata mmoja anayeweza kusimama mbele ya Mungu pasipo kupitia kwanza katika kipindi cha miaka mitatu na nusu katika ile miaka saba ya kipindi cha Dhiki Kuu iliyopangwa na Mungu, yaani wakati wa magumu utakapokuwa umewadia. Mungu anatueleza pia kwamba wafia-dini wengi watatoka katika kipindi cha Dhiki.
Ili kumwamini Yesu kiusahihi, imempasa mtu kujifunza Biblia kikamilifu na kuamini kile kilicho sahihi. Ikiwa watu wanahubiri na kuamini kivyao pasipo kusoma kila ukurasa wa Biblia kwa uangalifu, basi ni hakika kuwa wataishia kuwa wazushi. Sababu inayofanya kuwe na madhehebu mengi sana katika ulimwengu huu ni kutokana na ukweli kwamba watu wengi wameiweka imani yao kutokana na tafsiri zao binafsi za Biblia.
Kule kusema kwamba watu wa Israeli wataokolewa kuna tueleza kwamba mpango wa Mungu utatimizwa kwa mujibu wa Neno lake la ahadi. Hii pia inatueleza kwamba Mungu hatalivunja Neno lake la ahadi lililotamkwa kwetu bali atayatimiza yote. Hii ndio maana tuna tumaini kubwa sana.
Manabii wawili wa Israeli watafufuliwa baada ya siku tatu na nusu baada ya vifo vyao na kisha watapaa kwenda Mbinguni. Huu ni unyakuo. Tukio hili linatoa mfano wa jinsi ambavyo wafia-dini wakati wa ile Dhiki Kuu watakavyonyakuliwa, na hivyo inatuonyesha juu ya unyakuo wetu. Biblia inatueleza kwamba baada ya kupigwa kwa tarumbeta la saba, ulimwengu huu utakuwa ni Ufalme wa Kristo na kwamba atatawala katika ulimwengu huu milele. Vivyo hivyo, wale waliomwamini Yesu Kristo watatawala pamoja na Kristo.
Baada ya kuwanyakua watakatifu Mungu ataiangamiza dunia hii kikamilifu. Hatufahamu ikiwa maangamizi hayo yatakuwa ni kwa asilimia 100, kwa kuwa hili halijaandikwa katika Biblia, lakini katika Ufunuo 11:18 Mungu anatueleza kwamba, “Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.”
Ni hakika kwamba unyakuo utatokea wakati Dhiki Kuu itakapokuwa ikikaribia kilele chake cha miaka mitatu na nusu—yaani sio mwisho wa miaka mitatu na nusu, bali baada ya kuipita kidogo miaka hiyo mitatu na nusu. Katikati ya kipindi cha miaka saba ndio wakati ambapo Dhiki itakuwa imefikia kiwango chake cha juu. Huu ndio wakati ambapo watakatifu toka watu wa Israeli watauawa na kuifia-dini, na baada ya hapo unyakuo utafuata. Wakati unyakuo utakapotokea, sisi sote tutaungana katika karamu ya chakula cha harusi ya Mwana-kondoo angani.
Wakati tutakapokuwa tukishiriki katika chakula cha harusi ya Mwana-kondoo angani kama Mathayo 25 inavyotueleza, mapigo ya mabakuli saba yataishukia dunia hii. Hali tukiyaona mambo yote yatakayokuwa yakitokea katika dunia hii, tutakuwa tukimsifu Mungu angani na kumshukuru kwa neema yake.
Ninatumaini na kuomba kwamba kwa kupitia Neno la Ufunuo, utaweza kuzitofautisha nyakati wakati siku za mwisho zitakapowadia, pia utaweza kuliamini Neno kiusahihi, utaishi maisha yako kwa imani, na kisha utajiandaa kwa ajili ya yatakayojiri baadaye. Unapaswa kuiandaa imani yako ili uweze kushiriki katika kumsifu, kumheshimu, na kumwabudu Bwana huku ukishiriki katika chakula cha harusi ya Mwana-kondoo pamoja naye.
Ninatumaini kwamba Neno la Ufunuo litathibitisha kuwa ni mwongozo mkuu kwako kuhusu siku zinazokuja baadaye, hali likiukumbusha moyo wako tena kwamba unapaswa kuishi kwa uvumilivu na kwa uaminifu kwa imani yako katika injili ya maji na Roho.